Sunday, January 29, 2012

Mwandishi Shafi Adam Shafi

Tanzania tuna waandishi wengi maarufu katika lugha ya ki-Swahili. Mmoja wao ni Shafi Adam Shafi, kutoka Zanzibar, ambaye anaonekana nami pichani hapa kushoto. Tulikuwa New Africa Hotel, Dar es Salaam mwaka 2004 wakati wa tamasha la vitabu.







Shafi Adam Shafi anafahamika sana kwa riwaya zake. Riwaya aliyoichapisha kwanza ni Kasri Ya Mwinyi Fuad (Tanzania Publishing House, 1978). Ilikuwa maarufu tangu mwanzo. Sikupata muda wa kuisoma. Halafu, mwaka 1980 niliondoka Tanzania, kuwenda masomoni Marekani, hadi mwaka 1986.

Baada ya kukaa Marekani miaka sita hiyo, nilivyorejea Tanzania nilifanya juhudi ya kujipatia vitabu vya ki-Swahili. Nilinunua nakala ya Kasri Ya Mwinyi Fuad tarehe 28 Oktoba, 1987, ikasainiwa na Shafi Adam Shafi tarehe 29. Nina risiti ya kununulia kitabu, kutoka Tanzania Publishing House. Kwa hivyo, nina ushahidi kuwa nimeonana na Shafi Adam Shafi mara mbili.

Ingawa mara kwa mara ninapoongelea vitabu katika blogu zangu huwa naandika kuhusu yaliyomo, na uchambuzi wangu, leo nimependa tu kuchangia kumtangaza Shafi Adam Shafi na kazi zake. Nitakapokuwa nimezisoma kazi zake, Insh'Allah, nitaweza kuandika kwa undani zaidi.

Shafi Adam Shafi ameandika pia Kuli (Dar es Salaam: Tanzania Publishing House, 1979) , Vuta N'kuvute (Dar es Salaam: Mkuki na Nyota Publishers, 1999), na Haini (Nairobi: Longhorn Publishers, 2003).

Kuna taarifa ya mahojiano ya kina baina ya Shafi Adam Shafi na Freddy Macha ambayo unaweza kuyasoma hapa.

Thursday, January 26, 2012

Africonexion: Kampuni Chipukizi

Mwaka 2002 nilisajili kampuni katika jimbo la Minnesota ambayo niliita Africonexion. Nilichagua aina ya usajili iitwayo "sole proprietorship." Yaani mmiliki na mhusika mkuu ni mimi.

Nilianzisha Africonexion kama chombo cha kushughulikia elimu kuhusu tamaduni duniani, kwa kuandika, kuchapisha, na kuuza vitabu, na kutoa mihadhara na ushauri kwa watu binafsi, mashirika, taasisi, makampuni, na kadhalika, kama ninavyoripoti mara kwa mara katika blogu zangu.


Africonexion ni kampuni ndogo sana kwa wakati huu, kwa maana kwamba sina timu ya wafanyakazi au washiriki. Lakini nimeitumia vizuri kama fursa ya kujielimisha, kwa kuzingatia kuwa elimu ni mtaji bora kuliko hata fedha. Shughuli zote ninazofanya, iwe ni kuandika au kutoa mihadhara au ushauri kwa watu binafsi, ni kama shule kwangu. Hii picha hapa kushoto ilipigwa wakati wa maonesho fulani Brooklyn Park, Minnesota.



Ninataka kuipeleka kampuni hii Tanzania na kwingineko. Nimeshaendesha warsha Dar es Salaam, Zanzibar na Pemba, Tanga, na Arusha. Pia nilishiriki maonesho ya elimu na ajira yaliyofanyika Diamond Jubilee Hall, Dar es Salaam. Hapa kushoto naonekana na wadau kwenye meza yangu. Nilishiriki maonesho hayo ili kuwapata wadau wa kujiunga nami, kwani nimejenga msingi mzuri wa uzoefu, na mtandao thabiti, huku Marekani. Lakini, kutokana na shughuli zangu, watu hao inabidi wawe wapenda vitabu na elimu kwa ujumla.

Wednesday, January 25, 2012

Mfanya usafi akamatwa akimlawiti mtoto msikitini

Habari hii inahuzunisha, nikizingatia jinsi mtoto huyu alivyohujumiwa maisha yake na haki zake za kibinadamu, nikizingatia uchungu wa mama yake, ndugu, jamaa, marafiki na wapenda haki. Habari hii inapaswa kutangazwa, ijulikane, ili angalau iwe faraja kwa mtoto huyu na mama yake, kwamba tuko tunaojali utu na haki, na tuko pamoja nao.

Habari hii imetokea msikitini. Hivi juzi, wanafunzi wa ki-Islam walipoandika waraka wakiorodhesha hujuma walizosema wanafanyiwa wa-Islam mashuleni, niliandika ujumbe kuwaunga mkono katika kulaani hujuma hizo. Soma hapa. Nilisukumwa na maadili ya kuzingatia haki, niliyofundishwa katika imani yangu ya u-Katoliki.

Sasa basi, ni muhimu wa-Islam, wa-Kristu, na wengine wote tuungane kumpigania mtoto huyu aliyelawitiwa msikitini, na watoto wengine wanaotendewa vitendo hivi, na wengine wote wanaohujumiwa haki zao. Tuungane kukemea maovu yote na kupigania haki za wote.

Ni lazima tufanye hivyo, ili angalau kumpunguzia mtoto huyu matatizo ya kisaikolojia ambayo yatamwandama maishani. Akiwa ni mtoto mu-Islam, atakuwa anasikiliza mahubiri yanayosisitiza kwamba wa-Islam wanahujumiwa na wa-Kristu, hasa wa-Katoliki. Atakuwa anasikiliza mihadhara ambayo inawaongelea wa-Islam kama watu wasio na dosari, watu wasio na ubaya na mtu, bali wenye dosari ni wa-Kristo, na katika wa-Kristo, hasa wa-Katoliki. Ataambiwa adui yake mkuu ni mfumo Kristo. Hatasikia kuwa wa-Islam ni sawa na wa-Kristu katika uwezo wa kufanya mema au mabaya. Hatasikia kuhusu hujuma zinazoweza kufanywa na wa-Islam, hata dhidi ya wa-Islam wengine, kama ilivyomtokea yeye.

Hapa ndipo ninaposema pana hatari kubwa ya kumbebesha mtoto huyu mzigo wa machungu kisaikolojia. Kutokumweleza kuwa wa-Islam nao wanaweza kuwa wabaya itakuwa ni kumwongezea kejeli juu ya machungu. Tuungane kumwepusha na hayo, kwa kadiri iwezekanavyo. Labda kwa njia hii ya kuyatangaza na kuyakemea maovu yanayotokea nchini mwetu, tutayapunguza au kuyatokomeza.

--------------------------------------------------

Chanzo: MWANANCHI


Mfanya usafi akamatwa akimlawiti mtoto msikitini
Tuesday, 24 January 2012 20:40

Hamisi Mwesi, Dodoma
POLISI mkoa hapa inamshikilia mkazi wa Bahi Road, Manispaa ya Dodoma, kwa tuhuma za kumlawiti mtoto mwenye umri wa miaka tisa baada ya kumpa Sh500 ili kumfichia siri.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Zelothe Stephen, alisema mtuhumiwa huyo ambaye ni mfanya usafi wa Msikiti wa Ghazal uliopo eneo la Majengo, alitenda kosa hilo juzi saa 12:00 jioni.

Stephen alisema baada ya polisi kupewa taarifa na wananchi wa eneo hilo, walifika msikitini hapo na kumkamata mtuhumiwa akiwa ndani ya choo cha wanawake alipokuwa akifanyia mtoto kitendo hicho cha kinyama.

“Polisi walijulishwa na wananchi waliokuwapo eneo hilo kwamba mtuhumiwa alimuingiza mtoto huyo kwenye choo cha wanawake na kujifungia ndani, watu waliokuwa jirani na eneo hilo walifuatilia kwa makini ndipo waliposhuhudia mtuhumiwa akimlawiti mtoto huyo na kutoa taarifa polisi,” alisema Stephen.

Alisema mtoto huyo amelazwa Hospitali Kuu ya Mkoa wa Dodoma kutokana na maumivu, kutokana na kitendo hicho na hali yake inaendelea vizuri na uchunguzi juu ya afya yake unafanyika kubaini athari zaidi.

Alisema mama mzazi wa mtoto huyo, alimg’ata sikio la kulia mtuhumiwa huyo kwa hasira na kunyofoka nusu ya sikio lake na kwamba, hivi sasa wanashikiliwa.

Inadaiwa mtuhumiwa amekuwa na tabia hiyo muda mrefu na waumini wa msikiti huo waliwahi kumuonya, baada ya kutiliwa shaka kuhusu kujihusisha na vitendo hivyo ambavyo hawakuwa na ushahidi, ndipo walipoamua kuanza upelelezi dhidi yake.

“Waumini walishamshtukia mtuhumiwa, wakaanza kufuatilia nyendo zake kwani yeye muda mwingi hukaa msikitini kwa ajili ya kufanya usafi, wakati mwingine kutoa adhana kwa ajili ya swala, leo (juzi) amenaswa na mtego baada ya kumtanguliza mtoto choo cha wanawake na yeye kumfuata,” alisema mmoja wa waumini wa msikiti huo.

Tuesday, January 24, 2012

Maandamano ni Mpango wa Makafiri--'Allaamah al-Fawzaan

Video hii imenisisimua akili. Sikujua kuwa maandamano ni mpango wa makafiri na kwamba hakuna maandamano katika u-Islam

Monday, January 23, 2012

Mwandishi Lazima Awe Msomaji Sana

Yule mwandishi maarufu sana, Ernest Hemingway, alikuwa na mawazo ya kusisimua kuhusu masuala mbali mbali, likiwemo suala la uandishi. Aliandika sana kuhusu uandishi: mbinu za uandishi, uandishi bora, changamoto za uandishi na namna ya kuzikabili, raha na machungu ya kuandika. Aliongelea kazi za waandishi mbali mbali, na hakuficha hisia na mtazamo wake kuhusu ubora au mapungufu ya waandishi hao.

Kuna mengi sana ya kuongelea, kuhusu suala hilo la Hemingway na uandishi. Lakini hapa nataka kutaja jambo moja tu, nalo ni kauli ya Hemingway kwamba mwandishi ana wajibu wa kusoma kazi za waandishi wote waliomtangulia, ili ajue kazi inayomkabili ya kuwafunika hao waandishi.

Napenda kunukuu maneno ya Hemingway aliyomjibu kijana kutoka Minnesota aliyemfuata Hemingway umbali mkubwa ili kuuliza masuali kuhusu uandishi. Kiutani, Hemingway alimpa kijana huyo jina la Mice.

Mice alimwuliza Hemingway masuali mengi, ila suali ninalotaka kulileta hapa ni, "What books should a writer have to read?" Hemingway akajibu, "He should have read everything so he knows what he has to beat."(Ernest Hemingway, By-Line, New York: Touchstone, 1998, p. 217)

Kwa tafsiri ya juu juu, suali lilikuwa, "Je, mwandishi anapaswa asome vitabu gani?" Na Hemingway alijibu kwamba awe amesoma kila kitu ili afahamu kazi inayomkabili ya kuwashinda waliomtangulia.

Tuangalie kauli hizi kwa kuzingatia hali ya Tanzania. Kila mchunguzi anakubali kuwa utamaduni wa kusoma vitabu unazidi kufifia au umefifia Tanzania. Taarifa zinaeleza kuwa hata uwezo wa kusoma na kuandika unazidi kufifia. Asilimia ya waTanzania wasiojua kusoma na kuandika inaongezeka. Kwa maneno mengine, Tanzania inazidi kuwa nchi ya ngumbaru.

Katika hali hiyo, na kwa kuzingatia kauli ya Hemingway, tutawezaje kutegemea kuwa na waandishi wa kiwango cha juu kabisa? Kwa mujibu wa Hemingway, mwandishi m-Tanzania, ambaye labda tuseme anaandika kwa ki-Swahili, anapaswa kuwa amesoma waandishi wote waliotangulia. Kwa mfano awe amesoma Tambuka, Al-Inkishafi, Mwana Kupona, Miraji, Masahibu, Ngamia na Paa, Muyaka bin Haji, Rasi l'Ghuli, Shufaka, Fumo Liyongo, Maisha ya Tippu TIp, vitabu vyote vya Shaaban Robert, na kadhalika. Anapaswa afahamu jadi hiyo vizuri, apambane kiuandishi ili awe juu zaidi, aweze kweli kutoa mchango unaotupeleka mbele.

Sitaki kudanganya. Lazima nikiri kuwa Hemingway alitoa mtihani mkubwa sana. Kwa mfano, sijui kama kuna mtu leo anayeweza kumfikia Muyaka, au Mgeni bin Faqihi. Lakini Hemingway alifanya vizuri kuweka kigezo cha juu kabisa, hata kama kukifikia ni taabu sana au haiwezekani. Ni vibaya sana kujiwekea viwango vya chini na kisha kujipongeza kwa kufikia viwango hivyo. Naamini hili ndilo tatizo letu: tunajiwekea viwango vya chini, au tunababaisha bila viwango, na bado tunajipongeza au tunapongezana.

Sunday, January 22, 2012

Naikumbuka Matema Beach

Tanzania ina sehemu nyingi zinazopendeza sana, nami nimebahatika kuziona baadhi ya sehemu hizo. Mwaka jana, kwa mfano, nilipata bahati ya kufika Matema Beach, pwani ya kaskazini ya Ziwa Nyasa. Ni sehemu nzuri sana kwa mapumziko. Imetulia na haina msongamano na misuguano kama ya Dar es Salaam. Hapa kushoto naonekana nimetulia kwenye bembea, nikifaidi upepo mwanana. Huyu binti ni mmoja wa wanafunzi wawili niliowaleta hapo kwenye ziara ya kuifahamu nchi.

Ukifika ufukweni hapo, unaweza kujikalia mahali chini ya mti, unapiga mbonji, kama wasemavyo watoto wa vijiweni, au ukawa unasoma kitabu, kupiga michapo na wenyeji, au kuangalia Ziwa na mitumbwi ipitayo humo.

NImeandika mara kadhaa kuhusu Matema Beach katika blogu zangu, kwa mfano hapa na hapa, na napangia kuendelea kuandika.

Friday, January 20, 2012

Kitabu cha m-Tanzania Kuhusu Usimamizi wa Fedha

Hatimaye, nimejipatia na kusoma nakala ya kitabu kiitwacho Taking Control of Your Money, kilichoandikwa na Juanita Puja Kilasara. Huyu ni binti m-Tanzania ambaye amejipambanua katika fani ya uhasibu na masuala ya fedha kwa ujumla. Habari za kitabu chake hiki niliziona kwanza katika tovuti ya wavuti, kwani kwenye ukurasa wa mbele pana sehemu inayotangaza vitabu vya wa-Tanzania.

Kitabu hiki kinaeleza kwa njia rahisi masuala mbali mbali ya kuzalisha fedha na matumizi ya fedha kwa namna ya kumsaidia mtu kuwa mwangalifu na kumfanya asonge mbele kimaisha. Kuna mawaidha mengi ya manufaa, hata katika masuala ya kuanzisha na kuendesha biashara na shughuli zingine za kujipatia kipato.

Kwa kuzingatia mabadiliko ya dunia, hasa katika tekinolojia ya mawasiliano, kitabu hiki kinatoa dokezo mbali mbali za kumwezesha mtu kutumia fursa zilizopo mtandaoni. Ingekuwa vijana wa Tanzania wana mazoea ya kusoma vitabu, wakawa wanasoma vitabu kama hiki, hata suala la ajira wangeliangalia kwa upeo tofauti, kwani ni aina ya kitabu kinachofungua milango ya ujasiriamali. Nina jambo moja tu la kushauri, kwamba ingefaa kitafsiriwe pia katika ki-Swahili.

Unaweza kumsikiliza Juanita akiongelea kitabu chake hapa. Kitabu hiki kinapatikana sehemu mbali mbali, kama ilivyoelezwa hapa.

Monday, January 16, 2012

Kumbukumbu ya Martin Luther King Imefana

Kumbukumbu ya Martin Luther King, Jr. niliyohudhuria leo Chuoni Concordia imefana sana. Watu wengi walihudhuria, wakajaza ukumbi mkubwa sana wa chuoni hapo uitwao Gangelhoff. Kulikuwa na hotuba kadhaa za watu mashuhuri katika jamii na taasisi na serikali. Hapa kushoto anaonekana Askofu William Watson, III, ambaye ndiye alikuwa mtoa mada mkuu.





Hotuba zilisisitiza mambo muhimu aliyofanya na kusema Martin Luther King, Jr. Wasemaji walikumbushia wosia wake katika masuala kama haki, usawa, na elimu.










Walihudhuria watu wa kila aina: wa rangi na mataifa mbali mbali, watoto, watu wazima, na wazee, wake kwa waume. Hapo mtu ulijionea mwenyewe kuwa kweli Martin Luther King alikuwa mtu wa pekee sana, ambaye katika maisha yake aligusa mioyo ya watu sana na bado anawagusa na ataendelea hivyo kwa vizazi vijavyo.






Kulikuwa na vikundi kadhaa vilivyofanya maonesho. Waliburudisha kwa nyimbo, muziki, na staili za kucheza. Hapa kushoto ni kwaya ya watoto wavulana, ambayo ni ya watawa wa-Katoliki wa Monasteri ya St. John, iliyopo mjini Collegeville.









Hapa kushoto ni msichana Naajee Dennis, aliyeghani kwa umahiri mkubwa hotuba nzima ya Martin Luther King, Jr, "I Have a Dream." Hakuwa anaisoma, bali alikuwa ameikariri.









Kwenye shughuli kama hizi, sikosi kukutana na watu ninaofahamiana nao. Hapa kushoto ninaonekana na wa-Marekani Weusi wawili. Inapendeza kuongea na watu wa aina hiyo, kwa sababu mtazamo wao kuhusu masuala mbali mbali ya historia, maisha na ulimwengu kwa ujumla ni tofauti na wangu mimi niliyekulia Afrika.






Kulikuwa na sehemu ya maonesho ya kuelimisha umma. Nilikuwa mmoja wa washiriki. Hapa kushoto inaonekana meza yangu, nikiwa nimeanza kupanga vitabu vyangu. Kama kawaida, nilipata fursa ya kuongea na watu wengi waliofika hapa kwenye meza yangu.

Saturday, January 14, 2012

Januari 16, Kumbukumbu ya Martin Luther King,Tukutane St. Paul

Tarehe 16 Januari ni kumbukumbu ya Martin Luther King hapa Marekani. Zitafanyika shamrashamra nyingi sehemu mbali mbali. Kwenye miji kama Minneapolis na St. Paul, Minnesota, itakuwa vigumu hata kuamua wapi kwa kwenda.

Lakini mimi nilishajisajili kama mshiriki wa maonesho yatakayofanyika Chuoni Concordia, mjini St. Paul. Pamoja na waandishi wengine, tutakuwa pale na vitabu vyetu, tukikutana na wadau na kubadilishana mawazo, kuanzia saa 3:30 asubuhi hadi saa 9 alasiri.

Nafurahi kwamba miaka ya karibuni nimefanya juhudi ya kusoma habari za Martin Luther King na baadhi ya maandishi yake, hadi kufahamu jinsi alivyothamini elimu, sawa na Mwalimu Nyerere, na jinsi alivyotufundisha kujali usawa na haki za binadamu wote. Wala hakuwa upande wa watu weusi tu, kama wengi wanavyoamini.

Nimegundua kuwa wengi, hata hao wa-Marekani Weusi ambao wanapenda sana kumtaja na kumpigia mfano, hawamwelewi vizuri Martin Luther King. Nangojea kwa hamu kubadilishana mawazo na hata kulumbana na umati wa watu watakaohudhuria hiyo maadhimisho hiyo tareye 16 Januari. Karibuni.

Thursday, January 12, 2012

Nimerudi kutoka Chuoni Gustavus Adolphus

Leo nilienda Chuoni Gustavus Adolphus kutoa mhadhara katika darasa la Profesa Paschal Kyoore. Niliandika kuhusu habari hii hapa. Somo wanalosoma ni "African Tricksters." Wakati huu wanasoma kitabu changu cha Matengo Folktales, na niliona wanazo nakala.

Katika mhadhara wangu, uliodumu dakika 50, nilijikita katika kufafanua dhana mbali mbali zinazotumika katika utafiti na uchambuzi wa somo hili, ambazo chimbuko lake ni katika utafiti uliofanywa Ulaya, na jinsi dhana hizi zilivyopachikwa katika masimulizi ya sehemu zingine za dunia, kama vile Afrika. Nilihoji uhalali wa jambo hilo, ambalo tumelirithi na tunaliendeza.

Baada ya mhadhara wangu, tulikuwa na kipindi cha masuali, kilichodumu yapata dakika 40.

Wednesday, January 11, 2012

Kitabu Kinapatikana Chuoni Saint Benedict, Minnesota

Nimeona taarifa leo kuwa kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences kinapatikana katika duka la vitabu la Chuo cha Saint Benedict, Minnesota.

Nakumbuka kuwa niliwahi kutoa mihadhara miwili katika chuo hiki, kuhusu vitabu vyangu viwili. Mhadhara mmoja niliuelezea hapa. Mwanafunzi mmoja aliuongelea mhadhara wangu mwingine, kuhusu hiki kitabu cha Africans and Americans katika blogu yake.

Tuesday, January 10, 2012

Nimeenda Maktaba ya Southdale, Edina.

Leo nilienda mjini Edina, kwenye maktaba ya Southdale. Nilikwenda kukutana na mama mmoja m-Marekani Mweusi, ambaye ninamsaidia kuchapisha kitabu chake kwa kutumia tekinolojia ya uchapishaji mtandaoni, kama ninavyochapisha vitabu vyangu.

Niliposogea kwenye jengo hilo, niliona magari mengi yamepaki. Ni kama inavyokuwa kwenye sherehe nchini Tanzania.

Niliona watu wakiingia na kutoka, wakiwemo wazee. Hii ni kawaida hapa Marekani. Hapo mlangoni, nilipishana na wazee wawili wakitoka, mwanamme na mwanamke, wazee sana, na huyu mwanamme alikuwa anatembelea mkongojo. Pamoja na uzee wote huu, wanaona umuhimu wa kwenda maktaba. Humo ndani, kama kawaida, kulikuwa na watu wengi wakisoma, kuazima au kurudisha vitabu, na wengine kwenye kompyuta na kwenye sehemu za kusikilizia vitabu, maana siku hizi vitabu vinapatikana vikiwa vimerekodiwa katika kanda.

Ukiangalia maelezo ya maktaba hii Southdale, utaona kuwa wanavyoitumia maktaba hii inaendana vizuri na yale aliyoyawazia na kuyatamka Mwalimu Nyerere wakati anafungua maktaba ya Taifa Dar es Salaam, kama nilivyoandika hapa.

Monday, January 9, 2012

Mabepari wa Venisi: Tafsiri ya Julius Nyerere

Wiki kadhaa zilizopita, mawazo yangu yalitekwa sana na kumbukumbu za tafsiri za tamthilia za Shakespeare zilizofanywa na Julius Nyerere. Nilipata hamu ya kuziangalia na kuzisoma. Kwa kuanzia, niliagiza nakala ya Mabepari wa Venisi.

Kama nakumbuka sawa sawa, tulisoma The Merchant of Venice tulipokuwa kidatu cha nne. Tulikuwa tunafahamu ki-Ingereza kiasi cha kuweza kusoma na kuelewa maandishi hayo ya Shakespeare. Ni tofauti na leo, ambapo uvivu na uzembe vimesababisha ufahamu wa ki-Ingereza udidimie sana na hata kutoweka. Uvivu huo unajitokeza pia katika ufahamu wa ki-Swahili.

Nyerere aliichapisha tafsiri yake mwaka 1969, muda mfupi tu baada ya Azimio la Arusha. Kwa hivi, tafsiri yake ilikuwa na mvuto wa pekee miongoni mwetu, kwani tulikuwa tunavutiwa na nadharia za ujamaa. Hata neno mabepari lilikuwa likitumika sana, sambamba na maneno kama mabwanyenye. Ilikuwa rahisi kuelewa kwa nini Nyerere aliamua kuitafsiri tamthilia hii ya Shakespeare. Kwa kutumia tabia, fikra, na kauli za Shailoki, mfanyabiashara wa Venisi, Shakespeare alionyesha kwa umahiri mwenendo wa ubepari. Shailoki ni kielelezo bora cha dhana ya Nyerere kuwa ubepari ni unyama.

Mwanzoni mwa kitabu cha Mabepari wa Venisi kuna picha ya Shailoki, iliiyochorwa na Sefania Tunginie. Picha hii nayo inanikumbusha enzi za ujana wangu, nilivyokuwa naiangalia. Mimi mwenyewe nilikuwa mchoraji, na nilikuwa navutiwa na picha za wachoraji kama Sefania Tunginie, Sam Ntiro, na Elias Jengo.

Nimekumbuka hayo yote, na nimekitafuta kitabu cha Mabepari wa Venisi ili kujikumbusha umahiri wa Nyerere katika lugha ya ki-Ingereza na ki-Swahili. Kama kweli unakijua ki-Ingereza na ki-Swahili, huwezi ukasoma tafsiri ya Nyerere usikiri kuwa alikuwa na akili na ufahamu usio wa kawaida wa undani wa lugha hizo mbili. Hata hivi, kama wewe ni mtu makini sana, unaweza kubadili neno hapa au pale, katika tafsiri ya Nyerere. Angalia, kwa mfano, alivyotafsiri maneno ya Antonio, mwanzoni kabisa mwa tamthilia:



Ant. In sooth, I know not why I am so sad.
It wearies me; you say it wearies you;
But how I caught it, found it, or came by it,
What stuff 'tis made of, whereof it is born,
I am to learn;
And such a want-wit sadness make of me
That I have much ado to know myself.

Tafsiri ya Nyerere ni hii:

ANTONIO: Kusema kweli sijui kisa cha huzuni yangu;
Inanitabisha sana; wasema yakutabisha;
Bali nilivyoipata, au kuiambukizwa,
Au imejengekaje, imezawa jinsi gani,
Ningali sijafahamu,
Na huzuni yanifanya kuwa kama punguani,
Kunifanya nisiweze kujifahamu mwenyewe.

Kama nilivyosema, miaka ya ujana wetu, tuliweza kuelewa lugha ya Shakespeare, tena kwa undani. Leo sijui ni wa-Tanzania wangapi wanaoweza kumwelewa Shakespeare. Ngoja nilete kisehemu cha hotuba maarufu ya Portia, halafu ujaribu kutafsiri, uone unakifahamu ki-Ingereza na ki-Swahili kiasi gani:

Por. The quality of mercy is not strained,
It droppeth as the gentle rain from heaven
Upon the place beneath. It is twice blest--
It blesseth him that gives, and him that takes.
'Tis mightiest in the mightiest. It becomes
The throned monarch better than his crown.
His sceptre shows the force of temporal power,
The attribute to awe and majesty,
Wherein doth sit the dread and fear of kings;
But mercy is above this sceptred sway,
It is enthroned in the hearts of kings,
It is an attribute to God himself;
And earthly power doth then show likest God's
When mercy seasons justice.


Thursday, January 5, 2012

Mtu Anapobadili Dini

Blogu yangu hii iinashughulika na masuala ya aina aina, likiwemo suala la dini. Leo napenda kuongelea suala la watu kubadili dini.

Watu wengi wanabadili dini. Nikitoa mfano wa wa-Islam na wa-Kristu, wa-Kristu kwa maelfu wanabadili dini na kuwa wa-Islam, na wa-Islam kwa maelfu wanabadili dini na kuwa wa-Kristu. Kuna taarifa nyingi za watu hao mtandaoni.

Katika mtandao wa YouTube, unaweza kuwasikiliza watu wa aina hiyo wakijieleza. Kwa mfano, unawasikia watu wakielezea jinsi dini ya u-Islam ilivyoshindwa kukidhi mahitaji yao ya kiroho na kadhalika. Na unawasikia wengine wakielezea jinsi dini ya u-Kristo ilivyoshindwa kukidhi mahitaji yao ya kiroho na kadhalika. Nimewasikiliza baadhi kutoka pande zote, na nimeona jinsi wanavyoongea kwa masikitiko na hata jazba kuhusu dini walizozihama. Watu hao wanajisikia kuwa kubadili dini kumewapa mwanga na amani moyoni.

Kama nilivyosema, taarifa hizi zimezagaa mtandaoni. Sijui unajisikiaje endapo mtu wa dini yako akihamia dini nyingine. Wa-Islam wanajisikiaje pale wa-Islam wenzao wanapohamia katika u-Kristu? Wa-Kristu wanajisikiaje pale wenzao wanaposilimu? Naona hili ni suala la kusisimua akili, na ndio maana nimeamua kuliweka hadharani.

Tujaribu kulitafakari suala hili kwa undani. Binafsi natambua kuwa dini ni suala la imani ya mtu. Ni suala la mtu na dhamiri yake, yeye na Mungu. Endapo mtu akifikia hatua ya kuamini kwa dhati kabisa, katika dhamiri yake, kwamba akiwa katika dini fulani anakuwa karibu zaidi na Mungu kuliko katika dini yake ya sasa, halafu akahamia ile dini nyingine, kilichopo kwa sisi wengine ni kumwombea na kumtakia mema.

Wa-Islam na wa-Kristu tunajisikia sana kuwa msikitini na wa-Islam wenzetu, au kuwa kanisani na wa-Kristu wenzetu. Dini zetu zinajitahidi kwa namna mbali mbali kuwapata waumini zaidi. Utawasikia waumini wakitamba jinsi dini yao inavyoenea kuliko dini nyingine. Kwa upande wa Tanzania, utawasikia watu wakilumbana kuhusu dini ipi ina wafuasi wengi zaidi Tanzania. Suala la hizi takwimu limefanywa kuwa muhimu sana.

Lakini je, siku ya kiyama, tutasimama mbele ya Mungu na kuongelea haya masuala ya takwimu? La hasha. Wewe mu-Islam hutaweza kujikinga na hukumu ya Mungu kwa kuongelea umati wa wa-Islam uliokuwa nao hapa duniani. Na wewe m-Kristu itakuwa ni hivyo hivyo. Hutaweza kujinasua na hukumu ya Mungu kwa kuongelea utitiri wa wa-Kristu uliokuwa nao kanisani kwako au jimboni kwako. Itakuwa ni kila mtu kuchunguzwa yeye binafsi, imani yake, matendo yake, na maisha yake.

Ni kutokana na masuala kama haya ndio nasema kuwa tuwe waangalifu sana kuhusu suala la watu kubadili dini.

Monday, January 2, 2012

Maongezi na Wanafunzi wa Gustavus Adolphus

Leo nimeongea na wanafunzi wa Chuo cha Gustavus Adolphus ambao wanaenda Tanzania wiki hii kujifunza masuala ya afya na matibabu katika utamaduni tofauti na ule wa Marekani.

Kama nilivyoelezea katika blogu hii, nilialikwa na Profesa Barbara Zust, nikaongee na wanafunzi hao kuhusu masuala ninayoongelea katika kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences". Pichani kushoto, Profesa Zust ni kati ya waliosimama, wa nne kutoka kulia.

Profesa Zust ni mmoja wa walimu hapa Marekani ambao wanakipenda na kukitegemea kitabu hiki. Nami nashukuru kwa jinsi kinavyowasaidia walimu na wanafunzi wao. Mimi mwenyewe kama mwalimu siwezi kukaa na kutulia, bali natambua na kuzingatia wajibu wa kuendelea kutafiti na kuandika.

Leo, nilianza kwa kujitambulisha kwa kuelezea maisha yangu kwa ufupi hadi nilivyosoma Marekani na nikazingatia zaidi mchakato ulionifikisha kwenye kuandika kitabu hiki. Wale waliokisoma watakumbuka kuwa nimeelezea kiasi mchakato huo mwanzoni mwa kitabu.

Nilisisitiza mambo mhimu niliyojifunza katika kuandika kitabu hiki, kwa mfano umuhimu wa kuachana na dhana ya kuwa yale tuliyozoea katika jamii tuliyokulia ndio kigezo cha kufuatwa na watu wengine duniani. Nilielezea pia ugumu nilioupata katika kuandika kitabu hiki, nikiwa na lengo la kukifanya kiwe rahisi kusomwa, nikaelezea pia taabu niliyoipata katika kujieleza kwa hadhira mbili tofauti, yaani wa-Afrika na wa-Marekani, kwa wakati mmoja.

Baada ya utangulizi huo, kilifuata kipindi cha masuali, na hapo ndipo tulipotumia muda wetu mwingi. Kwa vile wanafunzi hao huwa wamekisoma kitabu, wanakuwa na masuali mengi ya kunitaka nifafanue vipengele mbali mbali. Maongezi yetu yalidumu kwa zaidi ya saa tatu. Nimeongea na makundi mbali mbali ya wadau hapa Marekani kuhusu kitabu hiki, lakini leo imekuwa ni rekodi, kwa maana ya kutumia muda mrefu namna hii.

Mkutano wa leo tulifanyia Mount Olivet Conference and Retreat Center, mwendo wa nusu saa tu kutoka Northfield ninapoishi. Ni kituo chenye ukumbi wa mikutano na vyumba vya kulala. Vyakula vinandaliwa hapa pia. Picha mbili zifuatazo nilipiga wakati wa chakula cha mchana.



Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...