Darasa Chini ya Mti

Makala hii, inayotokana na picha inayoonekana hapa chini, ilichapishwa katika gazeti la KWANZA JAMII. Ni makala ya pili. Kusoma makala ya kwanza, bofya hapa.


Darasa Chini ya Mti

Na Profesa Joseph L. Mbele

Nimeona picha kwenye blogu kadhaa ambayo inamwonyesha mwalimu na watoto wa darasa la kwanza, chini ya mbuyu. Ubao wa kuandikia umepigiliwa kwenye mbuyu. Kama inavyotegemewa, Watanzania wanalalamikia hali hiyo. Wanauliza kwa nini watoto wasome katika mazingira ya aina hii. Wengine, kama kawaida, wanaishutumu serikali.

Napenda kuliangalia zaidi suala la darasa kufanyika chini ya mti. Je, ni balaa kama tunavyodai au kunaweza kukawa na mtazamo mwingine?

Kuna vijiji na jumuia nyingi nchini mwetu ambazo hazina shule. Sababu moja ni kuwa idadi ya watu katika nchi yetu inaongezeka muda wote. Vijiji vinaenea sehemu za mbali ambazo zamani zilikuwa mapori au mashamba. Watoto wanatembea mwendo mrefu kwenda shuleni. Na kadiri watu wanavyoendelea kujenga mbali na shule, mwendo wa kutembea hadi shuleni unaongezeka.

Sasa je, ni bora watoto hao waendelee kwenda mwendo mrefu kila siku hadi kwenye shule au ni bora wapate fursa ya kusoma chini ya mti, hapo kijijini pao? Je, wangoje hadi wajengewe shule ya matofali iliyoezekwa bati, au ni bora wapewe fursa ya kuanza masomo chini ya mbuyu hapa hapa kijijini?

Katika vijiji vingi Tanzania, vikiwemo hivi vinavyoendelea kujitokeza, watu wana dhiki kifedha. Wanaishi kwenye nyumba za makuti na hawana kipato cha uhakika. Hawana uwezo kifedha lakini wanataka watoto wao waanze angalau kujifunza kusoma na kuandika. Wanafurahi kumpata mwalimu na wako tayari kuanzisha darasa chini ya mti. Kwa mtazamo wangu, watu hao wakifanikiwa kumpata mwalimu akaanzisha shule chini ya mti, ni hatua moja mbele.

Tuliangalie suala hili kwa mtazamo wa wanakijiji. Bila shaka walikaa, wakatathmini hali ya kijiji chao na mahitaji ya watoto wao, wakaamua kuanzisha shule. Walimtafuta mwalimu, wakatafuta huo ubao, na pia wakasogeza mbao za kukalia watoto. Walipitisha uamuzi kila mzazi atafute sare ya shule. Kwa kipato cha watu wa hapo, huenda huu mradi wa sare ulikuwa mgumu sana. Lakini wamejitahidi, na kila mtoto ana sare.

Hapo ubaoni zinaonekana hesabu za kujumlisha. Haya ni maendeleo kwa hao watoto na kwa hicho kijiji. Si sahihi kupuuzia ukweli huu. Tuwape wanakijiji wa hapo heshima wanayostahili, kwa juhudi waliyofanya hadi sasa. Sisemi turidhike na hali. Nasema kuwa wanakijiji hao wamepiga hatua inayostahili kutambuliwa.

Katika elimu, jambo la msingi si jengo. Wakristu tunafahamu kuwa Yesu alifundisha watu popote, na mafanikio yake hayakuathirika kwa sababu ya kukosa jengo. Watu wengi maarufu katika nchi yetu walianza shule chini ya mti. Marehemu Oscar Kambona, kwa mfano, alisoma shule ya msingi chini ya mwembe kijijini kwake Kwambe, karibu na Mbamba Bay. Mwembe huo bado uko.

Mwalimu Nyerere alipohamasisha kisomo cha watu wazima na kisomo chenye manufaa hakusema kuwa lazima pawe na majengo. Wengi walisoma chini ya mwembe au mkorosho.

Mambo mengi muhimu, kama vile mazungumzo na mijadala, yanaweza kufanyika chini ya mti. Mwalimu Nyerere alipoongelea demokrasia ya enzi za wahenga wetu, alisema kuwa wazee walikuwa wanakaa chini ya mti na kujadiliana hadi wakubaliane. Hakusema kuwa walikaa katika jumba la mikutano, nasi hatujawahi kulaumu kwa nini walikaa chini ya mti. Iweje suala la darasa kuwa chini ya mti litukera namna hii?

Katika kufundisha kwangu Marekani, nimeona kuwa nyakati ambapo jua linawaka vizuri, wanafunzi wanaomba tukafanyie darasa nje, chini ya mti. Ingawa mwanzoni, kutokana na mazoea, sikuwa napenda kuondoka darasani, hatimaye nilizoea. Siku inapokuwa nzuri, ni kawaida kuona madarasa yakifanyika chini ya miti. Ingawa Wamarekani hawafanyi darasa chini ya mti sababu ya kukosa majengo, hoja yangu ni kuwa kufanyia darasa chini ya mti haimaanishi kuwa elimu inadunishwa. Kuna mambo kadha wa kadha ya kuangalia kabla ya kutoa hukumu kama tunayotoa tunapoona watoto wakisoma chini ya mti.

Watanzania tunapoongelea elimu tuwe tunatofautisha kati ya mambo ya msingi na yasiyo ya msingi. Tukiona watoto wanasoma chini ya mti, tusitoe hukumu za upesi bila tafakari. Jambo la msingi ni somo au elimu, sio kuwepo au kutokuwepo kwa jengo. Jengo linaweza kuchangia ubora wa elimu katika mazingira fulani, lakini sio kila penye jengo bora pana elimu bora.

Tabia hii ya kutoangalia mambo ya msingi inajitokeza kwa namna nyingine pia katika nchi yetu. Watanzania wengi wanaamini kuwa watoto wakifundishwa kwa kiIngereza, elimu inakuwa bora. Wengi wanaamini kuwa watoto wakiweza kuongea kiIngereza wanakuwa wameelimika vizuri. Ndio maana kuna utitiri wa shule zinazotumia kiIngereza.

Siku hizi umezuka mtindo wa watoto kuvaa majoho na vikofia maalum wakati wanapohitimu shule. Majoho na vikofia vinachukuliwa kama dalili ya shule bora au elimu bora. Ukweli ni kuwa elimu si majoho wala vikofia. Watoto wanaweza kuwa wameelimika vizuri hata kama wanavaa kaptula na shati siku ya kuhitimu. Vivyo hivyo, kusoma chini ya mti si hoja. Cha msingi ni masomo yenyewe.

Ninaposema hayo yote simaanishi kuwa majengo hayana umuhimu. Lakini si vizuri kusema kuwa kila jamii ingoje hadi ijenge majengo mazuri ndipo watoto waanze kufundishwa na mwalimu. Ni bora mwalimu aanze darasa chini ya mti. Kama watoto wana daftari na kalamu, na mwalimu wao ana ubao na chaki, inatosha, kwa kuanzia.
Kadiri kijiji kinavyopata nguvu, kinaweza kujikongoja na shughuli ya majengo na mahitaji mengine.

Comments

nilikusoma hapa na kujifunza mengi. nikiwa mfanya tahajudi(meditation) pia naona umuhimu wa kukaa nje au juani nakufurahi uasili na nguvu zitokazo hapo. kuna mengi ya kujifunza katika hili pia

hata vile vijishule vya kata, kunajambo vimelifanya la msingi kadri nilivyoona kule kijijinikwetu, kuna wanaopata maarifana wasingeyapata kama sio shule kata zetu hizi
Ni darasa nzuri sana nimelipenda na nimekumbuka mbali sana. Miaka hii watu wanapenda sana kuiga na kutaka kusahau uasili wao. Pia je? haingewezekana wangeanza kujenga shule za misingi na kuendelea na kata, yaani za sekondari. Je wanadhani watapata wapi watoto wa kusoma sekondari kama hawajasoma shule ya msingi. Ni wazo tu lilinijia.
Mbele said…
Nimekuwa nikiwazia kuandika makala ya tatu kutokana na picha hii, kuhusu hivi vitoto, na hasa haka katoto kalikokaa pembeni kushoto, ambako hakataki hata kuangalia ubaoni.
ushauri wangu andika ili wengine tujifunze nadhali itakuwa safi sana. Nimeipenda sana hii makala.
KUMBUKUMBU said…
Haka katoto ambako hata hakaangalii ubaoni nahisi ni mtoto wa mwalimu ambaye anachuga mzigo wa mwalimu ulio pembeni.Bila shaka darasa lake ni la chini kidogo na ni lazima awe na baba kazini kwa kuwa mama hayupo nyumbani.
Albert Kissima said…
Naam, nami nimeipenda sana makala hii, na ni changamoto kubwa kwa walimu na wanafunzi hususani wa shule za kata. Ni changamoto pia kwa serikali.
Hebu tupate kujiuliza, mwalimu huyu karidhikaje hadi kufundisha ktk mazingira haya? Kajitolea? Au karidhika na anachokipata?
Au ni mwanakijiji aliyeamua kujitolea?
Je, serikali inakitambua kituo hiki cha elimu? Kwa maana ya usajili na mambo mengine.Si jambo la kushangaza pale utakaposikia serikali inakataa kukitambua kituo hiki kwa kigezo kuwa hakijakidhi au hakijafikia hadhi ya kuweza kusajiliwa(kwani destination ya watoto hawa ni muhimu ikitambulika). Na hapa ndipo itabidi tena kujiuliza nini tafsiri ya serikali ktk dhana nzima ya elimu na uelimishaji. Kweli, naheshimu jitihada za wananchi hawa, lkn najiuliza kama serikali nayo imeheshimu au itaweza kuheshimu jitihada hizo. Wananchi wameonyesha mwamko na umuhimu wa elimu ktk mazingira yao lakini serikali kwa kukwepa aibu itajifanya haijui kiendeleacho ktk kijiji hicho.

Darasa hili na madarasa mengine ya aina hii yana changamoto kubwa, kwani wakati wa mvua yabidi masomo yaahirishwe.
Christian Bwaya said…
Nimesoma na kutafakari. Nitasema wakati mwingine.

Asante sana Profesa kwa uchambuzi mzuri.
Sisulu said…
kusoma chini ya mti jambo zuri! upepo unapiga hali ya hewa nzuri na hivi lakini je hao watoto wakiuliza waseme kero zao je hawatalitaja hilo la kusoma kwenye mti hapo? tukubali tu kwamba maendeleo bado yako nyuma speed yetu ya kuendelea bado inasuasua. TUPAMBABANENI

Popular posts from this blog

Kumbukumbu ya Kuzaliwa

Tenzi Tatu za Kale

Pesa za Majini