Thursday, February 4, 2010

Kioo cha Lugha: Jarida la Kiswahili la Isimu na Fasihi

Leo nilienda posta nikakuta bahasha yenye vitabu ikiwa imetumwa Dar es Salaam. Sikujua ni vitabu gani. Nilipofungua nikakuta ni nakala za jarida la Kioo cha Lugha.
Nimefurahi kupata hazina hii nikiwa huku ughaibuni ambako natumia ki-Ingereza karibu muda wote. Sasa, kwa kusoma makala maridhawa zilizoandikwa na watafiti na walimu mahiri wa Tanzania, Kenya, na kwingineko, nitajiongezea ujuzi wa kutumia ki-Swahili katika taaluma, hasa isimu na fasihi.

Miaka ya karibuni nimepata msisimko wa kuandika kwa ki-Swahili, ili kujitoa katika giza la ujinga linalotukabili wasomi wengi. Ujinga huu ni pamoja na kutoelewa namna ya kutumia ki-Swahili ipasavyo, na pia kudhani kuwa ki-Swahili hakina uwezo sawa na lugha zingine katika kuelezea mambo, hasa taaluma.

Ninajitahidi kujikomboa. Mwaka jana, kwa mfano, niliandika makala nyingi kwa ki-Swahili, hadi nikachapisha kitabu. Wakati wa kuandika nilisoma kazi kadhaa za Shaaban Robert ili kujijengea uwezo na kujiamini katika kutumia lugha ya ki-Swahili. Ni kama muujiza kuwa leo nimeletewa majarida haya, kwani kiu yangu ya kujielimisha bado na itaendelea kuwa kubwa.

Natoa shukrani tele kwa Idara ya Kiswahili ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa kunikumbuka hivyo.

3 comments:

Masangu Matondo Nzuzullima (MMN) said...

Dah! Sijui hata niseme nini. Ni juzi tu hapa nilikuwa naulizia habari za jarida hili (na mengineyo) kwa Mkurugenzi Msaidizi wa Taasisi ya Taaluma za Kiswahili pale Mlimani. Nitajaribu kulitafuta hata kama ikibidi kumwambia mkutubi wetu hapa anayeshughulikia Afrika kuanza kuliagiza jarida hili na lile la KISWAHILI kila yanapotoka. Nikupe hongera prof. kwa KUKUMBUKWA!

pia sikujua kama jarida la tabaruku ya maprofesa Besha na Mochiwa lilishatoka. Hawa walikuwa walimu wangu wapendwa na ningependa sana kutoa mchango wangu kuwakumbuka.

Mbele said...

Hili toleo la tabaruku ya Profesa Besha na Mochiwa ni kati ya hayo niliyoletewa. Ni Juzuu namba 6, 2008.

Mimi nimo katika kamati ya uhariri, na ndio kisa cha kukumbukwa.

Nitaweza kukuletea angalau orodha ya makala zilizomo katika majarida haya.

Masangu Matondo Nzuzullima (MMN) said...

Nategemea kwenda huko hivi karibuni na nitakwenda kuyakusanya haya majarida na vitabu vingine. Kila nikienda huko begi langu huwa linajaa vitabu wakati wa kurudi mpaka wakati mwingine huwa inabidi kulipia faini kwenye ndege kwani vitabu ni vizito sana.

Orodha ya makala zilizomo katika jarida la tabaruku za profesa Besha na Mochiwa tu zinatosha.

Asante mwalimu

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...