
Nimerejea muda mfupi uliopita kutoka Faribault, kwenye maonesho ya utamaduni ambayo hufanyika mara moja kila mwaka, chini ya kamati ya
Faribault Diversity Coalition. Mimi ni mwanakamati.
Ingawa nilirejea hapa Marekani kutoka Tanzania wiki moja tu iliyopita, nilikuta ujumbe kutoka kwa mwenyekiti wa kamati, Milo Larson, akinikumbusha kuhusu maonesho hayo. Alinikumbusha kuwa nahitajika kupeleka vitabu vyangu kwenye maonesho. Katika picha hapo juu, Mzee Larson anaonekana akiandaa meza yangu.
Kwa hapa Marekani, nimezoea hali hii ya kuitwa sehemu mbali mbali nikazungumze na pia kupeleka vitabu. Ni tofauti na hali ninayoiona Tanzania.

Baada ya meza yangu kukamilika, niliketi nikingojea wateja na watu wa kuongea nao kuhusu shughuli zangu za uandishi na ushauri juu ya masuala ya elimu na tamaduni. Picha hii, na jinsi nilivyokaa imenikumbusha makala niliyowahi kuandika kuhusu
uuzaji wa vitabu. Kijuu juu naonekana nimekaa kama muuza dagaaa. Ukweli ni kuwa hapa huwa ni darasa zito siku nzima.

Walikuwepo wacheza ngoma za kabila la Aztec. Hao wamekuwa wakishiriki maonesho haya mwaka hadi mwaka, na huwa ni kivutio kikubwa.



Watu walileta vitu mbali mbali vya kuuza, kama vile vyakula, vinywaji, na kazi za sanaa. Katika maonesho haya, huwa napata fursa ya kukutana na watu wengi wapya.
Leo, kwa mfano, nimekutana na huyu mama, ambaye aliniambia kuwa alisoma katika Chuo Kikuu cha Wisconsin-Madison. Hii ilikuwa ni ajabu, kwani nami nilisoma katika Chuo hicho hicho, miaka ya kabla yake. Halafu, aliniambia kuwa alishachukua kozi moja ya Profesa Harold Scheub iliyohusu fasihi hadithi za Afrika. Profesa huyu ndiye aliyesimamia tasnifu yangu ya shahada ya udaktari. Kweli milima haikutani, binadamu hukutana.

Huyu kijana hapa kushoto, baada ya kununua
kitabu hiki alichoshika, aliomba tupige picha. Akanipa kitabu changu kingine nishike, na rafiki aliyekuja naye akatupiga picha.
Tabia hii si ngeni kwa wa-Marekani. Huwa wanapenda kumbukumbu za aina hii. Wengi wanapenda mwandishi atie sahihi kwenye kitabu wanachonunua. Nami leo nimefanya hivyo kwa wateja wangu.

Katika mji wa Faribault kuna wa-Somali wengi, ambao wamefika miaka ya karibuni. Leo hapo kwenye maonesho nilikutana na hao wa-Somali wawili. Huyu aliyeko kushoto anaishi kwenye mji mwingine. Lakini huyu wa kulia ni rafiki yangu, ambaye anafuatilia maandishi na shughuli zangu kuhusu masuala ya tamaduni. Ni kijana makini, na tunapangia kushirikiana katika shughuli hizo.