
Jioni ya tarehe 4 Aprili, baada ya kurejea kutoka Leech Lake Tribal College karibu na mji wa Bemidji, niliingia mtandaoni nikiwa na lengo la kuona kama kuna taarifa zozote kuhusu mkutano wetu. Katika ukurasa wa Facebook wa Chuo, niliona taarifa na picha za mkutano ule:
Hilo lilinivutia. Lakini niliona pia taarifa nyingine, kuhusu namna
mji wa Bemidji unavyomwenzi Mary Welsh, aliyekuwa mke wa nne na wa mwisho wa Ernest Hemingway. Mary Welsh alizaliwa karibu na Bemidji akakulia na kusoma mjini hapo.
Kisha alienda kusoma katika Chuo Kikuu cha Northwestern karibu na Chicago. Alikuja kuwa mwandishi katika magazeti hapo Chicago na hatimaye London, akajipambanua kama mwandishi wa habari za vita. Huko ndiko alikokutana na Ernest Hemingway na baadaye wakafunga ndoa.
Nilifahamu hayo yote na mengine mengi, kutokana na utafiti wangu wa miaka kadhaa. Nilifahamu tangu zamani kuwa Mary Welsh alizaliwa eneo la Bemidji, na nilikuwa nawazia kwenda kule kufanya utafiti juu yake. Mary Welsh Hemingway alitanguzana na Ernest Hemingway katika safari ya Afrika Mashariki mwaka 1953-54. Walizunguka Kenya, Tanganyika, hadi Uganda, ambako walipata ajali mbili za ndege, mfululizo.
.jpg)
Mary Hemingway alisafiri hadi Mbeya, na ameelezea hayo na mengi mengine katika kitabu chake kiitwacho
How it Was. Nasikitika kuwa wa-Tanzania, kwa kukosa utamaduni wa kununua na kusoma vitabu, hawafahamu hayo. Wangekuwa wana utamaduni huo, wangeweza kutumia habari na maandishi kama haya ya Mary Welsh Hemingway na Hemingway mwenyewe kwa manufaa makubwa, hasa katika utalii. Hali ni mbaya kwamba wa-Tanzania hawashtuki wakielezwa habari za vitabu namna hii. Nimethibitisha hayo, kama nilivyoandika
katika blogu hii.
Wenzetu katika nchi kama Cuba, Hispania na Marekani wanafaidika sana na maandishi ya Hemingway. Cuba wanaitunza sana nyumba ya Hemingway, Finca Vigia, na hata baa alimokuwa anakunywa, mjini Havana, ni kivutio kikubwa cha watalii. Kule Hispania kuna mji wa Pamplona ambao ulipata umaarufu duniani na umaarufu huu unaendelea, baada ya Hemingway kuutembelea na kuangalia mchezo wa "bull fighting," akaandika juu yake katika riwaya iitwayo
The Sun Also Rises. Maelfu ya watalii wanafurika Pamplona. Hapa Marekani, nyumba alimoishi Hemingway, kama vile kule Oak Park (Illinois)na Key West (Florida), ni vivutio vikubwa kwa watalii.
Hayo ndio yaliyonijia akilini wakati nasoma taarifa ya mji wa Bemidji kumwenzi Mary Welsh Hemingway. Jambo moja kubwa lililoelezwa katika taarifa ile ni utunzi wa tamthilia juu ya Mary Welsh Hemingway, unaofanywa na Catie Belleveau baada ya utafiti wa muda mrefu.
Hoja sio kwamba ni lazima nasi tujitose na kujishughulisha na Hemingway na mke wake, ingawa kufanya hivyo kungetuletea manufaa kama wanayopata wenzetu wa Cuba, Pamplona, Oak Park na Key West. Ninachotaka kusisitiza ni umuhimu wa kujifunza kutoka kwa hao wenzetu.
Sisi tunao waandishi maarufu kama Mgeni bin Faqihi wa Bagamoyo, aliyetunga
Utenzi wa Ras il Ghuli. Je, tunajua habari zake? Tunaye Shaaban Robert. Je, ni wa-Tanzania wangapi wanajua angalau mahali alipozaliwa, sehemu alimoishi, na mahali alipozikwa? Je? wahusika katika wizara za utalii na utamaduni wanafahamu habari hizo? Na je, wanafahamu kuwa taarifa hizo ni hazina ambayo tungeweza kuitumi? Binafsi ninatekeleza wajibu wangu kwa kuandika kuhusu mambo haya, kama nilivyofanya katika kitabu cha
CHANGAMOTO: Insha za Jamii, ambacho nitashangaa kikipata wasomaji Tanzania.