Wednesday, June 19, 2013

Wanafunzi Wangu Walipata Mkong'oto Babati

Nilikuwa Tanzania mwezi Januari mwaka huu na wanafunzi wa hapa chuoni St. Olaf katika kozi juu ya mwandishi Ernest Hemingway. Tulikaa siku nne Babati.

Siku moja wanafunzi waliniambia wameona kiwanja mjini hapo na wanataka kwenda kucheza kabumbu. Walipofika kiwanjani, waliwakuta vijana wenyeji wamevalia sare za kabumbu, wakapatana kuwa wapimane nguvu.

Wanafunzi walitwanga vibaya, ila sikumbuki walitwangwa magoli mangapi. Siku ya pili wanafunzi wakaenda tena. Nadhani walikuwa na ndoto ya kulipiza kisasi. Wapi, ndugu yangu. Waligaragazwa tena.

Nadhani siku hiyo Babati ilisisimka sana. Kwanza, sio kawaida kutembelewa na wazungu wengi namna hii. Halafu, huenda waliamini kuwa hao wazungu ni wacheza soka, na kwa maana hiyo, matokeo ya mechi yalikuwa kwamba wa-Marekani wamegaragazwa Babati. Yawezekana kuwa hayo ndio maneno yaliyoenea mitaani.

Ukweli ni kuwa hao wanafunzi wangu wala sio timu ya kabumbu. Walijikusanya tu kiholela wakaenda uwanjani. Ila, kwa vile ninapangia kuwapeleka wanafunzi wengine siku za usoni, labda itakuwa vema nikiwaambia kabla kuwa wafanye mazoezi ya kabumbu, ili kuwafundisha somo watu wa Babati. Kwa hivi, watu wa Babati subirini kichapo.

Hizo mechi za kabumbu zilifanikisha sana ndoto yangu ya kujenga mahusiano baina ya wa-Marekani na wa-Tanzania. Ni mbinu ambayo nitafanya juu chini niitumie siku zijazo. Hapo pichani, hao wanaume wanne walioko mstari wa mbele kabisa bila sare si watu wa Babati bali madreva wa msafara wetu.

No comments: