Aliniambia kuwa alifurahi sana kumsikia profesa akisema kuwa kitabu kimeandikwa na mTanzania. Alipiga picha kama kumbukumbu akawapelekea marafiki nyumbani. Kijana aliendelea kuniambia: "Nakupa hongera sana na mimi hii kwa njia moja ama nyingine imenitia nguvu ya kuendelea kusoma kwa bidii nifikie angalau nusu yako!"
Ninafurahi kuwa nimeweza kumtia kijana huyu hamasa ya kusoma kwa bidii. Kwangu kama mwalimu, haya ni mafanikio mazuri. Jambo mojawapo lililotamkwa katika "Azimio la Arusha" kuhusu mapinduzi yaliyokusudiwa Tanzania ni kwamba kazi iwe jambo la kujivunia. Nami najivunia kazi yangu.Vitabu vyangu kutumiwa katika vyuo vikuu si jambo geni kwangu. Vinatumiwa katika vyuo vya Marekani mara kwa mara. Lakini hii ni mara yangu ya kwanza kufahamu kuwa kitabu changu kinatumika China. Nimefurahi.
Ninamshukuru Seleman kwa kuniletea taarifa hii na kuniruhusu kuichapisha.
