Viumbe "Anonymous" Katika Blogu

Kila anayepitia blogu mbali mbali atakuwa anaona maandishi yaliyoandikwa na viumbe viitwavyo "Anonymous." Mwanzoni, nilikuwa sioni ajabu wala kufikiria suala la viumbe hivi. Lakini, siku za karibuni, nimeanza kuvifikiria.

Ninapoona ujumbe umeandikwa na "Anonymous" huwa sioni sababu ya kujibu, kwani sielewi ni kiumbe gani kilichoandika, kama ni binadamu au mzimu. Na hata kama ni binadamu, sielewi kama ni jirani yangu au rafiki, ni mtu anayenifahamu au hanifahamu, na kadhalika.

Halafu, nikiviwazia hivi viumbe, suala zima la mijadala linakuwa kama sinema au hadithi ya ajabu ya Ughaibuni, ilivyoandikwa na Shaaban Robert katika kitabu chake cha Adili na Nduguze.

Ninapoona mlolongo wa maandishi kutoka kwa "Anonymous," nitajuaje kama ni "Anonymous" tofauti, au ni yule yule mmoja anatuchezea akili? Ni mambo ya Ughaibuni kabisa. Ni rahisi sana kwa "Anonymous" yule yule kuandika tena na tena, akitoa hoja mbali mbali, na sisi wasomaji tusigundue kuwa tunachezewa akili. Ndio maana huwa sitaki kujibizana na "Anonymous."

Juzi hapo nimerushiwa makombora na viumbe hivi kule kwa Michuzi , nami nikaogopa kujibu mapigo.

Kama viumbe hivi ni wanadamu wenzetu, kwa nini wasijitambulishe? Mimi ninapoandika kwenye hizi blogu, naweka jina langu. Ninafahamu kuwa mbele ya Mungu hakuna anayeweza kujificha. Kwa sisi Wakristu, dini inatufundisha kuwa siku ya kiyama, kila kilichofichika kitafichuliwa. Hii inanipa faraja moyoni, kwani kama hao "Anonymous" ni wanadamu wenzetu, nao tutawafahamu siku hiyo. Na hata kama ni mizimu, itafahamika pia.

Comments

Simon Kitururu said…
Huwa najiuliza swala hili mara nyingi ingawa najua ni haki yao kutotaka kujulikana wao ni nani.

Ila kuna mtu kaniuliza juzi kuwa kama kweli jina langu la kikweli ni Simon Kitururu.

Usishangae kusikia kuna watu wanadhani Prof. Mbele ni jina la Mtandaoni na jina lako la kikweli ni Hamisi!:-(
Mbele said…
Ni suala gumu, na naandika hivi nikiamini kuwa ninayemjibu ni kweli Simon Kitururu :-)

Iwapo kweli ni yeye, basi napenda kuongeza tu kuwa hata tukisema watu waandike majina yao, hatuna namna ya kuthibitisha, maana hatuwafahamu wanaBongo wote maelfu na maelfu wenye uwezo wa kupitia hizi blogu.

Ila napenda kukuhakikishia kuwa mimi ninayeandika saa hii ni huyu unayemtaja, wala si yule Profesa Ndumilakuwili wa gazeti la "Sani" :-)
Anonymous almaaruf ANON ni waheshimiwa wanaochezea akili za wengi. Wanajibu na kuuliza tena na tena na nyakati nyingine wanaamua kuwa upande utakaoendeleza mjadala. Pengine ni sahihi kujiuliza kama mimi ndimi Mubelwa, lakini kwa kuwa ninajulikana nilipo, naweza kurekebishika ama kuonywa kirahisi pale mimi ninapokosea ama pale inapotokea mtu mwingine kanitumia mimi (jina langu) kuchafua hali ya hewa ya mahala. Mfano ni kama wewe Simon ama Prof Mbele hapo mkiandika yaliyo tofauti, nina hakika kuna awajuaye atakayewauliza kama mko Ok. Ama kama mtu mwingine atatumia utambulisho wenu kuwadhalilisha na kuwagasi wengine, basi mtu atauliza kulikoni mmeandika mlivyoandika (kwani hawatojua kuwa ni nyinyi) na kisha mtaweza kujua kuwa kuna aliye nyie asiye nyie.
Hili nililiona zaidi Jambo Tanzania Chat ambapo yeyote anaweza kuingia kwa jina lako na kusema lolote awezalo kisha kuondoka. Afadhali kule kuna uwezekano wa ku-track IP ya mtu, kwa hiyo wakati mwinine wenye uelewa wangeweza kuelewa kuwa MUBELWA yule aliyetusi watu hakuwa na IP Adress ya eneo niishilo mimi kwa hiyo ANON anakuwa ameshindwa.
Lakini Anon ni "viumbe" ambao (mara nyingi) huchafua hali mahali watuapo na ndio maana hawapendi kuonekana
Hili jambo la viumbe wasijulikana kwa kweli ni ngumu. na nani anajua kama ni hawajulikana kama mliotangulia mmesema utajuaje kama mimi niandikaye sasa au nitoaye maoni sasa ni Yasinta?
John Mwaipopo said…
Kwanza nimependa hiyo ya "kama kweli mimi ni John Mwaipopo". Imeisha hiyo.

Pili inawezekana Simoni Kitururu na mimi ni dam-dam (Prof kiswahili hiki unakiweza?). Halafu namuogopa kupindukia. Sasa naamua kuwa ANON ili nimdhalilishe pasi na yeye kujua (ndio undumilakuwili huo)

Yote juu ya yote mvinyo mwema hauhitaji kichaka.
Ni yale yale. Unakuta katika gazeti habari karibu zote zimeandikwa na "mwandishi wetu" Mimi wala huwa sijihangaishi kuzisoma hizi habari za "mwandishi wetu"
This comment has been removed by the author.
Mbele said…
Profesa Matondo, ni kweli unayosema kuhusu "mwandishi wetu." Vile vile, utaona magazeti yanamnukuu mtu ambaye "hakutaka jina lake liandikwe." Kwa miaka mingi, nilikuwa nashangazwa na tabia ya magazeti ya nchi za "Magharibi," wakati yanaripoti taarifa za nchi kama zetu, kwani yalikuwa daima yanawanukuu "western diplomats" bila kuwataja majina.

Sasa, tabia hii ya kuwanukuu hao "western diplomats" ilikuwa inaimarisha kasumba vichwani mwetu kuwa "western diplomats" ndio wasema ukweli. Na ukizingatia kuwa hasa enzi za "vita vya baridi" propaganda ilikuwa kali, basi utaona kuwa hivi vyombo vya habari ni hatari kwa usalama wa vichwa vyetu.

Kuhusu hivi viumbe vilivyonitolea uvivu kule kwa Michuzi, ni kwamba mimi huwa sitingishiki. Ninapoona mara ya kwanza huwa nashtuka kidogo, lakini baada ya hapo huwa naanza kucheka. Ukurasa ule wa Michuzi niliwapelekea waTanzania kwenye jumuia iitwayo Tanzanet, nikiwa nimeweka mchapo kuwaambia waangalie jinsi nilivyopewa vidonge vyangu :-)

Huwa napenda kufanya utani, hata baada ya kulipuliwa kama nilivyolipuliwa kwa Michuzi.
Sophie B. said…
Prof. huwa naburudika kusoma blog yako maana ina mambo mengi ya kujifunza. Kwanza kuhusu hawa annon. mtizamo wangu ni kuwa hawana comfidence ya kujitokeza na kusimamia comments zao kwa maana hiyo ni kupoteza muda kujibizana nao
Pili kuhusu "mwandishi wetu." hata mie ilikuwa inanishangaza,nchi za wenzetu hata kutoa comment wanataka wakujue wewe ni nani.Mf. niliwahi kutoa comment ktk Newyork Daily News waliiweka comment hiyo baada ya kuhakikisha address yangu na simu japo hawazichapishi na hiyo ni comment tu na siyo habari!Namna hii ni kwangu mimi naona vizuri.
Tatu kuhusu watoa maoni kuhusu habari yako kwa Michuzi Prof Matondo amesummarise vizuri sana "...tunaongea sana hata kama mtu hana cha kuongea ni lazima aseme kitu. Watu tunatofautiana kwa mitazamo na jambo la msingi ni kujibizana hoja kwa hoja (kukubali kutokubaliana kwa heshima)". Nafikiri tutakapoelewa hili na kulipa umuhimu wake tutafika mbali.Ni kweli ni aibu. Endelea kutuelimisha tupo wengi tunaopenda kujifunza.

Popular posts from this blog

Kumbukumbu ya Kuzaliwa

Tenzi Tatu za Kale

Pesa za Majini