Uandishi wa ki-Ingereza wa India unafahamika zaidi katika tanzu ya riwaya na hadithi fupi, ingawa waandishi wa mashairi pia wapo, kama vile Kamala Das, Nissim Ezekiel na Jayanta Mahapatra. Leo wanafunzi wangu wa somo la
fasihi ya Asia Kusini walifanya mtihani wa mwisho, na suali moja nililowapa lilihusu shairi la "Catholic Mother," lililotungwa na
Eunice de Souza.
Suali nililowapa ni hili: "Discuss the poem, "Catholic Mother," by Eunice de Souza. Say what you want about it. In addition, compare the woman in this poem with Anil, a key character in Michael Ondaatje's
Anil's Ghost."
Sijui kwa nini, baada ya mtihani kumalizika, nimepata wazo la kulitafsiri shairi hili na kuliweka hapa kwenye blogu yangu. Ingawa lugha aliyotumia mtunzi inaonekana ni ya kawaida tu, ameingiza tamathali za usemi kiurahisi, lakini kwa uhodari na kufikirisha. Amepenyeza na kuchochea uchambuzi wa masuala muhimu ya jamii, kama vile dini, udini na jinsia.
Vile vile, nimekuwa nikiangalia jinsi anavyotumia herufi kubwa na wakati mwingine herufi ndogo. Hili nalo ni suala la kufikiriwa. Kuna kejeli nzuri na ucheshi fulani ndani yake.
Kutafsiri kazi ya fasihi--iwe ni hadithi, riwaya, au shairi--ni suala tata na mtihani mkubwa. Ninajua ninalosema, kutokana na kusoma mawazo ya watalaam na pia kutokana na
uzoefu wangu. Kwa kweli, dhana yenyewe ya tafsiri ni ndoto, kwani lugha zinatofautiana, na tafsiri yoyote ni lazima itofautiane kwa namna mbali mbali na utungo unaotafsiriwa. Hali hiyo inajitokeza katika tafsiri yangu ya shairi la "Catholic Mother."
Msomaji ambaye anafahamu vizuri ki-Ingereza na ki-Swahili ataweza kutambua namna ambayo yeye angetafsiri shairi hili. Ingekuwa vizuri kuona wengine wangetafsiri vipi shairi hili, nami nakaribisha michango hiyo.
Mimi kama m-Mkatoliki nimevutiwa na shairi hili. Nimejikuta nikitabasamu kwa jinsi mshairi anavyotusanifu sisi wa-Katoliki. Mshairi Eunice de Souza ni mwanamke, na ni m-Katoliki kutoka jamii ya wa-Goa. Alizaliwa Pune, India, mwaka 1940. Amestaafu kazi ya ualimu wa ki-Ingereza katika chuo cha Mtakatifu Xavier, mjini Mumbai. Soma hilo shairi lake, na tafsiri yangu:
Catholic MotherFrancis X. D’Souza
father of the year.
Here he is top left
the one smiling.
By the Grace of God he says
we’ve had seven children
(in seven years)
We’re One Big Happy Family
God Always Provides
India will Suffer for
her Wicked Ways
(these Hindu buggers got no ethics)
Pillar of the Church
says the parish priest
Lovely Catholic Family
says Mother Superior
the pillar's wife
says nothing.
---------------------------
Mama m-KatolikiFrancis X. D’Souza
baba wa mwaka.
Yuko hapa juu kushoto
anayetabasamu.
Kwa Neema ya Mungu anasema
tumejaaliwa watoto saba
(katika miaka saba)
Sisi ni Familia Moja Kubwa Yenye Furaha
Mungu Daima Anaruzuku
India Itateseka
kwa Mwenendo Wake Mbaya
(hao wa-Hindu mabwege hawana maadili)
Ni Nguzo ya Kanisa
asema baba paroko
Familia Murua ya ki-Katoliki
asema Mkuu wa Masista
mkewe nguzo
hasemi lolote.