Tuesday, May 12, 2015

Vitabu vya Shaaban Robert

Jina la Shaaban Robert ni maarufu miongoni mwa wa-Tanzania na wengine wa nchi zingine wanaokijua ki-Swahili. Lakini, tujiulize ni wa-Tanzania wepi ambao wamesoma angalau vitabu vichache vya Shaaban Robert. Ni wangapi wamesoma au wanasoma mashairi yake, tenzi zake, insha zake, barua zake, na riwaya zake?

Ni wangapi wamesoma vitabu vyake vingine, kama vile Wasifu wa Siti Binti Saad, Maisha Yangu na Baada ya Miaka Hamsini, na tafsiri yake ya mashairi ya Omar Khayyam? Kama hatuna majibu ya kuridhisha, tuache kujigamba, kujidanganya na kudanganyana kuwa tunamwenzi mwandishi wetu huyu maarufu.

Ingawa kulikuwa na kipindi cha uhaba, leo vitabu vya Shaaban Robert vinapatikana kirahisi Tanzania, baada ya kampuni ya uchapishaji ya Mkuki na Nyota kuanza kuvichapisha upya. Mwaka hadi mwaka, ninapokwenda Tanzania, nimekuwa nikijinunulia vitabu hivyo, kama hivi vinavyoonekana pichani, sambamba na vitabu vya waandishi wengine maarufu katika lugha ya ki-Swahili.

Imekuwa ni faraja kwangu kuvisoma, baada ya kuzinduka kutoka katika mazoea ya kusoma zaidi maandishi ya ki-Ingereza. Ninajiona kama vile nimeanza kujikomboa kimawazo. Lugha yako ni utambulisho wako, na kuifahamu na kuitumia vizuri ni ishara ya kuiheshimu lugha hiyo. Ni ishara ya kujiheshimu.

Pamoja na kununua na kusoma vitabu alivyoandika Shaaban Robert, ninajitahidi kupanua akili yangu kwa namna nyngine pia. Ninayo maandishi yanayochambua maandishi ya Shaaban Robert. Mfano ni vitabu vinavyoonekana hapa pichani, kimoja cha A.G. Gibbe, na kingine cha Clement Ndulute. Maandishi mengine yamo katika majarida na vitabu vingine ambavyo baadhi ninavyo pia.

Ninajitahidi, kwa uwezo wangu, kushiriki katika kuandika kuhusu kazi za Shaaban Robert. Nimechapisha insha juu ya Shaaban Robert katika Encyclopaedia of African Literature iliyohaririwa na Simon Gikandi. Katika kitabu changu cha CHANGAMOTO: Insha za Jamii, kuna pia insha yangu iitwayo "Shaaban Robert: Mwalimu wa Jamii." Kadiri nitakavyokuwa naendelea kusoma maandishi yake, nategemea kuandika zaidi. Nina nafasi nzuri ya kufanya hivyo kwa kuwa ni mwalimu wa fasihi za kimataifa na nadharia ya fasihi.

7 comments:

emu-three said...

mkuu hongera sana, wakati mwingine nawaza kuwa huenda watu hawataki kusoma, bali wanataka kuangalia, lkn hata hizo mvie wanazoangalia chnazo chake ni vitabu, ni riwaya...sasa kwann watu wanakuwa hawana hamasa ya kusoma?

Mbele said...

Ndugu emu-three,
Shukrani kwa ujumbe wako. Kama ni hongera, unaweza kunipa hongera kwa kujitambua kwangu kuwa nina ujinga kichwani, na baada ya kujitambua hivyo, ninafanya juhudi ya kupambana na huu ujinga.

Kwa msingi huo huo, ni bora wapewe pole wajinga wasiojifahamu kuwa ni wajinga, na ni hao unaowaongelea, kwamba hawataki kusoma. Hao ni wajinga wa kupewa pole na kuhamasishwa wajitambue kama ninavyojitambua.

Adui ujinga, ambaye tulipopata Uhuru, Mwalimu Nyerere alituhamasisha tupambane naye, miaka ya baadaye adui huyo amekaribishwa kwa mikono miwili.

Hatuna uongozi unaoonyesha mfano wa kukabiliana na adui ujinga. Ujinga unatawala kiasi kwamba hata chama tawala, ambacho kinahujumu Mapinduzi, kinajiita na kinaitwa chama cha Mapinduzi. Wa-Tanzania wangekuwa wasoma vitabu, wangefahamu kuwa dhana ya Mapinduzi ilifafanuliwa katika "Azimio la Arusha," "Mwongozo," na kadhalika, na wangeelewa kuwa hiki chama tawala si chama cha Mapinduzi.

Hiki chama tawala kinatamba kwa kuwa jamii imegubikwa na ujinga. Jamii ingeamka, kwa kusoma vitabu, ingehoji mambo hayo.

Mambo ni mengi ya kuongelea. Nimegusia huu mfano moja tu wa siasa.

dogo said...

Nimefurahi kusoma maandishi yako. Nimejaribu kutafuta vitabu vya bwana Shaaban Robert hapa uingereza lakini sijafanikiwa. Naomba kama unajuwa njia ya kununua hivi vitabu kwa internet unisaidie kuvitafuta.

Mbele said...

Ndugu dogo, shukrani kwa ujumbe. Vitabu vya makampuni mengi ya uchapishaji ya Afrika, ikiwemo Mkuki na Nyota Publishers, vinasambazwa huko Ulaya na taasisi iitwayo African Books Collective. Hata hivi vitabu vya Shaaban Robert vinapatikana kupitia taasisi hiyo.

dogo said...

Ahsante sana bwana Mbele, nashukuru mwelekezo wako. Hongera kwa maandishi yako!

Unknown said...

Naomba msaada naweza kuvidowload wapi kupitia simu yangu? Au pdf

Unknown said...

Hizi nakala zaweza patikana wapi? Pdf

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...