Saturday, November 17, 2012

Mdau Wangu Mpya, Mhadhiri wa Mankato

Nimempata mdau mpya, mhadhiri katika chuo cha North Central, mjini Mankato, Minnesota. Natumia neno mdau au wadau kwa maana ya wasomaji wa vitabu vyangu ambao wanajitokeza na kujitambulisha kwangu. Nina kawaida ya kuwataja wadau hao katika hii blogu yangu, kama unavyoweza kusoma hapa na hapa.

Leo napenda nimwongelee huyu mdau mpya, Mhadhiri Davis. Wiki kadhaa zilizopita, nilipigiwa simu na Profesa Scott Fee wa Chuo Kikuu cha Minnesota, Mankato, akisema kuwa wakati anapiga simu, yuko katika mazungumzo na Mhadhiri Becky Davis, wakiongelea kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Alinipa fursa nikasalimiana na Mhadhiri Davis, ambaye anaonekana pichani hapa kushoto.

Waalimu hao walikuwa katika maandalizi ya kupeleka wanafunzi Afrika Kusini. Pamoja na kuongelea upatikanaji rahisi wa nakala za kitabu hiki, walikuwa wananialika Mankato kuongea na wanafunzi. Bila kusita, niliupokea mwaliko wao. Falsafa yangu ni kuwa Mungu kanipa fursa ya kuelimika sio ili nimwage mbwembwe bali niwafaidie wanadamu.

 Profesa Scott Fee tulifahamiana miaka kadhaa iliyopita, wakati anaandaa msafara wa wanafunzi wa kwenda Afrika Kusini. Katika maandalizi hayo, aliamua kutumia kitabu changu hicho. Kama sehemu ya maandalizi ya safari, alinialika chuoni kwake kuongea na wanafunzi kuhusu masuala ya tofauti za tamaduni, kama nilivyoelezea kitabuni. Nilienda, nikaongea na wanafunzi, ambao walikuwa wengi, kama ninavyokumbuka.

Baada ya kutajiwa jina la Mhadhiri Davis, niliingia mtandaoni kutafuta taarifa zake. Yeye ni mwandishi makini, kama ilivyoelezwa hapa. Nafurahi kuunganishwa na mwandishi mwenzagu, kwani kutakuwa na fursa ya kubadilishana mawazo na uzoefu.

Nashukuru kwamba kazi yangu ya kutafakari na kuandika kuhusu masuala ya tofauti za tamaduni inawagusa na kuwafaidia wengine. Insh'Allah, siku itakapowadia, nitaenda Mankato na kutoa mchango wa kiwango cha juu kwa kadiri ya uwezo wangu.

2 comments:

Anonymous said...

asanta Profesa Mbele ila ninaomba nikuulize kwni wewe sio mpenzi wa siasa?maana hukutumegea yaliyojiri wakati wa uchaguzi wa Marekani! samahani kwa usumbufu

Mbele said...

Mdau anonymous, shukrani kwa ujumbe wako. Kuhusu uchaguzi wa Marekani, mimi kama raia wa Tanzania ninaona yako ambayo tunaweza kujifunza kutoka kwao.

Moja ni utaratibu wa wagombea kujitokeza kwenye midahalo na kuhojiwa sana mbele ya wananchi na dunia kwa ujumla. Wagombea wanawekwa kwenye kitimoto na hapo wananchi wanapata fursa ya kumjua mgombea makini ni yupi na mbumbumbu ni yupi.

Ni fedheha sana kukumbuka jinsi wagombea wa CCM walivyokimbia midahalo mwaka 2010. Ni fedheha kubwa kukumbuka kwamba wapiga kura hawakuiadhibu CCM kwa dharau yake hiyo. Inaonekana CCM inaukumbatia umbumbumbu, na wananchi wengi nao ni mbumbumbu.

Kwa suala hilo, utaratibu wa Marekani ni mzuri.

Baada ya kusema hayo, napenda kusema pia kuwa siasa za Marekani zinaendeshwa na mfumo wa ubepari. Iwe ni chama cha Democrat au cha Republican, kimsingi vyote vinalinda maslahi ya mabepari ndani ya nchi na ulimwenguni.

Obama hawezi kukiuka mfumo huo, hata kama angalau anakubalika zaidi kuliko yule mwenzake. Hata kwa sisi wa nchi za nje, tunaona ni afadhali mtu kama Obama, kwa msingi kuwa angalau anaonyesha kuelewa umuhimu wa kutumia uungwana na heshima fulani katika kuwasiliana na dunia. Yule mwenzake alikuwa na kiburi kwa suala hilo, kwani alikuwa anaapa kwamba Marekani haipaswi kumwomba radhi yeyote hapa duniani.

Kifupi ni kwamba Marekani ni nchi ya kibeberu ("imperialistic") na kwa hivyo sisi wa-Gagagigikoko tusitegemee kuwa sera zake zinajali maslahi yetu.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...