Thursday, October 8, 2009

Uraia wa nchi Mbili

Makala hii imechapishwa katika KWANZA JAMII, Oktoba 6-12, 2009

Profesa Joseph L. Mbele

Tarehe 4 Septemba, 2009, nilipata fursa ya kukutana na ndugu Muhiddin Issa Michuzi, mwanablogu maarufu Tanzania. Pamoja na maongezi kuhusu masuala mbali mbali, alinifanyia mahojiano mafupi kwa ajili ya kuweka kwenye blogu yake. Suali moja aliloniuliza ni kuhusu msimamo wangu juu ya suala la uraia wa nchi mbili. Nilijibu kifupi, kutokana na uchache wa muda. Lakini suali hili limekuwa mawazoni mwangu kwa miaka kadhaa, tangu lilipoanza kuongelewa na waTanzania.

Nilimweleza Ndugu Michuzi kuwa binafsi sitaki uraia wa nchi nyingine. Nilililelewa katika misingi ya kujitambua kuwa mimi ni mTanzania tu. Isipokuwa, nilisema kuwa watoto wa siku zijazo, watakuwa waishi katika dunia tofauti na yetu, na itakuwa dunia ambayo itakuwa imefungamana sana na kuwa kama kjiji. Hata mipaka ya nchi huenda haitakuwepo, wala nchi hazitakuwepo. Kwa hivi suala la uraia nalo litakuwa na sura tofatuti.

Tukiacha suala la hisia binafsi, ni vema kuangalia upana wa suala la uraia wa nchi mbili. Jambo moja na msingi ni kuwa sheria na taratibu za nchi mbali mbali kuhusu uraia zinatofautiana. Hali kadhalika, sheria na taratibu kuhusu uraia wa nchi mbili zinatofautiana kutoka nchi hadi nchi. Ziko nchi zenye sheria ngumu kuliko ilivyo katika nchi zingine. Ziko nchi ambazo sheria zake ni nyepesi.

Marekani ni nchi moja yenye sheria ngumu kuhusu uraia wa nchi mbili. Watu wengi wanachukua uraia wa Marekani. Na nadhani waTanzania wengi nao wanataka kuchukua uraia wa Marekani. Lakini ukweli ni kuwa wanaochukua uraia wa Marekani wanakula kiapo ambacho ni kizito sana. Katika kiapo hiki, wanaukana kabisa utii na uaminifu kwa kiongozi au dola ya nchi walikotoka. Ndio kusema, Mtanzania anayechukua uraia wa Marekani, anaapa hatambui amri ya kiongozi wa Tanzania juu yake. Anaapa kuwa atabeba silaha kuitetea Marekani kwa mujibu wa sheria. Kiapo hiki kinanitisha, kwa jinsi Marekani ilivyo na historia ya kushambulia nchi zingine, hasa nchi maskini.

Katika mijadala kuhusu uraia wa nchi mbili, suala linajadiliwa kwa namna ya kuelezea faida tu. Sisikii maelezo kuhusu wajibu na majukumu yanayotokana uraia wa nchi mbili. Ukweli ni kuwa hakuna nchi inayotoa uraia kama njugu, bila masharti na bila kumtwisha mhusika majukumu. Marekani inamtegemea mtu anayechukua uraia wa nchi ile kuapa kuwa atashika silaha kuitetea Marekani kwa mujibu wa sheria. Huo ni mfano mmoja wa majukumu yanayoambatana na uraia wa nchi mbili.

Kama nilivyosema, nchi nyingine hazina masharti kama haya ya Marekani. Kuna nchi ambazo hazina kiapo kama hiki cha Marekani. Nikisikia Mtanzania amechukua uraia wa nchi hizo, sioni kipingamizi chochote.

Kitu kimoja ambacho naamini waTanzania wengi hawajui ni kuwa Marekani yenyewe haipendelei raia wake wachukue uraia wa nchi zingine. Inatambua kuwa uraia wa nchi mbili unaweza kuleta matatizo. Vile vile Marekani inawatahadharisha raia wake kuwa kuchukua uraia wa nchi nyingine kunaweza kuhatarisha uraia wao wa Marekani. Hii inaweza kuwa ni ajabu kwa wale wanaoamini kuwa Marekani ndio nchi yenye uhuru kuliko nchi zingine duniani.

Hata hivi, kuna aina ya uraia wa nchi mbili ambao Marekani inautambua bila kipingamizi. Mtoto anayezaliwa Marekani na ambaye wazazi wake si raia wa Marekani anahesabiwa kuwa raia wa Marekani na pia raia wa nchi ya wazazi wake. Huu uraia wa nchi mbili hauna mgogoro katika taratibu na sheria za Marekani. Kadhalika, sheria za Marekani zinamtambua mtoto wa waMarekani anayezaliwa nchi nyingine kuwa ni raia wa Marekani, pamoja na kuwa anaweza pia kuwa raia wa nchi ile alimozaliwa. Huu ni uraia wa nchi mbili ambao Marekani inautambua bila tatizo.

Kwa upande wa Tanzania, tunao pia watoto wanaozaliwa nchi za nje lakini wazazai wao ni waTanzania. Naona ni sahihi kuwatambua watoto hao kuwa raia wa nchi mbili. Vile vile, kuna mtoto ambaye mzazi wake mmoja ni Mtanzania na mzazi mwingine si mTanzania. Mtoto huyu naona anastahili kuhesabiwa kuwa raia wa nchi mbili.

Sababu moja wanayotoa Watanzania wanopigania uraia wa nchi mbili ni kuwa uraia wan chi mbili utawafungulia milango ya uwekezaji nchini Tanzania au itawaletea urahisi wa uwekezaji. Sina hakika kama hoja hii ina uzito, kwani watu wengi ambao si raia wa Tanzania wanawekeza Tanzania bila matatizo. Je, ni kweli kwamba uraia wa nchi mbili ndio utawafungulia njia waTanzania kuwekeza nchini? Ni kweli kuwa wanapokuwa hawana uraia wa nchi mbili wanakutana na vipingamizi katika uwekezaji nchini? Naona suala hili linahitaji ufafanuzi.

Katika mahojiano na Ndugu Michuzi, nilisema kuwa kwa jinsi dunia inavyokwenda, chini ya utawandazi, labda nchi zitatoweka, na itabaki dunia tu. Vizazi vijavyo, vinavyolelewa katika mazingira tofauti na yale niliyokulia mimi vitakuwa na hisia na msimamo tofauti na wangu kuhusu uraia. Katika dunia ya leo inayozidi kukumbwa na utandawazi, juhudi za nchi mbali mbali kuungana kiuchumi, kisiasa, na kadhalika, yawezekana mipaka ya nchi itatoweka. Suala la uraia litachukua sura mpya. Labda hapatakuwa na sababu ya uraia wa nchi yoyote, wala uraia wa nchi mbili. Labda watu watakuwa raia wa Afrika Mashariki, basi, au raia wa Afrika basi, badala ya kuwa raia wa Tanzania, Cameroon, au Sudan, kama ilivyo sasa. Malumbano ya uraia wa nchi mbili sherti yazingatie huu uyakinifu.

4 comments:

sanga said...

Prof. Mbele asante sana kwa huu mjadala wa uraia wa nchi mbili. Kwa kweli umeandika vizuri na umeeleza wazi msimamo wako na mtanzamo wako.

Najua umeongea kipengere cha waTanzania wanadai kwamba wakiwa raia wa nchi mbili watawekeza Tanzania umesema hudhani kwamba hii ni kweli lakini umeacha kwamba utafiti zaidi inabidi ufanyike. Hapa mimi nitakuwa wazi kwamba kwa uchunguzi wa kina ambao mimi mwenyewe nimefanya ni kwamba watanzania hata wawe na uraia wa nchi mbili HII HAIWEZI kuongeza uwekezaji Tanzania au kuwafanya wawekeze Tanzania. Hii ni kisingizio tuu cha sisi watanzania katafuta visababu ambavyo wala havina msingi na havina logic yeyote. Hivi leo hii nini kinanizuia mimi nisiwekeze Tanzania? Na hivyo hivyo nini kinamsumbua bwana Kyando wa kanada kuwekeza Tanzania? Mbona kuna watu wengi tuu wanawekeza Tz ambao siyo raia watanzania? Nilibahatika kwenda Zanzibar mwaka 1990 na kukaa pwani ya mashariki ya visiwa hivi hakukuwa na ujenzi wowote ule. Leo hii nimekwenda pale tena kuna hoteli nyingi mpya zimejengwa na eneo lote limechukuliwa sasa na wamarekani, wasomali, wa-Ulaya (European), wahindi na wengine. Hawa wote siyo watanzania na sisi watanzania tunabaki na visingizio tuu kwamba tuwe na uraia wa nchi mbili.

Sababu kubwa watu wengi hawasemi ni kwamba hawapo tayari na usumbufu wa kutafuta visa wakati wa kurudi Tanzania na wengine kama waliopo hapa Marekani pengine ingekuwa wa-save $100 ya visa. Najua hapa nifanya uchokozi lakini huu ndiyo ukweli wenyewe.

Pengine kuna sababu zingine ambazo watu wanataka kuwa raia wa nchi mbili lakini sababu ya kwamba kutokuwa raia wa nchi mbili kunazuia uwezekaji ni sababu tuu ya kisiasa at best kuliko kwamba ni sababu ya msingi. Nani asiyejua kwamba wale wahindi wote wa Iringa au Dar siyo raia wa Tanzania ki-ukweli isipokuwa tuu kuwa na passport kwa jina tuu? Sasa kweli wewe mtanzania mwenye bibi yako na babu yako mnyalukolo mtu akuzuie kuwekeza Tanzania? Pia ukweli niTanzania wangapi kweli watawekeza kama wakipewa uraia sehemu zote mbili? Je wamewekeza huko waliko? Enterprenuship ipo kwenye damu za watu na mazingira. Kizazi cha sisi tuliotoka kwenye ujamaa kwa kweli ni vigumu sana kuwa wawekezaji pengine tuombe mungu kwamba kizazi cha sasa hivi mungu akijalie kweli wawe wawekezaji kama walivyowasomali na wakenya. Kizazi cha ujamaa tunajua sana kuongea lakini vitendo almost hakuna. Kila siku vikao lakini hakuna utekelezaji.

Pengine nirudi kwenye kwenye kipengere cha kiapo cha uraia wa marekani. Ni kweli mtu unakula kiapo cha kuwa ni raia wa nchi ya marekani na kwamba utapigia nchi ya marekani. Sasa hapa ni swala la mtu kuangalia tuu uwezekani wa nchi yako kweli kupigana na marekani. Mimi binafsi sidhani kwamba kuna siku moja at least in my life time kwamba Tanzania itapigana na Marekani kwa hiyo mtu inatakiwa uchague nchi gani utapigania. Ila nchi zingine kama wakati wa vita baridi ukitoka urusi pengine kweli you have to consider hii possibility very serious. Au kwa miaka ya nyuma au mbele kama mtu umetoka china bado kuna possibility kwamba siku moja unaweza ukaambiwa kwamba China na marekani zipo vitani na wewe lazima upiganie upande wa marekani (hii kwa sasa inaendelea kuwa remote possibility) lakini inaweza kutokea. Ukiwa raia umetoka Iran or North korea kweli inaweza kutokea. Chukulia baadhi ya askari wa jeshi la marekani ambao asiri yao ni Iraq waliweza kwenda kupigana kule chini ya jeshi la marekani.

Ukiacha hilo la vita kuwa raia wa marekani na nchi nyingine siyo gumu kama ambavyo wengine wanasema. Chukulia wayahudi wengi nchi hii ni raia wa marekani na Israeli lakini huoni matatizo yeyote ya msingi ambayo yanawakumba. Vivyo hivyo raia wengi wa wenye asili ya India ni raia wa India pia raia wa marekani na sidhani kama unasikia matatizo mengi.

Mwisho napenda kusema asante kwa kuandika kwa uwazi juu ya swala hili ambalo mara nyingi linaongelewa katika muundo wa ushabiki bila kuwa na analysis yakutosha. Samahani kwamba nimechanganya kiswahili na kingereza that in part is my laziness.

Asante sana

Yasinta Ngonyani said...

Ni mada nzuri ahsante sana Nimefurahi na nimejifunza kitu.

John Mwaipopo said...

Prof mbele nadhani kwa mtu anayejitambua kuwa mtanzania uraia wa nchi moja tanzania unamtosha kuliko wa nchi mbili. wengi wa wanaopigia baragumu uraia wa wa nchi mbili ni 'wakimbizi' wa kitanzania walio marekani. walioko nchi nyingine sio sana. hata mie pia nadhani wanaodai urai wa namna hii wana ubinafsi zaidi kuliko ujamaa. ujamaa kwa maana ya umoja sio ososhalist. hivi wanaona nini kuachana na uraia wa tanzania ilihali bado tanzania haijapasisha uozo huu. hapa napata majibu kuwa kuna raha ya kuwa mtanzania.

hasara nyingine ni uhalifu. uraia wa nchi mbili unaharufu ya kuzalisha wahalifu wa kimataifa. kazi yao itakuwa kuharibu kumoja na kukimbilia kwingine. kwa hili najua watawaka moto kidogo.

swali: kwani kwa sasa wanakosa nini kuwa watanzania katika nchi isiyo tanzania?

Unknown said...

Kuna kuwekeza kisheria na kuwekeza kimazoea! sijui Prof analenga kipi hapo. Km sheria inapinga uraia wa nchi mbili na ukipata uraia wa Rwanda basi ww si mtanzania hii inamanisha kwamba unastahili vikwazo km mngarwanda...

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...