Thursday, September 12, 2013

Wa-Tanzania Tusiwachokoze Wanya-Rwanda

WaTanzania tunapaswa kuwa waangalifu sana tunapoongea na Wanya-Rwanda au tunapowaongelea. Hao ni watu ambao wamepitia majanga ambayo waTanzania hatuwezi hata kufikiria.

Wengi wao wameshuhudia ndugu, jamaa, marafiki wakiuawa kikatili. Wengi wameshuhudia familia yao yote ikichinjwa kwa mapanga. Wengi waliachwa wakiwa wakiwa tangu utotoni. Majanga yaliyowapata, sisi waTanzania hatujawahi kushuhudia katika maisha yetu, na hata tukijaribu kufikiria, tutakuwa tunaelea hewani tu. Undani wake na ukweli wake hatutaweza kuuelewa.

Wa-Tanzania tunashangaa kwa nini wanya-Rwanda wamepandisha jazba sana kutokana na ushauri wa Rais Kikwete kwamba wafanye mazungumzo na wapinzani wao walioko Kongo. Hatuelewi kwa nini ushauri uliotolewa kwa nia njema, kwa vigezo vyetu, umewatibua kiasi hicho. Wa-Tanzania wengi wameamua wanya-Rwanda wamevuka mpaka katika msimamo wao.

Ninaamini wa-Tanzania tunakosea katika kudhani hivyo. Angalia Israel. Mauaji ya kimbari yaliyowapata wa-Yahudi miaka ya elfu moja mia tisa arobaini na kitu hawajasahau hata chembe. Na mtu asithubutu kuwagusa kwa hilo; atatonosha vidonda na kuamsha jazba kali kuliko maelezo.

Hapa Marekani, kwa mfano, kila mtu, kila kiongozi wa serikali, anaogopa kulipuuzia au kulifanyia mzaha tukio la mauaji yale ya kimbari. Hakuna anayethubutu kuwashauri wa-Yahudi wafanye mazungumzo na yeyote ambaye ni mhusika au mtetezi wa mauaji yale. Hakuna mtu anayeweza kushinda urais hapa Marekani kama hathibitishi wazi wazi kuwa atasimama sambamba na Israel kama rafiki.

Wa-Yahudi waliunda kitengo cha utafiti cha Simon Wiesenthal, ambacho kazi yake kubwa ni kuwasaka na kuwanasa wote waliohusika na mauaji yale. Kitengo hiki kimefanya kazi sana na kinaogopwa kwa umakini wake katika kuwasaka na kuwanasa watuhumiwa popote duniani. Hisia za wa-Yahudi kuhusu mauaji ya kimbari yaliyowapata, ni kama vile yalitokea mwaka uliopita.

Ingawa wanya-Rwanda hawajaunda kituo kama hiki cha Simon Wiesenthal, sina shaka kwamba hisia zao ni sawa na zile za wa-Yahudi. Ni kitulizo cha aina fulani kwamba mahakama ya kimataifa ya mauaji ya kimbari imesaidia na inaendelea kusaidia kufanikisha jukumu la kuwasaka na kuwafikisha mahakamani wahusika au watuhumiwa wa mauaji ya kimbari.

Nimeona nitumie mfano huu wa wa-Yahudi, ili kufafanua ushauri wangu kwamba wa-Tanzania tuwe waangalifu sana tunapoongea na wanya-Rwanda.  Kitu tunachokiona sisi ni kidogo, kwao ni janga la kutisha kuzidi jinamizi lolote. Tahadhari hii inapaswa izingatiwe hasa na vyombo vyetu vya habari.

3 comments:

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Kaka Mbele wacha nikupinge. Hatuwezi kutumia kigezo cha yaliyowakuta wanyarwanda eti kukubali wafanye kila upuuzi bila kuwaambia kuwa hii siyo. Hii itakuwa ni kuwadekeza. Hata hao wayahudi kama si kutumia mkasa wao kujijenga bado wanaonywa wanapokosea. Mfano hakuna mtu mwenye akili anayewaunga mkono wayahudi wanaowaonea wapalestina utadhani wao ndiyo waliowaua sawa na Rwanda inavyowaonea Wakongoman utadhani ndiyo walisababisha mauaji ya kimbari. Kimsingi Kikwete alichotaka kuepuka ni kurudiwa kwa mauaji ya kimbari. Kwa wanaokumbuka ni kwamba hawa walio madarakani waliishi Uganda kwa miaka mingi wakijijenga kuja kuchukua madaraka. Walifanikiwa baada ya kuchapwa kwa muda mrefu walipodungua ndege ya rais na kuanzisha maafa.
Sidhani kama yaliyowapata Wanyarwanda yanahusiana na tabia ya kujiona bora kwa baadhi kutokana na kasumba waliyolishwa na wakoloni. Kama wakikosea wataambiwa ukweli bila kujali walipata maafa au la. Hii ndiyo tabia ya ukweli.

Mbele said...

Shukrani kwa ujumbe. Kwa watu walioelimika, na hapa namaanisha elimu kweli, sio wale wanaoringia vyeti vya chuoni, wakati hawajaelimika, kupinga na kupingana kwenye hoja ni wajibu.

Kwa kweli, binafsi falsafa yangu ni kwa nikishakuwa na msimamo fulani, ni wajibu kutafuta namna ya kuuhoji au kuupinga msimamo huo. Elimu haina mwisho, na unachoamini leo kuwa ndio ukweli ukikifanyia tafakari na utafiti unaweza kugundua kilikuwa na walakini.

Kwa hivyo, mtu anapopinga mawazo yangu kwa hoja, ni jambo jema.

Baada ya huu utangulizi, napenda kusema kuwa masuala ya jamii aghalabu huwa tata. Sio rahisi kuyafanyia uamuzi moja au kuyatafsiri kwa namna moja, ikawa ndio mwisho wa habari.

Inahitaji misimamo mingi, tathmini nyingi, napo hatuwezi kusema tumehitimisha masuala husika.

Kuhusu suala Rwanda, kama unavyofahamu, kuna tafiti nyingi zimefanywa na zinaendelea kufanywa. kuna vitabu na makala nyingi, na bado vitabu hivi na makala, zenye tafsiri mbali mbali vinaendelea kutolewa.

Kuna hata filamu iitwayo "Hotel Rwanda," ambayo wanya-Rwanda wengine wanadhani inasema ukweli na wako wanaoilaani.

Katika masuala haya ya jamii, sisi sote tunakuwa sawa na wale vipofu saba waliomshikashika tembo na kila mmoja akaja na tafsiri yake kuhusu tembo alivyo. Aliyeshika mkia akaja na lake; aliyemshika mguu akaja na lake; aliyemshika sikio akaja na lake; aliyemshika mkonga akaja na lake, na aliyeshika pembe akaja na lake.

Lililopo, na ndilo jambo la msingi, ni kuendeleza mjadala.

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Usomi kwangu si vyeti bali kuonyesha matunda ya unachojua ambacho kinaweza kuisogeza mbele jamii. Kwa mfano, mtu akiwa na PhD akatenda madudu kama ya akina Dk na Profesa Simone na Laurent Gbagbo au Dk Balali kwangu huyu si msomi bali mjinga aliyepoteza muda darasani.
Hivyo, turejee kwenye suala la Rwanda, kuwachokoza na yaliyowakuta. Bahati nzuri nilishaandika mengi kuhusiana na kadhia hii ambayo naijua tangu mwanzo hadi sasa. Tafiti zimefanyika ni kweli. Je nani walifanya hizo tafiti na walipewa pesa na nani? Ningepata tafiti angalau moja tukaizamia na kuona mashiko na upogo wake angalau tungepata pa kuanzia mjadala. Nijuacho, tamko na hitimisho la jumla lenye kujizungusha kwenye dhana ya woga, haliwezi kuwa nyenzo nuzuhu ya kuzalisha mjadala mkali kisomi.
Naomba nikupe kiungo au link ya makala yangu iliyochapishwa kwenye The African Executive Magazine kule Nairobi Kenya lau unaweza kujua nini ninachomaanisha.
http://www.africanexecutive.com/modules/magazine/articles.php?article=5138

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...