Tuesday, January 11, 2011

Wauza Vitabu wa Mitaani Dar es Salaam

Kitu kimojawapo kinachonivutia ninapokuwa Dar es Salaam ni wauza vitabu wa mitaani. Wako wa aina mbili. Wako wenye sehemu maalum ya kuuzia vitabu, iwe ni meza tu au kibanda. Hao wanaonekana sehemu mbali mbali za mjini Dar es Salaam, kuanzia katikati ya mji, kama vile barabara ya Samora, hadi sehemu za pembeni, kama vile Mwenge na Ubungo. Picha iliyoko hapa kushoto niliipiga Ubungo, mwaka jana, karibu na kituo kikuu cha mabasi. Pembeni ya mwuza vitabu kuna kibanda cha muuza machungwa.

Wako wauza vitabu wengine ambao hutembeza vitabu mitaani, sawa na wale vijana ambao wanatembeza bidhaa mbali mbali, ambao tunawaita machinga. Hapo kushoto kuna picha niliyopiga Sinza Kijiweni, mwaka jana, kwenye hoteli ya Deluxe.



Nilikuwa hapo, na hao vijana wawili wakaja, mmoja akiuza vitabu na mwingine peni za kuandikia. Nilivutiwa, nikaanza kuongea nao. Nilimwuliza huyu muuza vitabu kuhusu wateja, na kama wa-Tanzania wananunua vitabu, akanielezea uzoefu wake. Nilinunua vitabu viwili. Kimoja ni tafsiri ya maneno ya ki-Ingereza kwenda ki-Swahili, na kingine ni tafsiri ya maneno ya ki-Swahili kwenda ki-Ingereza. Vyote vimechapishwa Kenya, na walengwa ni wageni wanaotembelea Afrika Mashariki. Ni vijitabu vidogo vidogo sana, kimoja cha kurasa 30 na kingine kurasa 32.

Karibu na lango la kituo cha mabasi Ubungo nilipiga picha iliyo hapa kushoto, mwaka jana, baada ya kumwomba kijana mwenye kibanda hicho. Tuliongea kuhusu biashara yake, naye alinieleza kuwa biashara inaenda vizuri, ila ingekuwa nzuri zaidi kama angekuwa na mtaji wa kutosha ili kuwa na meza kubwa zaidi na vitabu vingi zaidi. Nilifurahi kusikia hivyo, ushahidi kuwa wako watu wanaonunua vitabu. Kinachobaki ni kufuatilia zaidi kuona ni watu wa aina gani. Yule kijana niliyeongea naye Sinza alisema kuwa wanaonunua vitabu zaidi ni watu wa Zambia. Nitafuatilia zaidi suala hili siku zijazo, panapo majaliwa.

Katika pitapita yangu na kuangalia nimeona kuwa kuna vitabu vya aina nyingi humo mitaani, kuanzia hadithi za waandishi maarufu wa sehemu mbali mbali za dunia, hadi taaluma mbali mbali. Kuna vitabu vilivyotumika na vipya pia. Mtu makini anaweza kujipatia vitabu vingi vya manufaa kutoka kwa hao wauzaji wa mitaani akawa na maktaba binafsi ya kueleweka.

6 comments:

Mbele said...

Baada ya kuandika makala hii, nimepita mtandaoni nikaona makala murua kuhusu suala hili. Soma hapa.

Fadhy Mtanga said...

Prof Mbele ni kweli Dar es Salaam kuna wauza vitabu wa namna hiyo maeneo mengi sana. Kuna mahali unakutana na vitabu ambavyo havipatikani kwenye maduka maalumu ya vitabu. Vipo vitabu vya zamani ambavyo vina utajiri wa maarifa huwezi kuvipata kwenye maduka makubwa mjini.

Pale kituo cha daladala Ubungo na pale darajani Sam Nujoma kwenye stendi ya daladala za Mlimani kuna vitabu vingi sana. Eneo jingine ni pale soko la Kisutu Mjini, kituo cha daladala Buguruni Chama.

Huwa nafaidi sana kupata nakala za vitabu vya zamani ambavyo pengine havichapwi tena sasa.

Mbele said...

Ndugu Mtanga, shukrani kwa ujumbe. Nilijisikia vizuri kununua vitabu kama nilivyoelezea hapo juu.

Hao vijana wanahangaika kujipatia kipato kwa jasho lao. Tunaponunua vitabu vyao tunatoa mchango muhim katika ajira yao. Sisi wenyewe tunafaidika pia, kwa kujiongezea hazina ya vitabu.

Hii Deluxe ni hoteli na baa. Nilikuwa hapo nikipata kabia. Lakini kitu nilichofanya ni kidogo tu, yaani kupunguza bajeti ya bia na badala yake kununua hivyo vitabu.

Ni ushahidi wa yale ninayosema daima katika blogu hii na blogu za wengine, kwamba wa-Tanzania tuache visingizio kuwa hatuna hela za kununulia vitabu. Tukipunguza kidogo tu bajeti ya ulabu, tunaweza kununua vitabu kila mwezi, kama sio kila wiki.

Masangu Matondo Nzuzullima (MMN) said...

Mimi nadhani kununua vitabu kutoka kwa hawa vijana ni bora kuliko kuvinunua madukani ambako bei yake yaweza kubwa sana ukiachilia mbali huduma mbovu. Nilikwenda pale TUKI na nikataka kununua vitabu kama saba hivi. Basi nikavikusanya na kuviweka kwenye kaunta. Kulikuwa na wanawake wawili hivi wakiwa wanapiga stori zao wakati nachagua vitabu.

Nilipotaka kulipa ndipo mmoja akaniambia tena kwa sauti ya kejeli kwamba vile nilivyokuwa nimechagua vilikuwa ni vya "display" tu na nilitakiwa kuvirudisha nilipovitoa halafu niwaambie vitabu ninavyotaka ili wanichagulie kutoka katika boksi moja kubwa lililokuwa pembeni mwa ofisi yao. Sasa mimi nikajiuliza, mbona waliniacha nikapoteza muda wa karibu nusu saa nzima nikichagua vitabu hivi kimoja baada ya kingine na kuvipanga pale kwenye dawati lao bila kuniambia kuwa nilichokuwa nakifanya hakiruhusiwi na kwamba vile vitabu vilikuwa ni vya kuonyesha wateja tu. Hili ni suala la huduma mbovu kwa wateja.

Kufupisha hadithi, niliishia kununua kitabu kimoja tu kwani vingine vilikuwa chini kabisa kwenye lile boksi lao na walinitaka mimi tena eti ndiyo nianze kufukua humo kwenye boksi lao ili kutafuta vitabu nilivyokuwa ninavitaka. Nilikasirika baadaye nilipogundua kwamba pamoja na maudhi yote yale, hata kile kitabu nilichokinunua pale kwao kumbe ningekipata kwa bei rahisi sana kwa hawa wauzaji wa mitaani. Kuanzia siku hiyo nimeshaacha kununua vitabu madukani!

Emmanuel said...

Prof Matondo Pole
Hiyo ndio Tanzania yetu, huduma ni mbovu kwa makusudi kabisa. Tena sijui Wanawake wakishafikia umri fulani Tanzania ndiyo wanakera zaidi, nafuu wasichana. Pia, suala la vitabu kuwa na bei kubwa wakati ubora hamna ni jambo la kushangaza Tanzania.
Lakini kila mmoja wetu akitoa wazo lake labda pataeleweka.

Mbele said...

Profesa Matondo, shukrani kwa mchango wako. Vile vile pole kwa udhia uliokumbana nao.

Kweli nimekubali, blogu ni shule. Unaweka kitu kidogo kama hiki nilichoweka, lakini matokeo yake ni kuwa unapewa data na mawazo ya kupanua na kutajirisha ufahamu wako wa suala ulilolianzisha.

Hii ni motisha ya kutosha kwa mtu kuendelea kublogu.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...