Tuesday, October 9, 2012

Programu za Kupeleka Wanafunzi Nje

Leo hapa chuoni St. Olaf, tumefanya shughuli ya kutangaza programu zinazowapeleka wanafunzi kwenye masomo nje ya chuo hapa Marekani na nchi za nje. Ni shughuli ambayo tunafanya kila mwaka, wakati kama huu. Tunawapa wanafunzi fursa ya kuzifahamu programu hizi. Mimi ni mshauri wa program ya ACM Tanzania, ACM Botswana, na Lutheran Colleges Consortium for Tanzania (LCCT).









Chuo cha St. Olaf kinaendesha programu nyingi sehemu mbali mbali duniani. Pia kinashiriki katika programu za vyuo na taasisi nyingine, kwa maana kwamba wanafunzi wa chuo hiki wanayo fursa ya kujiunga na programu zile. Kuna programu za mwezi mmoja, muhula mmoja, na hata mwaka.


















Chuo cha St. Olaf ni maarufu hapa Marekani kwa programu zake hizi za kupeleka wanafunzi nje. Wanafunzi wengi huja kusoma hapa kwa sababu ya fursa hizo. Nami kama mdau mkubwa wa masuala ya kujenga mahusiano baina ya mataifa na tamaduni mbali mbali nimejizatiti sana katika shughuli ya ushauri wa programu hizi. Mara kwa mara ninawapeleka wanafunzi Tanzania. Ni jambo lenye manufaa makubwa kwa wanafunzi hao, kwa Tanzania, kwa Marekani na bila shaka kwa ulimwengu kwa ujumla. Wanafunzi hao wanapata fursa ya kufanya masomo na wanafunzi wa kiTanzania, kufahamiana na wa-Tanzania, na kujipanua upeo kitaaluma na kimtazamo. Pia, ni lazima niseme kuwa wanaingiza hela nyingi za kigeni katika hazina ya Tanzania, kwa visa wanayolipia ubalozini, masomo wanayolipia mahali kama Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na mizunguko ya kitalii wanayofanya vipindi vya mapumziko.











Kwa upande wangu, shughuli hii ya leo, kama ilivyo kawaida kila mara, ni fursa ya kuonana na wanafunzi wengi na kuwaeleza habari za Tanzania na Botswana, na habari za masomo yanayotolewa katika programu husika katika nchi hizo. Ni fursa ya kujibu masuali yao mbali mbali na kuwavutia wajiandikishe kwenye programu hizi.

No comments:

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...