Tuesday, June 4, 2013

Sikujua Mwandishi Legson Kayira Alifariki

Leo katika kupitapita mtandaoni, nimeona taarifa kuwa mwandishi Legson Kayira alifariki mwaka jana, tarehe 14 Oktoba. Sikuwa nimepata taarifa hii ya kifo chake.

Kilichonifanya nikatafuta habari za Kayira ni kuwa siku chache zilizopita, niliongea na mzee mmoja m-Marekani na katika maongezi na mzee mmoja m-Marekani, mzee huyu alikumbushia kuhusu mwandishi fulani, na kutokana na maelezo yake, nikahisi anamwazia Legson Kayira. Nilipomtajia, pamoja na jina la kitabu chake maarufu cha I Will Try, mzee huyu alikubali kuwa ni yeye aliyekuwa anamwazia.

Basi leo, katika kuangalia mtandaoni, nimesoma kuwa kumbe mwandishi huyu alifariki mwaka jana, akiwa na miaka 70. Taarifa hii imenikumbusha miaka ya ujana wetu, tulipokuwa sekondari. Tulikipenda sana kitabu cha I Will Try.

Habari ya kijana fukara Legson Kayira kuamua kutembea kwa mguu kutoka kijijini kwake Malawi ili akafike Marekani kusoma, ilikuwa ni habari ya kusisimua, iliyotutia hamasa ya kuwa wakakamavu katika kufuatilia malengo bora ya maisha. Kwa kweli nashukuru tulielimishwa kwa namna ile, ya kuthamini juhudi na ustahimilivu, sio mambo ya mkato.

Miaka yetu ile tulikuwa tunapenda kusoma vitabu. Tulisoma vitabu vilivyohitajika kwa masomo darasani, lakini tulisoma pia vitabu nje ya mahitaji ya darasani. Kayira alikuwa mmojawapo wa waandishi waliotuvutia. Binafsi, pamoja na kusoma I Will Try, nilisoma pia kitabu chake kilichofuatia, kiitwacho Jingala. Sina hakika, lakini huenda nilisoma pia The Looming Shadow.Le3o nimeona pia taarifa kuwa kitabu cha I Will Try sasa kinapatikana kama kitabu pepe mtandaoni.

Sambamba na Kayira, waandishi wengine kutoka Malawi waliokuwa wakisifika walikuwa Aubrey Kachingwe na David Rubadiri. Hao wote ni kama makamanda waliojenga misingi ya uandishi wa ki-Kingereza Malawi. Leo Malawi iko mbali sana katika uwanja huo. Na kwa jinsi wa-Tanzania tunavyoendekeza uzembe na visingizio elfu, hatutawafikia.

1 comment:

tzforchange said...

Kweli ya kale na wa kale ni dhahabu