Mwalimu Julius Nyerere alikuwa mwalimu. Naamini ni sahihi kusema kuwa silika ya ualimu iliathiri siasa na matendo ya Mwalimu Nyerere kama kiongozi wa Tanganyika na hatimaye Tanzania. Aliiona nchi yake kama darasa, na daima alikuwa anafundisha.
Ninachotaka kuongelea hapa ni mchango wa Mwalimu Nyerere katika uwanja wa elimu. Elimu ni suala mojawapo ambalo Mwalimu Nyerere alilishughulikia sana. Katika kuelezea suala la elimu, Mwalimu aliweka na kufuata misingi kadhaa muhimu.
Tanganyika ilipopata Uhuru, Mwalimu Nyerere alikuwa ameshajizatiti kubadilisha mfumo wa elimu uliokuwepo wakati wa ukoloni, ambao ulikuwa mfumo wa kibaguzi. Kulikuwa na shule za wazungu, za Wahindi, na za watu weusi. Mara tulipopata Uhuru, Nyerere alifuta ubaguzi na kuwachanganya wanafunzi mashuleni. Tangu mwanzo, Mwalimu Nyerere aliamini dhana ya usawa wa binadamu.
Mwalimu Nyerere aliamini kuwa elimu ni haki ya kila mtu. Alifanya kila juhudi kutoa elimu kwa watu wote, kuanzia watoto hadi watu wazima. Mwalimu alijitahidi kujenga mfumo wa elimu ambao ulitoa nafasi kwa yeyote kutokana na uwezo wa akili yake, bila kujali kama alikuwa maskini au tajiri. Kwa msingi huu, watu wengi ambao hawangeweza kulipia masomo walisoma hadi vyuo vikuu.
Mwalimu Nyerere alitaka elimu iwe inamjenga mwanafunzi kuwa mdadisi wa mambo na mwenye kiu ya kutafuta elimu. Yeye mwenyewe alikuwa mwanafalsafa, mtu wa kutafakari mambo. Na hivyo ndivyo alivyotaka elimu iwe. Mwalimu alitaka elimu iwe nyenzo ya kumkomboa mwanadamu, tofauti na elimu ya kikoloni, ambayo ilikuwa inaendeleza fikra tegemezi, fikra za kujidhalilisha, fikra za kitumwa. Alitaka elimu ijenge tabia ya kuheshimiana, sio kiburi cha usomi.
Mwalimu Nyerere alitaka elimu ijumlishe nadharia na vitendo, na ijenge tabia ya kushirikiana, si kushindana na ubinafsi. Vijana mashuleni alitaka wawe pia wanajishughulisha na kazi za mikono, kama vile kulima au kufuga na useremala. Hii nayo ni elimu, na ni fursa ya kufahamu mengi ambayo hayapatikani darasani. Kazi za mikono aliziona ni njia moja ya shule kujenga msingi wa kujitegemea kwa mahitaji yake.
Mwalimu Nyerere alifundisha kuwa elimu haina mwisho. Aliwahimiza watu kujibidisha katika kutafuta elimu. Mbali ya kushughulikia elimu ya watoto na vijana mashuleni, alianzisha mpango wa elimu ya watu wazima. Vijijini na mijini watu walihimizwa na walipata fursa ya kujiongezea elimu, kuanzia kujifunza kusoma na kuandika hadi kujipatia ujuzi na maarifa katika fani na taaluma mbali mbali.
Kwa utaratibu ulioitwa kisomo chenye manufaa, wavuvi, wakulima, seremala, wafugaji, na wengine katika shughuli mbali mbali, walihimizwa kujiongezea ujuzi kwenye fani na shughuli zao. Vitabu vilichapishwa katika fani za aina aina, ambavyo viliwapa watu fursa ya kujifunza kusoma na pia kujiongezea maarifa na ujuzi.
Kama Watanzania tungefuata mawazo ya Mwalimu, leo tungekuwa mbali kimaendeleo, na tungekuwa na mategemeo ya kufanikiwa zaidi. Katika dunia ya leo ya utandawazi, elimu, ujuzi na maarifa ndio msingi wa mafanikio. Lakini, Tanzania tuna matatizo makubwa, kwani ari ya kujielimisha imepungua sana, na watu wanatafuta vyeti badala ya elimu. Wengi wanaamini kuwa njia ya mafanikio ni kutumia mambo ya ushirikina, badala ya kujiongezea maarifa katika fani na shughuli mbali mbali, iwe ni kilimo, uvuvi, au biashara.
Nimeona jinsi Wamarekani wanavyojali elimu. Wanatumia fedha kununua vitabu, kulipia semina, na fursa nyingine kadha wa kadha za kujiongezea elimu, ujuzi na maarifa, ili wapate mafanikio katika shughuli zao, kama vile biashara. Watanzania tungekuwa tumefuata nyayo za Mwalimu Nyerere tungefanya hivyo hivyo: tungeona umuhimu wa kutumia fedha kununulia vitabu na kulipia warsha za kujiongezea ujuzi na maarifa katika shughuli mbali mbali. Imani ya kuwa maendeleo na mafanikio yanatokana na mambo ya kishirikina ni dalili za kuanguka kwa ule msingi aliokuwa anaujenga Mwalimu Nyerere. Je, Watanzania tutaweza kushindana katika dunia ya leo na kufanikiwa bila elimu, ujuzi na maarifa? Hilo wimbi la ushindani wa kimataifa tutaliweza au litatuzamisha? Hilo ni suala la kulitafakari.
Kuufahamu mchango wa Mwalimu Nyerere katika elimu ni sherti kuyapitia maandishi yake na hotuba zake. Baadhi ya maandisho hayo na hotuba hizo zilihusu elimu moja kwa moja, na baadhi ya kazi zake hizo ni hazina ambayo inatuwezesha kukusanya dondoo mbali mbali za kutuwezesha kuielewa falsafa na sera ya Mwalimu Nyerere kuhusu elimu. Kwa bahati nzuri, kuna kitabu kimechapishwa, kinachokusanya maandishi muhimu ya Mwalimu Nyerere kuhusu elimu. Kinaitwa Nyerere on Education/ Nyerere Kuhusu Elimu. Ni kitabu muhimu sana ambacho kinapatikana hapa: http://msupress.msu.edu/bookTemplate.php?bookID=3032