Saturday, January 29, 2011

Mikataba Bomu Itaendelea Kutumaliza

Wa-Tanzania wanalalamika sana kuhusu mikataba bomu ambayo inalisababishia Taifa hasara kubwa. Tafsiri yao, kwa ujumla, ni kwamba tunaingizwa katika janga hili na mafisadi ambao wanasaini kwa makusudi mikataba hii, kwamba hao ni wa-Tanzania wenye ubinafsi na uroho, na hawana uchungu na nchi, bali wanatafuta namna ya kunufaika wao. Mafisadi wetu hao wanashirikiana na mafisadi wa nje kuitafuna nchi yetu.

Kwa ujumla, nami nina hisia hizo. Kwanza kuna ukweli usiopingika kuwa maadili katika nchi yetu yanazidi kuporomoka. Vile vile nazingatia usemi wa wahenga kuwa lisemwalo lipo, na kama halipo laja. Pia tunaona taarifa kutoka sehemu mbali mbali za dunia kuhusu uozo wa rushwa katika masuala ya mikataba, zabuni, na kadhalika.

Lakini msimamo wangu hauishii hapa. Naamini kuwa hata kama tukiondoa kabisa rushwa na ufisadi, tukawa na watu wanaojali maslahi ya nchi na hao ndio wakawa wanaosaini mikataba yetu, bado tutaendelea kulizwa na mikataba bomu.

Kitakachosababisha janga hili ni kuanguka kwa elimu katika Tanzania. Kama ninavyosema daima katika blogu hii na sehemu zingine, wa-Tanzania tumejichimbia kaburi kwa kutothamini elimu ipasavyo. Ushahidi ni ufahamu wa lugha ulivyo duni, na utamaduni wa kununua na kusoma vitabu ulivyofifia au kutoweka miongoni mwetu.

Nikifafanua suala la lugha na kulihusisha na suala la mikataba, napenda kusema kuwa tupende tusipende, mikataba ya kimataifa itaendelea kuandikwa kwa ki-Ingereza, nasi tutajikuta tunasaini bila kuelewa vizuri kilichomo. Kuna matapeli wengi duniani, ikiwamo katika uwanja wa biashara na uwekezaji.

Wajanja, kwa kutambua umbumbumbu wetu, watachukulia mwanya huu kama mbinu ya kutukomoa. Laiti tungekumbuka msisitizo wa Mwalimu Nyerere pale tulipopata Uhuru, kuhusu maadui watatu tuliopaswa kupambana nao: umaskini, maradhi na ujinga.

Mwaka jana, serikali ya CCM ilitamka mara kwa mara kwamba imefanya marekebisho katika mikataba ya madini, ili kuziba mianya iliyokuwepo, iliyokuwa inatukosesha mapato tunayostahili. Sasa hapo nina suali. Ni nini kilichotufanya tusione hizo dosari tangu mwanzo? Kama si ufisadi, labda ni huu ujinga ninaoongelea. Binafsi, nakerwa kwamba serikali haijatuelezea undani wa suala hilo.

6 comments:

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Tatizo si mikataba mibovu bali hata woga na ugeugeu wetu. Kwanini tusifanye kama walivyofanya Tunisia na sasa Misri? Yaani tunazidiwa akili na ujasiri na watu wa Tunisia wasiofikia hata nusu ya watu wetu? Hapa wa kujilaumi ni sisi tunaoendekeza watawala wetu mafisi na mafisadi.

Mbele said...

Ufisadi ni tatizo kubwa. Papo hapo nauona ujinga kuwa tatizo kubwa zaidi na ambalo kulitatua itachukua miaka mingi, tofauti na ufisadi ambao unaweza kuuvunja kwa urahisi. Ni kiasi cha kujitokeza kiongozi mwenye uwezo wa kuwakamata na kuwaadhibu mafisadi kikweli kweli. Watakoma.

Lakini ujinga ni tatizo kubwa zaidi ambamo tumejitumbukiza wa-Tanzania, na tukianza kurekebisha na kama kupanda upya mti wa mbao. Hadi uanze kupata mbao, ni miaka mingi.

Vile vile, tukiendelea na uchambuzi wa matatizo yetu, tatizo jingine ni mfumo wa kibepari tuliorithi kutoka enzi za ukoloni, ambao leo tunauita ukoloni mamboleo. Tumefungwa minyororo kiuchumi, kiutamaduni, kifikra, na kadhalika kwenye mfumo huo uliotuwala wakati wa ukoloni.

Hata fikra tunazodhani ni za ukombozi si za kikombozi, bali zimejengeka katika ukoloni mambo leo.

Kwa mfano hii imani kuwa tunahitaji chama cha siasa, au vyama vya siasa ni ukoloni mambo leo wa kifikra, kwa maana ya ukasuku.

Unknown said...

Katika Dunia Hii Hakuna Mtu wa Ziada Atakayeweza Kufikiria Kwa Niaba Yetu.

Mbele said...

Ndugu Mcharia, ni kweli usemayo. Nimekumbuka jambo jingine ambalo litatufanya tuendelee kusaini mikataba bomu, nalo ni tabia ya mTanzania (na mw-Afrika kwa ujumla) ya kumtetemekea na kumsikiliza mzungu kwa kila asemalo. M-Tanzania hafahamu kuwa huku ughaibuni kwa wazungu nako kuna wababaishaji na matapeli. Kuna tahadhari nyingi zinatolewa mahali kama huku Marekani, kuwaonya watu wajihadhari na utapeli. Lakini Tanzania hatuna tahadhari yoyote kuhusu matapeli wa kizungu.

Wababaishaji na matapeli hao wakija kwetu tunawapokea kwa heshima zote na kuwasikiliza kwa kila wanalosema. Kwa mtaji huu, itaendelea kuwa rahisi sana wao kuleta mikataba yao na kutuingiza mjini.

MAVERICK THINKING said...

Hii issue ni complex than we can imagine. Lkn ni hatua nzuri tumeanza angalau kuliongelea, maana sio zamani sana haya mambo yalikuwa kama taboo fulani. Iwe ni ukoloni mamboleo, ufisadi au ujinga bado lawama ni ZETU.Na kutafuta cosmetics solutions sio issue, tunahitaji katiba mpya, sheria mpya. Lakin zaid tunahitaji ukombozi wa kifikra. A New start, rethinking our formation and education process.

MAVERICK THINKING said...

Mda mrefu sana nimekuwa nafikiria kuhusu umaskini wetu, ushamba, ufisadi, udikteta, uafrika hasa nilipokuja amerika. Unapokutana na tamaduni nyingine ndio mara nyingi unajitafakari nafasi yako na mchango wa taifa lako duniani. Kwa ujumla niliona na naona kama sisi ni wasindikizaji, kama sio victims ktk hii dunia. Na hizi narratives za sisi kuwa unpeopled, inferior zimekuwa internalized kwetu mpaka basi. Hizi ni plan za mkoloni. Mbaya zaidi sio hizi preachings, propaganda fides bali ni utayari wetu, mapokezi yetu. Tumeacha yetu na kukupambatia ya wengine kukumbatia bila inculturation, bila critical analysis. Hii ndio root cause ya mazingaombwe yote haya. In fact hatujielewi, therefore hatueleweki. Tuliingilia madirishan ktk hiki kijijini cha Utandawazi.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...