Tuesday, February 17, 2015

Tatizo si Lugha ya Kufundishia, ni Uzembe

Jana, katika blogu hii, mdau mmoja aliniomba niandike makala kuhusu lugha ya kufundishia nchini Tanzania. Aliandika hivi:

Prof Mbele. Pole na kazi za kila siku.
Ningependa kujua nini maoni yako kuhusu kutumia kiswahili kama lugha kuu ya kufundishia mpaka chuo kikuu. Je unalionaje hili, unaona kutakuwa na athari zozote kutokana na elimu?. Je ni kweli tutakuwa tumejitenga na dunia?.

Ningeomba kama ungepata nafasi basi ukaliandika hili kama post katika blog na wala si comment. Nakutakia siku njema


Kwa kweli mada hii ya lugha ya kufundishia Tanzania imejadiliwa sana, katika vitabu, majarida, magazeti, mitandao, mikutano, na kadhalika. Siamini kama ninaweza kusema lolote ambalo halijasemwa. Hata hivi, nina mtazamo wangu, kama watu wengine.

Ninaamini kwa dhati kuwa tatizo si lugha ya kufundishia bali uzembe. Ingekuwa watu wanatambua umuhimu wa elimu, kwa maana halisi ya elimu, hawangekuwa wanatoa visingizio au lawama kama wanavyofanya. Hawangekuwa wanatumia muda wao katika kulalamika. Wangeelekeza nguvu zao na akili zao katika kutatua matatizo yoyote na kusonga mbele.

Kwamba mwanafunzi anafanya vizuri akifundishwa kwa lugha yake, ni hoja inayovutia, lakini sina hakika kama ninaikubali sana. Ingekuwa ninaikubali sana au kabisa, ningesema basi tuwafundishe watoto wetu kwa ki-Nyakyusa, ki-Sukuma, ki-Yao, na kadhalika. Kwa wengi, ki-Swahili ni lugha yao ya pili. Sisi hatukufundishwa kwa lugha mama, bali tulifundishwa kwa lugha ngeni ya ki-Swahili na baadaye ki-Ingereza, na hatukutetereka. Kwa nini mambo yawe kinyume leo, kama si uzembe?

Kama lugha ya ki-Ingereza ni tatizo, jawabu ni kufanya bidii kujifunza lugha hiyo. Kusema kwamba tuache kufundishia kwa ki-Ingereza eti kwa vile ufahamu wa ki-Ingereza ni mdogo ni kuhalalisha uzembe. Kinachotakiwa ni kufanya bidii kujifunza lugha hiyo kama tulivyokuwa tunafanya sisi.

Uzembe umetufikisha hapa tulipo. Kwa nini majirani zetu wa Malawi, Kenya, na Uganda hawatoi visingizio kama wanavyotoa wa-Tanzania? Ki-Ingereza sio lugha ya wenzetu hao, bali ki-Chewa, ki-Yao, ki-Ganda, ki-Acholi, ki-Kamba, Kikuyu, na kadhalika, kama ilivyo kwetu ki-Pare, ki-Luguru, ki-Makonde na kadhalika.

Kwa nini hao majirani zetu wawe wanatumia ki-Ingereza hadi chuo kikuu bila malalamiko kama wanayotoa wa-Tanzania? Enzi zetu, tulikuwa tunasomeshwa kwa ki-Ingereza sekondari (au kabla?)na kuendelea. Tulisoma chuo kikuu na hao wenzetu kutoka nchi za jirani, kwa ki-Ingereza bila matatizo. Leo ki-Ingereza kimekuwa shida. Ni nini kimetokea, kama si uzembe?

Ingawa nina mengine ya kusema, ninaamini kuwa blogu ni mahali pa makala fupi fupi, tofauti na kitabu. Kwa leo naona niishie hapa. Nitaendelea kuandika, ili kuongelea vipengele vya ujumbe wa mdau ambavyo sijavigusia hapa.

9 comments:

Anonymous said...

Prof Mbele, nashukuru kwa makala hii, nadhani huu ni mtazamo mpya kwangu. Kama ulivyosema, kuwa tatizo la elimu yetu ni uzembe wala si lugha nakuunga mkono kwa kiasi kikubwa. Uzembe umetamalaki kila mahali hapa Tanzania.

Lakini zaidi ya uzembe, watafiti wanaonesha kuwa lugha inauhusiano mkubwa na uwezo wawatu kuelewa na kuelimika. Kusoma lugha na kuielewa ni uwezo kama wa kujua hisabati na masomo mengine. Lugha mama itumikapo kuelimisha jamii ni rahisi pia kueleweka, na pia ndio hutumika kwa kiasi kikubwa kufikiri.

Mbele said...

Ndugu Anonymous, nawe shukrani kwa ujumbe. Sina namna ya kujua kama ni wewe ndiye uliyenihamasisha kuandika kuhusu mada hii, lakini hakuna tatizo.

Nami nazifahamu hizi nadharia za kitaaluma kuhusu lugha na fikra ("language and thought"), lugha na uelewaji ("language and understanding"), lugha na maana ("language and meaning"), na kadhalika.

Lakini tukiangalia suala hili kwa mtazamo wa nadharia za kichokozi kama za "deconstruction," ambazo zinahoji karibu kila kitu kinachoonekana kuwa ndio ukweli, basi tunaweza kujiuliza masuali magumu. Kwa mfano, je inawezekana kwa lugha yoyote au neno lolote kumaanisha chochote? Ni weli kwamba kuna uhusiano baina ya neno na kile kinachomaanishwa na neno hilo? Au tuseme kuwa haya maneno tunayotumia, na lugha kwa ujumla, si chochote bali makubaliano tu yasiyo na mantiki wala uhalisi zaidi ya hapo. Kwa Kiingereza neno lolote au lugha yoyote ni "arbitrary, a matter of convention."

Kwa hivi tunaposema tunatumia lugha ili kuwasiliana au kuelewana, au tunaposema lugha fulani ndiyo inaweza kuleta ufahamu wa jambo fulani, huwa tunaelea juu juu tu.Hatuzami katika utata wa masuala yenyewe.

Ila, katika maisha na mijadala yetu, tunamezea masuala hayo, au yako nje ya upeo wetu, na badala yake tunajidanganya kwamba, kwa mfano, lugha yangu ya kwanza inaweza kunifanya nielewe somo zaidi kuliko lugha nyingine. Hayo ni makubaliano tu; hayana uthibitisho. Tunaishi kwa hizo imani, basi. Hizo ni baadhi ya hizo nilizoziita nadharia za kichokozi, za watu kama Jacques Derrida.

babumbwa said...

Lugha ya kufundishia hapa Tanzania kwa shule ya msingi-darasa la kwanza mpaka la saba ni kiswahili kwa masomo yote(isipokuwa somo la kiingereza) tungetegemea wanafunzi wangekuwa wanafanya vizuri sana kwenye mitihani yao! lakini sio hivyo. Ufaulu wao umekuwa wa chini sana. Na kwa somo la hisabati mambo ni mabaya sana! kwa hiyo kisingizio cha lugha ya kufundishia ni duni sana. Watanzania na serikali yetu tumeshindwa kuwekeza kwenye Elimu! tunataka kuvuna bila kupanda.

Anonymous said...

Ndio ni mimi, na niliomba maoni yako nikiamini kama mtaalamu wa lugha nitajifunza kitu kipya na kweli nimejifunza.

Naona Babumbwa ameongezea kwa mfano halisi katika elimu yetu, hili linaendana na uzembe. Nikirudi katika hoja ninamifano mingine ambayo iko wazi.

Nayo ni kuwa, kuna utetezi ambao uko upande wa hoja, kuwa hakuna nchi duniani imeendelea kwa kutumia lugha ya kigeni. Kwani pamoja na siasa zao na misingi ya kitaifa, lakini uvumbuzi na changamoto za kutatua matatizo waliyonayo nikutokana na msingi wa elimu walioipata.
Hapa watetezi wa hoja hii wanahusisha lugha kama moja sababu. Lakini sasa kwa kutumia hoja yako ya kuwa kama tatizo la elimu yetu ingekuwa ni lugha basi tungejifunza kwa kisukuma, kihaya au kisafwa kabla ya kuzunguzia kiswahili kwani kiswahili sio lugha mama ya watanzania wengi.

Mbele said...

Ndugu babumbwa,naungana na Ndugu Anonymous katika kukubaliana na hoja yako. Umeiweka hoja yako kwa uwazi na ufasaha.

Kwa mtazamo wangu, suala hili, kama yalivyo masuala mengine yoyote ya jamii, hayana ufumbuzi rahisi. Jawabu tunaloweza kutoa huwa ni chimbuko la masuali zaidi.

Kwa hali hii, tuna wajibu wa kuendelea kutafakari na kubadilishana mawazo. Hakuna mtu anayeweza kudai kuwa yeye ndiye pekee mjuzi.

Ndio maana mimi hupenda kuwasikiliza wengine na kujifunza kutoka kwao. Nawashukuruni kwa kuchangia mada hii hapa kwenye blogu yangu. Insh'Allah, nitaandika makala nyingine au zingine siku zijazo.

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Kaka Mbele hujakosea kusema ni uvivu. Bila kuwekeza kwenye elimu yote ni bure. Isitoshe, Kiingereza kwa sasa si lugha ya waingereza tena bali ya dunia-tandawazi. Hata EAC pekee inahitaji Kiingereza kuliko hicho Kishwahili. Huwezi kuwa na walimu wasiolipwa vizuri wala kufanya kazi kwenye mazingira mazuri ukawa na ufaulu. Huwezi kuendekeza ufisadi na wizi wa mali ya umma ukafaulu. Kama lugha ni tatizo basi fundisheni kwa lugha za kikabila muone. Nadhani hivi ni visingizio na kutapatapa ukiachia mbali kuwa usanii wa kitoto. Acheni ufisadi na muanze kuongoza kwa mifano. Viongozi kama vile rais andikeni vitabu badala ya kuandikiwa utadhani maiti. Watu hawana motisha hasa tokana na ukweli kuwa baada ya wahalifu kuukata bila kuulizwa kila mtu anataka aukate bila kujali kama ni kihalali au kwa njia haramu. Vijana wanatamani wauze unga au kuwa wasanii na wanasiasa au majambazi ili waukate. Nyerere aliongoza nchi kwa mfano kiasi cha kuzalisha kizazi cha wasomi ambao nao wamemgeuka kwa ujinga wao toka na kutoelimika vilivyo. Tunapaswa kubadilika. Unafiki utajitokeza wakubwa watakapowapeleka watoto wao ima kwenye English Media Schools au nje huku wachovu wakiachwa na Kiswahili na uswahili wao. Aliyebuni wazo hili hakika ni mtu wa kuogopwa kama ukoma maana hajaona hali halisi ya mambo na jinsi dunia inavyokwenda kwa sasa.

Mbele said...


Ndugu Mhango, shukrani kwa ujumbe wako. Nami naamini kwa dhati kuwa hao wanaotunga sera hawasmini kwa dhati yale wanayosema.

Enzi zile walipoanza kukipigia debe ki-Swahili, nilikuwa nafundisha Chuo Kikuu Dar es Salaam. Ni miaka ilipozuka na kushamiri jadi inayojulikana kama "tuition."

Niliona watoto wa vigogo walivyokuwa wanakimbilia kwa walimu kwa "tuition" ya ki-Ingereza.

Hadi leo, kama ulivyogusia, watoto wa vigogo utawakuta kwenye hizi shule zinazotumia ki-Ingereza, na wengi unawakuta katika vyuo vya huku Marekani. Watoto wa wakulima, wafugaji, na wavuvi ndio watasota katika hizi shule za ki-Swahili, na ndio watakaoambulia patupu katika kushindania ajira katika ulimwengu wa utandawazi wa leo.

Ingekuwa kuna mkazo katika elimu ya kujitegemea, ingekuwa kuna mkazo katika elimu ya ujasiriamali, na ingekuwa serikali ina nia ya dhati ya kuwafundisha na kuwasaidia vijana kujiajiri, mambo yangekuwa afadhali kiasi.

Lakini kuhusu hili suala la lugha, kuna usanii unaofanyika kisera, na matokeo yake yalishaanza kujitokeza. Leo ukiangalia Tanzania, ajira nyingi zinachukuliwa na wa-Kenya. Nimejionea hayo katika sekta ya utalii, ambayo tunaambiwa ndio sekta inayokua kwa kasi kuliko zote hapa duniani.

Deo Ngonyani said...

Profesa Mbele, ningependa kuungana nawe kulaani uzembe uliofanywa katika elimu Tanzania kwa miongo kadha sasa.
Nimewahi kuandika kwamba Kiswahili kimekuwa kisingizio cha kuanguka kwa elimu. Kwa maoni yangu, tatizo lilikuwa uwekezaji mdogo katika elimu. Mojawapo ya matokeo ya jambo hilo ni ufundishaji mbaya si wa masomo mbalimbali tu, bali pia mitaala hafifu na ufundishaji hafifu wa lugha. Hakuna vitabu, mafunzo duni ya walimu, na je, tumesahau kwa miongo kadha ualimu ni kazi ya watu waliofeli? Hilo halikuonekana kwa Kiswahili mpaka hivi karibuni. Soma tu magazeti, blog na mitandao mbali mbali utabaini kwamba matumizi ya Kiswahili sasa hivi ni kashfa ya kutisha na kutia aibu kubwa kwa nchi inayojitangaza kama namba wani katika Kiswahili. Uzembe umetufikisha hapa tulipo: Leo hii, baada ya kujifunza Kiingereza kwa miaka zaidi ya 10 wanafunzi bado wanajikuta hawawezi kutunga sentensi ya Kiingereza, hawawezi kuchukua kitabu wakisome na kupata pointi, hawawezi kufanya mawasilisho yoyote kuelezea jambo lolote si kwa Kiingereza, bali hata kwa Kiswahili. Si tatizo la lugha tu. Ni mfumo mzima wa elimu umesambaratika. Kiswahili ni kisingizio tu.

Sitasema lolote kwa sasa kama uamuzi wa kufanya Kiswahili lugha ya kufundishia kama ni jambo la busara au la. Panapo majaliwa, ninataka hasa kujibu maswali manne:
1. Je, wataalamu wa elimu, makuzi na lugha wanatuambia nini juu ya lugha ya kufundishia? Na tajriba zetu zinatufundisha nini?
2. Je, nchi zinazofanya vizuri katika elimu duniani zinatumia lugha gani kufundishia?
3. Je, nchi zilizofanya vizuri sana katika uchumi na viwanda, Asian Tiger, wanatumia lugha gani kufundishia?
4. Je, nchi zilizoendelea za huko Yuropa zinatumia mfumo gani wa mitaala ya lugha katika mashule yao?
Ninaamini kwamba lugha tunayoichagua inaakisi na pia inaunda mtazamo wetu na jinsi gani tunavyojiona tunaweza kusonga mbele.

Mbele said...


Profesa Ngonyani, nafurahi kuona umepiga hodi hapa katika blogu ya hapakwetu. Tunahitaji mawazo ya kila mtu, katika hili jukumu la kutafuta ukweli na kuelimishana. Na nyinyi wafundishaji na watafiti wa masuala ya lugha mnaweza kutufikisha mbali katika safari hii.

Kuna jambo umeligusia, ambalo limenipa hamu ya kuandika makala siku si nyingi zijazo. Ni kuhusu vitabu vya mitaala, suala ambalo nimekuwa nikilifikiria kwa miaka mingi. Nitajaribu kuandika makala ndogo kama hizi zingine, ili kuendelea kuchochea mjadala.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...