Tuesday, May 31, 2011

Safari ya Bajaji: Lushoto Hadi Irente

Agosti 6, mwaka jana, nilisafiri kutoka Lushoto kwenda Irente. Nilishawahi kusafiri hadi Irente miaka michache kabla, nikitumia teksi. Lakini mwaka jana niligundua kuwa ningeweza kusafiri kwa bajaji. Bajaji yenyewe ndio hii inayoonekana katika picha, na dreva wake. Bajai hii ilikuwa maarufu mjini Lushoto.

Niliziona bajaji kwa mara ya kwanza nilipokuwa India, mwezi Aprili mwaka 1991. Wakati huo hapakuwa na bajaji Tanzania. Lakini kidogo kidogo, miaka iliyofuatia, bajaji zilianza kuonekana, na leo zimejaa katika miji mikubwa kama Dar es Salaam. Sasa zinaonekana hata kwenye miji midogo kama Lushoto. Ndio mambo ya ulimwengu katika utandawazi wa leo.

Safari ilikuwa murua. Bajaji ilikula milima na kukwepa mifereji na mashimo kama mchezo. Tulipofika Irente, nilianza kuwatafuta vijana wawili mapacha ambao niliwafahamu miaka iliyotangulia, wakati nafanya utafiti kuhusu masimulizi juu ya Osale Otango na Paulo Hamisi. Osale Otango na Paulo Hamisi ni maarufu katika historia ya miaka ya hamsini na kitu, walipokuwa wakisakwa na serikali ya wa-Ingereza kwa ujambazi. Walikuwa wakizunguka na kujificha maeneo hayo ya Irente.

Kwa bahati nzuri siku hiyo, hao mapacha walikuwa kijiji cha jirani wakati bajaji yangu ilipofika hapo. Tulifurahi kukutana, tukapandisha njia hadi nyumbani kwao.

Nilipiga picha hii wakati tunateremka kutoka kanisani. Hao marafiki zangu wametangulia. Bajaji ilikuwa imepaki kwenye nyumba zinazoonekana kule ng'ambo. Upande wa kulia, kule ukingoni, ndipo penye mwamba ambapo watalii na wageni wengine hufika kuangalia mandhari ya sehemu hizo na sehemu za mbali. Panaitwa Irente Viewpoint. Kuna picha nyingi za mahali hapo mtandaoni. Ni mahali maarufu kiasi kwamba kama hujafika hapo, inakuwa kama vile hujafika Lushoto.

Hapa ninaonekana nikiwa na hao marafiki zangu mapacha. Kule nyuma yetu ni miamba ambayo nayo imepigwa picha sana na watalii na wageni wanaofika hapa Irente. Kuna miteremko ya kutisha maeneo hayo. Hata mimi ambaye natoka sehemu za milimani, Umatengo, kwenye milima na miteremko, ninatishika na miteremko ya Irente.

Monday, May 30, 2011

Kanisa laingilia kati mauaji ya North Mara

Kanisa laingilia kati mauaji ya North Mara

By George Marato

30th May 2011

CHANZO: NIPASHE

Wiki chache baada ya Jeshi la Polisi Kanda Maalum Tarime na Rorya, kutuhumiwa kuwaua kwa risasi raia watano na kujeruhi wengine kadhaa wakidaiwa kutaka kuvamia mgodi wa North Mara, Kanisa la Anglikana Doyosisi ya Tarime limeitaka serikali kuacha kuingiza siasa katika kutafutia ufumbuzi wa mgogoro huo.

Kanisa hilo limesema mgogoro huo wa muda mrefu kati ya wawekezaji na wananchi wanaozunguka mgodi huo unaomilikiwa na kampuni ya African Barrick Gold, umechangiwa na serikali kushindwa kuchukua hatua za haraka za kuwapatia haki ya msingi wananchi wa eneo hilo.

Akizungumza katika mahojiano maalum na NIPASHE nyumbani kwake juzi mjini Tarime, Askofu wa Anglikana Dayosisi ya Tarime, Dk Mwita Akiri, alisema lazima serikali ibebe lawama kuhusu mgogoro huo na roho za watu zinazopotea kila wakati kwa kushindwa kuchukua hatua za kuwatengea eneo mbadala la uchimbaji wananchi hao.

“Ndio tunakubali sera ya uwekezaji ya serikali na ndio imefanya kuwapo kwa hawa wenzetu wageni katika eneo la Nyamongo na ni faida kwa taifa kwa kupata kodi lakini tunajiuliza serikali inatambua wazi wananchi wa pale miaka yote mashamba yao ni uchimbaji sasa ilitegemea imewanyang’anya maeneo na kuwapa wageni na baada ya hapo nini kifuate kama si kuruhusu uvamizi huo,”alisema na kuongeza.

“Huwezi kumaliza tatizo kwa kuongeza ulinzi wa askari polisi na kufanya matumizi makubwa ya nguvu za dola katika eneo hilo cha msingi hapa serikali imechelewa tu kuchukua hatua za kumaliza mgogoro huu..utaleta majeshi yote lakini ipo siku utakuja kujuta kwani ni hatari kuimba amani wakati vijana hawana ajira na watu wana njaa,”alisema askofu huyo.

Kiongozi huyo wa dini aliwashutumu baadhi ya viongozi wa serikali kwa kutokuwa wa kweli kwa mamlaka wanazowakilisha kuhusu hali ilivyo katika eneo hilo, badala yake wamekuwa wakitoa taarifa za kupika na za uongo ili kuwapendezesha wawekezaji kwa maslahi binafsi.

“Rais akija hapa Tarime anaelezwa mazuri tu ya mwekezaji na jinsi anavyolipa kodi serikalini lakini haambiwi ukweli shida wanazopata wananchi wa eneo hilo na baada ya hapo wanamchukua kiongozi wa nchi bila kumpeleka kwa wananchi wanamwingiza mgodini kisha anaondoka je hapa unatarajia nini,”alihoji kingozi huyo.

Alisema hatua iliyofikia sasa ni lazima serikali ikatambua wazi mgogoro huo ni janga la kitaifa na si la Tarime pekee na endapo itashindwa kuchukua hatua za haraka kumaliza suala hilo kuna hatari eneo hilo likakosa amani, kuongezeka kwa chuki hasa kutokana na ongezeko la watu wanaozidi kupoteza maisha kwa kupigwa risasi.

Kwa mujibu wa Kamanda wa polisi kanda hiyo maalum Constantine Masawe, waliouawa kwa kupigwa risasi na polisi hivi karibuni kuwa ni Chacha Mwita(25)Chacha Ngoka(25)Chawali Bhoke(26)Mwikwabe Marwa(35) na Emanuel Magige(27) ambapo mmoja kati yao mkazi wa wilaya ya Serengeti na wengine wakazi wa wilaya ya Tarime.

+++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++
Mimi mwenye blogu hii napenda kuongezea kuwa kwa taarifa zaidi kuhusu kampuni ya Barrick na mambo yake sehemu mbali mbali za dunia, fuatilia hapa.
+++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++

Thursday, May 26, 2011

Someni kwa Furaha

Wiki kadhaa zilizopita, nikiwa Madison, katika mkutano wa Peace Corps, niliingia katika maktaba ya Chuo Kikuu cha Wisconsin-Madison. Nilifurahi kuingia katika maktaba hii, ambayo niliizoea wakati nasoma katika chuo hicho, 1980-86.

Niliangalia vitabu vya ki-Swahili, ambavyo ni vingi katika maktaba hii, nikavutiwa na vitabu vya Someni Kwa Furaha, tulivyosoma tulipokuwa shule ya msingi.

Nilijikumbusha kuhusu Bulicheka na mke wake Lizabeta, Wagagagigikoko na mfalme wao, Makari Hodari, Kalumekenge, na Pauli mwenye mikono michafu.

Tulibahatika, enzi za utoto wetu, kuwa na vitabu vya kusisimua, vilivyotupa motisha ya kusoma. Vitabu hivi viliandikwa kuzingatia umri wetu. Walimu walikuwa makini, katika kufundisha, kwa mbinu mbali mbali, kama vile nyimbo. Tuliimba alfabeti hadi orodha. Nawasifu na kuwashukuru waalimu wale.

Tuesday, May 24, 2011

Nataka Tanzania Isitawalike Kamwe

Nataka Tanzania isitawalike kamwe. Kama hupendi kusikia hayo, shauri lako. Mimi si mwanachama wa chama chochote cha siasa, ila nataka Tanzania isitawalike.

Nataka Tanzania iwe na viongozi, sio watawala. Wanaotaka kutawala wasipate nafasi hiyo. Uongozi unahitaji busara na ushawishi, kukubalika na jamii husika. Kama ni kutawaliwa, tulitawaliwa na wakoloni. Masultani walikuwa wanatawala. Walikuwa wakandamizaji, sawa na wakoloni. Wazee wetu walipambana hadi Uhuru ukapatikana.

Nataka nchi yetu iimarishe misingi ya Uhuru na demokrasia. Kutawala ni suala la mabavu, kwani hakuna jamii inayokubali kutawaliwa, labda iwe ni jamii ya wajinga, au waoga, au ambao wamelishwa sana kasumba ili wasitambue haki zao.

Lakini jamii inayojitambua, inayotambua maana ya uhuru, haki, na demokrasia, jamii inayothamini na kutetea hayo, haiwezi kutawalika, labda kwa mabavu na vitisho. Itakuwa ni jambo la kuhuzunisha iwapo Tanzania itatawalika. Nataka tuwe macho, tuwe makini, nchi yetu isitawalike, kamwe.

Monday, May 23, 2011

Maktaba ya Mkoa, Kilimanjaro

Tarehe 3 Agosti, mwaka jana, nilikuwa mjini Moshi nikiwa na hamu ya kuufahamu zaidi mji huo. Lengo langu moja lilikuwa kuiona maktaba ya mkoa, kwani nilikuwa sijawahi kufika hapo.

Haikuwa vigumu kufika mahali hapo. Niliingia ndani nikaona kuwa ni maktaba yenye hali nzuri kwa ujumla, kwa upande wa vitabu na majarida, nikifananisha na maktaba kadhaa nilizoziona sehemu zingine za nchi.


Kwa kawaida, ninapoingia katika maktaba za Tanzania, nimezoea kuwaona zaidi wanafunzi. Katika maktaba ya Moshi, niliwaona watu wazima kadhaa wakisoma. Sijui kama hii ndio kawaida katika maktaba hii, lakini niliguswa na jambo hilo.

Kila maktaba duniani, hata kama ni bora namna gani, inahitaji vitabu na majarida mapya muda wote, pamoja na tekinolojia na vifaa vya kisasa vya kupatia maandishi na taarifa. Na ndiyo changamoto kwa maktaba za Tanzania. Nimeona niweke hii taarifa fupi na picha kwenye blogu yangu, ili wengine wapate angalau fununu kuhusu hii maktaba ya Moshi.

Friday, May 20, 2011

"Mama m-Katoliki" (shairi kutoka India)

Uandishi wa ki-Ingereza wa India unafahamika zaidi katika tanzu ya riwaya na hadithi fupi, ingawa waandishi wa mashairi pia wapo, kama vile Kamala Das, Nissim Ezekiel na Jayanta Mahapatra. Leo wanafunzi wangu wa somo la fasihi ya Asia Kusini walifanya mtihani wa mwisho, na suali moja nililowapa lilihusu shairi la "Catholic Mother," lililotungwa na Eunice de Souza.

Suali nililowapa ni hili: "Discuss the poem, "Catholic Mother," by Eunice de Souza. Say what you want about it. In addition, compare the woman in this poem with Anil, a key character in Michael Ondaatje's Anil's Ghost."

Sijui kwa nini, baada ya mtihani kumalizika, nimepata wazo la kulitafsiri shairi hili na kuliweka hapa kwenye blogu yangu. Ingawa lugha aliyotumia mtunzi inaonekana ni ya kawaida tu, ameingiza tamathali za usemi kiurahisi, lakini kwa uhodari na kufikirisha. Amepenyeza na kuchochea uchambuzi wa masuala muhimu ya jamii, kama vile dini, udini na jinsia.

Vile vile, nimekuwa nikiangalia jinsi anavyotumia herufi kubwa na wakati mwingine herufi ndogo. Hili nalo ni suala la kufikiriwa. Kuna kejeli nzuri na ucheshi fulani ndani yake.

Kutafsiri kazi ya fasihi--iwe ni hadithi, riwaya, au shairi--ni suala tata na mtihani mkubwa. Ninajua ninalosema, kutokana na kusoma mawazo ya watalaam na pia kutokana na uzoefu wangu. Kwa kweli, dhana yenyewe ya tafsiri ni ndoto, kwani lugha zinatofautiana, na tafsiri yoyote ni lazima itofautiane kwa namna mbali mbali na utungo unaotafsiriwa. Hali hiyo inajitokeza katika tafsiri yangu ya shairi la "Catholic Mother."

Msomaji ambaye anafahamu vizuri ki-Ingereza na ki-Swahili ataweza kutambua namna ambayo yeye angetafsiri shairi hili. Ingekuwa vizuri kuona wengine wangetafsiri vipi shairi hili, nami nakaribisha michango hiyo.

Mimi kama m-Mkatoliki nimevutiwa na shairi hili. Nimejikuta nikitabasamu kwa jinsi mshairi anavyotusanifu sisi wa-Katoliki. Mshairi Eunice de Souza ni mwanamke, na ni m-Katoliki kutoka jamii ya wa-Goa. Alizaliwa Pune, India, mwaka 1940. Amestaafu kazi ya ualimu wa ki-Ingereza katika chuo cha Mtakatifu Xavier, mjini Mumbai. Soma hilo shairi lake, na tafsiri yangu:


Catholic Mother

Francis X. D’Souza
father of the year.
Here he is top left
the one smiling.
By the Grace of God he says
we’ve had seven children
(in seven years)
We’re One Big Happy Family
God Always Provides
India will Suffer for
her Wicked Ways
(these Hindu buggers got no ethics)

Pillar of the Church
says the parish priest
Lovely Catholic Family
says Mother Superior

the pillar's wife
says nothing.

---------------------------

Mama m-Katoliki

Francis X. D’Souza
baba wa mwaka.
Yuko hapa juu kushoto
anayetabasamu.
Kwa Neema ya Mungu anasema
tumejaaliwa watoto saba
(katika miaka saba)
Sisi ni Familia Moja Kubwa Yenye Furaha
Mungu Daima Anaruzuku
India Itateseka
kwa Mwenendo Wake Mbaya
(hao wa-Hindu mabwege hawana maadili)

Ni Nguzo ya Kanisa
asema baba paroko
Familia Murua ya ki-Katoliki
asema Mkuu wa Masista

mkewe nguzo
hasemi lolote.

Wednesday, May 11, 2011

Nimekutana na Mpiga Debe Wangu

Leo nimekutana na mzee Don Fultz na Mama Eunice Fultz katika mji wa Eagan, Minnesota. Nilienda kule na mfanyakazi mwenzangu wa chuo cha St. Olaf ambaye tunashughulikia programu za kupeleka wanafunzi nchi za nje. Katika picha hizi, Mzee Fultz na Mama Fultz wameketi katikati.

Mzee Fultz ni mchungaji wa kanisa la ki-Luteri, sinodi ya St. Paul. Anaishi hapa Minnesota na Iringa, akiendesha programu za ushirikiano.

Mchungaji Fultz ni mtu wa pekee kwangu. Ni mfuatiliaji makini wa shughuli zangu za kuwaelimisha wa-Marekani na wa-Afrika kuhusu tofauti za tamaduni zao. Ni mpiga debe mkubwa wa kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences.

Tangu wakati kitabu hicho kilipokuwa ni kijimswada tu kisichokamilika, Mchungaji Fultz alikibeba na kukipigia debe hapa Marekani. Hakuwa peke yake katika kufanya hivyo. Nilivyoona hivyo nilishtuka, nikaamua kukifanyia kazi kimswada hiki na kukiboresha.

Kazi hiyo niliifanya kila siku kwa miezi minne, hadi nikakichapisha kitabu mwezi Februari 2005. Mchungaji Fultz alikiandikia makala kwenye kijarida cha kanisa mojawapo hapa Minnesota, mbali na kuendelea kukipigia debe kwenye mikutano mbali mbali na kwa watu binafsi katika maandalizi ya safari za Tanzania. Wa-Marekani wengi wameniambia kuwa walisikia habari za kitabu hiki kutoka kwake. Wengine wamewapelekea nakala wa-Tanzania.

Leo tulikutana kuongelea mambo ya Iringa, kwani ninapangia kuwepo kule kwa wiki mbili mwaka huu na wanafunzi katika programu ya LCCT ambayo ni ya ushirikiano na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Ingawa Iringa niliifahamu vizuri zamani, nimejifunza mengi kutoka kwa Mzee na Mama Fultz kuhusu Iringa ya leo.

Tuesday, May 10, 2011

Kitabu Kuhusu Mwanamuziki Salif Keita

Mchana huu nilikuwa kwenye chuo jirani cha Carleton kuhudhuria uzinduzi wa kitabu kuhusu Salif Keita, kilichoandikwa na Profesa Cherif Keita.

Profesa Keita ambaye anafundisha Carleton anatoka kijiji kimoja na Salif Keita, na walikua wakicheza pamoja utotoni. Ni marafiki hadi leo, na Profesa Keita alishamleta Salif Keita kwenye mji wetu huu wa Northfield kutumbuiza.

Profesa Keita ni mtafiti aliyezama sana katika masuala ya utamaduni, fasihi na falsafa ya jadi ya watu wa Mali. Ndiye hasa mtu anayeweza kutueleza kwa undani kuhusu maisha, sanaa na falsafa ya mwanamuziki Salif Keita.

Salif Keita ni miongoni mwa wanamuziki wa ki-Afrika ambao ni maarufu kabisa. Salif Keita ni albino, na maisha yake tangu alipozaliwa yamekuwa na misukosuko ya kusikitisha. Profesa Keita katika maelezo yake leo alidokezea hayo.

Salif pia ni mwanaharakati katika kutetea haki na maslahi ya albino. Ameanzisha na anaendesha taasisi inayoshughulikia suala hilo. Kiasi fulani cha mauzo ya kitabu hiki kitasaidia taasisi hiyo.

Nimenunua kitabu hiki leo na ninangojea kwa hamu kukisoma. Kama ilivyo kawaida ya blogu hii, Insh'Allah nitaandika habari zake baada ya kukisoma.

Sunday, May 8, 2011

Kikombe cha Mwenyekiti Maggid

Kama sote tunavyojua, wa-Tanzania tuko kwenye awamu ya vikombe. Waganga wamejitokeza nchini mwetu, wakiwa na vikombe vya kuponyesha magonjwa mbali mbali. Wateja wengi wanatoa ushuhuda kuhusu uponyaji wao.

Nami napenda kutoa ushuhuda kuhusu kikombe cha Mwenyekiti Maggid Mjengwa.

Nianze kwa kusema kuwa Mwenyekiti Maggid ni mwalimu, mwandishi na mwanablogu. Hajawa mganga wa kienyeji. Isipokuwa, kikombe ameninywesha. Tega sikio nikuhadithie.

Mwaka 2009 mwanzoni, Mwenyekiti Maggid alianzisha gazeti la Kwanza Jamii, akaniomba niwe mchangiaji. Nilikubali. Sikutambua kuwa nilijipalia mkaa, maana nilijikuta nahangaika kuandika hizo makala na kuzituma kwa muda uliotakiwa.

Ilikuwa ni kazi ya kuumiza kichwa. Kwanza kabisa, wakati mwingine nilikuwa sijui niandike kuhusu nini. Huku siku na saa za kuwasilisha makala zinaendelea kusogea, nami bila kujua mada ya kuandikia, nilibaki nimekodoa macho na jasho linanitoka. Mara kwa mara Mwenyekiti Maggid alikuwa ananiletea ujumbe usiku kwenye saa sita za hapa Marekani ya kati, iwapo nilichelewa.

Tatizo jingine nililopambana nalo ni kuandika kwa ki-Swahili. Nilizoea kuandika kwa ki-Ingereza, lakini kuandika ki-Swahili sanifu ulikuwa ni mtihani wa kuumiza kichwa.

Sisi wa-Katoliki, katika falsafa ya dini yetu, tunatumia dhana ya kikombe kuelezea magumu ya maisha au mateso ambayo Mungu anatuletea tuyakabili. Ni kama tunavyotumia dhana ya msalaba. Mungu ana malengo yake anapotutwisha msalaba maishani.

Napenda niendelee kufafanua falsafa za kidini zinazohusiana na mada yangu. Babu wa Loliondo ametueleza tena na tena kuwa kikombe si kikombe tu bali ni suala la imani, na uwezo wa kutibu ni wa Mungu, si binadamu.

Mungu anaweza kumtumia binadamu yoyote kuleta ujumbe au uponyaji duniani. Kwa imani yangu, ndivyo ilivyokuwa kuhusiana na hiki kikombe cha Mwenyekiti Maggid. Naamini kilipangwa na Mungu. Matokeo ya magumu niliyopitia, ambayo nayaita kikombe cha Mwenyekiti Maggid, yamekuwa mazuri. Makala nilizoandika zilisomwa na bado zinasomwa na watu wengi.

Makala mojawapo, baada ya mimi kuitafsiri kwa ki-Ingereza, ikachapishwa huku Marekani, ilimvutia Chad Brobst, mhariri wa jarida la Monday Developments. Aliiomba, nami nikairekebisha kidogo, akaichapisha. Kila toleo la Monday Developments huteua makala moja kama makala ya mfano. Kwa mwezi Aprili, iliteuliwa makala yangu. Watu wengi sana duniani wataiona.

Vile vile, makala nilizoandika katika Kwanza Jamii nilizikusanya nikazichapisha kama kitabu, CHANGAMOTO, ambacho watu waliokisoma wamekipenda. Ninajivunia kitabu hiki kwa vile ni kitabu changu cha kwanza kwa ki-Swahili.

Nimeshawahi kuandika kuwa wito wa Mwenyekiti Maggid kunitaka niandike makala za ki-Swahili ulisaidia kuniondolea kasumba tuliyo nayo wasomi wengi, ya kutoweza au kutotaka kutumia ki-Swahli ipasavyo. Nilifanya bidii kujiongezea ufahamu wa ki-Swahili. Nilisoma vitabu vya mabingwa kama Shaaban Robert na kujijengea nidhamu ya matumizi ya lugha.

Sisiti kukiri kuwa kikombe alichoninywesha Mwenyekiti Maggid kimechangia kunitibu ugonjwa sugu unaowaathiri wasomi wengi, mbali ya kuwaneemesha walimwengu kama nilivyoelezea.

Thursday, May 5, 2011

Mitaani Namanga, 2007

Ingawa mdogo, mji wa Namanga ni maarufu, kwa vile uko mpakani. Hapa naonekana nikiwa Namanga, upande wa Tanzania. Naelekea kwenye geti la mpaka, hatua chache mbele yangu. Kule mbali unaona Mlima Longido. Barabara inapita kulia kwake, inaingia Longido, nyuma ya mlima, na kuelekea Arusha.

Hii ni moja ya hoteli ambapo napenda kufikia, kwa Bwana Minja, kupata chakula na kinywaji. Nimeshalala hapo.








Nilipendezwa na mpangilio wa nyumba hizi na ile
milima. Hizi nyumba ziko mwanzoni mwa mji wa Namanga, kabla hujafika kwenye geti la mpaka baina ya Kenya na Tanzania.







Nilikuwa Namanga na kikundi cha wanafunzi kutoka Chuo cha Colorado na mwalimu wao, ambao walifika Tanzania katika kozi niliyoiunda, kuhusu mwandishi Hemingway. Hao ni wanafunzi waanzilishi wa kozi hii. Napangia kuibadili kidogo na kuiweka katika program ya Chuo cha St. Olaf.

Hapa nipo upande wa Kenya. Kama mdau unavyoona, mapokezi hayakuwa haba. Ndio mambo ya ujirani mwema hayo.








Namanga, kama ilivyo miji mingine, ina sehemu nyingi ambapo unaweza kupumzika, na kujipatia chakula na pia kukata kiu baada ya mizunguko yako mitaani.

Tuesday, May 3, 2011

Siku ya Waalimu

Leo, huku Marekani, ni siku ya kuwaenzi waalimu. Wiki hii nzima ni wiki ya kuwakumbuka, lakini leo ni kama kilele. Na mimi, mwalimu wa chuo kikuu, nimeshaandika kuwa namwenzi kwa namna ya pekee mwalimu wa shule ya msingi.



Kwa vile ualimu ni sehemu ya nafsi yangu, huwa natafakari suala la ualimu na dhima yake katika maisha yangu na maisha ya wanafunzi. Leo na wiki hii najisikia furaha kujumuika na wale wote wanaothamini mchango wetu.





(Picha ya kwanza hapo juu niliipata kwenye blogu ya Haki Ngowi, ambaye aliripoti kuwa ilipigwa na Brandy Nelson. Picha ya pili sikumbuki niliipata kutoka blogu gani. Ningependa kutoa shukrani).

Monday, May 2, 2011

Watu Wema Wasio na Dini

Katika mizunguko yangu hapa duniani, nimepata kukutana na watu wasio na dini, lakini ni watu wema sana, waungwana. Sio wachokozi au watu wa majungu. Ni waaminifu, wala hawatakudhulumu. Nimefanikiwa kufahamiana na kuishi na watu wa aina hiyo. Wengine wamekuwa wanafunzi wangu huku ughaibuni.

Ukiwauliza kuhusu dini, wanakuambia hawaamini kama kuna Mungu, na hawana dini. Hao watu ni changamoto kubwa kwetu sisi tunaosema tuna dini, hasa pale inapokuwa kwamba hatuwafikii kwa wema na utu. Ni kitendawili. Inakuwaje watu hao wawe hivyo walivyo, wakati hawana dini? Kazi kwenu wadau.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...