Thursday, March 12, 2015

Vitabu Nilivyonunua Jana na Leo

Kila mtu ana mambo anayoyapenda sana, na yuko tayari kuyapata au kuyafanya kwa gharama yoyote. Vitabu ni kati ya vitu ninavyovipenda sana, na niko tayari kutumia gharama yoyote kuvipata. Imekuwa hivyo tangu nilipokuwa shule ya msingi.

Mara kwa mara, katika blogu hii, nimeandika taarifa ya vitabu nilivyonunua. Siandiki taarifa ya kila kitabu, kwani wakati mwingine nasahau. Lakini leo nimekumbuka. Naandika kuhusu vitabu nilivyonunua jana na leo.

Nilitoka zangu ofisini, nikaelekea kwenye duka la vitabu. Nje ya duka kulikuwa na "seli" ya vitabu. Kulikuwa na vitabu vingi sana vikiuzwa kwa bei nafuu. Hapo hapo nilijiunga na wengine waliokuwa wanavichambua vitabu hivyo na kuvinunua.

Jungu kuu halikosi ukoko. Niliviona vitabu vinne vilivyonivutia kwa namna ya pekee, nikavinunua.

Kimojawapo ni Wine to Water: How One Man Saved Himself While Trying to Save the World. Hilo jina tu lilinivutia, nikakumbuka hadithi ya muujiza wa Yesu wa kugeuza maji kuwa divai. Katika kukiangalia, niliona kuwa mtungaji wake, Doc Hendley, ameandika kitabu hiki kuelezea harakati zake za kuwasaidia watu wa Darfur kuchimba visima vya maji, akipambana na hatari zote zilizoko Darfur. Niliona kitabu hiki kitanifundisha mengi, na nilitaka kiwemo kati ya vitabu vya nyumbani mwangu.

Kitabu cha pili ni Walk in Their Shoes: Can One Person Change the World? kilichoandikwa na Jim Ziolkowski. Hicho nacho kilinivutia. Jina lake lilinikumbusha kitabu ambacho nilikinunua miaka michache iliyopita, kiitwacho Leaving Microsoft to Change the World: An Enterpreneur's Odyssey to Educate the World's Children, kilichoandikwa na John Wood. Mtu unaposoma vitabu vya aina hii, unajikuta ukijifunza sio tu uwezekano bali umuhimu wa kujitoa katika ubinafsi na badala yake kutumia vipaji na uwezo wako kuwanufaisha walimwengu.

Nilikiona kitabu kingine, And Then Life Happens: A Memoir, chenye jina la Auma Obama kama mwandishi, na picha yake. Hilo jina peke yake lilinifanya nikiangalie, nikaona kuwa huyu dada ni binti wa Barack Hussein Obama, baba mzazi wa Rais Obama wa Marekani. Binti huyu alizaliwa Kenya, akaishi miaka mingi na kusoma Ujerumani. Kitabu chake hiki, ambacho ni juu ya maisha yake, alikiandika kwa ki-Jerumani, kikatafsiriwa na Ross Benjamin. Nilivutiwa na taarifa hizo, nikakichukua bila kusita.

Kitabu cha nne nilichokinunua hiyo jana ni Indigenizing The Academy: Transforming Scholarship and Empowering Communities. Wahariri wake ni Devon Abbot Mihesuah na Angela Cavender Wilson. Mimi kama mwanataaluma, nilivutiwa moja kwa moja na kitabu hiki. Nilivutiwa zaidi nilipogundua kuwa kinahusu utafiti na uandishi juu ya wenyeji asili wa Marekani, ambao tunawaita Wahindi Wekundu. Niliona kuwa ni kitabu kinachohoji jadi ya utafiti, taaluma, na uandishi kuwahusu hao Wahindi Wekundu, na, inavyoonekana, kinaleta fikra za kimapinduzi, kama yale ambayo kwetu Afrika yalianzishwa na wataalam kama Cheikh Anta Diop na Walter Rodney.

Katika maisha yangu, kununua vitabu na kuvisoma ni kama ugonjwa usiotibika. Leo nilipita tena pale kwenye duka la vitabu, nikaona "seli" bado inaendelea. Nilijitosa tena katika kuchambua vitabu, nikaibuka na kitabu kikubwa sana kiitwacho Beyond Human Nature: How Culture and Experience Shape the Human Mind, kilichotungwa na Jesse J. Prinz. Nilikiangalia, nikafahamu kuwa, kwa kutumia utafiti wa "neuroscience," "psychology," na "anthropology," mwandishi analeta fikra mpya juu ya mambo yanayomjenga binadamu kitabia. Bila kusita, nilikikwapua kitabu hiki. Kitabu chochote kinacholeta fikra mpya ni dhahabu.

3 comments:

babumbwa said...

Prof. Namna ulivyolitumia neno "kwapua" linaleta maana mbaya. Kukwapua ni kuiba au kunyang'anya kitu kwa nguvu. Ninakufahamu kama mwalimu wangu pale "University" ya D'salaam mwaka 1989/90, huwezi kukwapua. Naamini ulikosa neno sahihi kueleza kwamba ulikichukua kitabu hicho kwa hamu kubwa!

Mbele said...

Ndugu babumbwa, umenifurahisha kwa jinsi ulivyolivalia njuga hilo neno "kwapua" nililolitumia. Nakiri kuwa niliteleza, ingawa kichwani sikutambua kuwa nafanya kosa.

Nakiri pia kuwa namna ulivyobainisha kosa langu, sio tu kwamba nimetambua kosa langu, bali pia nimecheka.

Asante sana. Usichoke kunikosoa unapoona nimepotoka.

babumbwa said...

Asante Prof.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...