Sunday, August 9, 2015

Shaaban Robert na Mbaraka Mwinshehe Waliongelea Umuhimu wa Shule

Nikiachilia mbali jinsi wazazi wangu walivyohimiza elimu, nikiachilia mbali jinsi Mwalimu Nyerere alivyohimiza elimu, naukumbuka kwa namna ya pekee mchango wa mwandishi Shaaban Robert na mwanamuziki Mbaraka Mwinshehe katika kuhimiza elimu.

Ninakumbuka jinsi baba yangu, nilipokuwa shule ya msingi, alivyokuwa ananitia msukosuko iwapo nilishindwa kupata 100% katika zoezi lolote au mtihani wowote. Ninakumbuka pia jinsi Mwalimu Nyerere alivyokuwa anahimiza elimu, kwa watu wote, kuanzia watoto hadi wazee, kama nilivyowahi kuandika katika blogu hii.

Shaaban Robert ni mtu anayenifanya nimkumbuke baba yangu. Nilijionea hayo niliposoma kitabu kiitwacho Barua za Shaaban Robert, ambacho habari zake niliziandika katika blogu hii. Humo tunaona jinsi Shaaban Robert alivyokuwa anamhamasisha mdogo wake Yusuf Ulenge afanye bidii katika elimu, akimtimizia mahitaji yote ya shule. Kwa wazazi na walezi, Shaaban Robert ni mfano wa kuigwa.

Mbaraka Mwinshehe, mwanamuziki ambaye wakati wa ujana wangu alitingisha Afrika Mashariki, ya Kati, na Kusini kwa nyimbo na muziki wake, aliimba wimbo maarufu wa kuwaasa vijana wazingatie elimu. Wimbo huo, "Enyi Vijana Sikilizeni," unaweza kuusikiliza hapa:

https://archive.org/details/EnyiVijanaSikilizeni

2 comments:

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Kaka Mbele usemayo ni kweli, kwani bila elimu maendeleo ya jamii au mtu husika yanakuwa haba au siyo endelevu. Magwiji uliowataja waliona mbali hata kama walikuwa na elimu kidogo. Hata baba yako najua hakuwa na PhD. Lakini bado aliweza kumtengeneza mtu mwenye PhD. Wakati mwingine huwa nashindwa kuelewa kati yetu na hao walitugeneza nani msomi zaidi. Nasema hivyo kwa vile wameweza kututengeneza. je sisi tutawatengeneza wanetu kama walivyotutengeneza waliotutengeneza. Umenikumbusha mwalimu Nyerere. Kwa taarifa yako nilitumia sera yake ya viwanda katika kitabu changu kutaka Afrika iifuate na hoja hii imepita hadi profesa aliyehakiki mswada wangu kuniomba tuandike Manifesto ya Afrika pamoja. Kama siku zingekuwa zinarejeshwa nyuma na watu wakaona mbele, tuliosoma chini ya mwalimu Nyerere huenda tungesoma kwa woga wa kinachotungojea hadi tukaehuka. Hata hivyo Mungu amlaze mahali pema peponi pamoja na wazazi wetu na magwiji uliowataja.

Mbele said...

Ndugu Mhango

Shukrani kwa mchango wako. Baba yangu (marehemu sasa) alikuwa amesoma shule ya msingi. Lakini alikuwa mwenye busara kubwa. Watu kule nyumbani kwetu walikuwa wanamtafuta kwa ushauri kuhusu masuala mbali mbali. Alikuwa hakimu katika mahakama akitumia busara, mila na desturi za jadi, katika kuhukumu kesi. Alikuwa anatafutwa huko na huko kwa shughuli ya ushenga. Yaani alikuwa anahitajika kama mwakilishi wa familia mbali mbali ambazo vijana wao walikuwa wanataka kuoa.

Papo hapo, alikuwa anatubana watoto wake tuwe makini shuleni. Nakumbuka hayo niliyosema, kwamba kama aliona nimeshindwa kupata 100%, alikuwa anahoji, hata kama nilipata 95%. Alinihakikishia kuwa kuhusu utafutaji wa elimu, niende popote duniani, hata Marekani. Ni ajabu kwamba ndivyo ilivyokuwa. Nilikuja Marekani kusomea hiyo Ph.D.

Siwezi kusema nina busara kama za baba yangu, pamoja na elimu yangu yote ya shuleni. Ila daima ninamkumbuka kwa jinsi alivyonishinikiza niwe mwanafunzi bora.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...