Friday, July 25, 2014

Kitabu Kimefika Salama Dar es Salaam

Leo nimefurahi kumsikia mwanablogu Bwaya akielezea kuwa amepata kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, ambacho nilimpelekea Dar es Salaam, tarehe 14 Julai. Ameandika taarifa hii kwenye ukurasa wake wa Facebook na pia katika blogu yake, na sehemu zote mbili ameambatanisha picha inayoonekana hapa kushoto. Ni picha ya kitabu na pia bahasha ambayo nilitumia kitabu hiki.

Nimefurahi kwamba kitabu kimefika salama, kwani jana nilianza kuwa na wasi wasi kuwa labda kimepotelea njiani.

Namshukuru Ndugu Bwaya kwa kutoa taarifa hima alipopata, kama alivyoahidi. Kwa taarifa zaidi, pitia blogu ya Jielewe

3 comments:

Christian Bwaya said...

Profesa Mbele,

Kwa mara nyingine nakushukuru sana kwa jitihada unazofanya kuhakikisha kuwa vijana wa nchi yako angalau tunapunguza imani za kishirikina na mizimu na badala yake, angalau tuanze kuthamini maarifa na uelewa.

Nimejifunza jambo zito na muhimu kwako: Kwamba unapojua, usifurahi kwamba umejua peke yako. Hakikisha na wengine wanapata mwangaza wa ulichokijua. Kwa jinsi hiyo jamii nzima, hatua kwa hatua, hunufaika. Naahidi kuutumia vyema mfano huo nilioupata kwako. Nakushukuru sana.

Mbele said...

Ndugu Bwaya, shukrani kwa ujumbe wako. Umeelezea vizuri kipengele muhimu cha falsafa yangu kuhusu kujua na elimu.

Tangu zamani, imani yangu ni kuwa njia bora ya kuthibitisha kama unajua suala fulani ni kumweleza mwingine au kuwaeleza wengine. Hiyo ni fursa ya kuthibitisha kama unajua hilo suala, au ni kiasi gani unajua. Mapungufu katika ufahamu wako yatajidhihirisha kwa namna hiyo, na hii ni chachu ya kukufanya ujielimishe siku zote za maisha yako.

Nilipokuwa nafundisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, niliwahi kudosolewa na watu kadhaa kwamba tunapokuwa mahali kama klabu ya UDASA, ninawafaidia watu kwa vile ni muongeaji mno. Kwa maneno mengine, nikisoma kitu, nawamwagia wengine bila breki. Niliambiwa kuwa watu waliweza kupata mada au hoja ya kuandika kwenye "conference paper" namna hiyo. Nilikuwa nashauriwa nisiwafaidie watu kwa namna hiyo.

Msimamo wangu daima umekuwa tofauti. Mbali na hiyo hoja niliyotoa hapa juu, ya kujipima ufahamu wangu, mimi najua kuwa akili yangu ni kama chemchemi. Haipungukiwi kwa kumchotea mtu, hasa ukizingatia kuwa mimi najielimisha muda wote. Leo nitamwambia mtu hili na lile, na ndio ufahamu wangu, lakini nikitoka hapo naendelea kusoma na hivi kufahamu mengi zaidi. Sipungukiwi kwa kummegea mtu yote ninayoyajua leo.

Kwa hivi, sioni maana ya kuwa na uchoyo katika elimu.

NN Mhango said...

Laiti ningekuwa na muda ningetafuta Matengo Folktales na kujiongezea maarifa. Nakutakieni mafanikio katika maonesho haya mwanana.