Friday, August 21, 2009

Simlaumu JK kwa kuzunguka duniani

(Makala hii imechapishwa katika KWANZA JAMII, Agosti 18-24, 2009)

Profesa Joseph L. Mbele

Katika makala zangu za hivi karibuni, nimegusia suala la kuiga mambo, kama vile mashindano ya urembo na suala la vyama vya siasa. Inaonekana suala hili litahitaji kushughulikiwa tena na tena. Katika makala yangu moja, niliongelea safari za JK nchi za nje, na baadhi ya watu walilalamika kuwa JK anasafiri mno. Walikumbushia kuwa viongozi wa nchi zingine za jirani, kama vile Kenya, hawasafiri hivyo, lakini nchi zao zinapiga hatua kutuzidi. Hitimisho likawa kwamba JK awaige viongozi hao; atumie muda mwingi nchini badala ya nje.

Wazo kuwa JK afanye kama wanavyofanya viongozi wa nchi zingine linahitaji tafakari. Napenda kuliongelea wazo hilo, kwa kutumia mfano huo wa Kenya na Tanzania. Je, kiongozi wa Tanzania anaweza kuiendeleza Tanzania kwa kuiga anayofanya kiongozi wa Kenya? Tanzania inaweza kuendelea kwa kuiiga Kenya?

Tanzania ni nchi yenye upekee. Kenya nayo ina upekee wake. Hizi nchi mbili zinatofautiana, kama zinavyotofautiana na Uganda, Rwanda, Congo, au Burundi. Tanzania ina historia yake, jadi yake, mtazamo wake, na malengo yake. Mahusiano ya jamii ndani ya Tanzania ni ya kiTanzania. Na Kenya ni hivyo hivyo. Kenya ina historia yake, jadi yake, na malengo yake. Mfumo wake wa uchumi na kijamii ni tofauti na wetu.

Mahusiano ya Kenya na nchi za jirani au nchi za mbali ni tofauti na mahusiano ya Tanzania na nchi za jirani yake au za mbali. Kenya inapakana na Somalia, Sudan na Uganda. Somalia kuna matatizo yanayoitishia Kenya pia. Masuala ya kiusalama yanayoihusu Kenya si sawa kabisa na yale yanayoihusu Tanzania. Tanzania ina utulivu kwa kiasi kikubwa, na hakuna mpaka wenye matatizo kwa wakati huu. Kiongozi wa Tanzania hakabiliani na hali halisi anayokabiliana nayo kiongozi wa Kenya.

Wakenya ni watu tofauti, na Watanzania ni watu tofauti. Sasa je, anayofanya kiongozi wa Kenya, au anayotakiwa kufanya kiongozi wa Kenya, yanaweza kutumika katika Tanzania? Au anayofanya kiongozi wa Tanzania, anayotakiwa kufanya kiongozi wa Tanzania, yanaweza kuwa sawa na yale ya Kenya. Kiongozi wa Tanzania anaweza kweli kuiongoza Tanzania kama vile ingekuwa Kenya? Au je, kiongozi wa Kenya anaweza kuiongoza Kenya kama vile ingekuwa Tanzania?

Mtu anayezunguka duniani ataona kuwa Wakenya wametapakaa duniani kuliko Watanzania. Mahali kama Marekani, kwa mfano, kama kuna chuo chenye waAfrika labda watatu au wawili, uwezekano ni mkubwa kuwa Mkenya yupo, na Mnigeria. Wakenya wanaoishi nje wanajituma katika masuala kama biashara na jumuia za kuleta maendeleo nchini kwao. Wanafanya mikutano, ambayo inahudhuriwa na viongozi kutoka Kenya, kwa madhumuni hayo. Nimewahi kuhudhuria hapa Minnesota.
Wakenya huku Marekani wanayo magazeti na vyombo vingine vya habari ambavyo wanavitumia kuitangaza nchi yao. Kenya imefanikiwa sana kujitangaza.

Serikali ya Kenya inashirikiana na hao waKenya waishio nje. Ilishaweka kitengo katika wizara yake ya Mambo ya Nchi za Nje cha kushughulikia masuala ya Wakenya hao. Kenya inajua kuwa waKenya hao wana mchango mkubwa katika uchumi wa Kenya. Hela ambazo waKenya walioko nje wanaingiza katika uchumi wa nchi yao ni zaidi ya mara nne kufananisha na zile wanazoingiza waTanzania walioko nje katika uchumi wao. Kwa kiasi kikubwa hii ni kwa sababu waKenya walioko nje ya nchi yao ni wengi zaidi kuliko waTanzania walioko nje ya nchi yao.

Mbele ya yote hayo, Rais wa Kenya ana sababu gani ya kuzunguka duniani kuitangaza nchi yake? Watu wake wanafanya hii kazi vizuri kabisa. Watanzania tunalalamika kuwa Wakenya wamefanikiwa hata kuutangazia ulimwengu kuwa Mlima Kilimanjaro uko kwao. Ni wazi kuwa, hata rais wa Kenya akikaa nchini muda wote, watu wake wako makini, walioko nchini na nje.

Sasa sisi Watanzania tukoje, hadi tudiriki kusema kuwa JK abaki nyumbani kama anavyofanya rais wa Kenya? Watanzania huku ughaibuni hatuwafikii waKenya katika masuala ya maendeleo ya nchi. Jambo hili nililitaja katika makala yangu kuhusu safari za JK nchi za nje. Watanzania tunakutana kwenye sherehe au misiba. Siku hizi, waTanzania walioko Ulaya, hasa Uingereza, wanajibidisha katika kufungua matawi ya CCM, badala ya kufanya shughuli za maendeleo na kuitangaza nchi kama wanavyofanya waKenya. Tunaanzisha matawi ya CCM badala ya kuanzisha angalau magazeti ya kuitangaza nchi.

Kwa upande mwingine, tofauti na ilivyo Kenya, Watanzania walioko nyumbani na wale walioko nje hawana mshikamano. Mtanzania wa nyumbani akisikia kuhusu Mtanzania anayeishi nje anamkejeli kuwa ni mlowezi au msaliti. Anaisema kuwa huyu aliyeko nje arudi nyumbani kujenga Taifa. Hata serikali yetu haijawa na mkakati wa kuwatambua hao waTanzania walioko nje na kuwashirikisha kikamilifu katika ujenzi wa Taifa. Serikali haijawa na kitengo cha kushughulikia masuala ya waTanzania walioko nje. Ni wakati huu tu ndio tunasikia taarifa kuwa utaratibu wa aina hii utaanzishwa.

Kwa kifupi, Watanzania bado tuna njia ndefu. Simlaumu JK kwa kuzunguka duniani akijaribu kuitangaza nchi yetu. Wajibu wa kiongozi wa Tanzania ni kutathmini hali halisi ya nchi yake na kuamua nini kinachohitajika. Wiki chache zilizopita, uongozi wa Chuo Kikuu cha Dodoma katika kuongelea masuala fulani ya hapo Chuoni, ulisema kuwa unaona matunda ya ziara za JK nchi za nje. Nilitegemea wale ambao wamekuwa wakipinga sana ziara hizo wangetoa kauli. Labda bado wanatafakari. Papo hapo, kabla ya Chuo Kikuu cha Dodoma kutoa kauli hiyo, Mheshimiwa Charles Stith, aliyekuwa Balozi wa Marekani hapa Tanzania, naye alisema kuwa ziara za JK nchi za nje zina manufaa. Nilitegemea wapinzani wa ziara hizo wangejitokeza kuinga kauli hiyo, lakini hawajajitokeza. Kama wanaamini kuwa JK abaki nyumbani, kwa nini wasijitokeze na hoja yao wakati huu? Naamini kuwa kadiri siku zinavyopita, ukweli utaendelea kujitokeza, kuwa kiongozi wa Tanzania anapaswa kufanya yale yanayotokana na tathmini ya hali hali
si na mahitaji ya Tanzania.

Thursday, August 13, 2009

Tunahitaji Vyama vya Siasa?

(Makala hii imechapishwa katika KWANZA JAMII, Agosti 11-17, 2009)


Profesa Joseph L. Mbele

Jamii yetu, kama jamii zingine, inatafuta namna ya kujenga na kuimarisha demokrasia. Katika harakati hii, uamuzi ulifikiwa kwamba tuwe na vyama vya siasa, badala ya chama kimoja. Vyama vya siasa vinapiganiwa karibu kila mahali kwa imani kuwa ni njia muhimu ya kujenga demokrasia. Kama kuna nchi isiyo na vyama vya siasa, utawala wa nchi hiyo unahesabiwa kuwa si wa kidemokrasia.

Kwa maana hii, kuuliza kama tunahitaji vyama vya siasa inaonekana ni upuuzi. Lakini mimi sioni kama ni suali la kipuuzi.

Demokrasia ni nini? Ni aina ya utawala ambamo umma umeshika hatamu. Demokrasia ni utawala unaowakilisha na kuendeleza matakwa na maslahi ya umma. Hii ndio maana ya demokrasia. Dhana ya vyama haiko kwenye tafsiri hii, kwani sio msingi au uhai wa demokrasia. Ni namna gani demokrasia inaweza kujengwa? Ili demokrasia iwepo, ni lazima kuwe na vyama? Haya ndio masuali ya kujiuliza.

Huko Ulaya, katika historia yao na mazingira yao, waliamua kuwa mfumo wa vyama vya siasa ndio wanaouhitaji kwa kujengea na kuwezesha demokrasia. Huo ulikuwa uamuzi wao, kufuatana na hali halisi ya kwao.

Lakini je, Watanzania tulikaa lini tukatathmini historia na mazingira yetu, hadi kufikia uamuzi kuwa ili tuwe na demokrasia, tunahitaji mfumo wa vyama? Tumefanya hiyo tathmini au tumeiga tu? Je, kinachofaa au kuhitajika Ulaya ni lazima kiwe hiki hiki hapa kwetu? Hili ni suali muhimu.

Je, hatukuwa na historia na jadi yetu ambayo tungeweza kuitumia katika kujenga demokrasia yetu? Je, kwa nini tumeshindwa hata kuwazia hilo? Mataifa yanayotutawala kiuchumi nayo yanatushinikiza tuwe na vyama vya siasa. Je. huu si ukoloni mambo leo, ambao watu kama Frantz Fanon waliuelezea?

Vyama vya siasa tumevipata, na huenda vikaongezeka. Je, vimetusaidia au vimetuletea matatizo? Ni wazi kuwa katika nchi yetu, vyama vya siasa vimeleta mfarakano, ambao unazidi kuota mizizi. Kampeni za uchaguzi zinaendelea kuwa na sura ya magomvi. Kadiri siku zinavyopita, amani inazidi kuharibika. Hayo yote yako wazi, lakini wazo la kuhoji umuhimu wa vyama vya siasa halisikiki.

Mtu anaweza kusema kuwa tunaweza kuendesha siasa ya vyama vingi kwa amani na utulivu. Lakini hoja hii haitavunja hoja yangu ya msingi kuwa tumeiga mambo kikasuku.

Tunataka demokrasia. Hilo ni wazi. Ingekuwa bora iwapo tungetafuta mfumo tofauti wa kujenga na kuendeleza hiyo demokrasia, mfumo unaotufaa kwa mujibu wa historia, jadi na mazingira yetu. Mfumo huu ungekuwa ni wetu, usio na chembe ya kushinikizwa kutoka nje, kama ilivyo sasa.

Kuna tatizo gani, kwa mfano, kuwa na mfumo ambao ungetumia busara za wazee kama ilivyokuwa katika jadi zetu? Ingewezekana kila kijiji, tarafa, au wilaya kuwachagua wazee wenye busara na kukubalika, wakawa ndio wawakilishi kwenye ngazi hizo na kiTaifa pia. Kwa busara zao, hao wangewasilisha maoni na mahitaji ya jamii zao, kuanzia watoto hadi wazee, wanawake kwa wanaume.

Katika maisha ya kila siku ya jamii yetu, wazee wanashika wadhifa huo. Mbunge ambaye tunamchagua kwa mtindo huu wa vyama vya siasa anaweza kupotea muda mrefu, asionekane hadi wakati wa uchaguzi ujao, lakini masuala ya jamii anayopaswa kuiwakilisha yanatatuliwa na wanavijiiji wenyewe kwa njia zao za asili. Kuna wabunge ambao ni kama watalii kwenye majimbo yao ya uwakilishi, lakini maisha ya wanavijiji kwenye majimbo hayo yanaendelea kwa msingi wa utaratibu ambao si wa vyama, ikiwemo jadi ya kuwatumia wazee.

Miaka ya karibuni, tumeona kitu cha aina hiyo kikifanyika katika kutafuta ufumbuzi wa masuala ya bara la Afrika. Wazee kama Askofu Desmond Tutu, Jimmy Carter, na Kofi Annan, wamepekwa kushughulikia masuala kama yale ya Zimbabwe. Katika migogoro ya Somalia, mara kwa mara wazee wamekuwa ndio watafutaji wa suluhisho. Miezi kadhaa iliyopita, wazee hao walikusanyika Kenya, wakafanya mazungumzo ya muda mrefu kutafuta ufumbuzi wa matatizo ya nchi yao. Hapa Tanzania, tuliona jinsi Rais Ali Hassan Mwinyi alivyokuwa na utaratibu wa kuongea na wazee wa Dar es Salaam, kuhusu masuala muhimu ya kiTaifa. Binafsi, naona Mzee Mwinyi alikuwa na upeo mzuri ambao ungepaswa kuimarishwa. Mifano hii yote inaendana na hoja ninayojaribu kujenga hapa, kuhusu umuhimu wa waAfrika kutafuta mifumo inayofaa kwa demokrasia katika mazingira yetu.

Utawala wa nchi si lazima uwe kwa mfumo chama cha siasa au vyama vya siasa. Nchi inaweza kutawaliwa bila chama au vyama. Kuwepo au kutokuwepo kwa demokrasia ni suala ambalo si lazima lihusishwe na vyama. Unaweza kuwa na demokrasia bila vyama, kama ilivyokuwa enzi za mababu na mabibi zetu, kabla ya kuja wazungu. Hapakuwa na vyama. Lakini, kama Mwalimu Nyerere alivyoandika, wazee walikuwa wanakaa chini ya mti na kujadiliana masuala hadi kukubaliana. Hii ilikuwa ni demokrasia, bila vyama.

Kinachohitajika ni sisi kufanya tafakari sisi wenyewe, si kudandia mambo ya Ulaya kama tunavyofanya. Uganda imeonyesha mfano, ina mfumo ambao inaona unafaa katika nchi ile, kufuatana na historia na mazingira yake. Mfumo wao unaweza kuwa na dosari, lakini angalau ni matokeo ya tathmini yao wenyewe. Wanaweza kuubadili wakaunda mwingine, kufuatana na hali halisi, bila kuiga kikasuku. Hizi ni fikra za watu huru. Kwa kutumia na kuthibitisha uhuru wa fikra na uamuzi, kila nchi katika bara letu, ingeweza kujitungia mfumo wa aina yake, kwa mujibu wa hali halisi ya nchi ile. Kwa mtindo huu, tungejenga demokrasia ya kweli, kudumisha amani na mshikamano, na kuleta maendeleo, sio fujo hizi tunazoziendekeza sasa kwa kisingizio cha ushindani wa kisiasa.

Tunahitaji demokrasia, yaani mfumo wa utawala ambao chimbuko lake na nguvu zake ni umma, mfumo ambao unasimamia na kuendeleza maslahi ya umma. Lakini je, ili hayo yawepo, tunahitaji vyama vya siasa? Hili ndilo suali linalohitaji jibu.

Saturday, August 8, 2009

Je, Tunaweza Tukawa na Mrembo wa Tanzania?

(Makala hii ilichapishwa katika KWANZA JAMII, Agosti 4, 2009)

Profesa Joseph L. Mbele

Kwa wiki kadhaa nimewazia kuandika makala kuhusu mashindano ya urembo. Katika Tanzania ya leo, mashindano hayo yameshamiri katika miji mikubwa na yanazidi kuenea.

Kwa upande moja nimekuwa sipendezwi na mashindano hayo. Nimekuwa nikijiuliza kama yana maana gani katika jamii yetu, kwani ni wazi kuwa mwenendo wake ni wa kuigwa kutoka nchi za magharibi. Ninayachukulia kama ishara nyingine ya ukoloni mambo leo.

Kwa upande mwingine, nimelazimika kukubali kuwa yamesaidia kwa namna mmoja au nyingine kuitangaza nchi yetu, wakati washiriki wanapoenda nje wakiwa na bendera ya nchi yetu. Vile vile, washindi wa mashindano hayo wameweza kufanya mambo ya maana katika jamii yetu. Wamekuwa watu maarufu nchini, wenye mvuto na uwezo wa kuhamasisha shughuli mbali mbali za manufaa kwa jamii. Wengine wameweza kujijengea msingi wa kujiendeleza kimaisha, kama vile kuwa wanamitindo katika nyanja za kimataifa. Hayo nimeyawazia na kuyazingatia. Ni mifano ya manufaa yatokanayo na mashindano hayo.

Lakini duku duku haziishi. Masuali hayaishi. Bado ukweli uko pale pale kuwa mashindano hayo yanayoshamiri siku hizi ni mambo ya kuiga. Si yetu. Vigezo vinavyotumiwa ni vya kuigwa; si vyetu. Tunashinikizwa tufuate vigezo vya Ulaya. Kwa mfano, wanawake wanaoshiriki mashindano hayo ni lazima wawe wembamba, au wembamba sana. Wanene hawakubaliki.

Hii ni ajabu katika nchi yetu na bara letu kwa ujumla, ambamo vigezo vya uzuri wa mwanamke ni tofauti. Katika mila na desturi za makabila yetu, kuna vigezo vya urembo, tofauti na hivi vya Ulaya. Kwa ujumla, unene ni uzuri, jambo la kujivunia. Katika makabila mengi, kulikuwa na mila ya kuwanenepesha wasichana kabla ya kuolewa.

Pamoja kushamiri kwa mashindano ya urembo, siamini kuwa katika mioyo ya waTanzania, dhana ya kuuenzi unene wa mwanamke imetoweka. Bado unene wa mwanamke ni jambo linalomfanya avutie. Kwa nini basi, tunajitumbukiza katika mashindano ya urembo ambayo vigezo vyake ni tofauti na hisia zetu? Naamini kuna baadhi ya waTanzania, kama vile vijana waliokulia Ulaya au Marekani, ambao wanalelewa katika mtazamo wa huko walikokulia hata kwenye suala la vigezo vya urembo. Lakini je, hisia za Mtanzania wa kawaida ni zipi?

Mashindano ya urembo ni jambo la kawaida katika jamii za binadamu. Hapa Afrika hali ni hiyo hiyo, tangu enzi za mababu na mabibi. Kwenye ngoma ilikuwa ni sehemu maalum ya mashindano hayo. Katika utungo wake maarufu uitwao “Wimbo wa Lawino,” mwandishi Okot p’Bitek wa Uganda alielezea vizuri jadi hii ya wasichana na wavulana kushindana kwenye ngoma katika kabila la Acholi.

Ili tuwe na upeo mpana wa kujitambua, tujiulize, je, kwa mila na desturi zetu, vigezo vya urembo wa mwanamke ni vipi? Vigezo vya Mmasai ni vipi? Vigezo vya Mnyakyusa, Mmakonde, au Mhaya ni vipi? Je, tunaweza tukawa na mrembo wa Tanzania? Naamini kuwa, ili tuwe na mrembo wa Tanzania, ingebidi sisi wenyewe tukae tukubaliane vigezo badala ya kuiga vigezo vya Ulaya.

Leo hii, mashindano haya ya urembo ambayo yanatumia vigezo vya Ulaya yanazidi kushamiri nchini mwetu. Mwishowe yatafika hata vijijini. Hata katika vyuo vikuu vya Tanzania, mashindano hayo yanayotumia vigezo vya Ulaya yanapamba moto. Nilitegemea kuwa vyuo vikuu ni sehemu ya kutafakari masuala na mambo ya jamii, mahala pa kufanya uchambuzi na kujua baya na jema. Haipendezi kuona kuwa chuo kikuu, badala ya kuwa mahali penye watu wa kuongoza njia, panakuwa ni mahali pa watu waliopotea njia.

Huko Ulaya na Marekani baadhi ya watu wameanza kutambua madhara yanayoendana na mashindano ya urembo. Watu wameanza kutambua kuwa shinikizo wanalowekewa wanawake kuwa wembamba linawafanya wajitese kwa mazoezi, wajinyime chakula au wale vyakula vya aina fulani tu na kwa mpangilio fulani maalum. Matokeo yake, angalau kwa baadhi ya wahusika, ni kujikosesha lishe bora, kudhuru afya, na kuugua maradhi mbali mbali. Kuna pia matatizo ya kisaikolojia miongoni mwa wasichana. Hawajisikii vizuri au wanajichukia kwa kuambiwa kuwa hawapendezi kutokana na umbo lao. Wasichana na wanawake wanene wengi wanaishi na masononeko na hata kujichukia kutokana na suala la unene.

Nafahamu kuwa unene wa aina fulani ni dalili ya afya mbaya, au ni hatari kwa afya. Hakuna ubishi kuwa unene wa aina hiyo ni jambo lisilohitajika. Tatizo la mashindano ya urembo ni kuwa hata unene wa kawaida tu hauruhusiwi. Hapo ndipo penye tatizo.

Tufikirie masuala haya ili tuweze kuinusuru jamii yetu. Huko Ulaya, baadhi ya wanawake wanene wamechoshwa na hali ilivyo, na wanarudisha hadhi ya unene katika urembo. Wanaendesha mashindano ya uzuri wa wanawake wanene, kupinga haya mashindano yanayotamba, ambayo yanasifu wembamba tu.

Labda tunahitaji kujielimisha upya, ili tuweze kuliona suala la urembo kwa upeo mpana zaidi. Mwandishi wetu maarufu, Shaaban Robert, aliwahi kutunga shairi ambamo tunawasikia wanawake wakisifia uzuri wao. Mwanamke mnene anasifia unene wake, na mwembamba anasifia wembamba wake. Na wote wanafanya hivyo kwa ufasaha na mantiki nzuri. Naamini kuwa Shaaban Robert alituelekeza katika njia nzuri.

Saturday, August 1, 2009

Nilivyoenda Zanzibar na Pemba Kuwaongelea Wamarekani

Tarehe 16 Machi, 2005, nilipata barua pepe kutoka Ubalozi wa Marekani Tanzania. Ujumbe ulikuwa ni ombi kama nitakapokuwa Tanzania nitaweza kutoa mihadhara kwa waTanzania kuhusu utamaduni na jamii ya Wamarekani. Ujumbe ulifafanua kuwa itakuwa ni juu yangu kuamua nini cha kuongelea: mazuri, mabaya, hata mabaya kabisa. Nilikubali ombi hilo. Nilipofika Tanzania, niliwasiliana na Ubalozi, na maandalizi yalifanyika, kuniwezesha kwenda Zanzibar na Pemba, tarehe 15 na 16 Agosti, 2005.

Matangazo yalitayarishwa na kubandikwa sehemu mbali mbali Zanzibar na Pemba. Nilisindikizwa kwenye ziara hii na Bwana David Colvin, ofisa utamaduni katika Ubalozi wa Marekani. Yeye ndiye aliyekuwa ananitambulisha kwa wenyeji wangu, kwani alikuwa amewazoea. Mhadhara wa kwanza ulifanyika katika Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar.


















Walikuja watu wengi. Kwa bahati nzuri baadhi nilikuwa nawafahamu, tangu walipokuwa wanafunzi wangu katika chuo kikuu cha Dar es Salaam. Walikuwepo pia wanafunzi kutoka Ulaya, waliokuwa wanasoma kiSwahili hapo Chuoni. Mhadhara wangu ulitokana na yale niliyoandika katika Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Ilikuwa fursa nzuri ya kuwaleza waTanzania mambo kadhaa yanayoweza kuleta matatizo ya kutoelewana baina ya waTanzania na waMarekani. Baada ya mhadhara, kilifuata kipindi cha masuali. Jambo mojawapo lililoleta msisimko ni jinsi dhana ya tabia njema au heshima ilivyo katika jamii ya kiMarekani, na jamii ya kiTanzania.













Nililala Zanzibar na siku ya pili nikaenda Pemba. Nilipokelewa uwanja wa ndege na bwana mmoja ambaye alinikumbusha kuwa alikuwa mwanafunzi wangu Chuo Kikuu cha Dar es Salaama miaka iliyopita. Tulienda hadi mjini Chake Chake, na hapo nilipokelewa kwa ngoma ya Msewe.
Nilifurahi sana kuiona Pemba. Ilikuwa ni mara yangu ya kwanza. Mhadhara wangu ulifanyika katika jumba la makumbusho, ambalo Ubalozi wa Marekani umegharamia ukarabati wake. Ukarabati huu umewezesha kuhifadhiwa kwa vitu vingi vya thamani katika historia na utamaduni wa Pemba. Ni hazina kubwa kwa vizazi vijavyo.













Mhadhara wangu ulikuwa sawa na ule wa Zanzibar. Watu walijaa ukumbini, na wengi walilazimika kusikiliza wakiwa nje ya ukumbi.
Wakati wa masuali, wengi waliulizia kwa huzuni kuhusu sera za Marekani kwa nchi za kiIslam. Walitaka ninaporudi Marekani nielezee hisia na masikitiko yao kuhusu sera hizo huko Iraq, Afghanistan, Palestina, na kwingineko. Niliwahakikishia kuwa Wamarekani wenyewe hawana kauli moja kuhusu sera hizo. Wananchi wengi wanazipinga. Niliwaelezea kuwa hata wakati niliposoma Marekani, miaka ya Rais Reagan, niliona Wamarekani wengi wa kawaida walivyokuwa wanapinga sera za serikali ya Reagan huko Nicaragua na sehemu zingine.













Hii ni kati ya ziara ambazo sitazisahau. Pamoja na yote niliyoweza kuongea kuhusu waMarekani, nilifurahi kupata bahati ya kuiona Pemba kwa mara ya kwanza maishani. Nawajibika kutoa shukrani kwa Ubalozi wa Marekani Tanzania kwa kunipa fursa hii ya kuiona sehemu ya nchi yangu. Namshukuru sana Bwana David Colvin kwa kunipa picha nyingi, zikiwemo nilizotumia hapa.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...