Tuesday, July 15, 2014

Leo Nimeongea Tena na Mzee Patrick Hemingway

Leo, saa kumi na dakika hamsini na mbili, nilimpigia simu Mzee Patrick Hemingway. Niliona tu nimpigie, baada ya kimya cha miezi mingi, wakati nilipozidiwa na homa. Sasa, kwa vile najisikia nafuu sana, niliamua kumpigia Mzee Hemingway. Nilimweleza kuwa nimekuwa kimya kwa muda mrefu kwa sababu ya kuugua, ila sasa hali yangu ni nafuu sana na inaendelea kuimarika. Tumeongea hadi saa kumi na mbili na robo.

Baada ya kusalimiana tu, Mzee alinifahamisha kuwa yeye na ndugu yake Sean Hemingway wamechapisha toleo jipya la kitabu cha Hemingway, The Sun Also Rises. Nami hapo hapo nikamwambia kuwa nimempigia simu leo baada ya kusikiliza, jana, mahojiano baina ya mtangazaji wa redio na Sean Hemingway, kuhusu kuchapishwa kwa toleo hili

Mada hii tumeiongelea kwa muda mrefu, tukijumlisha pia mawazo na maandishi mengine ya Hemingway, kama vile True at First Light na Under Kilimanjaro. Tuliongelea kuhusu wahakiki wa Hemingway na jinsi Hemingway alivyokuwa hawapendi. Mzee Hemingway aliniambia kuwa kuna makala yenye mawazo mazuri kuhusu Hemingway ambayo ameisoma mtandaoni, iliyoandikwa na mhakiki wa Iran.

Hiyo mada ya uhakiki nayo tumeiongelea kwa muda mrefu, na Mzee Hemingway akasisitiza kuwa waandishi wengi hawatumii ki-Ingereza vizuri. Hapo hapo akaongezea kuwa mimi ni tofauti; naandika vizuri. Nimefurahi sana kumsikia akisema hivyo, na baadaye katika maongezi yetu alirudi tena kwenye suala hili, akasema anakipenda kitabu changu na anakiongelea kwa watu. Hilo nalo limenifurahisha. Nilijua kuwa Mzee Hemingway anakipenda kitabu changu, lakini amenishtua leo kwa kukiongelea wakati ambapo tulikuwa tunaongelea mambo mengine.

Kama kawaida, tumeongelea pia habari za kuishi kwake Tanganyika (hatimaye Tanzania). Nilimwuliza zaidi kuhusu suala hilo, nikimkumbushia kuwa nilishamwambia napangia kwenda Iringa kufanya utafiti. Hii mada nayo tumeiongelea kwa muda mrefu, na amenipa dokezo zaidi kuhusu yale ninayotaka kutafiti.

Amenielezea kuhusu waandishi, tukaongelea nadharia ya Hemingway juu ya uwindaji wa kweli, na nadharia ya ukweli katika uandishi. Nilimwambia kuwa kadiri siku zinavyopita, na kadiri ninavyozidi kusoma maandishi ya Hemingway, napata picha kuwa itabidi nisome maandishi yake yote, kwani mara kwa mara kuna vipengele vinavyojitokeza tena na tena katika vitabu vmbali mbali.

Nilimwambia kuwa moja ya ndoto zangu ni kuandika kitabu "Hemingway's Africa," naye akasema itakuwa vizuri, hasa kwa vile mimi ni mw-Afrika. Nami nakubaliana naye. Amenisikiliza tangu tulipofahamiana mara ya kwanza, jinsi ninavyomwenzi Hemingway kwa jinsi alivyoandika kuhusu nchi yangu na Afrika Mashariki kwa ujumla, juu wa mazingira ya nchi, watu, na wanyama, na jinsi alivyoipenda sehemu hii ya dunia, akafanya kila juhudi ya kuwashawishi wanafamilia waende kule. Nilishamwambia Mzee Hemingway jinsi ninavyomshukuru Hemingway na jinsi nilivyo na msimamo tofauti katika masuala mengi yanayomhusu Hemingway, tofauti na watafiti wengine.

Ninafurahi kwa jinsi Mzee Patrick Hemingway anavyonisaidia kufahamu zaidi mambo ya Hemingway. Ni bahati ya pekee kwangu, na kwa yeyote yule, kwamba tuna fursa ya kuongea na huyu Mzee, ambaye ndiye motto pekee wa Hemingway aliye bado hai. Ana umri wa miaka 87 sasa. Kama kawaida yake, Mzee Hemingway amenieleza mambo ya kusisimua kuhusu watafiti wa kigeni waliofika Afrika na kukaa muda mfupi tu, wakarudi wakijifanya ni wataalam wa mambo ya Afrika.

Ili kugusia kila mada tuliyoongelea, itabidi niandike insha ndefu, na hapa sio mahali pake. Kumbukumbu zangu za maongezi ya leo nitaziandika mahali pengine, panapo majaliwa.

2 comments:

Unknown said...

Hongera sana bwana mbele. Naamini kabisa ndoto yako itafanikiwa ya kuandika "Hemingway's Africa,". Kila la heri

Mbele said...

Shukrani kwa ujumbe wako, ndugu Abraham Thomas. Sijakusikia kwa miaka kadhaa, nikajiuliza kulikoni. Kila la heri.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...