Wednesday, December 31, 2008

Warsha: Utamaduni, Utandawazi na Maendeleo

Kati ya mambo ninayofanya ni kutoa ushauri kwa mashirika, taasisi, vyuo, vikundi na watu binafsi kuhusu masuala ya tofauti baina ya utamaduni wa Mwafrika na ule wa Mmarekani. Ninafanya hivyo kwa njia mbali mbali, kama vile kuandika makala na vitabu, kuendesha warsha, au kukutana watu binafsi ana kwa ana.

Ninaposema utamaduni, namaanisha vitu kama hisia, tabia, maadili, namna tunavyofikiri na tunavyoongea. Vipengele hivi vyote vinatutofautisha watu wa tamaduni mbali mbali, na ni muhimu kuvielewa ili kuepusha migongano. Katika dunia ya leo, ya utandawazi, masuala ya tofauti za tamaduni yanahitaji kupewa kipaumbele, kwani yanaweza kuwa pingamizi kubwa, chanzo cha migogoro, au chachu ya hii migogoro.

Nitaendesha warsha kuhusu masualaa hayo tarehe 4 Julai, 2009, kwenye kituo cha Meeting Point Tanga. Watu kutoka mashirika, makampuni, taasisi, na jumuia mbali mbali watapata fursa ya kuyatafakari masuala kadha wa kadha yanayojitokeza wakati huu ambapo watu wa tamaduni mbali mbali wanalazimika kukutana, kufanya kazi pamoja, kuwasiliana au kuhusiana kwa namna moja au nyingine. Kwa taarifa zaidi soma hapa

Saturday, December 27, 2008

Kijitabu Changu Kipya















Miaka miwili iliyopita niliombwa kushiriki katika maonyesho ya utamaduni wa Mwafrika, soma hapa, yaliyofanyika kwa mara ya kwanza mjini Minneapolis katika jimbo la Minnesota, Marekani. Maonyesho hayo yalipangwa kujumlisha mambo mengi: historia ya Mwafrika duniani na harakati alizopitia, mafanikio na mchango wake, na hali yake ya sasa na baadaye.

Wasanii, wabunifu wa mavazi, wanamuziki, na wengine walialikwa kutoa mchango wao. Mimi nilialikwa kuandaa vielelezo vya mambo muhimu katika historia ya Mwafrika, kuanzia chimbuko la binadamu Afrika hadi kusambaa kwa Waafrika sehemu mbali mbali za dunia, kama vile Marekani, Ulaya, na Asia.

Nilifanya utafiti nikaandika habari hizo kwa mtindo wa insha fupi kumi. Kila insha niliiweka kwenye bango kubwa na kila bango liliambatana na picha kadhaa. Siku ya tamasha, niliyabandika mabango hayo kwenye kuta za ukumbi niliopangiwa. Watu walifika humo na kusoma kwa wakati wao, wakiangalia pia zile picha.

Mama mmoja aliyehudhuria na kuangalia maonyesho yangu alipendekeza kuwa nitoe kitabu, ili watu waweze kuendelea kusoma majumbani. Nilifuata ushauri wa huyu mama, na kitabu nilikitoa, chenye habari na picha zile zile zilizomo kwenye mabango.

Kitabu ni kidogo, maana nilikuwa na mabango kumi tu, lakini kinaibua masuala mengi. Kwa mfano, nawakumbusha wasomaji kwamba Afrika ndipo binadamu walipotokea. Pamoja na kuongelea masuala kama utumwa, ukoloni, harakati za kupigania uhuru, na majukumu yanayotukabili leo na siku za usoni, nawakumbusha wasomaji kuhusu mchango wa Waafrika katika nyanja mbali mbali, mchango ambao haujulikani vizuri au umesahaulika kabisa hata miongoni mwa Waafrika wenyewe.

Kuhusu upatikanaji wa kijitabu hiki, tuma barua pepe info@africonexion.com.

Friday, December 26, 2008

CCM: Ni chama cha Mapinduzi?

Sielewi kwa nini watu wanaamini kuwa CCM ni chama cha mapinduzi. Sijawahi kuelewa na bado sielewi kwa nini. Dhana ya mapinduzi ilielezwa vizuri na TANU, katika "Azimio la Arusha," "Mwongozo," na maandishi, hotuba na mahojiano mbali mbali ya Mwalimu Nyerere. Matokeo ya yote hayo ni kuwa Watanzania tulifahamu vizuri na kukubali dhana na maana ya mapinduzi katika nchi yetu. Yeyote ambaye hajasoma maandishi hayo, au kusikiliza hotuba hizo, ningemshauri afanye hivyo, ili aweze kufahamu msingi wa ujumbe wangu.

CCM ilipoanza, ilijinadi kuwa ni chama cha mapinduzi. Lakini baada ya muda si mrefu, mwelekeo wake ulijionyesha kuwa si wa mapinduzi. Badala ya kuendeleza fikra na mwelekeo wa "Azimio la Arusha," "Mwongozo" na mengine yote niliyoyataja hapo juu, CCM ilitoa "Azimio la Zanzibar." Ingawa CCM haikutoa fursa iliyostahili kwa wananchi kuliangalia na kulijadili "Azimio la Zanzibar," habari zilizojitokeza ni kuwa Azimio hili lilikiuka yale yaliyokuwemo katika "Azimio la Arusha." Mwalimu Nyerere alilishutumu "Azimilo la Zanzibar" kwa msingi huo.

Kitu kimoja kilichokuja kufahamika wazi ni kuwa "Azimio la Zanzibar" lilibadilisha masharti ya uongozi yaliyokuwemo katika "Azimio la Arusha" na "Mwongozo." Kwa mfano, "Azimio la Zanzibar" liliondoa miiko ya uongozi iliyokuwepo.

Baada ya CCM kuvunja misingi ya mapinduzi, kilichofuatia ni kuimarika kwa ubepari, matabaka, na ufisadi. Chini ya himaya ya CCM, "Azimio la Arusha" halisikiki, "Mwongozo" hausikiki, wala maandishi na hotuba zingine zilizofafanua maana ya mapinduzi hazisikiki. Inaonekana kuwa CCM ilikusudia tangu mwanzo kuwafanya watu wasahau hayo yote, ili iendelee na sera za kujenga ukoloni mamboleo nchini mwetu.

Inakuwaje basi CCM ijiite chama cha mapinduzi wakati inahujumu mapinduzi? Inakuwaje Watanzania hawahoji jambo hilo? Elimu ni ufunguo wa maisha; bila elimu kuna hatari ya kurubuniwa na kuburuzwa kama vipofu.

Sunday, December 21, 2008

Kuku kwa Mrija

Watanzania wana uwezo mkubwa wa kubuni misemo na kudumisha uhai na utamu wa lugha ya kiSwahili. "Kuku kwa mrija" ni usemi moja ambao umepata hadhi ya pekee katika kiSwahili cha mazungumzo.

Naamini kuwa wengi wanaweza kueleza maana ya usemi huu na matumizi yake, lakini napenda kuelezea machache, kwa kuchambua mantiki yake.

Kuku kwa mrija ni usemi unaobeba dhana ya maisha ya raha, starehe, na vyakula tele. Kwa vile kuku ni nyama inayothaminiwa sana katika utamaduni wetu, kula kuku sana ni dalili ya kuishi maisha ya raha na mafanikio.

Kwa ujumla, Watanzania wanaamini kuwa maisha hayo yanapatikana nchi za nje, hasa Ulaya na Marekani. Mtanzania anayeishi huko anahesabiwa na Watanzania walioko nyumbani kuwa anakula kuku kwa mrija. Maisha yake ni ya starehe na kuku ndio chakula chake kikuu.

Mimi mwenyewe nilikuja Marekani mara ya kwanza mwezi Agosti 1980, kusoma katika chuo kikuu cha Wisconsin-Madison, nikitokea Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambapo nilikuwa nafundisha. Wakati ule, ninavyokumbuka, dhana ya kuku kwa mrija haikuweko katika kiSwahili. Lakini utamaduni wa kuthamini kuku kuliko nyama zote ulikuwepo, kwani ni utamaduni wa tangu enzi za mababu na mabibi.

Kwa hivyo, nilipofika Marekani, nilikuwa na tabia ya kununua sana kuku. Nina hakika kuwa Watanzania wanaofika huku wanafanya hivyo hivyo, kutokana na utamaduni wetu.

Kitu ambacho sikujua, na Watanzania kwa ujumla hawajui, ni kuwa kuku wa kijijini Tanzania si sawa na kuku wa hapa Marekani. Kuku wa kijijini anakua katika mazingira muafaka kwa afya yake na afya ya wale wanaomla. Anakula punje, mabaki ya ugali au wali, na vidudu mbali mbali ambavyo havina madhara kwa afya yake, na nyama yake haina madhara kwa binadamu.

Kwa ujumla, kuku wa huku Marekani hawako hivyo. Makampuni ya kibepari ndio yameshika hatamu katika kuzalisha kuku na vyakula vingine. Lengo la hao mabepari ni kupata fedha, si kuangalia afya za binadamu. Kuku wao wanakuzwa katika mazingira ya aina yake na kulishwa vyakula na madawa ili wakue upesi, wakauzwe. Baada ya muda mfupi tu wanakuwa wakubwa na tayari kuchinjwa na kuliwa. Madawa wanayolishwa ni hatari kwa afya ya binadamu. Lakini mabepari wakipata mwanya, bila kubanwa, hawaangalii hayo. Naafikiana na Mwalimu Nyerere alivyosema kuwa ubepari ni unyama.

Kwa hivi, Mtanzania anayekuja Marekani au Ulaya na mawazo ya kuku kwa mrija anajitakia matatizo. Hapa Marekani penyewe, na Ulaya pia, baadhi ya watu wameshaanza kampeni ya kuelimishana kuhusu madhara ya ufugaji huu wa kisasa, iwe ni wa kuku au wanyama mbali mbali tunaowala.

Kampeni hii inahusu pia mboga za aina mbali, matunda, mayai, na vyakula vingine. Hofu ya madawa yanayotumika katika kilimo na ufugaji inazidi kuwahamasisha watu waingie kwenye mkondo wa kutafuta vyakula ambayo vimetokana na kilimo kisichotumia madawa, au mifugo isiyotumia madawa.

Watanzania hawaonekani kufahamu suala hilo. Wakati huu, ambapo nchi yetu imefungua milango na kuwaruhusu wawekezaji kuingiza vitu vyao vya kila namna, hata sekta ya vyakula imeathirika. Vyakula vinavyotoka nchi za nje vimejaa madukani, hata vile ambavyo vimetokana na kilimo au ufugaji wa kutumia madawa. Kuku kwa mrija sio tena kitu cha kukiwazia tu, kwamba kinapatikana Ulaya na Marekani. Yeyote mwenye hela Tanzania anakula kuku kwa mrija kutoka nje. Katika hali hii, wale mabepari wanaotafuta hela wanazidi kuneemeka nchini kwetu, na kwa vile sisi inaonekana hatutambui ujinga wetu, wao wataendelea kuchuma, kama methali inavyosema: wajinga ndio waliwao.

Mambo haya yanasikitisha. Jambo linalosikitisha zaidi ni kuwa Tanzania kuna vyakula vya kila aina ambavyo wakulima wanalima bila madawa, kama vile matunda, mboga, viazi, na maharagwe. Kuna mifugo ambayo ni salama kabisa kwa afya ya binadamu, kama vile kuku, mbuzi, na ng'ombe.

Lakini, Watanzania wengi wenye hela wanaona ni fahari kununua vyakula kwenye haya maduka ya kisasa, ambavyo vimetoka nje ya nchi na vimefungwa vizuri kwenye vifurushi, kuliko kwenda sokoni kununua viazi, mchele, na mboga zinazotoka kijijini.

Watanzania wengi wanaona fahari kununua vikopo vya juisi ya machungwa au maembe ambavyo vimeagizwa kutoka nchi za nje, kuliko kununua maembe au machungwa yanayotoka kijijini hapo hapo Tanzania. Akili ya kuelewa kwamba kadiri vyakula hivi vinavyokaa dukani, ndivyo vinavyopoteza lishe haiko vichwani. Ingawa tunda likikaa dukani wiki nzima baada ya kuchumwa linabaki tunda, thamani yake kama lishe haifanani na thamani ya tunda lililochumwa leo hii kijijini na kuletwa sokoni.

Elimu ni nguzo na kinga ambayo tumeendelea kuipuuzia katika nchi yetu. Matokeo yake ni kuwa tunashabikia kuku kwa mrija na vyakula ambavyo wenzetu Marekani na Ulaya wameanza kuviogopa kwa vile vina madhara kwa afya. Madhara ya vyakula vibovu yanaonekana sana katika nchi zinazosemekana zimeendelea, kama zile za Ulaya na Marekani. Tatizo la watu kunenepa kupita kiasi, kwa mfano, ni tishio, na watu wa huku wanaendelea kutambua hilo. Lakini, Watanzania ndio wanaanza kuvishabikia vyakula vinavyoleta madhara haya, na ambayo huku Marekani vinaitwa "junk food" (vyakula takataka), kwani tunaviona ni vyakula vya kisasa.

Tulipopata Uhuru, mwaka 1961, kiongozi wetu wa kwanza, Julius Nyerere, alitangaza kuwa nchi yetu ina maadui wakuu watatu, ambao itakuwa kazi yetu kuwapiga vita. Maadui hao ni ujinga, maradhi na umaskini. Kwa miaka yote ya maisha yake, Nyerere alijitahidi na kuongoza vita hivi na kutuelimisha kwa kila namna. Leo, inaonekana tunaukaribisha ujinga na hivi kujihumu sisi wenyewe.

Tuesday, December 9, 2008

Ubora wa huduma: msingi wa mafanikio

Ni muhimu kuelewa misingi ya mafanikio katika dunia ya leo, yenye ushindani mkubwa. Ushindani huu uko ndani ya nchi na kimataifa. Wapende wasipende, wafanya biashara na watoa huduma mbali mbali wanajikuta katika mazingira ya mashindano ambayo yanaongezeka kwa kasi na yanazidi kuwa magumu. Katika hali hii, ni muhimu kwa kila mhusika kujua siri za mafanikio.

Siri mmoja ni ubora wa huduma. Kuna usemi kuwa mteja ni mfalme. Nimeona sehemu mbali mbali duniani ambapo dhana hii inazingatiwa sana. Wako watu wanaofahamu vema umuhimu wa mteja. Wawe ni wafanyabiashara au watoa huduma, wanaonyesha kumjali sana mteja. Hata kama mteja ni msumbufu wafanyabiashara na watoa huduma hao wako tayari kumsikiliza, kumvumilia na kumsaidia hadi aridhike. Sio rahisi kuwaona wafanyabiashara au watoa huduma hao wakimkasirikia mteja.

Hapa Marekani, kwa mfano, mteja anaponunua kitu, anapewa risiti, na kama hataridhika na kitu alichonunua, ana uhuru wa kukirudisha na kurudishiwa hela yake, au kubadilisha alichonunua akapata kingine, bora alete ile risiti. Hali hii si ya kawaida Tanzania, ambako risiti mara nyingi huwa imeandikwa kwamba bidhaa ikishauzwa haiwezi kurudishwa dukani. Hata kwenye vyombo vya usafiri Tanzania, hali hii ni ya kawaida. Nimeona mara kwa mara tikiti za kusafiria zimeandikwa ujumbe kwamba tikiti ikishakatwa, haiwezi kurudishwa.

Sehemu ambazo nimepita hapa Marekani, nimeona kuwa wahudumu wanawaheshimu wateja. Wanafanya kila juhudi kumsaidia mteja. Kama mhudumu analegea katika kutoa huduma, labda kwa sababu ya kutoelewa, au kazidiwa na shughuli, mkuu wake wa kazi, hata meneja, yuko tayari kuja kutoa hiyo huduma. Si ajabu hapa Marekani kumwona meneja akitoa huduma ambayo kwa kawaida inatolewa na mfanyakazi wake. Tanzania nimeona mambo tofauti. Meneja wa baa, kwa mfano, hawezi kuchukua kitambaa na kusafisha meza ya wateja. Atamtafuta mhudumu wa baa aje asafishe. Meneja anajiona mtu bora kuliko wahudumu. Ni kawaida kumwona meneja amekaa kwenye meza na watu anaowajua yeye, na kazi yake ni kunywa pombe na kuongea nao.

Nikiwa kwenye baa za Tanzania, nimewahi kuwa na masuala ya kuwaeleza mameneja, iwe ni malalamiko au ushauri kuhusu huduma, lakini imetokea mara kadhaa kuwa meneja alishalewa, na hana uwezo wa kusikiliza na kuzingatia niliyokuwa nasema. Naamini kuwa, ili tuweze kufanikiwa katika dunia ya ushindani, tabia hizi lazima tuzibadili.

Watu wa nje watakuja na taratibu zao za kujali wateja. Kila mteja anafurahia huduma nzuri. Matokeo yake ni kuwa, wafanyabiashara na watoa huduma wasiozingatia suala la kumridhisha na kumfurahisha mteja watapoteza wateja. Na katika ulimwengu huu wa ushindani, mtoa huduma nzuri ndiye atapata wateja wengi. Kutakuwa na wafanya biashara ambao wanauza kitu kile kile, kwa mfano nguo za aina ile ile, lakini baadhi watafanikiwa na baadhi watazorota, kutokana na kiwango cha ubora wa huduma kwa mteja. Mteja akiwa na hela yake, anaweza kuipata nguo hiyo kutoka sehemu yoyote. Lakini anapoamua kuja sehemu moja, wahudumu wa sehemu hiyo wanapaswa kuelewa kuwa hii ni bahati ambayo hawapaswi kuichukulia kijuu juu.

Mteja anapoingia dukani, hotelini, au sehemu yoyote inayotoa huduma, ajisikie kuwa yuko mahali anapothaminiwa na kufurahiwa. Wako wahudumu ambao wanampokea mteja kama vile angekuwa mtu asiyetakiwa, adui, au mhujumu. Wanampa maneno ya mkato, kuudhi, au kukatisha tamaa. Watoa huduma wa aina hii, au wenye biashara wa aina hii, wanahujumu wenyewe hizo biashara au huduma zao.

Fundisho hili, ingawa rahisi, halijaingia vichwani mwa wengi katika Tanzania. Wengi wanapoona biashara zao zinazorota au huduma zao hazivutii wateja, wanatafuta visingizio kama vile kulogwa na washindani. Wengi wanaamini kuwa ili wafanikiwe katika biashara, lazima watumie mizizi na mambo ya kishirikina. Huku Marekani, kuna vitabu vingi ambavyo vinafundisha masuala ya aina aina, likiwemo suala la kuendesha biashara na huduma mbali mbali. Vitabu hivi vinafundisha mbinu, misingi na mikakati. Vinaelezea saikilojia ya wateja, umuhimu wa kuwajibika, kujenga mahusiano na wengine, na kadhalika. Sijawahi kuona kitabu hata kimoja kinachoelezea umuhimu wa kutumia mizizi. Hiyo mbinu ya mizizi inaonekana inafanya kazi huko kwetu tu. Suali linalonijia kichwani ni je, katika ushindani wa kimataifa, ambamo wenzetu wanatumia ujuzi, maarifa na elimu, sisi tutafanikiwa kwa kutumia mizizi?

Dunia ya leo inaendeshwa na ujuzi na maarifa. Hilo linafahamika sana duniani. Tanzania bado tuko nyuma. Suala la kutafuta ujuzi, elimu, na maarifa tumelipuuzia. Hatutaweza kufanikiwa katika dunia ya leo iwapo tutaendekeza hali hii. Ushindani wa kimataifa utakuwa ni tishio kwetu. Wakati huu, tayari, uwoga wa ushindani wa kimataifa umeshaanza kujitokeza nchini mwetu. Hayo ni matokeo ya kupuuzia suala la elimu, suala ambalo Mwalimu Nyerere alilizingatia tangu tulipopata uhuru, pale aliposema kuwa tuna maadui watatu: ujinga, umaskini, na maradhi.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...