Tuesday, December 17, 2019

Kofia ya CCM Nchini China

Naleta picha ya ujumbe wa CCM kwenye kikao na wenyeji wao mjini Shanghai, China, mwaka 2018. Hapo mezani upande wa kushoto kuna kofia ya CCM. Yawezekana walikwenda ziarani na magwanda yao na vikofia. Je, kuna sababu gani mimi kuandika ujumbe kuhusu kofia? Sina jambo la maana zaidi la kuongelea? Kwa nini nisiongelee madhumuni ya ziara na mafanikio yake?

Ninaandika ujumbe huu kama mtafiti, mwandishi, na mtoa ushauri juu ya masuala ya utamaduni na utandawazi. Nimekuwa nikifanya shughuli hizo hapa Marekani na Tanzania pia, ambako nimeendesha warsha mara kadhaa kuanzia mwaka 2008 katika miji ya Arusha, Tanga, na Dar es Salaam.

Ninajaribu kuwaelewesha watu kuwa tofauti za tamaduni zina athari kubwa, hasa katika dunia ya utandawazi wa leo. Tunapokutana na watu wa tamaduni tofauti na wetu, tuwe makini. Tunaweza tukaelewana vibaya, au tunaweza tusielewane. Ni muhimu tujielimishe kuhusu tofauti hizo kabla hayajatupata hayo.

Kofia ya CCM ni sehemu ya vazi rasmi la wana CCM. Ni utambulisho wao. Hata mimi ambaye sina chama ninawatambua kwa mavazi yao. Vyama vingine navyo vina mavazi yao. Kwa hapa nchini Tanzania, hakuna utata juu ya hayo mavazi. Lakini je, hali ni hiyo hiyo nje ya Tanzania kwenye tamaduni tofauti?

Nchini China, kofia ya kijani ni mkosi. Mwanaume kuvaa kofia ya kijani maana yake anatangaza kwamba mke wake ni mzinzi.

Kuhusu asili ya tafsiri hii ya waChina kuhusu kofia ya kijani, maelezo yanatofautiana. Baadhi ya maelezo ni kwamba zamani za kale, ndugu wa malaya walilazimishwa kuvaa kofia ya kijani wabebe aibu. Maelezo mengine ni kwamba zamani za kale, wahudumu katika madanguro walikuwa wanavaa kofia za kijani. Lakini kama nilivyogusia, maelezo yanahitilafiana. Ila jambo ambalo halina utata ni kwamba katika utamaduni wa China, kofia ya kijani ni mkosi kwani inatangaza habari ya uzinifu wa mke.

Sasa fikiria hiyo ziara ya ujumbe wa CCM China. Wafikirie wako sehemu mbali mbali kama wageni rasmi, wamevalia kofia za kijani. Bila shaka, wenyeji wao walifanya ukarimu na heshima kama ilivyo desturi. Lakini bila shaka, makada hao wa CCM watakuwa wameacha gumzo na taswira ambayo hawakutegemea.

Katika warsha ambazo nimeandaa Tanzania tangu mwaka 2008, waTanzania wachache sana wamekuwa wakihudhuria. Mbali ya warsha, nimekuwa nikielezea katika blogu zangu masuala ya athari za tofauti za tamaduni katika dunia ya utandawazi wa leo. Nimeandika hata kitabu, kiitwacho Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, ambacho kinapatikana Tanzania pia, kutoka katika maduka ya Kimahama (Arusha), Soma Book Cafe (Dar es salaam), na A Novel Idea (Arusha na Dar es Salaam).

Pamoja na kujaribu njia zote hizo, nimeona kuwa labda, kwa kuandika ujumbe huu kuhusu kofia ya CCM nchini China, waTanzania watanielewa vizuri na watachukua hatua stahiki katika masuala yote husikka, iwe ni mahusiano binafsi, biashara za kimataifa, utalii, diplomasia na kadhalika.

Thursday, December 5, 2019

Maongezi Kuhusu Fasihi Simulizi ya Africa

Jana jioni, kwa mwaliko wa chama cha wanafunzi kiitwacho Karibu, nilitoa mhadhara hapa chuoni St. Olaf kuhusu fasihi simulizi ya Afrika. Tuna wanafunzi wachache kutoka Afrika, lakini wanajitahidi kuitangaza Afrika kwa namna mbali mbali, kama vile mihadhara, filamu, ngoma, muziki, michezo ya kuigiza, na maonesho ya mavazi.

Mara kwa mara wananialika kuelezea utamaduni wa Afrika, hasa unavyojitokeza katika fasihi simulizi. Nami hupenda kufanya hivyo. Ninauenzi mchango wa Afrika duniani. Afrika ni chimbuko la binadamu. Ni chimbuko la tekinolojia, sayansi, lugha, fasihi, falsafa, na kadhalika.

Hiyo jana nilelezea hayo, nikaleta methali kadhaa kuthibitisha uzito wa falsafa ya wahenga wetu kuhusu masuala ya maisha na maadili. Tulitafakari methali hizo, na mwishoni nilisimulia hadithi iitwayo "The Donkey Who Sinned," iliyomo katika kitabu cha Harold C. Courlander kiitwacho A Treasury of African Folklore. Nayo tuliitafakari, kwa jinsi inavyoonyesha athari za ubabe kwa wale wasio na nguvu. Katika hadithi hiyo, wenye mabavu wanaogopwa hata pale wanapokosea, na asiye na nguvu anadhulumiwa.

Saturday, November 30, 2019

Wadau wa Utalii wa Kielimu Tumekutana

Tarehe 2 Novemba nilikutana na mama Georgina, ambaye anatoka Ghana na ni mmiliki wa kampuni iitwayo African Travel Seminars. Anapeleka wasafiri kwenda nchi za Afrika, kuanzia kaskazini, hadi kusini, mashariki hadi magharibi, na Tanzania imo. Mbali ya kuwaonesha vivutio vya utalii, anawaelimisha kuhusu maisha na tamaduni za waAfrika.

Niliifahamu kuhusu kampuni yake kuanzia miaka ya tisini na kitu, nikaona jinsi shughuli zake zinavyofanana na zangu, ambazo zimeelezwa katika tovuti ya Africonexion. Hivi karibuni nilianza kuwasiliana na huyu mama, na tukapanga kukutana.

Kabla hatujakutana, mama huyu alisoma kitabu changu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Ameamua awe anawapa wageni anaowapelea Afrika. Yeye nami tunafahamu kuwa hii itawawezesha wageni kuelewa mwenendo na tabia za waAfrika na pia kujielewa namna wao wenyewe wanavyoeleweka kwa mtazamo wa waAfrika.

Tumejithibitishia kuwa malengo yetu yanafanana. Tunapenda kuendeleza elimu kuhusu Afrika kwa waMarekani na tunapenda kujenga maelewano baina ya waMarekani na waAfrika. Yeye nami tuna uzoefu wa kuongelea masala haya hapa Marekani, kwa wanafunzi na walimu, watu wanaoenda Afrika kwa shughuli za kujitolea, watalii, nakadhalika.

Thursday, November 14, 2019

Kijana Msomali Amekipenda Kitabu Hiki

Jana, nilikuwa posta hapa chuoni nikipata huduma. Ghafla nikasikia kwa nyuma ninaitwa, "Professor Mbele!" Nilipinduka nikamwona kijana mmoja, mwanafunzi wetu mSomali ananisogea. Aliniambia amesoma kitabu changu, akimaanisha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences.

Nilifurahi, ila sikujua nimwambie nini, ila aliongezea kuwa alitamani kipatikane kama "audio book" ili mama yake aweze kusikiliza. Niliguswa sana, kwa sababu ninaelewa hali ya waSomali hapa Minnesota na Marekani kwa ujumla.

Wako wengi sana, wakimbizi au wahamiaji kutoka nchini kwao. Jimbo hili la Minnesota lina idadi kubwa ya waSomali kuliko sehemu nyingine duniani ukiachilia mbali Somalia yenyewe.

Ninafahamu pia kuwa waSomali hawakuwa na jadi ya maandishi. Utamaduni wao ni wa masilimuzi. Walipata mwafaka wa namna ya kuandika lugha yao mwaka 1972. Watu wazima wengi hawajui kuandika na kusoma, na wazee ndio kabisa.

Wote hao wako hapa Marekani, ambapo utamaduni ni wa maandishi. Ninafahamu changamoto zinazowakabili, kwani nina uzoefu katika masuala yao, ikiwemo fasihi simulizi na elimu. Kijana huyu alivyoniambia kuhusu mama yake, niliguswa sana. Nimeshampelekea ujumbe rafiki yangu mSomali kumwelezea suala hilo. Huyu tulishaongelea kutafsiri kitabu changu kwa kiSomali. Nimemwambia kuwa kutokana na kauli ya huyu kijana ya kutaka mama yake asome kitabu hiki, inabidi tukamilishe tafsiri halafu irekodiwe kama "audio book." Itachukua muda, lakini hii si hoja.

Saturday, June 15, 2019

Wenzetu Wanasoma Vitabu

Nilikwenda Mall of America  Juni tarehe 8, nikapitia kwenye duka la Half Price Books mjini Apple Valley, kama ilivyo kawaida yangu.

Nilianzia sehemu ambapo vinawekwa vitabu vya Ernest Hemingway, halafu nikaenda sehemu yenye vitabu vilivyopunguzwa bei zaidi ("clearance."). Halo niliona hali inayoonekana pichani, watu wakiwa wanapekua na kuangalia vitabu, na wengine wakisubiri fursa hiyo.

Hao wenzetu wamelelewa hivyo. Wanaona vitabu ni muhimu maishani mwao. Dunia ya leo na kesho ni ya maarifa na ujuzi. Itawaendea vizuri wanaowekeza katika elimu. Utamaduni wa kusoma vitabu uwe kipaumbele cha wote.


Wednesday, May 29, 2019

Nimekutana na Mdau wa Kitabu Changu

Tarehe 19 Mei nilikwenda kukutana na mama Luanne Kallungi Skrenes katika mahafali ya 150 ya Luther Seminary. Mama huyu tumefahamiana kwa miaka kadhaa katika mtandao wa Facebook. Yeye ni mratibu wa programu ya kanisa la kiLuteri eneo la Michigan inayoendeleza mahusiano baina ya waLuteri wa Marekani na wenzao wa Tanzania.

Ni mpenzi wa kitabu changu, Africans and Americans:Embracing Cultural Differences, ambacho anakipendekeza kwa waMarekani wanaoenda Tanzania katika programu hiyo. . Yeye ni mratibu wa programu ya kupeleka waLuteri ya kupeleks watu Tanzania. Hata mwaka huu nilipoandaa warsha kuhusu "Culture and Globalization," aliwaandikia waTanzania anaofahamiana nao kuwahimiza wahudhurie. Kwa hayo yote, mama huyu amekuwa otu muhimu kwangu.

Tulifurahi kuonana. Nilifurahi kumwona mume wake, Askofu Thomas a Skrenes. Wote ni waongeaji wachangamfu. Niliwaambia kuwa ninaandika kitabu cha mwendelezo wa hicho cha kwanza, yaani "sequel," kwa kiIngereza. Mama aliniuliza kitaitwaje, nami nikamjibu "Chickens in the Bus." Tulicheka. Lakini hili ndilo jina la kitabu ninachoandaa.

Kati ya mambo ninayoyafurahia sana kama mwandishi ni kukutana na wasomaji na kusikia maoni yao kuhusu vitabu vyangu. Ni baraka kubwa kuwa na watu wenye moyo huu wa kunipa mrejesho, na ninawashukuru daima.

Sunday, May 12, 2019

Furaha ya Kujipatia Kitabu

Tarehe 26 hadi 28 Aprili, palifanyika maonesho ya vitabu Blaine, Minnesota, kama nilivyoelezea katika blogu hii. Nilishiriki, na kati ya watu waliokuja ni huyu binti ninayeonekana naye pichani.

Alifika kwenye maonesho tarehe 27, ila mimi sikuwepo. Tarehe 28 alifika tena na hapo ndipo nilipoambiwa kuwa huyu binti alishakuja akanunua kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Aliponiona alifurahi, akaniambia kuwa alitaka nisaini kitabu, lakini alikuwa amekiacha nyumbani. Nilisaini kitabu kingine nikampa. Hii ndio habari nyuma ya tabasamu la binti pichani.

Ninafurahi kuona vijana wenye mwamko wa kusoma vitabu. Huyu binti aliniambia kuwa anatoka Sudani ya Kusini. Alivutiwa na kitabı kwa sababu anaona utamaduni wa wazazi wake na yeye anakulia hapa Marekani. Hivi karibuni nimemwambia nitafurahi kusikia maoni yake kuhusu kitabu hiki.

Tuesday, April 30, 2019

Maonesho ya Vitabu Blaine, Minnesota

Aprili 26-28, nilishiriki maonesho ya vitabu yaliyoandaliwa na Bukola Oriola kusherehekea miaka kumi tangu kuchapishwa kwa kitabu chake cha kwanza, Imprisoned: The Travails of a Trafficked Victim. Kwa kuwa nimeshiriki maonesho mengi ya vitabu, naweza kusema kwamba maonesho haya aliyoandaa Bukola yalikuwa ya pekoe.

Kwa uzoefu wangu, nimeona maonesho yakidumu siku moja, lakini haya ya Bukola yalidumu situ tutu. Kwa hovyo, yalitoa fursa kwa yeyote kuhudhuria siku mojawapo, ambaye hakuweza kuhudhuria siku nyingine.

Ingawa Bukola aliandaa maonesho haya kusherehekea miaka kumiss ya kitabu shake, aliwaalika waandishi wengine kushiriki. Nami niliwasilisha  vitabu vyqngu. Hakuhitaji tuwepo muda wote wa maonesho, bali wakati maalum uliopangwa kwa mwandishi moja moja kuonekana jukwaani kwa saa moja.

Nilitumia muda mrefu kiasi kwenye maonesho, tarehe 26 na 28. Nilionana na waandishi kadhaa, wakiwemo ninaowafahamu, kama vile Rita Apaloo, mwandishi wa African Women Connect: How I started and grew a networking group of African immigrant women for friendship, business, and community.

Nilikutana na kuongea na watu wengi, nikaongea nao na kubadilishana mawazo na uzoefu. Kila maonesho ya vitabu ambayo nimehudhuria yamekuwa ya manufaa sana.  Haya maonesho ya Bukola mayo yalikuwa hovyo, na anastahili kushukuriwa kea juhudi zake za kuhamasisha usomaji na kuwawezesha waandishi.



Friday, April 26, 2019

Mhadhara Wangu Yankton, South Dakota

Tarehe 19 Aprili, nilienda Yankton, jimbo la Dakota Kusini, kufuatia mwaliko kutoka kwa Michael Schumacher, mratibu wa A.M.E. Allen Church. Alinitafuta baada ya kusoma taarifa juu ya mhadhara niliokuwa nimetoa mjini Red Wing, Minnesota, kuhusu jadi ya hadithi simulizi katika Afrika I

Katika kunitambulisha kwa watu waliohudhuria, ndugu Schumacher aliwaelezea jinsi kitabu changu cha Matengo Folktales kilivyokuwa kimetajwa katika programu ya television ya Jeopardy  Hiyo ni programu maarufu hapa Marekani.
Mhadhara wangu ulihusu chimbuko na kukua kwa utamaduni na tofauti za tamaduni. Niliongelea Afrika kama chimbuko la binadamu, lugha na masimulizi, kisha nikaelea jinsi kutawanyika kwa wanadamu sehemu mbali mbali za kulivyoleta tamaduni na lugha mbali mbali.

Niltumia kitabu changu, Africans and Americans: Embracing Cultural Diiferences kuainisha uhlisia na athari za kuwepo kwa tamaduni tofauti. Katika kuelezea kuzuka na kustawi kwa matumizi mbali mbali ya masimulizi nilinukuu na kuelezea methali kadhaa na halafu nikasimulia hadithi ya "The Monster in the Rice Field" iliyomo katika kitabu changu cha Matengo Folktales.

Wahudhuriaji walichangia mifano ya tofauti za tamaduni ambazo wamewahi kukumbana nazo. Mmoja alisema kwamba ni mwalimu na kwamba ana wanafunzi anaowapeleka Tanzania hivi karibuni. Nilifurahi kusikia hivyo.

Tulipomaliza kikao, watu walinunua vitabu vyangu nilivyoleta. Huyu mwalimu niliyemtaja alisema atavitumia vitabu hivi kama mwongozo kwa wanafunzi katika safari yao. Ninafurahi kwamba vitabu vyangu sasa viko katika maktaba ya AME Allen Church. Hili ni jambo kubwa, nikizingatia historia ya jengo  hili ambalo lilijengwa mwaka 1885 na watu weusi baada ya kukombolewa utumwani.

Saturday, March 9, 2019

Kitabu Kinatumika Chuo Kikuu China

Tarehe 7 Februari, wakati namalizia maandalizi ya warsha kuhusu Culture and Globalization, niliyofanya Dar es Salaam, nilipata taarifa ya kufurahisha kutoka kwa kijana mTanzania asomaye China. Kijana huyu, Seleman Pharles Mabala, aliniambia kuwa siku moja profesa wao mChina aliwaambia wasome kitabu changu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differenceskatika kozi ya "Cultural Differences and Cross-cultural Communication." Chuo hicho kiitwacho University of Electronic Science and Technology, kiko katika mji wa Chengdu, katika jimbo la Sichuan.
 Aliniambia kuwa alifurahi sana kumsikia profesa akisema kuwa kitabu kimeandikwa na mTanzania. Alipiga picha kama kumbukumbu akawapelekea marafiki nyumbani. Kijana aliendelea kuniambia: "Nakupa hongera sana na mimi hii kwa njia moja ama nyingine imenitia nguvu ya kuendelea kusoma kwa bidii nifikie angalau nusu yako!"

Ninafurahi kuwa nimeweza kumtia kijana huyu hamasa ya kusoma kwa bidii. Kwangu kama mwalimu, haya ni mafanikio mazuri. Jambo mojawapo lililotamkwa katika "Azimio la Arusha" kuhusu mapinduzi yaliyokusudiwa Tanzania ni kwamba kazi iwe jambo la kujivunia. Nami najivunia kazi yangu.

Vitabu vyangu kutumiwa katika vyuo vikuu si jambo geni kwangu. Vinatumiwa katika vyuo vya Marekani mara kwa mara. Lakini hii ni mara yangu ya kwanza kufahamu kuwa kitabu changu kinatumika China. Nimefurahi.


Ninamshukuru Seleman kwa kuniletea taarifa hii na kuniruhusu kuichapisha.

Thursday, February 21, 2019

Tumefanya Warsha ya Culture and Globalization

Tarehe 9 Februari 2019, niliendesha warsha kuhusu "Culture and Globalization." Tulifanyia Lion Hotel, Sinza, Dar es Saalam. Washiriki tulikuwa wachache, lakini tuliongelea na kueleweshana mambo mengi. Tulianza kwa kujitambulisha, kila mtu na shughuli zake. Kisha nilitoa maelezo kuhusu dhana ya "globalization," nikifuatilia historia na aina za "globalization." Halafu nilielezea jinsi tofauti za tamaduni zinavyohusika katika "globalization," na athari zake hasa katika hizi zama zetu na zijazo. Baada ya maelezo yangu, washiriki wa warsha tulijumuika na kutoa mifano ya athari hizo. Washiriki wa warsha walipata fursa ya kununua nakala za Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, ambacho ni msingi mojawapo wa mada ya warsha. Kitabu hiki kinapatikana katika duka la vitabu la A Novel Idea, lililopo Slipway, Msasani, na pia duka la Kimahamana Literature Center, Arusha.





Saturday, January 19, 2019

Kitabu Changu Kutafsiriwa kwa kiSomali

Mara moja moja, katika miaka kadhaa iliyopita, nimekuwa nikiwazia kufanya mpango wa kutafsiriwa kitabu changu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, kwa kiSomali. Niliwazia lugha hiyo kwa kuwafikiria waSomali waishio Marekani. Hapa kuna waSomali wengi kuliko sehemu yoyote duniani ukiachilia mbali Somalia yenyewe. Jimbo hili la Minnesota ninapoishi linaongoza kwa kuwa na waSomali wengi.

Nimekuwa na mahusiano ya miaka mingi na waSomali wa Minnesota, hasa katika miji ya Faribault na Minneapolis. Nimehusika katika kuwashauri kuhusu maisha ya hapa Marekani, mifano ikiwa ni mihadhara yangu Mankato na Faribault.

WaSomali ambao wamesoma kitabu changu wanakipenda sana na wananikumbusha tunapokutana. Mmoja wao ni rafiki yangu Mohamed Dini. Huyu ndiye tumekubaliana akitafsiri kitabu hicho. Yeye ni mmoja wa waSomali wachache sana wanaotambulika katika fani hiyo hapa Minnesota. Kazi hiyo itaanza mwezi huu.

Ni faraja kubwa kwangu kwamba tafsiri hii itakapochapishwa itapunguza kwa kiasi kikubwa matatizo yanayowakabili waSomali Marekani, ambayo ni mara dufu kuliko yanayowakabili waAfrika wengine wengi. Tofauti na waAfrika wengi, waSomali wengi hawajui kiIngereza ambayo ndio lugha ya Marekani. Vile vile, waSomali ni waIslam, dini ambayo ni ya wachache hapa Marekani, na sehemu nyingi hakuna yale ambayo waIslam wanahitaji kwa mujibu wa dini yao. Kuna juhudi zinafanyika, lakini bado hazijatosheleza.

Ninangojea kwa hamu maendeleo ya shughuli hii hadi ifikie lengo.

Saturday, January 12, 2019

Mwongozo wa "Song of Lawino"

Nimechapisha kijitabu ambacho ni mwongozo wa Song of Lawino. Wanafunzi na wasomaji wa fasihi ya Afrika, angalau wa enzi za ujana wangu, wanafahamu kwamba Song of Lawino ni utungo maarufu wa Okot p'Bitek wa Uganda. Mwongozo wangu unaitwa Notes on Okot p'Bitek's Song of Lawino.

Huu ni mwongozo wangu wa pili kuuchapishwa, baada ya Notes on Acebe's Things Fall Apart, mwongozo ambao umekuwa ukitumiwa na wanafunzi na waalimu wa fasihi sehemu mbali mbali duniani kama nilivyowahi kugusia katika blogu hii.

Kila mwongozo unaongelea kazi tajwa lakini pia unagusia kazi zingine za fasihi ili kupanua uwanja wa ufahamu juu ya fasihi. Kila mwongozo unaingiza pia vipengele vya nadharia ya fasihi vinavyohusika katika kazi inayojadiliwa.  Kwa hiyo, kwa kusoma mwongozo moja, mtu anajifunza au anapata fursa ya kutafakri mambo mengi.

Nina nia ya kuandika miongozo mingine ya kazi muhimu za fasihi ya Afrika. Unaweza kujipatia mwongozo huu mpya na vitabu vyangu vingine katika duka la mtandaoni

Friday, January 11, 2019

Wanachuo wa Gustavus Adolphus Wameenda Tanzania

Tarehe 7, nilikwenda kukutana na wanachuo wa Gustavus Adolphus College ambao walikuwa wanaondoka kwenda Tanzania katika programu ya masomo. Hii ni programu ambayo imekuwepo miaka mingi. Wanafunzi wengi zaidi wanasomea uuguzi, na wanakwenda Tanzania ili kuelewa suala la uuguzi linakuwaje katika utamaduni tofauti na wa Marekani.

Nimekuwa nikialikwa kila mara kuongea nao kuhusu masuala ya tofauti za tamaduni kutokana na kwamba wanasoma kitabu changu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, na tunapokutana wananiuliza maswali yatokanayo na niliyoandika au mengine. Maswali yalikuwa ya aina mbali mbali, yakiwemo kuhusu mtazamo wa waTanzania juu ya waMarekani na pia kuhusu hali ya kisiasa Tanzania.

Hapa kushoto ninaonekana na viongozi wa msafara, Profesa Barbara Zust na Mchungaji Todd Mattson. Profesa Zust ndiye mwaandaji wa kozi na kila mwaka anaweka kitabu changu kama muhimu kwa wanafunzi. Maelezo mafupi ya programu ya mwaka huu ni haya hapa.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...