Saturday, February 28, 2015

Kitabu Kinapoingia Amazon

Kati ya majina yanayojulikana sana mtandaoni ni Amazon, duka la mtandaoni ambamo vinapatikana vitu mbili mbali. Wengi wetu, kama sio wote, tunalihusisha jina la Amazon na vitabu.

Wanunuaji wa vitabu mtandaoni moja kwa moja huwazia duka la Amazon. Mimi mwenyewe, katika matamasha ya vitabu ninayoshiriki, nimezoea kuulizwa na watu iwapo vitabu yangu vinapatikana Amazon. Hao ni watu ambao wangependa kununua vitabu vyangu ila hawana hela wakati huo. Waandishi wanaitegemea Amazon kama sehemu ya kuuza vitabu kwa urahisi, hasa ikizingatiwa kwamba Amazon imejijenga sehemu nyingi za dunia.

Binafsi, sikutaka kuviweka vitabu vyangu Amazon. Sikupendezwa na jinsi kampuni hii kubwa inavyowaharibia biashara wauzaji wadogo wadogo, kama yanavyofanya makampuni makubwa katika mfumo wa ubepari.

Nilitaka vitabu vyangu viuzwe na maduka madogo madogo, ya watu wa kawaida au taasisi za kawaida. Niliridhika kuona vitabu yangu vinauzwa na duka la vitabu la Chuo cha St. Olaf, kwa mfano.

Lakini, nilikuja kushangaa baadaye kuwa, ingawa sikuvipeleka vitabu yangu Amazon, vilianza kuonekana kule. Hapo nilitambua kuwa Amazon ina nguvu au mvuto kuliko nilivyodhania. Ni kama kifaru anayetembea nyikani bila kubughudhiwa na wanyama wadogo wadogo.

Amazon inauza vitabu vipya na pia nakala zilizotumika. Mtu akishanunua na kusoma nakala yake, anaweza kuiuza Amazon. Ukiangalia tovuti ya Amazon, utaona vitabu vyangu vipya vinauzwa sambamba na vilivyotumika.

Kutokana na hali halisi ya ushindani katika uchumi wa kibepari, Amazon inauza au inaweza kuuza vitabu kwa bei ya chini kidogo au sana, ukifananisha na wauzaji wengine, kuanzia wachapishaji hadi hasa wauzaji wadogo wadogo. Vile vile, malipo ("royalties") anayopata mwandishi kutokana na mauzo ya vitabu vyake Amazon huwa ni pungufu kuliko yale ayapatayo au anayoweza kuyapata kutoka kwa wachapishaji, ingawa nayo si makubwa, bali ni asilimia ndogo ya bei ya kitabu.

Pamoja na yote hayo, Amazon imetamalaki katika uwanja huu wa uuzaji wa vitabu mtandaoni. Ingawa kuna makampuni mengine pia, kama vile Barnes and Noble, Amazon ndio inayoonekana kutawala vichwani mwa watu.

Amazon inauza vitabu halisi, yaani vya karatasi, na vitabu pepe. Ni juu ya mwandishi kuamua kama anataka kukiweka kitabu chake katika mtindo wa kielektroniki. Inavyoonekana, kadiri siku zinavyopita, watu wengi zaidi na zaidi wanaingia katika mkondo huu wa kununua vitabu pepe. Mimi mwenyewe nimeshuhudia hayo, na nimekuwa nikijitahidi kwenda na wakati. Baadhi ya vitabu vyangu vinapatikana kama vitabu pepe kwenye mtandao wa lulu na mtandao wa Amazon.

Hata hivi, kuna mjadala mkubwa unaoendelea kuhusu hatima ya vitabu tulivyovizoea, yaani vya karatasi. Wakati wengine wanaamini kuwa vitabu hivi vitadidimizwa na vitabu pepe, wengine wanasema kuwa hilo halitawezekana, kutokana na mazoea na mapenzi yaliyojengeka kwa vitabu kama vitabu. Wanasema kuwa hivi vitabu vya jadi vitakuwepo sambamba na hivi vya kielektroniki.

Nimeona niseme hayo, kwa manufaa ya wengine ambao ni waandishi au wanawazia kuwa waandishi.

2 comments:

Mwl. said...

Habari Prof.
Kwa heshima na taadhima, naomba nikupongeze kwa kazi kubwa sana unayoifanya tena kwa kujitolea kutusaidia sisi tulio chini/nyuma yako.
Umekuwa ni mtu wa pekeena muhimu sana katika mioyo ya waandishi wachanga hususani katika Taifa lako na dunia kwa ujumla.

Binafsi nimekutafta muda mrefu lakini sijakupata mtandaoni, Naomba unisaidie namba zako ninazoweza kukupata wewe binafsi kwa njia ya Whsassap lakini pia nisaidie emailaddress yako kwa mawasiliano ya dharura.

Mbele said...

Asante sana kwa ujumbe. Samahani sikuwa nimepitia hapa kwa muda muafaka, na ndio sababu ya kutojibu mapema. Nashukuru kusikia kuwa unapendezwa na kazi zangu. Namba yangu ni 507 403 9756.

nakutakia kila la heri.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...