Picha hii ilipigwa tarehe 27 Julai, 2019, Soma Book Cafe, Dar es Salaam. Wadau wa vitabu, yaani waandishi, wachapishaji, wauzaji, na wasomaji wa vitabu, tulikusanyika kuongelea masuala yanayotuunganisha.
Huyu ninayeonekana naye pichani ni Chiombola Joseph ambaye nilimfahamu siku hiyo. Nilikuwa nimetoa mhadhara kuhusu "Writing About Americans," naye akawa mmoja wa wale walionunua vitabu vyangu vilivyokuwa vikiuzwa na Soma Book Cafe. Napenda kusema neno juu ya hilo na mengine yatokanayo.
Uamuzi wa kununua kitabu si wa kawaida na si rahisi katika jamii yetu waTanzania. Huyu ndugu alinunua viwili. Sikumbuki wanauzaje, lakini lazima nusu laki au zaidi ilimtoka. Zingatia kuwa vitabu vyangu si udaku na haviko katika orodha ya vitabu vinavyofundshwa mashuleni na vyuoni nchini.
Anayeamua kununua vitabu vyangu Tanzania ninamwona kama mtu wa pekee. Najiuliza, ni nini kinachomtuma kufanya hivyo? Bila shaka ni hamu tu ya kutaka kujua mambo. Mimi mwenyewe niko hivyo. Sichoki kununua na kusoma vitabu.
Kwa upande wangu kama mwandishi, na ili kuwajuza wasomaji wangu, napenda niseme kwamba kitu kimojawapo kilichonisukuma kuandika hivi vitabu viwili ni kule kutoridhika kwangu na vitabu vya wengine nilivyovisoma.
Nilikuwa ninafundisha "Oral Literature" (fasihi simulizi) Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kuanzia mwaka 1976. Mwaka hadi mwaka, sikuona kitabu cha nadharia kilichoniridhisha kwa kufundishia somo hilo.
Jawabu likawa kwamba kulalamika kuhusu hali hakutoshi. Ni lazima kutafuta suluhu. Nikaamua kuanza kuandaa kitabu ambacho kingeniridhisha. Baada ya miaka 23 nilichapisha kitabu cha "Matengo Folktales." Hadi sasa ninaridhika nacho, na waalimu wengine wanakitumia kufundishia, kama vile hapa Marekani na Uingereza.
Habari ni hiyo hiyo kuhusu kitabu cha "Africans and Americans: Embracing Cultural Differences." Tangu kuja kwangu kufundisha hapa Marekani, mwaka 1991, nilihusika kama mshauri katika programu za ushirikiano baina ya vyuo vya Marekani na nchi za Afrika, ikiwemo Tanzania.
Nilikuwa mtoa ushauri katika masuala ya tofauti za tamaduni, ili kuwaandaa wanafunzi kabla hawajaenda Afrika, na pia baada ya wao kurejea tena Marekani, kujibu masuali yao kuhusu yale waliyoyashuhudia Afrika.
Niliona mapema kuwa hapakuwa na kitabu cha kuniridhisha kuhusu masuala hayo. Suluhisho likawa kuandaa kitabu changu, kazi iliyonichukua muda mrefu, hasa mwaka 2005 ambapo nilizama katika kazi hiyo tu kwa miezi yapata mitano. Ninaridhika na kitabu hiki, na maelfu hapa Marekani wamekisoma na wengi wanakisoma.
Hata hivi, ninaandika kitabu kingine juu ya mada hii ya tofauti za tamaduni, ili kufafanua zaidi mawilii matatu niliyoongelea au kugusia, na pia kuleta mapya.
Kwa hiyo, utaona kwamba kwa kiasi fulani, vitabu ninaandika kujiridhisha mimi mwenyewe, ingawa nina lengo la kuelimisha wengine pia. Ni kazi ngumu inayohitaji ustahimilivu mkubwa. Kama unawazia hela, utaona kuwa ni kazi isiyolipa. Ukitaka hela, achana na wazo la kitabu, uende Mererani ukatafute mawe ya tanzanite.
Mtu anayenunua kitabu changu namwona kama ameanzisha uhusiano fulani nami. Anaingia katika nafsi yangu na kujionea, angalau kwa kiasi fulani. Uhusiano huo ni wa kudumu, kwani si rahisi mtu kusahau kila alichosoma kitabuni, hasa pale anapokutana na jina la mwandishi au taarifa yoyote juu yake.