
Kitu kimojawapo kinachonivutia ninapokuwa Dar es Salaam ni wauza vitabu wa mitaani. Wako wa aina mbili. Wako wenye sehemu maalum ya kuuzia vitabu, iwe ni meza tu au kibanda. Hao wanaonekana sehemu mbali mbali za mjini Dar es Salaam, kuanzia katikati ya mji, kama vile barabara ya Samora, hadi sehemu za pembeni, kama vile Mwenge na Ubungo. Picha iliyoko hapa kushoto niliipiga Ubungo, mwaka jana, karibu na kituo kikuu cha mabasi. Pembeni ya mwuza vitabu kuna kibanda cha muuza machungwa.

Wako wauza vitabu wengine ambao hutembeza vitabu mitaani, sawa na wale vijana ambao wanatembeza bidhaa mbali mbali, ambao tunawaita machinga. Hapo kushoto kuna picha niliyopiga Sinza Kijiweni, mwaka jana, kwenye hoteli ya Deluxe.
Nilikuwa hapo, na hao vijana wawili wakaja, mmoja akiuza vitabu na mwingine peni za kuandikia. Nilivutiwa, nikaanza kuongea nao. Nilimwuliza huyu muuza vitabu kuhusu wateja, na kama wa-Tanzania wananunua vitabu, akanielezea uzoefu wake.

Nilinunua vitabu viwili. Kimoja ni tafsiri ya maneno ya ki-Ingereza kwenda ki-Swahili, na kingine ni tafsiri ya maneno ya ki-Swahili kwenda ki-Ingereza. Vyote vimechapishwa Kenya, na walengwa ni wageni wanaotembelea Afrika Mashariki. Ni vijitabu vidogo vidogo sana, kimoja cha kurasa 30 na kingine kurasa 32.

Karibu na lango la kituo cha mabasi Ubungo nilipiga picha iliyo hapa kushoto, mwaka jana, baada ya kumwomba kijana mwenye kibanda hicho. Tuliongea kuhusu biashara yake, naye alinieleza kuwa biashara inaenda vizuri, ila ingekuwa nzuri zaidi kama angekuwa na mtaji wa kutosha ili kuwa na meza kubwa zaidi na vitabu vingi zaidi. Nilifurahi kusikia hivyo, ushahidi kuwa wako watu wanaonunua vitabu. Kinachobaki ni kufuatilia zaidi kuona ni watu wa aina gani. Yule kijana niliyeongea naye Sinza alisema kuwa wanaonunua vitabu zaidi ni watu wa Zambia. Nitafuatilia zaidi suala hili siku zijazo, panapo majaliwa.
Katika pitapita yangu na kuangalia nimeona kuwa kuna vitabu vya aina nyingi humo mitaani, kuanzia hadithi za waandishi maarufu wa sehemu mbali mbali za dunia, hadi taaluma mbali mbali. Kuna vitabu vilivyotumika na vipya pia. Mtu makini anaweza kujipatia vitabu vingi vya manufaa kutoka kwa hao wauzaji wa mitaani akawa na maktaba binafsi ya kueleweka.