Katika mizunguko yangu Tanzania mwaka huu, nilitembelea Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mara kadhaa, kwa shughuli rasmi na pia shughuli binafsi. Kwa vile nilisoma na kufundisha hapo, daima ninakutana na watu wengi tuliosoma au kufundisha pamoja au niliowafundisha ambao baadhi yao ni walimu pale. Kwa mfano, soma
hapa na
hapa.
Mmoja wa wale niliokutana nao mwaka huu ni Edwin Semzaba, mwandishi maarufu wa tamthilia na riwaya na ni mwigizaji hodari. Anaandika kwa ki-Swahili. Tamthilia zake, kama vile
Ngoswe, zinafahamika Tanzania nzima na nje.

Baadhi ya riwaya zake, ambazo ninazo, ni
Tausi Wa Alfajiri (Heko Publishers Limited, 1996), na
Funke Bugebuge (Dar es Salaam University Press, 1999).


Semzaba ni rafiki yangu wa siku nyingi. Tulisoma darasa moja, kuanzia Mkwawa High School, Iringa, 1971-72, hadi Chuo Kikuu Dar es Salaam, 1973-76. Mwaka huu, aliposikia kuwa niko nchini, Semzaba alinipa nakala mpya ya
Ngoswe, iliyochapishwa na Nyambari Nyangwine Publishers, 2008.
Nilikuwa na nakala ya
Ngoswe tangu zamani, toleo lililochapishwa na Education Services Centre Ltd, 1988. Vile Vile, miaka kadhaa iliyopita, Semzaba alinipa nakala ya video ya tamthilia hii.

Mwaka huu alinipa pia nakala ya riwaya yake mpya,
Marimba ya Majaliwa. Sikujua kuwa alikuwa ameandika riwaya hii. Alinieleza kwamba ni riwaya aliyoshinda kwenye shindano la hadithi za kusisimua, mwaka 2007. Shindano hili lilifadhiliwa na SIDA na kusimamiwa na Mradi wa Vitabu vya Watoto, Tanzania.
Nilifurahi kusikia hivyo, kwani nafahamu alivyo makini na kazi yake, na jinsi alivyochangia fasihi na sanaa Tanzania na duniani kwa miaka mingi. Nafurahi kuwa mchango wake unatambuliwa kwa namna hiyo.

Kwa miaka kadhaa nimewazia kutafsiri baadhi ya maandishi ya Semzaba. Nilianza kutafsiri
Mkokoteni, ila sikumaliza. Lakini katika kuongea na Semzaba mwaka huu, ilionekana kuwa tafsiri ya
Tendehogo inahitajika mapema zaidi. Kazi hizi, na za waandishi wengine wa nchi yetu, inafaa zitafsiriwe, kwa manufaa ya vizazi vijavyo.