Monday, January 25, 2010

Kiapo cha Uraia wa Marekani

Mtu anapoomba uraia wa Marekani, anakula kiapo, wakati wa kupewa uraia huo, na katika kiapo hiki anatamka kuwa hatambui mamlaka ya kiongozi wa nchi anakotoka juu yake, wala hatambui mamlaka ya serikali ya nchi anakotoka juu yake. Anaukana kabisa utii na uaminifu kwa kiongozi, serikali au himaya ya nchi alikotoka. Kiapo ni hiki hapa:

I hereby declare, on oath, that I absolutely and entirely renounce and abjure all allegiance and fidelity to any foreign prince, potentate, state, or sovereignty of whom or which I have heretofore been a subject or citizen; that I will support and defend the Constitution and laws of the United States of America against all enemies, foreign and domestic; that I will bear true faith and allegiance to the same; that I will bear arms on behalf of the United States when required by the law; that I will perform noncombatant service in the Armed Forces of the United States when required by the law; that I will perform work of national importance under civilian direction when required by the law; and that I take this obligation freely without any mental reservation or purpose of evasion; so help me God.

7 comments:

Anonymous said...

Shikamoo Profesa Mbele!Asante kwa makala-kwa kweli inaserious implications.Lakini binafsi naona inaupungufu kwasisi wenye vichwa vizito kwavile haujatuelezea ubaya au uzuri wa kiapo hicho(although this is implied within the post) pamoja na historia yake(kwanini kiapo hiki kimetungwa kwa uzito huo?
).Nahisi pengine post itakua related na mada ya Uraia wa Nchi mbili Tz au? Mimi nimeomba kutoa hoja:http://wachumi.blogspot.com/

Mbele said...

Ndugu Majaliwa, shukrani kwa ujumbe. Mimi si mtaalam wa mambo ya sheria. Ila nilipoona kiapo hiki nilishtuka, na kwa wakati huu ambapo wa-Tanzania wanajadili suala uraia wa nchi mbili, naona ni vema wakaangalia suala zima kwa undani, na hasa kuangalia kwa makini sheria na masharti ya uraia wa kila nchi.

Nimeweka taarifa hii hapa kama changamoto, na nafurahi ulivyosema kuwa kuna "serious implications." Kama ni hivyo, tunawajibika kutafakari hizi "implications."

Isipokuwa nchi zinatofautiana sana katika sheria zao za uraia. Kwa maana hii, tunawajibika kuzichungulia nchi hizi moja moja, si mkupuo kama vile zote ni sawa. Lakini, kwa vile mimi si mtaalam wa sheria, nawaachia watalaam.

Hadi sasa, waTanzania wanaopigania uraia wa nchi mbili wametumia uhuru wao wa kujieleza, na wamefanikiwa kuandaa "petition" ambayo waliisambaza mtandaoni, na watu wengi wakatia sahihi. Kwa vile walitumia mtandao, inamaanisha kuwa hata mtu alikuwa Arusha au Mbeya, aliweza kuingia mtandaoni na kusoma "petition" ile na kutia sahihi.

Kitu cha msingi ni kuwa uhuru huu wanao wa-Tanzania wote. Kwa mfano, wale wanaopinga uraia wa nchi mbili, wanaweza pia kuandaa "petition" wakitaka, wakaisambaza mtandaoni au sehemu mbali mbali nchini. Wanaweza kuzunguka na petition yao mitaani, kwenye dala dala, na vijijini. Wana uhuru sawa wale wenzao walioandaa ile "petition" ya mwanzo.

Hata mimi ninao uhuru huo. Kwa mfano, ningeweza kuandaa "petition" yenye kiapo hiki cha Marekani ili kujenga hoja kuwa tunapoongelea suala la uraia wa nchi mbili, Marekani tuiweke kando kwa sababu ya kiapo chake cha kihasama kwetu. Nina uhuru wa kuandaa "petition" ya aina hiyo na kuisambaza ili kutafuta sahihi za watu.

Isipokuwa, msimamo wangu kwa sasa ni kama ifuatavyo.

Ninatambua kuwa wako watoto ambao wamezaliwa nchi za nje, kwa wazazi wa ki-Tanzania. Inawezekana wamezaliwa katika nchi ambazo zinawatambua kuwa ni raia wa nchi zile. Lakini naamini hao wana haki ya kuwa pia raia wa Tanzania.

Uraia wa nchi mbili naona wanastahili pia wale ambao mzazi wao mmoja ni m-Tanzania, na mwingine si m-Tanzania.

Kuhusiana na mjadala uliopo wa hii mada unayoitaja, ya uraia wa nchi mbili, msimamo wangu ni kuwa ziko nchi rafiki ambazo tungeweza kufanya nazo makubaliano ya uraia wa nchi mbili. Nchi hizi hazina masharti au sheria zenye hizi unazoita "serious implications."

Basi, ninapendekeza kuwa tutafakari uwezekano wa kutumia hali hiyo ya nchi rafiki na kuwa na uraia wa nchi mbili.

Tufanye tafakari kwa kila nchi, ili tunapoongelea kuruhusu uraia wa nchi mbili, tujue kinaga naga ni nchi gani hizo. Lakini nchi zenye sheria za utata, au "serious implications," sioni kama tuna sababu ya kujisumbua nazo kwenye hili suala la uraia wa nchi mbili. Tuachane nazo.

Labda huko mbele ya safari nchi hizo zitabadili sheria zao, na utata utakuwa haupo tena. Haya ndio mawazo yangu. Hii Marekani yenyewe tunayoiongelea haipendelei raia wake waombe uraia wa nchi zingine.

Halafu, tujiulize: Marekani yenyewe itamvumilia raia wao akienda kuapa kwenye nchi ya nje kiapo cha kuikana Marekani kwa lugha hiyo hiyo inayoonekana kwenye kiapo chao? Kama jibu ni hapana, kwa nini Tanzania ijidhalilishe?

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

PRof, huna mpango wa kbadili uraia wewe? ilikuwaje mpaka ukapata kiapo hiki?


ila tukijadili suala la uraia mimi sijaelewa vizuri juu ya Tanzania na utanzania wangu.

naiona tanzania kama colonial territory zaidi na hivyo labda ni y a wakoloni zaidi

ishu ya uraia sio shida. kimaumbile hakuna mipaka na unaweza ishi popote, leo unakana Utz, Kwsho Umarekani NK, ndio maana Prof.uko States leo! unaweza jiita mtz? si unalipa kodi huko na kuwatumikia huko? tuseme basi wewe ni raia wa huko kila unapokuwa huko na ni mtz kila unapokuwa Tz

nawapenda sana wafugaji na wakulima wa mipakani, wao hawajui mamboya mipaka ila wanajua ardhi nzuri kwa mifugo au kilimo, wanaenda popote bila pasport hata wakikamatewa na kushitakuwa wanaonewa, haiwahusu hiyo

Mbele said...

Ndugu Kamala, masuali yako ni murua sana, kwa sababu yanachangamsha akili. Na mimi nataka tuwe na tabia ya kuyashughulikia masuala kwa namna hiyo, kama fursa ya kujielimisha, si kwenda kipapara.

Niliwahi kusafiria pande za mwambao wa Kenya, nikifanya utafiti juu ya tungo za ki-Swahili na utamaduni wao. Kwenye mji moja mdogo uitwao Witu, kati ya Mombasa na Lamu, niliongea na wazee wa kiSwahili ambao walilalamikia sana suala la kuwepo mpaka baina ya Tanzania na Kenya. Wao waliniambia kuwa asili yao ni huku Tanzania. Walisema kuwa ni fedheha kuwa tuko kama Berlin. Walitaja Berlin kwa sababu ya ule ukuta uliokuwa unatenganisha mji ule.

Utaona kuwa kuwa na hizi tunazoziita nchi, ni mwendelezo wa ukoloni, kama unavyogusia. Na hapo tunakubaliana kuwa wafugaji kama Wamaasai, wana jambo la kutufundisha.

Ni kweli, mimi sijabadili uraia, ingawa nafanya kazi huku Marekani. Najihasabu kuwa ni m-Tanzania, na nitabaki hivyo.

Lakini ukihoji zaidi, hasa kuhusiana na hiki kiapo cha uraia wa Marekani, utaona kuwa kwa namna moja au nyingine, kwa kufanya kazi Marekani na kulipa kodi hapa, ninachangia uchumi wa Marekani, na pia ninachangia kulipia majeshi ya Marekani.

Ukiangalia hivyo, utaona kuwa siwezi kukwepa lawama. Lakini, ukiendelea kuchunguza zaidi, utaona kuwa mfumo wa uchumi wa dunia ya leo ni wa kibepari, na ni mtandao uliozagaa duniani kote.

Mkulima wa kahawa wa Bukoba au Mbinga, kwa vile kahawa hii inaingia kwenye hili linaloitwa soko la dunia, ambalo ni la hao mabepari, naye anachangia mfuko wa Marekani kwa namna moja au nyingine.

Makampuni mengi ya Marekani, ambayo yanalipa kodi hapa Marekani, yanafanya shughuli zake huko Tanzania pia, kwa mfano makampuni ya utalii. Na waTanzania wengi wanafanya kazi humo, kama vile mimi ninavyofanya kazi huku Marekani. Kwa hivi, maelfu ya wa-Tanzania hapa nchini wanatunisha mfuko wa Marekani, na wanachangia jeshi la Marekani.

Wafanyabiashara wengi hapa Tanzania wanauza bidhaa kutoka Marekani, kuanzia vipodozi, hadi viatu, nguo na vifaa vya ofisini au majumbani. Watanzania tunachangia mfuko wa Marekani kwa namna hiyo.

Mtanzania anapokunywa Coca Cola hapo nchini, anachangia mfuko wa Marekani, na anachangia jeshi la Marekani. Nikiendelea na huu mfano wa Coca Cola, napenda kusema kuwa kwa jinsi waTanzania wanavyopenda sherehe kubwa, kila sherehe ya arusi kwa mfano, ambako tunakuwa na kreti nyingi za Coca Cola, ni neema kwa Marekani na jeshi lao. Kwa namna hiyo, mamilioni ya waTanzania wanachangia uchumi na jeshi la Marekani.

Kwa hivi, utaona kuwa, kwa upande wa kuchangia Marekani kiuchumi, wote tunahusika, na hatuna kwa kukimbilia, hadi hapo tutakapokuwa tumeutokomeza mfumo wa ubepari. Sijui, labda siku itakuja.

Suali linalobaki sasa ni hili la kiapo. Mkulima wa kahawa wa Bukoba hajala kiapo cha kumkana rais wake au serikali yake. Mtanzania anayekunywa Coca Cola hapa Mbulu hajamkana rais wake wala serikali yake.

Kwa hivi, kinachobaki ni hiki kiapo. Ndicho kinachowatenganisha wa-Tanzania katika makundi mawili ambayo nadhani yataendelea kupingana. Sijui kama wazo hili ni sahihi, lakini kwa sasa ndio wazo langu.

Narudia kusema kuwa tuendelee kuangalia masuala kwa mtazamo wa kuzama katika tafakuri. Tujiulize masuali bila kusita wala kuchoka.

Anonymous said...

Asante profesa, ni kweli"tujiulize masuali bila kusita wala kuchoka."Na mnswali nimeongezea hapa,kwa vile nilipita idadi ya maneno yanayoruhusiwa na comments hapa!

http://wachumi.blogspot.com/2010/02/naomba-kutoa-hoja-nyongeza.html

Mzee wa Changamoto said...

Ninaloomba ni Maswali ya Kaka Kamala na majibu yako Profesa Mbele viwe topic kamili.
Binafsi naomba nikipata nafasi kuyanyofoa na kuwashirikisha wanitembeleao. Uchanganuzi wako Profesa katika maswali ya Kaka Kamala nimeupenda. Lakini naamini usingeandika hivyo bila kaka Kamala kuuliza. Kwa hiyo NAKUSHUKURU SAANA KAKA KAMALA KWA KUWAZA MASWALI UWAZAVYO. NA PIA KWAKO PROFESA KWA KUYAJIBU KWA UFASAHA.
Nimejifunza na sina la kuchangia.
Baraka kwenu

Mbele said...

Mzee wa Changamoto

Shukrani kwa ujumbe. Kwa vile sisi wanablogu tunahamasisha suala la kuelimishana, sina kipingamizi na wazo lako la kuyakarabati mawazo yangu au kuyatumia kwenye blogu yako. Nakutakia kila la heri.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...