Saturday, February 27, 2016

Nimezuru Nyumba ya Hemingway, Oak Park

Leo nilizuru nyumba ya Hemingway, kitongoji cha Oak Park, karibu na Chicago. Kwa miaka kadhaa, nilikuwa nimewazia kufanya hivyo.  Nyumba hii ambayo ni namba 339 katika mtaa wa Oak Park Avenue, ndimo alimozaliwa Ernest Hemingway na kuishi hadi alipokuwa na miaka sita. Sasa ni nyumba ya hifadhi ya mambo mengi ya familia ya Hemingway.

Nimejifunza mengi katika kutembelea nyumba hii.  Nilipoingia, nilijumuika na wageni wengine wanne, tukafanya ziara pamoja, tukiongozwa na dada aliyejitambulisha kwa jina la Michelle ambaye anaonekana pichani. Alitupitisha sehemu zote za nyumba hii, akatuelezea historia yake na habari za vitu vilivyomo.

Alituelezea mambo muhimu yaliyomlea Ernest Hemingway katika nyumba hii. Mfano ni namna mama yake alivyotaka kila mtoto na mtu mwingine katika nyumba hii awe na ujuzi wa muziki. Kabla ya ziara hii, nilijua kuwa mama yake Ernest Hemingway alitaka Ernest ajifunze muziki, lakini sikujua kuwa alitaka hivyo kwa kila mtoto na wengine pia. Ziara hii pia imenifungua macho kuhusu namna mtindo wa usimuliaji hadithi aliokuwa akitumia Ernest Hemingway ulivyojengeka tangu utoto wake katika nyumba hii.

Friday, February 26, 2016

Jumuia ya Vyuo (ACM) Yakihitaji Kitabu

Leo nimeshinda hapa mjini Chicago nikihudhuria mkutano wa bodi ya programu ya Tanzania ya ACM. ACM ni jumuia ya vyuo vikuu 14 vya hapa Marekani ambayo inaendesha programu za masomo na utafiti sehemu mbali mbali za dunia. Kwa upande wa Afrika, kuna programu ya Tanzania na programu ya Botswana. Mimi ni mjumbe katika bodi za programu hizi mbili.

Mkutano kama wa leo tunafanya mara moja kwa mwaka kwa program ya Tanzania na vivyo hivyo kwa programu ya Botswana. Kila mwaka tunapeleka wanafunzi kwenye nchi hizi kwa muhula moja. Tunapokutana tunatathmini mwenendo wa masomo kwa mwaka husika. Tunapitia ripoti mbali mbali na kuzijadili, kubaini mapungufu na mafanikio na mapungufu, kutoa mapendekezo na kujiwekea malengo.

Leo, pamoja na yote hayo, limetokea jambo ambalo sikutegemea. Profesa Paul Overvoorde, aliyeambatana na wanafunzi Tanzania muhula uliopita, alianza hima kunieleza kuwa alikuwa ametumia kitabu changu cha Africans and Americans Embracing Cultural Differences na kilimsaidia sana katika kuendesha programu. Profesa huyu nilikuwa sijawahi kuonana naye, kwa sababu sikuwa nimehudhuria mikutano yetu kwa miaka mitatu. Alivyokuwa anaelezea kitabu hiki, nilijikuta nina hisia mchanganyiko: shukrani, furaha, na mshamgao.

Kama vile hii haikutosha, wakati wa mkutano, Profesa Karl Wirth naye akakitaja kitabu hiki. Huyu tumefahamiana tangu miaka ya mwanzo ya programu hizi. Wakati tulipokuwa tunahitimisha mkutano alitoa wazo kwa uongozi wa ACM kuwa kitabu hiki kifanywe msingi wa "webinar" itakayovihusisha vyuo vyetu vyote kwa ajili ya kufundishia mambo yiliyomo, na hii iwe ni mkakati wa kuwavutia wanafunzi kwenye programu.

Wazo hili limeshapita. Wakati wajumbe tulipokuwa tunaagana, mhusika wa tekinolojia za mawasiliano katika ACM aliniambia kuwa atanitafuta ili nichangie hiyo "webinar." Nami nilimwambia nangojea kwa hamu kushirikiana naye, kwani ninamini kuwa nitajifunza mambo mapya.

Nimeandika habari hii kwa sababu maalum. Kwanza ni kujiwekea kumbukumbu, kama ilivyo desturi yangu katika blogu hii. Pili ni kwa sababu ninawakumbuka watu kadhaa ambao wamejaribu kuzibeza juhudi zangu, nami nikawa siyumbishwi. Ninafanya shughuli zangu kwa bidii na umakini niwezavyo na baada ya hapo ninayathamini matokeo yake. Mtu lazima ujiamini na ujithamini. Ukithamini kile unachokifanya. Ukiwa na mtazamo huu, huwezi kuyumbishwa. Matokeo yanakuja kuonekana baadaye. Chambilecho wa-Swahili wa zamani mgaagaa na upwa, hali wali mkavu.

Tuesday, February 23, 2016

"So Long a Letter" Katika Kozi ya "Muslim Women Writers"

Kozi yangu ya Muslim Women Writers inaendelea vizuri. Tulianzia India, na hadithi ya Sultana's Dream ya Rokeya Sakhawat Hossain. Baada ya hapo tunasoma So Long a Letter, utungo wa Mariama Ba wa Senegal, nchi mojawapo maarufu katika uwanja wa fasihi ya Afrika.

Senegal imetoa watunzi kama Leopold Sedar Senghor, Cheikh Hamidou Kane, Birago Diop, na Sembene Ousmane, kwa upande wa wanaume, na kwa upande wa wanawake kuna watunzi kama Aminata Sow Fall na Mariama Ba.

So Long a Letter ni utungo ulioandikwa kwa mtindo wa barua, ambayo mhusika mkuu anamwandikia mwanamke mwenzake, rafiki yake. Kwa hali hiyo, utungo huu unafuata jadi ambayo wanafasihi huiita "epistolary." Neno "epistolary" linatokana na neno la ki-Latini ambalo maana yake ni barua.

Suala moja muhimu linaloongelewa ni la wake wenza. Ni suala lenye chimbuko lake katika Qur'an, Sura iv aya 3:

     If ye fear that ye shall not
Bes able to deal justly
With the orphans,
Marry women of your choice,
Two, or three, or four;
But if ye fear that ye shall not
Be able to deal justly (with them),
Then only one, or (a captive)
That your right hand possess.
That will be more suitable,
To prevent you
From doing injustice.

Yusuf Ali, ambaye tafsiri yake ya Qur'an nimeinukuu hapa juu, anafafanua aya hii vizuri. Anakumbushia kwamba aya hii ilitokea katika mazingira maalum, ambamo kutokana na vita ya Uhud, jamii ya wa-Islam ilikuwa na wajane na yatima wengi, pamoja na mateka wa vita. Ilikuwa lazima watu hao watendewe kwa ubinadamu na haki kwa kiwango cha juu kabisa. Ruhusa ya kuwaoa wajane hao imewekewa masherti.

Kabla ya u-Islam, watu walikuwa wanaoa walivyopenda, lakini aya hii inaweka mipaka. Mtu anaweza kuoa hadi wake wanne, si zaidi, lakini kama Yusuf Ali anavyosema, "provided you could treat them with equality, in material things as well as in affection and immaterial things." Yaani masherti ni kwamba uweze kuwatendea wake hao kwa usawa katika mahitaji ya vitu, katika upendo, na mengine ya aina hiyo.

Kutokana na masherti hayo, Yusuf Ali anasema: "As this condition is most difficult to fulfill, I understand the recommendation to be towards monogamy." Yaani, kwa jinsi masherti yalivyo magumu kutekelezeka, nachukulia kwamba agizo hili linaegemea kwenye kuwa na mke moja.

Huu ndio msingi katika Qur'an wa suala la mitara. Wanawake wa-Islam wamekuwa wakilalamika kwamba fundisho la Qur'an limepotoshwa. Wanaume wamejitwalia mamlaka ya kupindisha mafundisho ya Qur'an na kuhalalisha mambo wanayoyapenda wao.  Hii ndio hali inayojitokeza katika So Long a Letter.

So Longer a Letter ni andiko linalohuzunisha kwa jinsi Ramatulaye anavyoelezea roho mbaya ya baadhi ya wanaume. Mume wake mwenyewe alijiolea binti kinyemela, na wanawake wengine wanakutana na adha za aina hiyo. Lakini, hasemi kuwa wanawake muda wote hawana dosari. Anakiri kuwa katika ndoa zingine, wanawake wanawatesa wanaume.

Hatimaye, So Long a Letter inaelezea matumaini ya kubadili mambo na kuwawezesha wanawake kushika nafasi wanazostahili katika jamii, wakitumia vipaji ambavyo wanavyo.

Friday, February 19, 2016

"Tenzi Tatu za Kale:" Makala Inayosomwa Kuliko Zote

Mara kwa mara, ninaangalia takwimu zinazohusu blogu yangu hii: idadi ya watembeleaji, makala wanazozitembelea, na nchi walimo. Kuanzia wiki kadhaa zilizopita, makala inayotembelewa kuliko zote ni "Tenzi Tatu za Kale." Idadi ya watembeleaji iliongezeka ghafla pale Ndugu Michuzi alipoiweka makala hii katika blogu yake.

Ninajiuliza kwa nini makala hii inawavutia wasomaji namna hii. Je, hii ni ishara ya kupendwa kwa somo la fasihi ya ki-Swahili? Siamini kama ni hivyo, kwani ninaandika makala nyingi kuhusu fasihi, ambazo zinagusia tungo mbali mbali. Ingekuwa uwingi wa wasomaji unaonekana kwenye makala hizo pia, ningeamini kuwa kuna msisimko wa kupenda fasihi.

Ninapata hisia kwamba labda uhusiano na mahitaji ya shuleni au vyuoni. Ninahisi kuwa labda wanaosoma makala ya "Tenzi Tatu za Kale" ni wanafunzi ambao wanatakiwa kusoma Utenzi wa Al Inkishafi, au Utenzi wa Mwana Kupona, au Utenzi wa Fumo Liyongo: moja, mbili, au zote tatu.

Kama ni hivyo, si jambo la kuridhisha wala kufurahisha. Uwanja wa fasihi ya ki-Swahili ni mpana, na mwenye mapenzi na fasihi hii ninamtegemea awe anasoma tungo nyingi. Hata wanafunzi wa fasihi wanatakiwa kusoma tungo mbali mbali, si zile zilizomo katika mitaala tu.

Ningependa sana kuona mijadala ya fasihi ya ki-Swahili katika blogu hii. Ndio maana ninaweka taarifa mbali mbali kuhusu tungo za ki-Swahili. Tuienzi fasihi hii kwa kuisoma bila mipaka, kuichambua, na kuitangaza.
 

Tuesday, February 16, 2016

Tumeanza Kujadili "Sultana's Dream" na U-Islam

Katika siku chache zilizopita, nimesoma Sultana's Dream, hadithi iliyotungwa na Rokeya Sakhawat Hossain aliyeishi 1880-1932 nchi ambayo leo ni Bangladesh. Sultana's Dream ni kianzio cha kozi yangu ya Muslim Women Writers.

Nilikuwa nimesoma kuhusu hadithi hii mtandaoni, nikaamua kuijumlisha katika kozi yangu. Nimefurahi kuwa nilifanya uamuzi huo. Nimejionea jinsi mwandishi Rokeya Sakhawat Hussain alivyokuwa mwanaharakati aliyepigania ukombozi wa wanawake kutokana na jadi ya wao kufungiwa ndani na kubanwa kimaisha, jadi iliyojengeka katika imani kwamba ni wajibu wa u-Islam.

Rokeya alikuwa mwanamama shujaa, ikizingatiwa wakati alioishi. Alibahatika kuwa mumewe alimwachia uhuru na kumsaidia katika uandishi na uhamasishaji wa wanawake. Alichapisha Sultana's Dream mwaka 1905. Ni  hadithi ya kubuniwa, ambayo inaelezea ndoto ya Sultana. Katika ndoto hiyo, Sultana anajikuta katika nchi ambayo inatawaliwa na wanawake, huku wanaume wakiwa ndani katika purdah. Utawala wa hao wanawake ni wa neema kubwa kwa nchi, kuanzia uadilifu hadi usafi. Ni nchi ya neema kabisa. Ni utopia.

Leo tumeanza kujadili hadithi hiyo. Nimewaeleza wanafunzi aina ya fasihi ("genre") iitwayo "utopia." Nimewaelezea nafasi ya utopia katika maisha ya binadamu kijamii na kisaikolojia kama njia ya kukabiliana au kuacha kukabiliana na hali halisi ya maisha. Nimeelezea dhana hiyo kwa kutumia mifano ya itikadi ya ki-Marxisti ya ukomunisti na pia mafundisho ya dini kuhusu paradiso au ahera. Utopia ni mkakati wa kuichambua na kuikosoa jamii, kama ilivyo katika Sultana's Dream.

Kwa kuwa Sultana's Dream inahusu purdah na imejikita katika kuukosoa utamaduni wa purdah kama utamaduni kandamizi kwa wanawake, niliona ni muhimu kuwasomea wanafunzi sehemu ya Qur'an ambayo inaongelea purdah. Kwa bahati nzuri, jana usiku nilivyoipitia Qur'an niliona sehemu husika, nayo ni Sura XX1V aya 27-31. Aya hizi zinaongelea masuala ya "privacy" ya nyumba na "modesty" kwa wanaume na wanawake, hasa suala la kujisetiri kwa wanawake.  Baadhi ya aya ni hizi:

30. Say to the believing men
     That they should lower
     Their gaze and guard
     Their modesty: that will make
     For greater purity for them:
     And God is well acquainted
     With all that they do.

31. And say to the believing women
     That they should lower
     Their gaze and guard
     Their modesty; that they
     Should not display their
     Beauty and ornaments except
     What (must ordinarily) appear
     Thereof; that they should
      Draw their veils over
     Their bosoms and not display
     Their beauty except
     To their husbands, their fathers,
     Their husbands' fathers, their sons,
     Their husbands' sons,
     Their brothers or their brothers' sons,

     Or their sisters' sons,
     Or their women, or the slaves
     Whom their right hands
     Possess, or male servants
     Free of physical needs,
     Or small children who
     Have no sense of shame
     Of sex; and that they
     Should not strike their feet
     In order to draw attention
     To their hidden ornaments.
     And O ye Believers!
     Turn ye all together
     Towards God, that ye
     May attain Bliss.

Zaidi ya hadithi ya Sultana's Dream, Rokeya aliandika pia insha na taarifa mbali mbali kuhusu hali za wanawake na ulazima wa kuleta mapinduzi. Alichapisha maandishi yake katika magazeti, na baadhi ya maandishi haya yamo katika kitabu tunachosoma katika kozi hii.

Saturday, February 13, 2016

U-Islam ni Dini ya Amani?

Wiki hii, tumeanza muhula mpya wa masomo hapa chuoni St. Olaf. Kozi mojawapo ninayofundisha ni Muslim Women Writers, ambayo nimeshaiongelea katika blogu hii.

Nimeshaanza kuwaelezea wanafunzi kuhusu u-Islam. Nimeongelea kuhusu Muhammad, Qur'an, hadith, na nguzo tano za u-Islam: shahadah, salah, zakah, sawm, na hajj. Nimefafanua maana ya kila nguzo. Nimeuelezea u-Islam kwa mtazamo wangu kama mtu ninayeziheshimu dini zote.

Kozi yangu hii ni muhimu kwa wanafunzi hao, ambao wengi wao hata msikiti hawajawahi kuuona na hata adhan hawajawahi kuisikia. Ni muhimu katika mazingira ya sasa ya Marekani, ambapo kuna propaganda nyingi dhidi ya u-Islam na wa-Islam. Kwa mfano, siku chache zilizopita, hapa mjini petu, kuna mtu ameandika katika Northfiled News, akiushambulia u-Islam kwamba si dini ya amani.

Kwangu ambaye ninatoka Tanzania, nchi ya watu wa dini mbali mbali, makala hii ambayo imezuka hapa ninapofundisha si ya  kuifumbia macho. Nitaipeleka darasani nikaijadili na kisha wanafunzi watoe dukuduku na mitazamo yao. Darasa la chuo kikuu ni mahala pa kuchambua masuala kwa uhuru na uwazi. Yeyote kati ya wasomaji wa blogu hii ambaye ana jambo la kuchangia namkaribisha afanye hivyo.  Mawazo muafaka yatasaidia juhudi zangu za kuwaelimisha wanafunzi wangu.

Kutokana na hali ilivyo hapa Marekani, na kutokana na kuwa nimeamua kufundisha kozi juu ya waandishi wa kike wa ki-Islam, kuna uwezekano wa mimi kuitwa kwenye mahojiano katika vyombo vya habari hapa Northfield au kwenye mikutano, kuongelea u-Islam. Iliwahi kutokea hivyo baada ya shambulio la kigaidi la tarehe 11 Septemba, 2001, lililoangusha majengo New York. Uliandaliwa mkutano mkubwa wa watu wa mji huu, pia jopo la maprofesa, nami nikiwemo, kujadili tukio lile na mengineyo. Mimi nilielezea u-Islam na kuupambanua na ugaidi.

Saturday, February 6, 2016

Shairi Linaposomwa kwa Sauti



Jana nilijirekodi katika video nikisoma kwa sauti shairi la W. B. Yeats liitwalo "The Second Coming." Niliweka video hiyo katika mtandao wa Facebook, katika You Tube, na katika blogu hii. Niliiweka katika You Tube baada ya kushindwa kuiweka katika blogu moja kwa moja, na katika kutafuta ufumbuzi wa tatizo, nilisoma mtandaoni kuwa kwa kuanzia kuiweka You Tube kunaweza kutatua tatizo. Ndivyo ilivyokuwa. Kutokea You Tube, nilifanya "embedding" kwenda kwenye blogu.

Napenda kwanza nikiri kuwa nimefurahishwa na jinsi usomaji wangu wa "The Second Coming" ulivyopokelewa na watu wa mataifa mbali mbali. Ni wazi kuwa wameguswa, nami nashukuru. Labda nitaandika zaidi kuhusu hilo. Lengo langu hapa ni kuongelea masuala ya kinadharia na kifalsafa juu ya usomaji wa shairi kwa sauti. Nilidokeza masuala haya katika  ujumbe wa jana.

Kwanza, tutafakari dhana ya uandishi. Tuanzie na chimbuko lake, yaani utungaji. Utungaji wa shairi, au kazi yoyote ya sanaa, hufanyika mawazoni mwa mwandishi au msanii, katika hisia za mwandishi au msanii. Utungaji huu mawazoni au katika hisia ndio unaomwongoza mwandishi  au msanii katika kuunda kazi ya sanaa tunayoiona, kama vile andiko au picha, au sanaa tunayoisikia, kama vile wimbo, muziki, au mapigo ya ngoma. Mpiga ngoma ana mtihani mkubwa kuliko wengine kwa kuwa uundaji na upigaji vinakuwa ni papo kwa papo, kwa kasi ya ajabu.

Hapa ninapenda kuongelea shairi. Shairi kama "The Second Coming" lilitungwa katika mawazo na hisia za Yeats, akaliandika ili tuweze kulisoma. Haikuwa lazima aliandike. Lingeweza kubaki mawazoni mwake na katika hisia zake. Angeweza kulighani kama wafanyavyo washairi wa jamii mbali mbali, kama ilivyokuwa jadi katika jamii zisizo na utamaduni wa maandishi.

Lakini Yeats aliamua kuliandika shairi lake, na hivyo kutuwezesha kulisoma. Kwa kuliandika na kulichapisha, ameliwezesha shairi lake kuenezwa popote duniani ambapo ki-Ingereza kinatumika kimaandishi. Hata pale ambapo ki-Ingereza hakitumiki, kuna uwezekano wa shairi hili kutafsiriwa kimaandishi, na tafsiri zikasomwa katika lugha mbali mbali.

Suala hili la tafsiri ni kubwa na tata, na siwezi kuliongelea sana. Lakini tukumbuke kwamba shairi kama "The Second Coming" likitafsiriwa katika ki-Swahili, ki-China, ki-Jerumani, ki-Zulu, na kadhalika, litakuwa si shairi lile lile aliloliandika Yeats. Lugha na tamaduni hazifanani kiasi cha kuwezesha utungo katika lugha moja kutafsirika kwa lugha nyingine. Mabadiliko hayakwepeki.

Nikirejea kwenye suala la usomaji wangu wa "The Second Coming," napenda kusema kwamba nilichofanya ni kutafsiri shairi lile. Ingawa nilisoma shairi katika lugha yake ya asili ya ki-Ingereza, nililisoma kwa sauti, vituo, na viashiria vingine vya mawazo na hisia zangu. Kwa maana hiyo, kwa usomaji wangu nilikuwa ninalitafsiri shairi.

Yeats mwenyewe kama angelisoma kwa sauti angelisoma kwa sauti, vituo na viashiria vingine vya hisia na mawazo yake. Wewe unayesoma makala hii ukilisoma shairi la Yeats kwa sauti utakuwa pia unalitafsiri kwa namna yako.

Roman Jakobson aliongelea vizuri dhana ya tafsiri katika makala yake, "On Lingustic Aspects of Translation," akabainisha aina tatu za tafsiri ambazo aliziita "interlingual," intralingual" na "intersemiotic." Niliwahi kugusia mchango wa Jakobson katika makala niliyoandika kuhusu nilivyotafisiri hadithi ya ki-Matengo. Bila shaka, kulisoma shairi kwa sauti kama nilivyofanya ni aina ya tafsiri ambayo Jakobson anaiita "intersemiotic."

Ninategemea kuwa wanafunzi, wafundishaji, na watafiti wa fasihi na nadharia ya fasihi watazitafakari dondoo nilizoweka hapa katika kuendeleza taaluma.

Friday, February 5, 2016

"The Second Coming:" Shairi la W. B. Yeats

"The Second Coming," shairi la William Butler Yeats wa Ireland, ni kati ya mashairi maarufu kabisa katika ki-Ingereza. Yeats aliliandika shairi hili baada ya vita kuu ya kwanza ambayo ilisababisha vifo vya mamilioni ya watu na uharibifu mkubwa. Simanzi ilitanda ulimwenguni, na ilikuwa rahisi kukata tamaa kuhusu hatima ya binadamu na ulimwengu.

Hisia hizi zinajitokeza kimafumbo katika "The Second Coming." Kinachoshangaza ni jinsi shairi hili lilivyoonekana kubashiri majanga yaliyoikumba dunia miaka iliyofuata. Adolf Hitler aliibuka na himaya yake ya ki-Nazi iliyosababisha mauaji ya mamilioni ya watu na kisha ikaja vita kuu ya pili.

"The Second Coming" ni shairi ambalo wengi tulilisoma tulipokuwa sekondari, na wengi wetu tunakumbuka lilivyonukuliwa na Chinua Achebe mwanzoni mwa riwaya yake ya Things Fall Apart. Kati ya mambo mengi, riwaya hii nayo ilielezea mtafaruku uliotokea katika jamii ya asili ya ki-Afrika kufuatia kuingiliwa na wazungu.

Kila mtu anaweza kulisoma shairi hili la "The Second Coming" kimya au kwa sauti. Jaribu kulisoma kwa sauti, uone linasikika vipi na linatoa maana au hisia gani. Haiwezekani kwa shairi hili kusomwa kwa namna ile ile lilivyokwishasomwa, hata kama msomaji ni yule yule. Lazima zitajitokeza tofauti, hata kama ni ndogo sana.

Hata mimi ambaye nimerekodi usomaji wangu katika video niliyoiweka hapa, siwezi kurudia kulisoma shairi hili sawa sawa kama nilivyofanya. Jambo hili linatulazimisha kujiuliza: kusoma ni nini? Bila shaka kusoma ni kutafsiri, na kila usomaji wa shairi kama hili ni tafsiri tofauti na nyingine yo yote.

Tunaweza kujiuliza masuali mengine. Kwa mfano, Je, shairi linabaki lile lile kila linaposomwa? Tunaposema shairi, tunamaanisha nini? Nini maana ya kusema "The Second Coming" ni shairi? Inakuwaje liitwe shairi lile lile iwapo kila usomaji wake unaleta maana na hisia tofauti?

Watu wengi wanaamini kuwa inawezekana kuelezea maana ya shairi na kuhitimisha. Wanaamini kuna ujumbe katika shairi ambao unaweza kufafanuliwa. Ni lazima tujifunze kutafakari zaidi masuala haya kwa kusoma nadharia mbali mbali za fasihi badala ya kuridhika na dhana zilizozoeleka.

Nisikilize ninavyolisoma shairi la "The Second Coming." Nilirekodi video hii jana, ghafla tu, bila mazoezi, nikaiweka kwenye ukurasa wangu wa Facebook. Watu wamejitokeza kutoka pande zote za dunia wakionyesha kuipenda. Siwezi kujua ni nini kilichowagusa; labda ni shairi lenyewe, au labda ni usomaji wangu, na hata hivyo, ni lazima kila mtu ameguswa kwa namna tofauti na mwingine. Ni kitendawili.




The Second Coming

Turning and turning in the widening gyre
The falcon cannot hear the falconer;
Things fall apart; the centre cannot hold;
Mere anarchy is loosed upon the world,
The blood-dimmed tide is loosed, and everywhere
The ceremony of innocence is drowned;
The best lack all conviction, while the worst
Are full of passionate intensity.

Surely some revelation is at hand;
Surely the Second Coming is at hand.
The Second Coming! Hardly are those words out
When a vast image out of Spiritus Mundi
Troubles my sight: somewhere in sands of the desert
A shape with lion body and the head of a man,
A gaze blank and pitiless as the sun,
Is moving its slow thighs, while all about it
Reel shadows of the indignant desert birds.
The darkness drops again; but now I know
That twenty centuries of stony sleep
Were vexed to nightmare by a rocking cradle,
And what rough beast, its hour come round at last,
Slouches towards Bethlehem to be born?

Source: The Collected Poems of W. B. Yeats (1989)

Thursday, February 4, 2016

Ganesha: Mungu Maarufu

Ganesha ni mmoja wa miungu wa dini ya Hindu. Dini hii ilianzia India, miaka zaidi ya elfu tatu iliyopita. Leo ina waumini yapata bilioni sehemu zote za dunia, kuanzia India na nchi za jirani, hadi Afrika Mashariki, visiwa vya Caribbean, na visiwa vya Pacific.

Ganesha ni mtoto wa kiume wa Shiva na Parvati. Ni mungu maarufu katika dini zingine pia, kama vile u-Buddha na u-Jaini. Katika michoro na sanamu anatambulika kirahisi, kwa kuwa ana kichwa cha tembo. Kuna masimulizi mbali mbali juu ya asili ya hiki kichwa chake.

Ganesha anategemewa kama mungu anayeondoa vikwazo. Anasafisha njia ya mafanikio. Mtu anapoanza safari, biashara, au mradi wowote, huelekeza maombi kwa Ganesha. Lakini pia, Ganesha huwawekea vikwazo wenye kiburi.

Ganesha ni mungu mwenye akili sana. Ndiye mlezi wa wanataaluma. Ni mungu wa uandishi pia, na inasemekana alitumia pembe yake kuandika sehemu ya utungo maarufu wa Mahabharata. Washairi na watunzi wa vitabu humtegemea. Aghalabu, katika picha na sanamu, Ganesha anaonekana akicheza. Ni mlezi wa wanamuziki na wasanii wengine.

Ganesha ni mmoja wa miungu wanaotajwa sana katika fasihi, nami ninapofundisha kozi kama South Asian Literature, napata fursa ya kuwaeleza wanafunzi habari za miungu hao. Ninashukuru kwa bahati niliyo nayo ya kujifunza fasihi, tamaduni, na dini mbali mbali na kuwafundisha wengine. Ni njia bora ya kujenga maelewano duniani.

Imani za watu zinanivutia, kama zinavyonivutia fasihi na tamaduni. Niliwahi kuandika katika blogu hii jinsi nilivyozuru nyumba za ibada za wa-Hindu nchini India. Napenda kusema kuwa mimi ambaye ni mwanataaluma, mwandishi, na mwanablogu, kama ningekuwa m-Hindu, ningekuwa ninamtegemea Ganesha.

Jambo moja ambalo linaweza kuwa gumu kwa sisi ambao si wa-Hindu kulielewa ni kuwa ingawa kuna miungu wengi katika dini hiyo, kwa undani wake u-Hindu ni dini inayotambua kuwepo kwa "Supreme Being," na kwamba hao miungu wengi ni nafsi za "Supreme Being." Ni kitendawili kama kile wanachokumbana nacho watu wasio wa-Kristu wanapoambiwa kuwa sisi wa-Kristu tuna dhana ya Utatu Mtakatifu katika Mungu Mmoja.
 

Monday, February 1, 2016

Dini sio Misahafu Pekee

Leo ninapenda kuendelea kuongelea dini, kujenga hoja kwamba dini si misahafu pekee. Ninaongelea mada hii kwa kuwa ninaamini umuhimu wa mijadala ya dini, na kwa kuzingatia tabia ambayo imejengeka Tanzania ya baadhi ya wa-Islam na wa-Kristu kulumbana kuhusu dini zao. Wanaonekana viwanjani wakihubiri dhidi ya dini ya wapinzani wao. Wananukuu misahafu katika kujenga hoja kwamba dini yao ni bora zaidi au ndio dini ya kweli.

Binafsi, naona kuwa malumbano haya ni upuuzi mtupu. Dini haiko katika misahafu tu. Ni mfungamano wa nadharia na vitendo. Dini ni mfungamano wa mafundisho ya misahafu na maisha ya kila muumini. Bila mfungamano huo, dhana ya dini inapwaya.

Kuna maana gani kwa muumini wa dini kuringia msahafu wa dini yake iwapo maisha yake hayaendani na mafundisho yaliyomo katika msahafu? Badala ya kulumbana kuhusu misahafu, tuangalie maisha ya waumini. Je, tabia za mu-Islam ni bora kuliko za m-Kristu? M-Kristu ni bora kuliko mu-Islam? Jamii ya wa-Islam ni bora kuliko jamii ya wa-Kristu? Wa-Kristu ni bora kuliko wa-Islam? Tofauti za imani zina uzito gani? Je, wa-Kristu, ambao wanaamini kuwa Yesu ni mwana wa Mungu, ni watu waovu kuliko wa-Islam, ambao hawaamini kuwa Yesu ni mwana wa Mungu bali ni nabii?

Kama waumini wa dini fulani ni wema, waungwana, wakarimu, wastahimilivu, wenye huruma, wa amani kuliko wengine, ninaamini kuwa waumini hao watawavutia hata watu wasio na dini. Dini si misahafu tu; ni mfungamano wa nadharia na vitendo.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...