Friday, December 31, 2010

Mafisadi Wanaufurahia Mwaka Mpya

Mwaka unaoisha leo, mafisadi wanaoihujumu Tanzania walikuwa na sababu ya kukosa usingizi, kutokana na kampeni kali iliyofanyika dhidi yao.

Ingekuwa vipi, mwaka huu mpya ungekuwa ni mgumu kwa mafisadi, lakini moto uliowashwa dhidi yao umeendelea kuwa hafifu, kwa juhudi za zimamoto. Tumerudi katika amani na utulivu.

Thursday, December 30, 2010

Utamaduni na Utandawazi: Tunawafahamu wa-Turuki?


Wasomaji wa blogu zangu wanafahamu kuwa suala la utamaduni na utandawazi ni moja ya masuala ninayoyatafakari sana. Ninaelezea umuhimu wa suala hili kwa namna ya pekee katika kitabu changu cha CHANGAMOTO: Insha za Jamii.

Dhana ya utamaduni ina maana nyingi, na ni muhimu kwa mtumiaji wa dhana hii kuelezea anaitumia kwa maana ipi. Ili nieleweke vizuri na kiurahisi, singependa kuleta nadharia na mambo ya kufikirika. Badala yake, nimeamua kuuliza suali: Tunawafahamu wa-Turuki?

Leo hii, Tanzania na u-Turuki zinajenga uhusiano kwa kiwango ambacho hatujawahi kuona kabla, katika nyanja kama biashara, utalii, na elimu. Shirika la ndege la u-Turuki linapiga hatua katika kuimarisha safari baina ya Tanzania na u-Turuki. Ni wazi kuwa watu wa nchi hizi mbili wataendelea kuwa na mahusiano ya karibu katika nyanja mbali mbali.

Kama ninavyosema mara kwa mara, naamini kuwa mahusiano yoyote baina ya watu wa tamaduni mbali mbali yanaathiriwa moja kwa moja na tofauti za tamaduni hizo. Ndio maana ninauliza iwapo tunawafahamu wa-Turuki.

Sambamba na kuanzisha uhusiano na watu wa utamaduni tofauti na wetu, kuna umuhimu wa kujielimisha. Jambo moja ni kusoma vitabu. Nikiendelea na mfano huu wa u-Turuki, kuna waandishi maarufu wa ki-Turuki, kama vile Nazim Hikmet na Orhan Pamuk, ambaye alipata tuzo ya Nobel mwaka 2006. Kuna masimulizi ya kale, kama yale ambayo mhusika wake ni Nasreddin Hodja, maarufu kwa wa-Turuki na wasomaji wengine duniani.

Kwa miaka kadhaa nilifahamu kuhusu utungo maarufu unaojulikana kama The Book of Dede Korkut. Nilinunua nakala, lakini sikupata fursa ya kuisoma. Wiki hii nimeanza kuisoma, nikiwa nimesukumwa na hili suala la kukua kwa uhusiano baina ya Tanzania na u-Turuki. Lakini vile vile ni kwa sababu nimeamua kufundisha kitabu hiki katika kozi ya fasihi nitakayofundisha kuanzia wiki ijayo.

Kama nilivyotegemea, kitabu hiki ni hazina kubwa na njia nzuri ya kuwafahamu wa-Turuki: mtazamo wao wa maisha na mahusiano ya jamii, maadili yao na kadhalika. Kitabu hiki ni maarufu duniani. Wenzetu wa Brazil kwa mfano, ambao tunawaona kama rafiki zetu, wanakienzi kitabu hiki. Soma hapa.

Katika makala hii, juu ya kupokelewa kwa tafsiri ya The Book of Dede Korkut Brazil, tunaona wenzetu wanavyoelewa umuhimu wa kujisomea vitabu ili kujenga maelewano na watu wa nchi zingine na kuboresha mahusiano. Ni elimu ambayo inatufaa sote, kuanzia wafanya biashara, wadau wa elimu, diplomasia, utalii na kadhalika. Hayo ni baadhi ya mambo muhimu ninayomaanisha ninapoongelea suala la utamaduni na utandawazi.

Ingawa nimewataja wa-Turuki, siwaongelei wao tu. Tujiulize kama tunawafahamu wa-Hindi, wa-Australia, wa-China, wa-Marekani, wa-Rusi, na kadhalika. Jambo la kuzingatia ni kuwa dunia ya utandawazi wa leo inakuja na mitego na mitihani mingi, si ya kuivamia kichwa kichwa, bila elimu.

Sunday, December 19, 2010

Kitabu Kimetua St. Cloud, Minnesota

Wasomaji wa blogu zangu, hii na ile ya ki-Ingereza, wanafahamu ninavyopenda kujishughulisha na masuala ya tofauti za tamaduni na athari zake katika ulimwengu wa leo.

Nafanya shughuli hizi si kwa ajili ya kutafuta umaarufu, bali naamini ni wajibu kwa wanadamu kusaidiana katika maisha na kuifanya dunia iwe bora kuliko ilivyo.

Miezi ya karibuni nimejishughulisha sana na matatizo yanayowapata wahamiaji wa ki-Somali katika jimbo la Minnesota, ambalo linaongoza kwa idadi ya wahamiaji wa ki-Somali. Wasomaji wa blogu zangu watakumbuka taarifa za shughuli zangu katika mji wa Faribault.

Matatizo kama haya ya Faribault yako pia katika miji mingine, kama vile St. Cloud. Kutokana uzoefu nilioupata Faribault, nimeanzisha mawasiliano na ndugu Mohamoud Mohamed, mkurugenzi wa SASSO, jumuia inayoshughulikia masuala ya wa-Somali mjini St. Cloud.

Nilimpelekea nakala ya kitabu cha Africans and Americans, kama mchango wangu na changamoto. Jana ameniambia kuwa kitabu amekipata, anaendelea kukisoma, na anakipenda. Atawaonyesha wadau wa St. Cloud: halmashauri ya mji, shule na vyuo, idara ya polisi, mahospitali, na kadhalika. Nami nilimhakikishia kuwa ni jambo bora. Badala ya watu kununiana tu au kugombana, ni vema wakaanza utaratibu wa kuzungumzia matatizo kama ilivyofanyika Faribault, na ikapokelewa vizuri.

Kama ninavyosema katika mihadhara, blogu na maandishi mengine, matatizo ya aina hii yanayoikumba miji ya Faribault na St. Cloud yanajitokeza katika miji na jamii nyingine duniani: Afrika, Asia, Australia, Marekani, Ulaya, na kwingineko, na yataongezeka, kutokana na mwenendo wa utandawazi wa leo. Ninapokuwa Dar es Salaam, kwa mfano, nasikiliza na kutafakari minong'ono na majungu kuhusu wa-China, ambao wanaendelea kuja katika mji ule. Niliwahi pia kuongelea tafrani iliyotokea Zanzibar. Kinachobaki ni sisi kujizatiti kwa kuelimishana kuhusu tofauti zetu na kutafuta namna ya kuishi bila matatizo.

Najiandaa kushiriki katika masuala ya St. Cloud. Mbali ya umuhimu wake kwa jinsi hali ilivyo, ni fursa ya mimi kujiongezea ujuzi na uzoefu nitakaoutumia katika kuwasaidia wengine.

Friday, December 17, 2010

Nimenunua Kitabu Kipya cha Chimamanda Ngozi Adichie

Leo nimenunua, The Thing Around Your Neck, kitabu kipya cha Chimamanda Ngozi Adichie. Huyu dada ni mwandishi wa ki-Nigeria, mwenye kipaji sana cha kuandika riwaya na hadithi fupi. Pia ana mawazo ya kusisimua na kufikirisha kuhusu simulizi. Umaarufu wake unakua kwa kasi. Amepata tuzo mbali mbali, ikiwemo ya Taasisi ya MacArthur

Riwaya yake ya kwanza, Purple Hibiscus, niliifundisha hapa chuoni St. Olaf. Inavutia sana kwa dhamira, maudhui, na matumizi ya lugha. Inaongelea maisha ya familia ya profesa wa chuo kikuu cha Nsukka, Nigeria, kwa namna ya kukufanya msomaji ujisikie uko sehemu hiyo. Matukio na migogoro baina ya wahusika imeelezwa kwa uhalisi wa kuvutia.

Mwaka 2006 nilipata bahati ya kumwona Chimamanda Ngozi Adichie, alipofika mjini Minneapolis kwenye tamasha la vitabu. Alikuja kuzindua kitabu chake cha pili, Half of a Yellow Sun. Nilinunua nakala, ambayo aliisaini, na tulipata muda wa kuzungumza kiasi, hata akaniambia kuhusu anavyoendesha blogu. Tulipiga picha inayoonekana hapa chini.
Bado sijapata muda wa kusoma Half of a Yellow Sun, ila ninayo hapa ofisini muda wote, na auala la kuisoma limo kwenye orodha yangu ya mambo muhimu ya kufanya.

The Thing Around Your Neck ni mkusanyo wa hadithi fupi. Nimeanza kusoma hadithi ya kwanza, ambayo inakumbusha Purple Hibiscus, kwa vile wahusika ni familia ya profesa katika chuo kikuu cha Nsukka. Lakini kwa kuangalia haraka haraka, nimeona kuwa kitabu hiki kina hadithi zinazohusu Nigeria na pia Marekani. Kwa maneno mengine, wahusika wa ki-Nigeria wako Nigeria na pia Marekani.

Hii imenikumbusha kitabu kingine cha hadithi kiitwacho Tropical Fish: Tales from Entebbe. Mwandishi ni Doreen Baingana wa Uganda, dada ambaye naye ana kipaji sana. Baadhi ya hadithi zilizomo katika kitabu hiki zinahusu matokeo yanayotokea Uganda na zingine zinahusu maisha ya wa-Ganda wakiwa Marekani.

Mpangilio huu wa hadithi za Adichie na Baingana unaendana na ukweli kwamba waandishi wote wawili wana uzoefu wa kuishi nchini kwao na pia Marekani. Ni katika kizazi kipya cha waandishi ambao wanailetea sifa sana Afrika.

Nina hamu ya kusoma The Thing Around Your Neck. Nina mategemeo ya kuandika makala katika blogu hii.

Friday, December 10, 2010

Laiti Ningekuwa Kama Hemingway

Laiti ningekuwa kama Hemingway, mwandishi maarufu sana duniani. Ningeandika kuhusu nchi yangu na watu wake kwa umakini, ubunifu, na ukweli wa kumgusa kila msomaji. Ningeandika kuhusu maziwa, mito, milima na mabonde. Ningeandika kuhusu fukwe, nyanda na visiwa. Ningeandika kuhusu miji na vijiji, mitaa na vitongoji.

Nimetamka hayo, na nimeanza kufanya mazoezi. Lakini bado njia ni ndefu mbele yangu.

Laiti ningekuwa kama Hemingway, aliyeangalia mazingira, matukio, na tabia za wanadamu kwa macho na akili yote, aliyejawa nidhamu ya kutumia lugha, akiangalia kila neno, tena na tena, akibadili na kusahihisha tena na tena, akitafuta namna ya kuandika sentensi sahihi yenye ukweli mtupu.

Laiti ningekuwa kama Hemingway, aliyetufundisha kuwa kazi ya mwandishi ni kujitoa mhanga ili nafsi yake yote ibakie katika kitabu tu, asibakishe hata chembe nje ya kitabu. Kila kitabu kiwe ni mauti ya mwandishi, vinginevyo kitabu hiki ni mzaha na udanganyifu. Je, nitayaweza hayo?

Hemingway aliandika kuhusu nchi mbali mbali alizozitembelea, ikiwemo nchi yangu. Nimekutana na watu wa nchi mbali mbali wanaomshukuru Hemingway kwa hilo. Tutalipaje fadhila, isipokuwa kwa kujijengea nidhamu ya kuyaangalia mazingira na maisha, nidhamu ya kuiheshimu lugha na sentensi, tuweze nasi kuandika mambo ya thamani? Tutalipaje fadhila kama hatuna ushujaa wa kuwa wakweli kama Hemingway?

Saturday, December 4, 2010

Nimekutana na Mratibu wa Chuo Kikuu cha Njombe

Tarehe 9 Oktoba nilipigiwa simu na mtu aliyejitambulisha kwa jina la Bill, akisema kuwa angependa kumleta kwangu mgeni kutoka Tanzania, kwa mazungumzo. Alimtaja mgeni kuwa ni Dr. Peter Kimilike.

Basi, tarehe 11 walifika hapa Chuoni St. Olaf. Tulifurahi kufahamiana. Dr. Kimilike ni mchungaji m-Tanzania ambaye anaratibu shughuli za kuanzisha Chuo Kikuu cha Njombe. Tulifurahi kutambua kuwa kuna watu maarufu ambao yeye na mimi tunafahamiana nao, kama vile Danford Mpumilwa, afisa habari wa Mahakama ya ki-Mataifa inayoshughulikia mauaji ya Rwanda (ICTR), na Rev. Dr. Anneth Munga, mkuu wa Chuo cha Sebastian Kolowa

Maongezi yetu yalilenga zaidi kwenye Chuo Kikuu cha Njombe. Nilimweleza Dr. Kimilike kuwa ninafuatilia kwa karibu maendeleo ya vyuo Tanzania. Kila ninapoenda kule, ninatembelea vyuo. Nikampa mifano ya vyuo nilivyotembelea: Tumaini (Iringa), Makumira (Arusha), na Sebastian Kolowa (Lushoto). Ninaelimika sana ninapoongea na walimu na wengine kuhusu hali halisi ya vyuo vyetu na mahitaji yaliyopo. Kwa mtu anayekaa ughaibuni, kuna fursa za kuchangia vitu kama vitabu.

Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ninakitembelea mara kwa mara. Nilisoma na kufundisha hapo, na kila mwaka napita hapo kufanya utafiti, kuongea na walimu na pia wanafunzi. Napenda kutembelea shule za kila aina, kuanzia shule za msingi, kujielimisha kuhusu hali halisi.

Kuhusu Chuo Kikuu cha Njombe, nilimwambia kuwa nimefuatilia habari zake kwa miezi mingi, mtandaoni, kama vile Arusha Times. Alinieleza hatua iliyofikiwa na mipango inayoendelea. Kuna mahitaji mengi, kuanzia ya kukarabati majengo na kujenga mengine, kununua vitabu na majarida, vifaa vya maabara, kompyuta, na kuleta walimu.

Mwanzo ni mgumu, kama kawaida. Unahitajika mtandao wa wadau na washiriki wa aina mbali mbali. Cha kutia moyo ni kuwa msingi umeshajengwa kwa kutumia uwezo na nguvu za wananchi, ambao wamechanga chochote walicho nacho, iwe ni fedha, mazao, hata jogoo.

Chuo kina mikakati ya kujiendesha, kwa kuanzisha miradi kama ya kupanda miti kwa ajili ya mbao za kuuza, na pia kupanda mazao kama vile matunda. Dr. Kimilike anaelezea zaidi suala hili hapa.
Nimewekwa katika mtandao wa wahamasishaji wa Chuo Kikuu Cha Njombe. Nimelipokea jukumu hili kwa mikono miwili. Hizi picha tulipiga ndani ya uwanja wa ndege wa Minneapolis, Minnesota, wakati Mchungaji Kimilike alipokuwa anarudi Tanzania, Oktoba 24, baada ya ziara yake ya Marekani.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...