Wednesday, January 18, 2017

Vitabu Nilivyojipatia Leo

Leo, baada ya wiki nyingi kidogo, nimeona nirejee tena kwenye mada ambayo nimekuwa nikiiandikia tena na tena katika blogu hii. Ni juu ya vitabu ninavyojipatia, iwe ni kwa kununua, au kwa namna nyingine.

Leo asubuhi, kama kawaida, nilienda chuoni St. Olaf kufundisha. Nilipoingia katika jengo la maktaba, ambamo pia ni makao ya idara yangu ya ki-Ingereza, nilipita kwenye meza ambapo huwekwa vitabu na makabrasha kwa ajili ya yeyote anayehitaji. Niliona meza imejaa vitabu kuliko siku nyingine yoyote iliyopita, nikaamua kuviangalia.

Niliona kuwa vyote vilikuwa vitabu vya taaluma, hasa masuala ya wanawake na jinsia. Niliamua kujichukulia vitatu, baada ya kuangalia ndani na kuona maelezo ya vitabu hivi. Kitabu kimojawapo ni Sex & Power, kilichotungwa na Susan Estrich. Niliona maelezo kuwa mwandishi alikuwa profesa wa sheria katika Chuo Kikuu cha Harvard na baadaye profesa wa sheria katika Chuo Kikuu cha California ya Kusini. Ameandika vitabu kadhaa na makala mbali mbali. Alikuwa mwanamke wa kwanza kuwa rais wa Harvard Law Review. Huenda msomaji wa taarifa hii utakumbuka kuwa hiki ni cheo ambacho Barack Obama aliwahi kushika. Kutokana na mada ya kitabu, na orodha ya sura zake niliona kuwa kitabu hiki kitanielimisha sana kuhusu nafasi ya wanawake katika jamii.

Kitabu cha pili kilichonivutia kwa namna ya pekee ni Globalization: The Making of World Society, ambacho kimetungwa na Frank J. Lechner. Kama tunavyofahamu, mada ya utandawazi inavuma sana miongoni mwa wanataaluma, wanasiasa, na jamii kwa ujumla. Hata hivi, mitazamo kuhusu nini maana ya utandawazi, chimbuko lake, faida na hasara zake, ni masuala ambayo yanajadiliwa na yamegubikwa na utata.

Mimi mwenyewe, kwa miaka kadhaa, nimetafakari suala la utandawazi, nikilihusisha na tofauti za tamaduni. Nimewahi hata kuendesha warsha kadhaa, nchini Tanzania, katika miji ya Arusha, Dar es Salaam, na Tanga. Kwa hivi, nilipokiona kitabu cha Globalization: The Making of World Society, nilikuwa na hamu ya kukisoma. Hiki kitaongeza idadi ya vitabu vyangu kuhusu utandawazi.

Kitabu cha tatu, Behind the Veil in Arabia: Women in Oman, kilichoandikwa na Unni Wikan, kilinivutia pengine zaidi ya hivi vingine. Nilipoona jina la kitabu hiki, nilikumbuka mara majina ya vitabu vingine, kama vile Beyond the Veil, cha Fatima Mernissi wa Morocco. Suala la wanawake katika nchi za ki-Arabu limeshika nafasi ya pekee kichwani mwangu kutokana na kozi niliyoanzisha na ninaifundisha, "Muslim Women Writers."

Simaanishi, na mtu asidhani, kwamba wa-Arabu wote ni wa-Islam, bali kuna suala la jinsi utamaduni unavyoingiliana na dini kiasi kwamba pamoja na tofauti za dini, kuna mambo kama mila, desturi, na lugha, ambayo yanawaungamisha wa-Arabu.

Katika kufundisha kozi ya "Muslim Women Writers" imedhihirika kuwa vazi kama hijab ni suala la utamaduni zaidi kuliko dini. Qur'an inasema wanawake wajisitiri na wainamishe macho, lakini haisemi wavae nini. Hili ni suala la kila utamaduni, na ndio maana mavazi ya wanawake wa ki-Islam katika tamaduni mbali mbali yanahitilafiana.

Maktaba yangu imetajirika leo kwa kuongezewa vitabu hivi muhimu. Ni raha iliyoje kujipatia hazina kubwa namna hii bila gharama yoyote kwa upande wangu.

3 comments:

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Ndugu Mbele hongera kwa kuendeleza utamaduni wa kuthamini vitabu. Hata mie huwa na tabia hiyo hasa nipitapo kwenye meza zenye vitabu ambavyo yoyote anaweza kuchukua. Hakuna kitu cha thamani kama kupata kitabu tena cha kitaaluma kikiwe hakina price tag.
Endelea kukusanya vitabu kwani scripta est manent yaani lililoandikwa ni la milele. Afrika sasa inahangaishwa na kuhujumiwa kwa sababu ya vitabu vya dini vilivyoletwa kueneza mila za hovyo za wengine kama ulivyomalizia kuwa Quran haisemi wanawake wavae nini zaidi ya kujihifadhi. Kuna aya mbili nilizipata jana wakati nikifanya utafiti wa mswaada wangu juu ya Ugaidi na namna Marekani na mataifa ya Ulaya na mengine yenye nguvu yanavyoitumia kuikalia Afrika kijeshi ili kuendelea kuinyonya. Haya hizi ni Qurans (42:7) “Hivyo, tumedhihirisha Korani kwako, ili muweze kuonya mji mkuu na waishio karibu yake...”
Na nyingine ni Quran (14:4) “ Hatkutuma mtume yeyote ila kwa lugha ya watu wake ili kufanya mambo kuwa rahisi. Allah humpotosha amtakaye na humuongoza yeyote amtakaye. Tafsiri ni yangu. Pamoja na haya kuwa wazi, wengi hawajui kiasi cha kupwakia kila upuuzi kwa sababu ni wavivu wa kusoma.

Mbele said...

Shukrani kwa ujumbe, ndugu Mhango. Mara nyingi ninajikuta nikiwa na masikitiko kwamba sitaweza kuvisoma vitabu vyangu vyote vilivyoko Tanzania na hapa Marekani. Ni vingi mno, na bado ninapenda kujipatia vitabu sawa na nilivyopenda nilipokuwa kijana mdogo.

Dini nyemelezi, kama unavyoziita, zimechanganywa na ukasuku katika bara letu la Afrika, na matokeo yake ni majanga. Waumini wengi wamezipeleka akili zao likizoni.

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Ndugu Mbele umenikumbusha nami vitabu nilivyoacha nyumbani. Kwa wanaonijua, kila aliyetembelea kwetu alikuwa akiuliza huyu mtu anafanya nini na vitabu vyote ni vya nini? Kwa familia changa ya mtoto mmoja kipindi kile kuwa na sebule iliyoshiba shelf ya vitabu ukuta hadi ukuta chini hadi juu na kushoto kulia halikuwa jambo la kawaida. Huo ndiyo utajiri nilio kuwa nao na wakati wa kuondoka hakuna kilichoniumiza kama kuacha vitabu vyangu ambavyo vingine havichapishwi tena. Ilikuwa sawa na kuwaacha marafiki zangu wapendwa.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...