Walikuwa wakijadili utendi wa Hamziya, nami nilikaribishwa kuongelea tendi kwa ujumla.
Wazo moja ambalo lilionekana kuwasisimua wanafunzi ni mchango wa wanawake katika tendi, suala ambalo nililiongelea kwa kirefu kiasi, nikatoa mifano ya utafiti na uandishi wangu kuhusu suala hili. Mfano moja niliotoa ni utafiti wangu juu ya Gindu Nkima, shujaa katika masimulizi ya wa-Sukuma.
Maongezi haya yalikuwa ni changamoto kwangu, kwa sababu daima nimeongelea masuala haya ya tendi kwa ki-Ingereza, iwe ni kwa maandishi au kwa mihadhara. Niliwahi kuandika makala moja tu kwa ki-Swahili kuhusu tendi, “Ushujaa Katika Ras il Ghuli.”
Kutokana na hali hiyo, mara kadhaa katika mhandara wangu niliwajibika kuuliza tafsiri ya ki-Swahili ya dhana kadhaa za ki-Ingereza. Kwa mfano, nilipowauliza tafsiri ya “destiny,” nilifurahi kuambiwa kuwa tafsiri ni hatima.
Niliulizwa masuali mengi ya kufikirisha, baadhi yakiwa yamejengeka katika falsafa. Suali moja ninalolikumbuka lilikuwa maana ya kifo cha shujaa. Suali hili nililiona lenye upana na kina, kwani dhana ya kifo cha shujaa hujitokeza au kutojitokeza kwa namna mbali mbali katika tendi za tamaduni mbali mbali. Dhana ya kifo cha shujaa imefungamana na falsafa, imani, na hisia za jamii husika.