Monday, May 28, 2012

Uamsho (Zanzibar): Taarifa kwa Vyombo vya Habari

Jumuia ya Uamsho (Zanzibar) imetoa taarifa kufuatia maandamano na kisha vurugu zilizotokea Zanzibar wiki hii. Nimezipata picha na taarifa kutoka Zanzibar Yetu. Inatia moyo kuona jinsi taarifa hiyo inavyoanza kwa kumtaja Allah na Mtume Muhammad na kisha kusisitiza suala la amani na kuheshimu haki za watu wote. Inatia moyo kuona jinsi taarifa hii inavyotaja wazi kuwa tunawajibika kuheshimiana, kutunza amani, kuheshimu mali na haki za kila mtu, ikiwemo kuheshimu dini na nyumba za ibada. Hayo ni mawaidha mema kabisa.

Ingekuwa mawaidha hayo yanatolewa na kusisitizwa kila wakati, katika mihadhara yote na mahubiri mengine, nje na ndani ya nyumba za ibada, nina imani amani ingedumu katika jamii. Lakini je, mawaidha hayo ndiyo yanayotolewa na kusisitizwa katika mihadhara na mahubiri yote?
Hapa kushoto ni picha mojawapo ya uharibifu uliofanyika wakati wa vurugu za wiki hii, ambapo kanisa lilichomwa moto, sambamba na hilo gari.
Waumini wa dini zote tunaweza kunukuu misahafu na kuthibitisha kuwa dini zetu zinafundisha amani. Lakini jambo la msingi zaidi sio kunukuu na kujadili misahafu, bali matendo yetu katika jamii na mbele ya Muumba. Hiki ndicho kigezo muhimu zaidi cha kupima kama sisi ni waumini kweli.

Taarifa tulizopata katika vyombo vya habari zimesema kuwa maandamano haya ya Uamsho yalikuwa ya kupinga Muungano. Tulisoma pia kuwa wana-Uamsho wanataka kupeleka malalamiko yao Umoja wa Mataifa.

Kilichonishangaza ni jinsi wana-Uamsho walivyojifanya kuwa wao ndio sauti ya wa-Zanzibari. Wanachotaka wao kifanyike. Nashangaa kwa nini wana-Uamsho wawe na msimamo huo, wakati wao ni sehemu tu ya jamii ya Zanzibar na kuna wenzao wenye mitazamo tofauti. Kwa mfano, Sheikh Muhidin Zubeir Muhidin, katibu wa jumuia ya maimam wa Zanzibar (JUMAZA) amenukuliwa kwamba "alisema Jumuiya yake ni tofauti na Jumuiya ya Uamsho hivyo watu wasizichanganye." Soma hapa.

Kwa nini wana-Uamsho wawe na msimamo wao huu hasa wakati huu ambapo wa-Tanzania tuko katika mchakato wa kutafuta maoni kuhusu Katiba na tume imeshaundwa ambayo itasikiliza maoni hayo. Nini kinachowafanya wana-Uamsho wachukue hatua ya kutaka kwenda Umoja wa Mataifa, wakati kuna hiyo fursa ya kuelezea mtazamo wao na kujumuika na wa-Tanzania wengine katika kutafuta suluhu ya matatizo? Kuhusu nani aliyechoma moto kanisa na kufanya uharibifu mwingine, tutajua baada ya uchunguzi kukamilika, na bora zaidi iwapo kesi itafika mahakamani na kuamuliwa.

Baada ya hizo kauli zangu, naleta tamko la Jumuia ya Uamsho:

THE ASSOCIATION FOR ISLAMIC MOBILISATION AND PROPAGATION

P. O. BOX: 1266 
Tel: +255-777-419473 / 434145-
FAX +255-024-2250022
E-Mailjumiki@hotmail.com
MKUNAZINI ZANZIBAR

Tarehe 27MAY2012 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI 

Kila sifa njema anastahiki ALLAH (S.W) na Rehma na Amani zimuendee 
Mtume Muhammad (S.A.W), ahli zake, Maswahaba zake na walio wema katika
Uislamu.

Jumuia ya UAMSHO inatoa taarifa rasmi kwa umma wa Wazanzibari na 
Watanzania wote kwa ujumla kwamba haihusiki na vitendo vyote vya
uvunjaji wa amani vilivyotokea usiku wa tarehe 26 Mei 2012. Kama
alivyosema Mtume (S.A.W) katika Hijatul Wadaa, kwamba ni haramu
kumwaga damu zenu, kuharibiana mali zenu, kuvunjiana heshma zenu ila
kwa haki ya Uislamu (maana yake pale mtu anapofanya kosa na
likathibitika atahukumiwa kwa hukmu ya Kiislamu). Vile vile Uislamu
unaheshimu nyumba za ibada (Makanisa, Mahekalu na n.k) zisivunjwe wala
zisiharibiwe.

Jumuia inatoa wito kwa Waislamu na Wazanzibari wote kuendelea 
kudumisha amani na utulivu wa nchi na kutoharibu mali za serikali,
mali za wananchi, mali za taasisi za dini zenye imani tofauti, kwani
kufanya hivyo ni kwenda kinyume na mafundisho ya dini ya Kiislamu.
Jumuiya inayachukulia matukio yaliyotokea usiku wa jana, na
yanayoendelea tangu alfajiri leo, kama ni njama za makusudi za wale
wasioipendelea amani nchi hii, pamoja na kutaka kuipaka matope jumuiya
na kutaka kuzuia lengo la Wazanzibari kudai nchi yao.

Tunatoa wito kwa Jeshi la Polisi na Vyombo vyote vya Dola wafanye kazi 
zao kama wanavyotakiwa kwa mujibu wa muongozo wa haki za binadamu kwa
Polisi na vikosi vingine unaosema kwamba polisi na vyombo vingine vya
dola wana jukumu la kutunza amani na utulivu na jukumu la kutoingilia
haki za watu. Kila mtu anayo haki ya kuwekewa mazingira muafaka ya
kitaifa na kimataifa yatakayomuwezesha kupata haki zake za binadamu.

Polisi na vyombo vingine vya dola wana jukumu la kutunza amani na 
utulivu na jukumu la kutoingilia haki za watu isipokuwa tu kwa minajil
ya kulinda haki za wengine.

Polisi na vyombo vingine vya dola wana jukumu la kuheshimu, kulinda na 
kutetea haki za binadamu kwa watu wote.

WABILLLAH TAWFIQ 

4 comments:

Christian Sikapundwa said...

Hili si jambo la mzaha kabisa kama hali imefikia katika hatua hiyo,basi Serikali ifike mahali ikemee,kama kweli kuna watu wanamitazamo tofauti kuhusiana na suala la Muungano.
Unajua sisi Binadamu tuna matatizo ya kutochanganua baya na zuri,Muungano ndiyo umefanya Wa- Pemba wengi wako Dar es Salaam na nimatajiri wakubwa,kwa kuwa kwao wana zao la karafuu,lakini Pemba yenyewe kutokana na hali Pemba ilivyo ingewawia vigumu kuwekeza pale.
Sasa huo 'Uamsho ( Zanznibar) unasahau kuwa kuna ndugu zao wakao Dar es Salaam kwa amani na utulivu kwa sababu ya Muungano.Hivyo leo itolewe amri kuwa Wapemba warudi kwao watafurahia ?.Kuna kazi ya ziada.Prf.Unadhani ni kwanini hali inafikia hapo ? Unadhani ni nani na kwa mazingira gani aweze kuzima moto huo wa vikundi vinavyo ibuka kila kukicha vinavyoa ashiria utovu wa Amani katika Taifa letu linalo jilikana kama kisima cha Amani ?.Nakushukuru kwa taarifa kama hizi.Mungu akubariki sana.

Mbele said...

Inavyoonekana, kuna mengi yataibuka kuhusiana na suala hili. Kwa mfano, kuna taarifa kuwa CCM inataka Jumuia ya Uamsho ifutwe usajili. Soma hapa.

Anonymous said...

ndio upeo wa watz siku zote....hivi hao viongozi wakiristo huko zenji wajinga km mnavyodhania,walipize kisasi cha na dili limepangwa pamoja nao?
makanisa yamechomwa na wanaccm kwa kusaidiwa na kulindwa na usalama wa taifa-baada ya hao maaskofu kufahamishwa mtego ulivyo,kuhakikishiwa dili,
ndio hawakua na wasiwasi coz wanajua watajengewa na fidia.....mradi mnono wa watu.......kakanisa hakana mbele wala nyuma unaambiwa hasara m120 !!!
msikubali kirahisi kutumbukizwa ktk chuki za kidini-na kutimiza malengo ya wanaotegeneza migawanyiko hiyo kwa ajenda zao.

Mbele said...

Anonymous, shukrani kwa kupita hapa kwangu na kuweka maoni.

Pamoja na kwamba watu wanaweza kuwa na hisia na dhana mbali mbali kuhusu matukio haya, naona kwamba jambo linalotakiwa ni kufanya uchunguzi wa kina. Pawepo na tume huru ya uchunguzi na hapo ndipo tutapata ukweli wa nini kilichotokea, na kwa nini, na wahusika ni akina nani, na namna ya kuondoa tatizo ni ipi, na kadhalika.

Uchunguzi utakaotupa ukweli kamili wa hayo ndio jambo pekee litakalotuweka mahali pazuri. Kama sisi ni waumini wa dini, tunapaswa kukubaliana hivyo, maana dini zetu zinataka tuwe watu wa kuzingatia ukweli.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...