Vitabu Vyangu Vimeingia Longitude Books

Siku chache zilizopita, nilileta ujumbe kuwa kampuni ya Longitude Books, inayouza vitabu kwa wasafiri na watalii, iliniulizia namna ya kupata vitabu vyangu. Mara baada ya kuwajibu, wamefanya hima na kuvijumlisha vitabu hivyo katika orodha yao.

Huu ni mfano wa jinsi wenzetu walivyo makini katika kuzichangamkia fursa. Niliwaambia kuwa vitabu hivi vinapatikana lulu.com kwa bei ya dola 12, na wao wajipangie bei ya kuviuza kwa wateja wao. Wameamua kuuza kwa dola 19.95.

Ukitaka kuvitafuta vitabu hivyo hapa Longitude Books, andika Mbele katika kidirisha cha "Search" halafu bonyeza "Go."

Comments

Sophie B. said…
Hongera sana Prof. kwa kazi nzuri ya kuelimisha jamii. Inabidi nitafute na hivyo vingine nivisome.Nawish hiki kitabu chako cha "Africans and Americans: Embracing Cultural DifferencesAfricans and Americans: Embracing Cultural Differences " watu zaidi wangekisoma maana kinakupa ufahamu mkubwa katika mambo mengi ugenini labda mambo ambayo yangekuchukua miaka mingi kuyaelewa.Hongera na usichoke kutuelimisha.
Mbele said…
Shukrani kwa ujumbe wako. Ulivyogusia mambo ya ugenini "ambayo yangekuchukua miaka mingi kuyaelewa," umenikumbusha jinsi ilivyonichukua miaka mingi ya kuishi na Wamarekani, kabla sijaanza kuelewa nini hasa kinachoendelea katika utamaduni wao. Ilinichukua miaka mingi kabla sipata imani ya kuanza kuandika kama ninavyoandika.

Kama unavyogusia, kazi ya kuufahamu utamaduni wa kigeni ni ngumu na inahitaji miaka mingi. Vinginevyo, utaishi humo ugenini ukiwa unashangazwa au unakerwa na mambo mengi, kila siku. Hii ni kwa sababu unakuwa bado hujaelewa undani wa utamaduni wenyewe, kujua kwa nini watu wanafanya hivi au vile, na kwa nini wanaongea hivi au vile. Unaweza kuona matendo ya watu au kusikia maneno yao, lakini unakuwa bado hujaielewa misingi ya wao kufanya vile, kuwaza vile, au kusema vile. Hii ndio inayochukua miaka kuifahamu.

Utamaduni ni mfumo, ambamo vipengele mbali mbali vinahusiana. Unaweza kuwaona watu wakifanya kitu fulani, lakini ili uwaelewe, inabidi ufahamu mambo mengi mengine ya utamaduni wao. Ukikiangalia hiki kitu kimoja tu, unaweza kupotea njia, usiwaelewe. Hii ndio kazi inayochukua muda mrefu na subira isiyo kifani.
Nami napenda kusema Hongera sana kwa kazi yako ya kuelimisha watu. Binafsi nimejifunza mengi sana katika kukusikiliza na pia makala zako. Nami nata au nakisaka hicho kitabu Tofauti za tamaduni ni lazima nikipate. Mungu akubariki
Mbele said…
Dada Yasinta, nashukuru kusikia umejifunza mawili matatu, au mengi, kama unavyosema, kutoka kwangu. Mimi naamini kuwa Mungu alinitaka niwe mwalimu, kwani nilisikia wito huu tangu nilipokuwa mtoto mdogo, kabla ya kuanza shule.

Kwa hivi, nazingatia wajibu wa kujielimisha kwa kila namna, kuanzia vitabuni hadi vijijini, ambako nafanya utafiti, kwa wazee na wengine.

Kujielimisha huku ndiko kunakoniwezesha kufundisha na kuandika kama ninavyofanya. Kwa hivi, naendelea kumshukuru Mungu kwa kunionyesha njia na kunipa neema mbali mbali, niendelee kuwa mtumishi wake kwa wanadamu, kwa heshima na unyenyekevu.

Ni wajibu wangu kama mwalimu kuwamegea wengine chochote ninajua katika taaluma zangu. Huwezi kusema wewe ni mwalimu, halafu unaficha ujuzi wako. Utakuwa si mwalimu, labda mchawi. Kwa msingi huu, napenda kusema kuwa vitabu vyangu vinapatikana Dar es Salaam, simu namba 0754 888 647 au 0717 413 073

Popular posts from this blog

Kumbukumbu ya Kuzaliwa

Tenzi Tatu za Kale

Pesa za Majini