Friday, October 15, 2021

Mdau Kajipatia Kitabu

Huyu dada, Tanya, alihudhuria mazungumzo yangu na wana Rotary Club of Brooklyn Park tarehe 6 Oktoba. Mada yangu ilikuwa "Cultural Differences in the Global Village."

Nilipomaliza hotuba yangu, wakati wa masuali na majibu, dada huyu alijitokeza akasema kuwa yeye ni mfanyakazi katika sekta ya elimu na kwamba kwamba alivutiwa na mhadhara wangu akaongeza kuwa mawazo na maudhui yangu yanahitajika mashuleni.

Tulikubaliana kushirikiana kushughulikia changamotto zilizopo mashuleni. Baadaye nilimpelekea hiki kitabu changu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, kama hatua ya kwanza katika safari yetu hiyo.

Tuesday, October 12, 2021

KITABU MUHIMU KWA MAJADILIANO

Tarehe 5 Oktoba, Profesa Artika Tyner anayefundisha sheria katika Chuo Kikuu cha St. Thomas, alikweka picha hii hapa kushoto, akaambatiisha ujumbe huu: "New book alert: This book is an essential guide for intercultural dialogue. Thank you Dr. [Mbele] for sharing knowledge and wisdom." 

Nitafsiri kwa kiSwahili: "Tangazo la kitabu: Kitabu hiki ni mwongozi muhimu kwa majadiliano baina ya tamaduni. Asante Daktari Mbele kwa kutushirikisha ujuzi na hekima."

Profesa Tyner ni mmoja wa maprofesa wanaokitumia kitabu changu cha awali, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, katika masomo. Yeye alianza kukitumia katika programu ya kuwapeleka waMarekani Ghana kujifunza. Ni mmoja wa waMarekani weusi wenye mshikamano na Afrika. Pia ni mwandishi maarufu katika taaluma ya sheria na uongozi, na pia huandika vitabu kwa watoto. 

Kauli yake juu ya kitabu changu ina uzito wa pekee.

Friday, October 8, 2021

Maongezi yangu na Rotary Club ya Brooklyn Park, Minnesota

Tarehe 6 Oktoba, nilikwenda Brooklyn Park, Minnesota, kufuatia mwaliko wa Rotary Club. Tulikuwa tumekubaliana kuwa nikahudhurie mkutano wao na kuongelea mada ya  "Cultural Differences in the Global Village."

Siku iliyofuata, Rotary Club waliandika ujumbe katika ukurasa wao wa Facebook:

“We had the honor to hear from Professor Joseph Mbele at our Wednesday meeting. His incredible wisdom, insight, knowledge, passion, and heart to connect people across all cultures was so inspiring. We can create united and connected communities if we change our approach and adopt the strategies and mindset that Professor Mbele shared. Thank you Professor for joining us!”

Wednesday, October 6, 2021

NIMEHUTUBIA MKUTANO WA AMERIKA YA KUSINI

Jana, tarehe 5 Oktoba, jioni, nilihutubia mkutano ulioandaliwa na vyuo vikuu viwili vya Colombia, Amerika ya Kusini. Mada yangu ilikuwa "Culture and Business: a Broad Perspective From Africa to. Latin America." 

Kwa zaidi ya mwaka, mada ya utamaduni na biashara imenivutia. Nilipoanza kuipenda, niliandika "Culture and Business Between Africans and Americans." Halafu, nilihutubia Trade With Africa Business Summit nikiwa nimealikwa kuongelea kitabu changu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences.

Hatimaye sasa, nilipopata mwaliko kutoka Colombia, nilijikuta niko tayari kutosha. Kasoro pekee ilikuwa kwamba sikuufahamu utamaduni wa Amerika ya Kusini kama ninavyoufahamu ule wa Afrika na Marekani. Kwa hiyo, nilijielimisha kiasi kabla ya siku ya mkutano.

Nilijifunza mengi ya msingi, ambayo yalinifanya nitamke na kusisitiza mkutanoni kwamba utamaduni wa Amerika ya Kusini unafanana kiasi kikubwa na ule wa Afrika. Kwa hiyo, biashara baina ya pande hizi mbili itakuwa rahisi. Nilitoa angalizo kuwa itabidi kuzingatia tofauti za lughha zilizopo katika hizi pande mbili za dunia, ili kuleta uangalifu katika mawasiliano, utangazaji wa biashara, na kadhalika.
 

Saturday, October 2, 2021

Uandishi si Lelemama

Mimi kama mwandishi, ninakumbuka juhudi ninayofanya na taabu ninayopata katika kuandika vitabu. Kitabu cha Matengo Folktales, kwa mfano, kilichukua miaka yapata 23 kukiandaa, yaani tangu kurekodi hadithi, kazi yenye usumbufu mwingi, kuzitafsiri, kurekebisha tafsiri tena na tena, tena na tena, halafu kuziandikia uchambuzi, na kurekebisha tena na tena, huku nikifanya utafiti maktabani juu ya mada ya hadithi za jadi, ili niweze kuchambua hadithi zilizomo kitabuni kwa upeo unaofaa katika kufundishia vyuoni, na kadhalika. Nilijikuta nikitafakari mambo mengi ya aina hiyo, wakati mwingine nakwama kabisa, halafu baada ya muda najikongoja tena, hivi hivi, na baada ya miaka yapata 23 ndio nikachapisha "Matengo Folktales." Kitabu cha Chickens in the Bus: More Thoughts on Cultural Differences, ingawa ni kidogo sana, kurasa 43 tu, nacho kilinichukua yapata miaka 15 kukiandaa. Nilipigika na kuchakarika. Lakini baada ya kuchapisha, najiona mwenye faraja kubwa na ushindi.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...