Sunday, March 8, 2020

Vitabu Nilivyonunua Leo

Ni muda mrefu umepita, nami sijaandika kuhusu vitabu nilivyonunua kama nilivyokuwa naandika miezi iliyopita. Leo nimeona nifanye hivyo.

Nilienda Apple Valley kukutana na mkurugenzi wa African Travel Seminars ambaye tunafanya shughuli za kutangaza utalii Afrika. Baada ya kikao, nilienda katika duka la Half Price Books, ambalo nimelitembelea mara nyingi. Kama kawaida, nilikwenda kwanza kuona vitabu vya Hemingway. Nilichagua Paris Without End: The True Story of Hemingwahy's First Wife na Ernest Hemingway: Artifacts From a Life.

Nilichagua Paris Without End kwa sababu nilitaka kujua zaidi juu ya Hadley Richardson, mke wa kwanza wa Hemingway. Nimesoma habari zake hapa na pale, lakini si kwa undani. Ninafahamu jinsi anavyoelezwa na Hemingway katika riwaya ya A Moveable Feast. Vile vile niliguswa sana na barua alizoandika Hemingway kwa mke wake huyo pale alipokuwa ameanzisha uhusiano na mwanamke mwingine, Pauline. Hemingway anaelezea namna alivyosongwa na mawazo kuhusu tatizo hilo. Kwa hivyo, ninataka kufahamu undani wa maisha ya mama huyu.

Nilichagua Ernest Hemingway: Artifacts from a Life kwa kuwa nilishaona baadhi ya vitu vya Hemingway katika ziara yangu nyumbani alikozaliwa, katika kitongoji cha Oak Park, karibu na Chicago. Nilishaona vitu vingine vya Hemingway katika maktaba ya J.F. Kennedy mjini Boston. Kitabu hiki kitaniwezesha kufahamu mengi zaidi, kwani kina picha na maelezo.

Baada ya hapo, nilienda sehemu ambapo huwekwa vitabu vya bei rahisi zaidi. Nilichagua Anna Karenina, riwaya ya Leo Tolstoy, kwa sababu sijisikii vizuri kwamba sijasoma riwaya za mwandishi huyu maarufu wa uRusi. Ninatamani hapa nilipo ningekuwa nimesoma War and Peace na Anna Karenina. Nimechukua hatua kuelekea kwenye lengo hilo.

No comments:

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...