Friday, May 30, 2014

Tembo wa Hifadhi ya Tarangire, Tanzania

Tarangire ni moja ya hifadhi maarufu Tanzania, yenye wanyama mbali mbali.

Nimefika katika hifadhi hii mara nne, kwa miaka tofauti. Mwezi Januari, mwaka juzi, 2013, nilipiga picha mbali mbali. Baadhi ni picha za tembo zinazoonekana hapa. Nilikuwa naongoza darasa la wanafunzi 29 wa chuo cha St. Olaf, katika kozi ambayo nilikuwa nimeitunga, kumhusu Ernest Hemingway.





Mwandishi Ernest Hemingway aliitembelea hifadhi hii mwaka 1933. Aliandika hayo katika kitabu chake cha Green Hills of Africa ambamo amezitaja na kuzielezea sehemu nyingi za Tanganyika alimopita.

Green Hills of Africa, kwa mtazamo wangu, ni kitabu bora sana, ambacho kiliitangaza nchi yetu vizuri kabisa, kuliko ambavyo sisi wenyewe tumefanya, kuliko tunavyoweza. tunaendekeza uzembe katika lugha na katika nidhamu ya uandishi kama ille ya Hemingway.. 



Kila ninapofika sehemu kama Tarangire, ninamkumbuka Hemingway na maandishi yake, hasa hiki kitabu chake cha Green Hills of Africa. Haiwezekani kujizuia.

4 comments:

Anonymous said...

Ndugu, Ningependa kusoma andiko lako lolote kuhusu Maya Angelou

Mbele said...

Ndugu Anonymous, shukrani kwa ujumbe wako. Sijasoma maandishi ya Maya Angelou, labda mashairi mawili matatu. Sina utaalam wowote juu yake, ingawa najua kiasi habari zake.

Nilimsikiliza siku moja, miaka mingi kidogo iliyopita, akitoa mhadhara katika chuo cha jirani cha Carleton. Pia, siku nyingine, nilimsikiliza kwenye mahojiano katika TV.

Kwa miaka, nimekuwa na baadhi ya vitabu vyake, lakini sijavisoma, labda kwa kugusia gusia tu. Sina ufahamu wa kuweza kuandika makala juu yake.

Kuna mamia ya waandishi ambao kazi zao sijazisoma, na hakuna anayeweza kuzisoma zote. Wengi wa waandishi hao wameshinda tuzo kubwa kubwa, kama vile tuzo ya Nobel, lakini mtu hata kama ni profesa wa "Literature" kama mimi, huwezi kuwasoma wote.

Nakumbuka niliwahi kuelezea tatizo hili, au ukweli huu, katika blogu yangu hii. Siku hiyo, kama sikosei, nilimtaja mwandishi Orhan Pamuk wa Uturuki, ambaye alikuwa ameitwaa tuzo ya Nobel, nami ingawa nilikuwa, na bado nina vitabu vyake viwili vitatu, sijavisoma bado.

Inasikitisha, kwamba ningependa kuwa na ufahamu wa kutosha wa waandishi wote maarufu, lakini haiwezekani.

Anonymous said...

Nashukuru kwa ufafanuzi wako mzuri, Nimekuwa nikisoma habari zake na kusukiliza baadhi ya mahojiano yake radio 4(http://www.bbc.co.uk/programmes/p01zxd06).
Kwa bahati mbaya sijaweza kuona kitabu chake chochote wala kukisoma.
Mdau

Mbele said...

Ndugu Anonymous, nimeguswa na ujumbe wako. Navutiwa na nawaheshimu kwa namna ya pekee watu wanaosoma vitabu, sio kwa sababu ya mitihani bali kujipanua ufahamu wa mambo ya aina mbali mbali.

Nipe anwani yako ya posta, nami naahidi nitakuletea nakala ya kitabu maarufu cha Maya Angelou, "I know Why the Caged Bird Sings." Nitafurahi ukiwa na angalau hiki kimoja.

Unaweza kutumia anwani yangu: info@africonexion.com

Kila la heri.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...