Friday, August 5, 2011

Mitaani Mbamba Bay

Agosti tarehe 2 nilisafiri kutoka kijijini kwangu Lituru nikapitia Mbinga, na kufika Mbamba Bay, mwambao wa Ziwa Nyasa kwa matembezi.

Mbamba Bay, ingawa mji mdogo sana, unavutia kwa utulivu wake na mazingira, ukiwa ufukweni mwa Ziwa linalomeremeta kwa maji yake maangavu, kama nilivyowahi kuandika hapa.

Nilikuwa na bahati kwamba tarehe 3 Agosti ilikuwa siku ya jua na hali ya hewa ya kuvutia sana. Nami nilitumia fursa hii vilivyo. Niliteremkia ufukweni kufurahia upepo mwanana na mandhari murua ya Ziwa.


Kukaa nje ya nchi yako kunakupa mtazamo tofauti wa masuala ya nchi yako. Kwa mfano, hapa Tanzania, watoto wetu wana uhuru sana wa kucheza na kuzunguka mitaani, tofauti na Marekani, ambako watoto huangaliwa sana muda wote na wazazi au walezi wao, kwani si salama kuwaacha watoto bila uangalizi. Wa-Marekani wanaokuja huku kwetu wanashangaa wanapowaona watoto wakijizungukia wenyewe mitaani, raha mstarehe. Nimeongelea tofauti hizo katika kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences.

Joto la Mbambay ni kishawishi kikubwa cha kutafuta sehemu ya kujipatia kinywaji baridi. Nami nilisogea baa hii iitwayo Bush House, nikatuliza kiu.



Hali ya Mbamba Bay ni ya utulivu usio kifani. Ni mahali pazuri kwa mapumziko. Kadiri siku zinavyopita, nina imani kuwa Mbamba Bay patakuwa kivutio kikubwa kwa watalii wa nje na ndani ya nchi. Nami niliamua kufika Mbamba Bay ili kupiga picha nichangie katika kuitangaza sehemu hii ya Tanzania.










3 comments:

tz biashara said...

Profesa naona upo vekesheni unakula raha.Nilikuwa nawazo moja kuhusu watoto kutembea peke yao na uhuru wao.Mimi pia nipo uingereza na hali ni kama unavyoisema ya kutokuwa huru.Lakini kwa jinsi nionavyo mimi kwa sasa binaadamu tumebadilika sana na sidhani kama kuna uhuru uliokamilika kwa watoto wetu.Kwa kweli waharibifu wamekuwa wengi mno bila hata kujali utu.Nauhakika hawa watoto wenyekuachiwa huru basi wapo wanaokutana na mazingira mabaya lakini kwa kwetu sio rahisi mtoto kusema ukweli kwa namna moja au nyingine inawezekana kupewa pesa kwa kutokusema jambo au kwa vitisho.Nadhani ni wakati sasa wazazi kuwa makini kwa hilo japokuwa maisha ni magumu.Hapa juzi nilisoma habari moja ya kutisha na kusikitisha.Mtoto wa miaka 7 anauza vyuma chakavu aligongwa na gari na ikisha yule aliyemgonga alishuka kwa haraka na kumchukua mtoto yule na watu wakidhani akifanya utu wa kumuwahisha Hospitali.Lakini alikutwa ametupwa akiwa maiti.Sasa hebu niambie huyu mtu hata kama mtoto yule alifia ktk gari alitakiwa pia ampeleke Hospitali?Hakuna utu tena Profesa lazima watoto wachungwe kwanza kunatisha maana kuna baa nyingi zinafunguliwa mitaani na ni hatari kwa watoto.Ni bora watoto wapewe vitabu wajisomee nyumbani na wacheze nje nyumbani kwao kuliko kuwaachia wanatembea mitaani.

Mbele said...

tz biashara, shukrani kwa mchango wako murua. Ni changamoto safi, nami sina la kuongezea bali kutafakari.

Ni kweli, nilitua Mbamba Bay nikafaidi vekesheni vilivyo. Nawashauri wadau kutembelea sehemu kama hizo.

Emmanuel Sulle said...

Salam Prof. Aksante sana kwa kutujulisha habari za Mbamba Bay. Wengine mpaka leo hii sehemu tunaikumbuka kwa kuisoma kwenye jiographia ya shule ya msingi. Aksante pia kwa moyo wako wa kuitangaza Tanzania na vivutio vyake. Naendeleza ombi langu kukuona hapa Dar kabla hatajageuza wote Marekani.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...