Sunday, June 2, 2013

Nimehudhuria Ibada ya Ki-Swahili, Minneapolis

 Leo, baada ya kukosekana kwa miezi mingi, nilienda kuhudhuria ibada ya ki-Swahili Minneapolis. Ni ibada ya madhehebu ya ki-Luteri, ambayo hufanyika katika kanisa la Holy Trinity Lutheran Church.

Ibada iliendeshwa na mchungaji Dr. Mwalilino. Kwaya iliendeshwa na ndugu Smart Baitani, mwanzilishi na mkurugenzi wa COSAD. Nilipopata fursa ya kuongea na Baitani, ambaye tumefahamiana kwa zaidi ya miaka ishirini, nilimtania kuwa sikutegemea kumwona Minneapolis wakati huu, kwani nilidhani yuko Muleba (Bukoba).

Kwenda kwangu leo kulitokana na mwaliko wa rafiki yangu, Mzee Paul Bolstad, anayeonekana wa pili kutoka kulia hapo pichani.

Aliniambia kuwa leo angekuwepo mchungaji mgeni, Herb Hafermann, ambaye anaonekana kushoto kabisa. Mchungaji huyu anaifahamu sana Tanzania, na ameishi kule miaka mingi. Mara yake ya kwanza kuja Tanzania ni mwaka 1963, na bado yuko kule. Alitoa mahubiri leo, kwa ki-Swahili. Anaongea ki-Swahili sawa na wa-Swahili, na michapo juu. Wakati huu mchungaji huyu yuko Lutheran Junior Seminary, Morogoro.

Nilimwambia kuwa nimewahi kufika katika chuo kile. Mzee Bolstad alimweleza kuhusu shughuli zangu za uandishi, na alitaja hasa kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Tulikubaliana kuwa niandae nakala nimpelekee mchungaji wakati akiwa bado hapa Marekani, ili ikawekwe katika maktaba ya Lutheran Junior Seminary. Mzee Bolstad ni mdau na mpiga debe mkubwa wa kitabu hicho, na pia mdau mkubwa wa blogu hii ya hapakwetu. Alizaliwa Tanganyika (Tanzania) na kukulia kule.

Nilikutana na watu wengi, wale tunaofahamiana na wengine tukafahamiana leo hii. Nilikutana na hata mdau wa blogu yangu, ambaye nilikuwa simjui. Aliniambia anaitwa Eric. Alinikosoa kwa kutoweka taarifa kila siku katika blogu, akatoa mfano wa namna taarifa yangu kuhusu safari ya Montana kumwona Mzee Patrick Hemingway ilikaa kwenye blogu siku nyingi, bila kuwekwa nyingine. Nami nilikubaliana naye kwamba huu ni udhaifu, nikaongezea kuwa Michuzi ndio anaiweza kazi hii, kwani anaweka taarifa nyingi kwenye blogu yake kila siku. Nilikiri wazi kuwa mtu kama mimi nababaisha tu kadiri ninavyoweza. Hata hivi, nilimwambia kuwa nimeguswa kumkuta mdau kama yeye, na kwamba itabidi nijitahidi kufuata ushauri wake, ili angalau iwe ni shukrani yangu kwa wadau wanaofuatilia blogu yangu.

Huyu mwenye Kaunda suti ni ndugu Charles Semakula, mratibu wa ibada ya ki-Kiswahili.

No comments: