Kwa mawazo yangu, hiyo si fursa ya kuvipigia debe vitabu hivyo. Ninachofanya ni kujibu masuali niulizwayo. Kama suali linahusu kitabu au vitabu moja kwa moja, naelezea pia chimbuko la kitabu na uhusiano wake na shughuli zangu.
Ninaposema shughuli zangu, ninamaanisha ufundishaji wa fasihi na lugha ya ki-Ingereza, utafiti katika masimulizi ya jadi, uandishi, utoaji wa ushauri kuhusu tofauti za tamaduni kwa wa-Marekani waendao Afrika. Pia naongelea kuhusu kuwaandaa wanafunzi na kuwapeleka katika safari za masomo Afrika.
Kwa namna moja au nyingine, masuala ya aina hiyo yanajitokeza katika vitabu vyangu. Ni kawaida kwamba mtu anayekuja kwenye meza yangu anakuwa na hamu zaidi ya mada fulani, na hiyo inamfanya aulizie zaidi kuhusu kitabu fulani, na huamua kukinunua.
Tarehe 2 Agosti, katika tamasha la Afrifest litakalofanyika North View Junior High School, Brooklyn Park, hapa Minnesota, nitapeleka vitabu vifuatavyo.

Kitabu hiki nimekiandika kwa namna ya kuweza kusomwa na yeyote, na pia katika masomo ya kiwango chochote, hadi chuo kikuu.
.jpg)
Kitabu kingine ni Notes on Achebe's "Things Fall Apart". Maelezo ya historia ya kitabu hiki niliyaandika katika blogu hii.

Kitabu kingine ni Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Wasomaji wa blogu hii watakuwa wamekisikia, na wengine wamekisoma.
Kitabu hiki nilikiandika katika mazingira maalum. Nikiwa mmoja wa washauri katika pogram za Associated Colleges of the Midwest za kupeleka wanafunzi Afrika, nilikuwa nikiongelea sana, kwenye mikutano yetu masuala ya athari za tofauti za tamaduni, kwani wanafunzi wanaporudi kutoka Afrika, wanakuwa na masuali mengi kuhusu mambo waliyoyaona kule. Mengine yalikuwa ya kustaajabisha na mengine ya kukera, na mengine ya kukanganya akili. Kazi yangu ilikuwa kufafanua, kwa sababu nawafahamu kutosha wa-Marekani na wa-Afrika. Basi washauri wenzangu katika program hizi walinishawishi niandike mwongozo, uweze kutumiwa nao na wanafunzi wao wanapokwenda Afrika.

Kingine ni CHANGAMOTO: Insha za Jamii. Ni mkusanyo wa insha kuhusu masuala ya siasa, uchumi, elimu, na utamaduni, kwa kuzingatia hasa hali ya Tanzania.
Lengo lilikuwa kuwajibu wale waliokuwa wananiuliza kwa nini siandiki kwa ki-Swahili, ili wa- Tanzania walio wengi waweze kusoma. Pamoja na kukubaliana na mtazamo wao, sherti niseme pia kuwa wa-Tanzania waache kujiziuka; wajifunze ki-Ingereza na ikiwezekana, lugha zingine pia. Kiswahili kina manufaa, lakini hakitawafikisha mbali katika dunia ya utandawazi wa leo. Shaaban Robert, ambaye wa-Tanzania hupenda sana kuunukuu usemi wake kuwa titi la mama li tamu, akimaanisha lugha yake ya ki-Swahili, hakuwa mvivu kama walivyo wa-Tanzania wa leo. Pamoja na kuwa hakuwa na fursa kama tulizo nazo leo, alijitahidi akajifunza ki-Ingereza na hata kukitumia. Aliziheshimu lugha na tamaduni za kigeni.
Kitabu kingine ni Africans in the World. Hiki ni kijitabu kidogo sana. Kinahusu historia ya wa-Afrika na wengine wenye asili ya Afrika, pamoja na siasa, utamaduni, na mengine kama hayo. Kilitokana na Afrifest ya kwanza mwaka 2007. Niliandaa magango kumi, kila bango likiwa linaelezea kipengele fulani. Hatimaye, yaliyomo kwenye mabango niliyachapisha kwa umbo la hiki kijitabu. Hakuna tofauti yoyote kati ya yale mabango na hiki kijitabu, isipokuwa ukubwa tu. Ufundishaji wangu wa somo la "Africa and the Americas," chuoni St. Olaf, ulinirahizishia kazi ya kuandika kazi hii.