Sunday, July 9, 2017

Wole Soyinka na Madikteta wa Afrika

Wole Soyinka ni mmoja wa waandishi bora kabisa kutoka Afrika. Ameandika tamthilia, riwaya, mashairi, insha, na wasifu wake. Pia ametafsiri riwaya ya ki-Yoruba ya D.O. Fagunwa. Tafsiri hiyo inaitwa Forest of a Thousand Daemons: A Hunter's Saga.

Pamoja na umahiri wake katika kubuni visa na katika kuimudu lugha ya ki-Ingereza, Soyinka anachota sana mbinu na vipengele vingine vya sanaa na masimulizi ya jadi, hasa ya wa-Yoruba, lakini pia ya mataifa mengine, akienda mbali hadi u-Griki ya kale. Umahiri wake kama mwandishi umetambuliwa kwa namna mbali mbali, ikiwemo tuzo ya Nobel katika fasihi, ambayo alitunukiwa mwaka 1986.

Katika kazi zake, anashughulikia masuala ya aina mbali mbali, kama vile siasa, itikadi, ukoloni, ukoloni mambo leo, utamaduni, na fasihi ya Afrika na kwingineko. Udikteta ni mada ambayo Soyinka ameishughulikia tangu zamani, sio tu katika maandishi na mahojiano, bali pia kama mwanaharakati. Tamthilia ya Kongi's Harvest ni mfano mzuri. Tamthilia hii tuliisoma nilipokuwa mwanafunzi katika idara ya "Literature," Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, 1973-76.

Wiki hii nimesoma A Play of Giants. Ni tamthilia ambayo inazama zaidi katika mada ya madikteta wa Afrika. Nilifahamu jambo hilo tangu zamani, kama nilivyoelezea siku chache zilizopita katika blogu hii. Soyinka anawaumbua madikteta hao. Anatumia kejeli kuelezea fikra na matendo yao, ulevi wa madaraka, uduni wa akili zao, na ukandamizaji wa haki za binadamu. Uduni wa akili zao unadhihirika kwa namna wanavyoongelea mambo yasiyo na maana, na kama wanaongelea mambo ya maana, hoja zao ni za ovyo kupindukia.

Madikteta hao wanaongelea jinsi wanavyoweza kudumu madarakani. Wanabadilishana mawazo na uzoefu wao. Wazo moja ni kutawala kwa mkono wa chuma na kuwafanya raia waishi kwa hofu. Hofu inaweza kujengwa mioyoni mwa raia kwa kutumia ushirikina na kuwafanya waamini kuwa mtawala anaona kila kinachoendelea nchini, Kwa njia hiyo, raia wanaogopa hata kuwazia kupinga utawala, kwani wanaamini kuwa mtawala atajua.

Udikteta ni mada ambayo imeanishwa katika kazi za fasihi tangu zamani sana. Tunaisoma katika The Epic of Gilgamesh, kwa mfano, na katika baadhi ya tamthilia za Shakespeare. Katika kusoma A Play of Giants, nimewazia sana riwaya ya Ngugi wa Thiong'o, Wizard of the Crow, ambamo dikteta anaumbuliwa pamoja na mfumo wa utawala wake kwa njia ya kejeli, sawa na anavyofanya Soyinka.

Ingawa kuna matumizi ya kejeli, A Play of Giants si tamthilia ya kufurahisha, bali inatibua akili na kunifanya nijiulize binadamu tunawezaje kuishi katika himaya ya udikteta. Kejeli ya mwandishi inanifanya mimi msomaji nicheke, lakini si kicheko cha furaha, bali dhihaka juu ya madikteta na aibu juu yetu wanadamu.

Friday, July 7, 2017

Wadau Wangu Wapya

Nina furaha kama mwandishi kuwa nimejipatia wadau wapya, na ninawatambulisha hapa kama ilivyo kawaida yangu. Hao ni Brian Faloon na mkewe Kristin, wenyeji wa Rochester, Minnesota. Brian ni rais wa Rochester International Association (RIA). Kristin na mimi ni wanabodi katika bodi ya RIA, ambamo nilijiunga mwaka jana kama nilivyoelezea katika blogu hii.

Baada ya mimi kujiunga na bodi, nilipata fursa ya kutoa mhadhara katika chuo kikuu cha Minnesota Rochester, mada ikiwa "Folklore as Expression of Ethics," kama nilivyoeleza katika blogu ya ki-Ingeeza. Brian alihudhuria.

Brian aliuongelea mhadhara ule katika mkutano uliofuata wa bodi ya RIA. Baada ya muda, nilipata mwaliko wa kutoa mhadhara chuo kikuu cha Winona, mwaliko ambao niliuelezea katika blogu hii. Kristin aliniuliza iwapo itawezekana yeye kuhudhuria. Niliwasiliana na waandaaji, kuwauliza iwapo ninaweza kumwalika mgeni kuhudhuria, nikajibiwa kuwa ni ruksa. Nilimweleza Kristin hivyo.

Nilisafiri tarehe 27 Juni hadi Winona, mwendo wa saa mbili. Nilivyoingia ukumbini, niliwakuta Kristi na Brian wameketi, pamoja na wasikilizaji wengine yapata 50. Nilitambulishwa na wenyeji wangu, nikatoa mhadhara kama nilivyoelezea katika blogu ya ki-Ingereza. Nilivyomaliza mhadhara na muda wa masuali na majibu, Kristin na Brian walinisogelea tukaongea. Walifurahia mhadhara. Nilivyowashukuru kwa kusafiri mwendo mrefu na kuhudhuria, walinijibu kuwa wao ni mashabiki wangu. Walichosema ni ukweli, kwani walianza kuwa wadau tangu waliposoma kitabu changu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences.

Tarehe 4 Julai, nilipata ujumbe kutoka kwa Kristin. Kati ya mambo aliyoandika ni haya:

We greatly enjoyed hearing your presentation and thought it was very good! Thank you for letting us attend! I believe it would be an excellent presentation to do in our community and schools here in Rochester as we have the same tensions between the two groups....I would like to coordinate something when we have time. We can discuss it at the next meeting if you're interested.

Ninajivunia hao wadau wangu wapya. Moyo wangu wa kutumia ujuzi wangu kwa manufaa ya walimwengu unaniletea fursa kama hii anayoongelea Kristin. Ninazipokea fursa hizi kwa moyo mkunjufu. Ninaamini ni mipango ya Mungu, wala sijali suala la kulipwa au kutolipwa fedha, kama nilivyoelezea katika blogu hii. Mungu ana mipango yake, na anasawazisha mambo.

Monday, July 3, 2017

Ninapenda Muziki wa Reggae

Ukivaa kofia kama hii niliyovaa pichani hapa kushoto, halafu useme hupendi reggae, hakuna atakayekuelewa. Kofia, sawa na vazi lolote, inawasilisha ujumbe. Ni tamko. Kofia hii niliyovaa inawafanya watu wafikirie vitu kama Rastafari, reggae, Bob Marley, na Jamaica, ambako muziki wa reggae ulianzia.

Muziki wa reggae umeenea sana duniani, kuanzia visiwa vya Pacific, hadi Afrika Kusini; Senegal hadi Sweden. Reggae haichagui kabila, taifa, wala utamaduni. Niliwahi kwenda chuo kikuu cha Arizona, Tucson, nikaambiwa kuwa Wahindi Wekundu wanaipenda reggae. Siku moja, nilitembea katika mtaa mdogo mjini Tel Aviv, Israel, nikaona mbele yangu bango kubwa la picha ya Bob Marley.

Kwa hiyo, kutokana na kwamba siwezi kujumlisha habari za muziki wa reggae ulimwengu mzima, ninawazia zaidi Jamaica. Kutokana na kusoma vitabu juu ya Rastafari na reggae, ninavutiwa na jinsi muziki wa reggae ulivyounganika na itikadi ya Rastafari, ukawa ni sauti ya walalahoi dhidi ya unyonyaji, ukandamizaji, na dhulma za kijamii, kiuchumi, na kadhalika, ndani na nje ya Jamaica.

Saturday, July 1, 2017

Vitabu Nilivyonunua Leo

Ninaamini kuwa kila mtu ana kitu anachokipenda sana. Kuna watu wanaopenda sana soka. Ni mashabiki ambao daima wanafuatilia mechi. Wako tayari kukopa hela ili waende uwanjani kuangalia mechi. Wengine wanapenda bia. Katika baa za Tanzania, nimeona watu wanaokunywa na kuandikiwa deni walipe baadaye. Kama huku kupenda kitu namna hii ni ugonjwa, basi vitabu ndio ugonjwa wangu. Ndio maana katika blogu hii ninaandika mara kwa mara habari za vitabu.

Mtu anaweza kuuliza, inakuwaje katika ulimwengu huu wa vitabu pepe, tuko watu ambao tunaendelea kung'ang'ania vitabu vya jadi? Je, hatuoni udhia wa kubeba vitabu hivyo, na pia udhia wa kuvitafutia sehemu ya kuviweka, badala ya kutumia kifaa cha kuhifadhia vitabu pepe, ambacho kinaweza kubeba mamia ya vitabu au zaidi? Ukweli ni kwamba, mazoea yana taabu. Sio rahisi kuachana na mazoea.

Leo nilikwenda Minneapolis, na wakati wa kurudi, nilipita katika duka la vitabu la Half Price Books, mjini Apple Valley. Kama kawaida, niliangalia kwanza sehemu vinapowekwa vitabu vya Ernest Hemingway au vitabu juu ya Hemingway. Sikuona kipya, nikaelekea sehemu vinapouzwa vitabu vya bei rahisi kabisa. Hapo nilichagua vitabu vinne.

Kitabu kimoja ni Gilgamesh: A Verse Narrative, cha Herbert Mason. Wafuatiliaji wa fasihi simulizi za kale wanafahamu juu ya Gilgamesh, mtu maarufu katika masimulizi ya watu wa himaya ya Sumer, katika nchi ambayo leo inaitwa Iraq, na pia nchi zingine za Mashariki ya Kati. Masimulizi haya hatimaye yaliandikwa, katika lugha kadhaa za wakati ule, kwa hati iitwayo "cuneiform," ambayo ni tofauti kabisa na hizi hati tunazotumia leo, kama vile ya ki-Rumi, au ki-Arabu. Ugunduzi wa maandishi yale ulitokana na juhudi za wana akiolojia.

Lakini baada ya ugunduzi, hakuna aliyeweza kusoma hati ya "cuneiform." Baadaye sana siri ya hati hii iligunduliwa na usomaji wake ukawezekana. Tafsiri za masimulizi ya Gilgamesh zikaanza. Kwa upande wangu, kwa miaka mingi nimefundisha masimulizi ya Gilgamesh kwa kutumia tafsiri ya N. K. Sandars. Nilifahamu, hata hivyo, kwamba ziko tafsiri zingine pia. Kwa hivyo, leo niliona ninunue hii tafsiri ya kishairi ya Herbert Mason.

Kitabu kingine nilichonunua leo ni A Play of Giants, ambayo ni tamthilia ya Wole Soyinka. Nimesoma na kufundisha maandishi ya Soyinka kwa miaka mingi, kuanzia tamthilia, riwaya, mashairi na insha. Ninavyo vitabu vyake kadhaa, lakini si A Play of Giants. Hata hivyo, nilifahamu tangu zamani kuwa tamthilia hii inawaumbua madikteta wa Afrika. Sasa nitaisoma.

Kitabu cha tatu nilichonunua ni Theban Plays of Sophocles. Ni tafsiri ya David R. Slavitt ya tamthilia tatu za Sophocles. Huyu ni mwanatamthilia maarufu wa u-Griki ya kale. Ninazo tatsiri tofauti za tamthilia hizo, lakini niliamua kununua hii pia. Ni jambo bora kusoma tafsiri mbali mbali za kazi ya fasihi, kwani kila tafsiri inaleta ladha tofauti na hata tofauti za ujumbe.

Kitabu cha nne nilichonunua ni Speaking of Books: The Best Things Ever Said About Books and Book Collecting, kilichohaririwa na Rob Kaplan na Harold Rabinowitz. Hicho sikuwahi hata kukisikia, lakini nilivyoangalia ndani, nilivutiwa. Ni mkusanyiko wa kauli za watu mbali mbali kuhusu vitabu, usomaji, uandishi, waandishi, wasomaji, na kadhalika. Nilikuwa ninafahamu baadhi ya mambo ambayo yamewahi kusemwa kuhusu vitabu, kama vile kauli ya Ernest Hemingway, "There is no friend as loyal as a book," yaani hakuna rafiki wa kweli kama kitabu. Kutokana na kupendezwa kwangu na mambo hayo, niliona ninunue kitabu hiki.

Saturday, June 24, 2017

Eti Tundu Lissu Anapinga Kila Kitu

Kuna wa-Tanzania wanaomlalamikia au kumshambulia Tundu Lissu eti anapinga kila kitu. Napenda kusema kuwa malalamiko na mashambulio haya ni ujinga.

Kutoa mawazo na kujieleza ni haki ya kila binadamu, ambayo imetambuliwa katika tangazo la kimataifa la haki za binadamu na imetambuliwa katika katiba ya Tanzania. Tundu Lissu anatumia haki yake. Haingilii wala kuzuia haki ya mtu yeyote kutoa mawazo. Watu wajibu hoja zake. Watu wenye akili hufanya hivyo.

Kama Tundu Lissu hakubaliani na yale wanayosema wengine, na anahoji au kupinga muda wote, tatizo liko wapi? Masuala yenyewe yanahusu maslahi ya Taifa. Kila mzalendo anawajibika kutoa mchango kadiri ya uwezo wake. Mawazo ni mchango mmoja wapo. Na hiki ndicho Tundu Lissu anachofanya. Akae kimya kwa nini? Hata mimi sikai kimya ninapoona maslahi ya nchi hayafuatiliwi ipasavyo au yanahujumiwa. Kutoa mawazo ni muhimu, na kukosoana, inapobidi.

Ni ujinga kutotambua kuwa anavyofanya Tundu Lissu anatoa changamoto ya kuwafanya watu wafikiri nje ya upeo waliozoea au nje ya upeo wanaouwazia wao. Elimu haisongi mbele kama hakuna watu wachochezi wa fikra kama Tundu Lissu. Watu wanaohoji fikra zinazokubalika na jamii wanaipa jamii fursa ya kufungua milango mipya ya fikra. Siafiki uwekaji wa mipaka katika kufikiri na kutafuta ukweli. Elimu haiwekewi mipaka.

Mimi kama mwalimu ninawajibika kuwalea vijana wawe watu wa kuhoji mambo bila ukomo. Vinginevyo, kuna sababu gani ya kujiita mwalimu? Kuna sababu gani ya kuwa na vyuo na kusema kuwa tunaelimisha? Watu makini ulimwenguni kote wanatambua kuwa dunia inazidi kuwa ya "knowledge economy." Bila tabia ya udadisi usiokuwa na mipaka, tutajengaje "knowledge economy"? Kwa maana hiyo, ninamwona Tundu Lissu kama mtu muhimu kwa maendeleo ya nchi, na ni mfano wa kuigwa.

Monday, June 19, 2017

Mzalendo Tundu Lissu Aliyasema Haya Mambo

Leo nimeona taarifa za kufikishwa mahakamani watuhumiwa wakuu wawili wa ufisadi mkubwa nchini Tanzania. Watuhumiwa hao ni Harbinder Singh Sethi na James Rugemalira. Wananchi wengi tunalichukulia jambo hili kama mwendelezo wa juhudi za Rais Magufuli kusafisha nchi. Lakini kitu kimoja kinachonikera ni jinsi watu wengine wanavyojaribu kupindisha historia ya suala hili. Hapa naleta hotuba ya Tundu Lissu aliyoitoa Bungeni kabla ya ujio wa Rais Magufuli.

Wednesday, June 7, 2017

Umuhimu wa Kumpigia Mbuzi Gitaa

Katika jamii yetu wa-Tanzania, usemi kwamba usimpigie mbuzi gitaa unachukuliwa kuwa ni ukweli usiopingika, busara isiyo na walakini. Ni kile kinachojulikana kama busara ya kawaida, yaani "common sense," kwa ki-Ingereza. Lakini je, mtazamo huu ni sahihi? Hili ndilo suala ninalopenda kulijadili hapa, kwa mtazamo wangu kama msomi, mtafiti na mwalimu.

Napenda kutamka wazi kuwa kwa msomi au mwalimu au mtafiti, "common sense" ni kitu cha kujihadhari nacho. Kazi ya msomi, mwalimu au mtafiti si kuzingatia, kuafiki, au kuhalalisha "common sense," bali kuhoji na kudadisi "common sense." Ndivyo alivyofanya mwelimishaji maarufu Socrates. Kuna wengi wengine, kama vile Galileo. Jamii yote ilielewa kuwa jua linaizunguka dunia, kwani kila mtu alijionea mwenyewe. Ilikuwa ni "common sense." Lakini Galileo, akiendeleza mawazo ya Copernicus, alisema kuwa ni dunia ndio inayolizunguka jua. Jamii ya Galileo ilimtia matatani, kama vile jamii ya Socrates ilivyomtia matatani.

Turudi kwenye suala la kumpigia mbuzi gitaa. Ninapenda kusema kuwa ni wajibu wa msomi, mtafiti, au mwalimu kuhoji hii busara ya jamii kwamba kumpigia mbuzi gitaa ni kupoteza muda au ni ujinga. Msimamo huu wa jamii una walakini mkubwa. Ukipiga gitaa, inatoa sauti. Je, jamii inamaanisha kuwa mbuzi hana uwezo wa kutambua na kuguswa na sauti? Kama jamii inaamini hivyo, inakosea.

Sisi ambao tulikulia kijijini tukichunga mbuzi tunajua kuwa mbuzi wana milio yao ambayo wanatumia kuwasiliana. Hata wakati wa kuchunga, tulikuwa tunaweza kutambua mlio wa mbuzi mwenye dhiki. Tulikuwa tunawaita mbuzi kwa majina tuliyowapa au kwa kupiga mluzi. Kwa hivi, jamii inakosea iwapo inaamini kuwa mbuzi hawana uwezo wa kujieleza, kutambua au kuguswa na sauti.

Suala la kulitafakari ni sauti ipi ambayo mbuzi anaitambua na kuguswa nayo, na ipi hawezi kuitambua na kuguswa nayo. Kinachohitajika si hiyo "common sense" kwamba usimpigie mbuzi gitaa, bali utafiti. Tunatakiwa kumpigia mbuzi gitaa tena na tena, kwa mitindo mbali mbali.

Utafiti hauwekewi kikomo. Hata pale tunapodhani tumepata ufumbuzi wa suala, hatupigi marufuku utafiti zaidi wa suala hilo. Badala ya kuridhika na busara ya jamii kuwa tusimpigie mbuzi gitaa, mtafiti au msomi huwaza: kwa nini nisimpigie mbuzi gitaa? Itakuwaje nikimpigia mbuzi gitaa? Ngoja nimpigie mbuzi gitaa nione kitakachotokea. Huu ndio mtazamo wa mtafiti, msomi, na mwalimu. Hii duku duku ya kujua huitwa "intellectual curiosity" kwa ki-Ingereza.

Msomi au mtafiti au mwalimu ni mtu anayetafuta elimu muda wote. Thomas Edison, mvumbuzi maarufu, alifanya majaribio ya kuvumbua na kuunda vitu akashindwa mara nyingi sana, lakini hatimaye alivumbua balbu ya umeme. Huu ndio moyo unaohitajika katika suala hili la kumpigia mbuzi gitaa. Tukitaka mfumo wa elimu wa kweli, inatubidi tujenge mtazamo na mwelekeo huu wa kutambua umuhimu kumpigia mbuzi gitaa.

Unapofanya utafiti kwa ajili ya kuchunguza suala fulani huwezi kujua matokeo yatakuwa yepi. Unaweza kupata matokeo ambayo hukutegemea. Katika majaribio yake ndani ya maabara, mwaka 1928 Alexander Fleming aliona kitu kimejitokeza kwenye kisahani kimojawapo alimoweka vitu vya kuvichunguza. Kitu hicho kilikuwa kimejitokeza bila yeye kutegemea, lakini ndicho kilikuja kubainika kuwa ni penicillin.

Kwa hivyo, mtu ukianza kumpigia mbuzi gitaa, ukawa anafuatilia kwa makini kila kinachotokea, huenda utajifunza mambo ambayo hakutegemea kuhusu tabia na hisia za mbuzi. Inawezekana ukipiga gitaa mara ya kwanza usione lolote likitokea. Lakini je, unajuaje kama hakutakuwa na mabadiliko yoyote ukimpigia mara kumi, au mara mia, au zaidi?

Kama unadhani ninatania, napenda tujikumbushe utafiti na uvumbuzi aliofanya Ivan Pavlov akitumia mbwa. Pavlov alifanya majaribio ambayo yalitoa mchango mkubwa katika taaluma ya saikolojia. Nashauri msomaji utafute taarifa za Pavlov na majaribio yake na uvumbuzi aliofanya. Huenda utakubaliana nami kuwa suala la kumpigia mbuzi gitaa si la kupuuzwa. Ni muhimu.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...