Thursday, July 16, 2020

Sasa Nimesoma "The Comedy of Errors" (Shakespeare)

Jana nilimaliza kusoma "The Comedy of Errors," tamthilia mojawapo ya Shakespeare, ambaye alliandika tamthilia 37, na labda zaidi kidogo. Katika ulimwengu wa fasihi, Shakespeare ni kinara. Wanafasihi wanaweza kuhoji kwa nini ninatumia neno fasihi kuziongelea tamthilia. Malumbano huenda yasiishe.

"The Comedy of Errors" ni tamthilia inayoelezea matatizo na mikanganyiko itokanayo na uwepo wa watu kadhaa katika jamii ambao wanafanana maumbile na sura kiasi kwamba ukikutana na mmoja, halafu baadaye ukakutane na mwingine, hutajua hata kidogo kuwa ni mwingine. Tamthilia hii inaonyesha migogoro, kutoelewana, na magomvi kwa sababu hiyo.

Kusoma maandishi ya Shakespeare kunahitaji mwendo wa taratibu. KiIngereza chake ni cha zamani, miaka mia tano iliyopita, na utamaduni ni vile vile. Ni chemsha bongo kwa sisi watu wa leo, sawa na kusoma tungo za zamani za kiSwahili kama vile "Al Inkishafi" au "Utenzi wa Rasi 'lGhuli." Kwa mtazamo wangu, chemsha bongo hii ina manufaa kwa afya ya akili, sawa na mazoezi ya mwili yalivyo na manufaa kwa afya zetu.

Shakespeare ni mwandishi wa waandishi. Alitambuliwa na anaendelea kutambuliwa hivyo na waandishi wakuu duniani. Shaaban Robert, mwandishi wetu maarufu kuliko wote, alisema kuwa akili ya Shakespeare ni kama bahari kubwa sana, ambayo mawimbi yake yalitua kwenye fukwe zote za dunia.

No comments:

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...