Leo ni siku ya furaha kwangu kwani nimechapisha kitabu kipya Chickens in the Bus: More Thoughts on Cultural Differences. Wasomaji wa kitabu changu cha mwanzo Africans and Americans: Embracing Cultual Differences, walikuwa wakiniuliza iwapo ninapangia kuandika kitabu cha pili katika mada ya hicho. Nami nilikuwa nikiwazia, na kwa miaka yapata kumi na tano, nilikuwa nikiandika insha fupi fupi kwa lengo la hatimaye kuzikusanya na kuzichapisha kama kitabu.Mtu anaweza kushangaa iweje nikatumia miaka kumi na tano kuandika kijitabu cha kurasa 40. Ni kwa sababu ninatambua kuwa uandishi bora unahitaji umakini wa hali ya juu. Ninaandika kiIngereza. Papo hapo somo mojawapo ninalofundisha hapa chuoni St. Olafni uandishi bora wa kiIngereza. Ninajua kuwa uandishi wa aina hiyo vigezo vyake ni "simplicity" na "clarity" ya hali ya juu kabisa. Kila sentensi ikidhi vigezo hivyo, na insha nzima ikidhi vigezo hivyo. Ninajikuta nikirebisha andiko langu mara nyingi sana, na ninajikuta ninakwama mara nyingi sana. Lakini baada ya miaka, matunda yanaonekana. Ndivyo ilivyokuwa kwa Chickens in the Bus.








