Mafuriko Marekani

Wa-Tanzania tumezoea kusoma habari za mafuriko yanayotokea Dar es Salaam wakati wa mvua. Tumezoea kutoa lawama kwa wahusika wanaopaswa kushughulikia miundombinu na pia tunatoa lawama kwa watu wanaoishi mabondeni, kwani tunasikia ripoti kadha wa kadha kuwa wanagoma kuhama. Kumbe, adha ya mafuriko na maafa mengine ya aina hiyo hutokea sehemu mbali mbali za dunia, kama tunavyosikia katika vyombo vya habari. Hapa Marekani, kwa mfano, mafuriko hutokea mara kwa mara, sababu ya mvua kubwa, au wakati barafu na theluji zinapoyeyuka kufuatia kumalizika kipindi cha baridi kali. Mito hujaa, madaraja hufurikwa, nyumba za watu na sehemu za biashara huathirika.

 Wiki hii, katika jimbo hili la Minnesota na sehemu za jirani, kuna mafuriko makubwa kutokana na mvua kubwa. Uongozi wa jimbo unahangaika kujiandaa kutathmini hasara inayotokea, na kuna taarifa kuwa uongozi huo umepeleka habari kwa Rais Obama, ili atangaze hali ya dharura. Tangazo la aina hii huiwezesha serikali kutoa pesa za kufidia hasara. Serikali ina fungu maalum la fedha kukabiliana na dharura kama hizo Nimepiga picha hizi katika mji mdogo wa Northfield, ambapo ninaishi. Kuna mto unaopita mjini humo, ambao unaitwa Cannon River. Unaweza kuona jinsi ulivyofurika, hali ambayo hutokea mara moja moja, wakati wa mvua kubwa au kuyeyuka kwa barafu na theluji. Mito mingine ya sehemu hii ya Marekani imefurika pia. Taarifa zilizopo ni kuwa mto Mississippi, ambao hauko mbali na hapa, unaendelea kufurika, ingawa tayari umeshafurika.

Nimeleta habari hii, ili kukumbushia kuwa maafa hutokea sehemu mbali mbali za dunia, hata katika nchi zenye miundombinu imara na bora kama Marekani. Mbali ya mafuriko, hapa Marekani kuna vimbunga viitwavyo "tornado" ambavyo uharibifu wake hausemeki. "Tornado" ikitua kwenye mji, inavunja majumba na hata kurusha magari hewani na kuyabwaga sehemu tofauti, pengine mbali na pale yalipokuwepo. Sehemu zingine za dunia zinakumbwa na kimbung, sehemu zingine zinakumbwa na tetemeko la nchi na kusababisha uharibifu mkubwa. Hivi karibuni, kwa mfano, tumeshuhudia jinsi sehemu ya mlima ilivyoporomoka kule Afghanistan na kupoteza maisha ya watu wengi na mali zao. Kilichopoo, pamoja na kuchukua tahadhari, kama vile kujenga katika maeneo yanayoonekana yana usalama, tukae tukiomba Mungu atuepushie mbali majanga hayo.

Comments

Anonymous said…
mungu awape subra hao wananchi, ila Tanzania tukubali Kule mabondeni na Kama Gongolamboto kulikotokea mabomu wananchi wanajitakia, sehemu zile sio za kujengwa nyumba ila wanaotowa vibali vya kujengwa na wananchi wanaokubali ili wapate kujenga tu bila muundo mbinu ni wanamakosa huo ndio ukweli ila wote tunajuwa mafuriko yanaweza kumkuta mtu popote pale ila ujengaji wa ovyo Tanzania upingwe Usalama wa mazingira hakuna.
Mbele said…
Asante kwa ujumbe wako. Tunakubaliana kuwa kuna aina fulani ya uzembe Tanzania ambayo husababisha hasara ya maafa haya ya mafuriko kuwa makubwa mno.

Popular posts from this blog

Kumbukumbu ya Kuzaliwa

Tenzi Tatu za Kale

Pesa za Majini