Tulipomtembelea Mzee Patrick Hemingway, kule Montana, alituzawadia nakala za kitabu cha Ernest Hemingway, True at First Light. Tayari nilikuwa na nakala mbili hivi za kitabu hiki, na nilikuwa nimekisoma. Pia ni kitabu kimojawapo ambacho nilikitumia katika kozi yangu ya "Hemingway in East Africa."
Hata hivi, zawadi hii kutoka kwa Mzee Patrick Hemingway ilinigusa sana. Jalada lake tu lilinivutia kwa namna ambayo siwezi kuelezea. Pili, ilikuwa ni bahati ya pekee kupata nakala kutoka kwa mhariri wa kitabu.
Ernest Hemingway aliandika mswada mrefu sana kutokana na safari yake ya pili Afrika Mashariki. Alisafiri na kuishi kule miezi kadhaa, kuanzia mwaka 1953 hadi 1954. Hakuuchapisha mswada huu, bali aliuhifadhi Cuba, ambako aliishi miaka mingi. Alisema kuwa ni urithi kwa watoto wake.
Miaka ya hivi karibuni, mswada huu ulitayarishwa na kuchapishwa kitabu, Under Kilimanjaro. Ni kitabu kikubwa sana, ila nilikuwa nimekisoma. Humo, Hemingway anaelezea vizuri hali ilivyokuwa miezi aliyokaa Afrika Mashariki, akiwa na Mary Welsh, mke wake wa nne, na wa mwisho. Anaelezea vizuri maisha ya wenyeji, hasa wa-Kamba na wa-Maasae.
Mzee Patrick Hemingway ametufanyia msaada mkubwa kwa kuuhariri mswada ule upya na kuchapisha True at First Light, ambacho ni kitabu cha wastani, sio kikubwa kama Under Kilimanjaro. Katika kozi yangu ya "Hemingway in East Africa," nilijaribu kutumia Under Kilimanjaro, lakini niliona kuwa ni kazi nzito mno kwa wanafunzi, na muda haukutosha. Lakini kwa sisi watafiti, ni wajibu kulisoma na kulitafakari buku hili lote.
Jambo jingine la peke kwangu ni kuwa Mzee Patrick Hemingway alisaini nakala hizo alizoutuzawadia. Hapa naleta picha ya kumbukumbu hiyo adhimu. Kwa watu wenye uzoefu wa vitabu, ni bahati ya pekee kusainiwa nakala ya kitabu chako na mwandishi au mhariri.
Nimalizie tu kwa kusema kuwa baada ya kurejea kutoka Montana, nilikuwa na dukuduku ya kufahamu zaidi kuhusu mchapishaji wa hili toleo tulilozawadiwa na Mzee Patrick Hemeingway.
Nilishaona, mwanzoni mwa kitabu, kuwa mchapishaji ni Arrow Books wa Uingereza. Katika kutafuta zaidi mtandaoni, niliona pia picha ya hilo jalada inayoonekana hapa juu, ambayo sikuwa nimeionaa popote kabla. Kama ilivyo kwa vitabu vingi, kitabu cha True at First Light kimechapishwa kikiwa na majalada tofauti.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault
Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...
-
Leo ni kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa kwangu, ambayo ni tarehe 17 Agosti, 1951. Familia yangu, ndugu, na marafiki wamejumuika nami kushereh...
-
Leo napenda kukitambulisha kwako mdau kitabu muhimu cha ki-Swahili, Tenzi Tatu za Kale . Nilinunua nakala yangu miaka kadhaa iliyopita katik...
-
Kutafsiri kazi ya fasihi ni kazi ngumu ya kuchemsha bongo. Inahitaji ufahamu wa hali ya juu wa lugha husika, na pia hisia makini za kifasih...
No comments:
Post a Comment