Leo ni siku ya kumbukumbu ya kuzaliwa Ernest Hemingway. Alizaliwa tarehe 21 Julai, 1899, Oak Park, kitongoji cha Chicago.
Hemingway ni mwandishi maarufu pengine kuliko wote walioandika ki-Ingereza katika karne iliyopita, na bado yuko juu sana. Anasifika kwa mengi, ikiwemo kuasisi mtindo wa uandishi ambao wengi wameufuata, hasa msisitizo katika uandishi wa sentensi fupi.
Haiwezekani kwa mtu yeyote kukumbuka tarehe za kuzaliwa kwa kila mtu maarufu. Imekuwa bahati tu kuwa nimekumbuka kuwa leo, tarehe 21 Julai, ndio tarehe ya kuzaliwa Hemingway.
Hemingway ni mwandishi ambaye maandishi yake nayasoma sana, pia maandishi ya wengine kumhusu yeye, na tahakiki mbali mbali za maandishi yake.
Kitu kimoja kinachonivutia sana ni kauli mbali mbali za Hemingway kuhusu masuala kadha wa kadha ya maisha, uandishi, falsafa, na kadhalika. Ukizingatia kwamba Hemingway alipenda sana kunywa, hebu fikiria, kwa mfano usemi wake huu: "I drink to make other people more interesting."
Alisema mengi kuhusu hali halisi ya uandishi, kwa mfano: "There is nothing to writing. All you do is sit down at a typewriter and bleed." Mengine machache nimeyanukuu katika makala yangu, "Writing as hard Labour."
Aliipenda sana Afrika, na alisema mengi kuhusu hilo, ambayo nimeyasoma hapa na pale, kwa mfano katika kitabu chake cha The Green Hills of Africa. Jana, katika kupitia kitabu cha Papa Hemingway, kilichoandikwa na rafiki yake A.E. Hotchner, nimeona kauli ya Hemingway ambayo sikuwa nimeiona kabla. Hemingway alikuwa katika mipango ya kwenda tena Afrika, na Hotchner, ambaye alikuwa New York, alimwuliza kama angepitia New York. Hemingway alijibu:
Sure, I'll see you before we leave, either in New York or here if we by-pass New York. Going back to Africa after all this time, there is the excitement of a first adventure. I love Africa and I feel it's another home, and any time a man can feel that, not counting where he's born, is where he's meant to be.
Wasomaji wa blogu yangu hii na ile ya ki-Ingereza, watakuwa wanafahamu kuwa mimi ni msomaji na mfuatiliaji mkubwa wa Hemingway. Nina ndoto ya kuandika kitabu kumhusu Hemingway, kitakachohusu uhusiano wake na Afrika.
Juzi hapo, tarehe 15 mwezi huu, nilipoongea na Mzee Patrick Hemingway, ambaye anafahamu ninavyomheshimu Hemingway kwa uandishi na msimamo wake kuhusu Afrika, nilimwambia kuwa ninapangia, hatimaye, kuandika kitabu, ambacho nitakiita "Hemingway's Africa." Mzee Hemingway aliafiki, akisema kuwa itakuwa bora kwa vile mimi ni mw-Afrika.
Ningeweza kuandika sana kuhusu mada hii, lakini leo nilitaka tu kujikumbusha kuwa tarehe kama hii, yaani Julai 21, ndio tarehe aliyozaliwa Hemingway.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault
Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...
-
Leo ni kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa kwangu, ambayo ni tarehe 17 Agosti, 1951. Familia yangu, ndugu, na marafiki wamejumuika nami kushereh...
-
Leo napenda kukitambulisha kwako mdau kitabu muhimu cha ki-Swahili, Tenzi Tatu za Kale . Nilinunua nakala yangu miaka kadhaa iliyopita katik...
-
Kutafsiri kazi ya fasihi ni kazi ngumu ya kuchemsha bongo. Inahitaji ufahamu wa hali ya juu wa lugha husika, na pia hisia makini za kifasih...
No comments:
Post a Comment